KITABU CHA SHETANI (7)

Zephiline F Ezekiel
Mtunzi: Aziz Hashim

SEHEMU YA SABA
TULIPOISHIA...
“Hapana, sihitaji ambulance, nimekuja na gari langu,” alisema Samantha huku akivaa tena ile nikabu yake na kuuficha uso wake, manesi na madaktari wakasaidiana kumpakiza mgonjwa kwenye gari kisha baada ya hapo daktari mkuu akataka manesi wawili waongozane naye lakini Samantha alikataa,

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

TUENDELEE...
jambo lililowashangaza wote.

Harakaharaka akaingia kwenye gari na kupiga ‘starter’ kisha akawasha taa za mbele za gari hilo, akaondoka kwa kasi mpaka getini. Akiwa anataka kutoka na kuingia barabarani, alishtuka baada ya kuliona gari la baba yake nalo likiwa linakata kona ya kuingia hospitalini hapo.

“Mungu wangu!” alisema Samantha kwa hofu kubwa.

Harakaharaka msichana huyo alipandisha vioo vya gari lake, akamuona baba yake akivua miwani na kulikodolea macho gari hilo akiwa ni kama haamini. Akaingia barabarani na kukanyaga mafuta kwa nguvu, gari likawa linakimbia kwa kasi kubwa.

“Dereva hebu geuza gari mara moja, lile gari siyo analoendesha mwanangu Samantha?” alisema baba yake Samantha baada ya gari alilokuwa akiliendesha Samantha kuwapita kwa kasi pale getini wakati wakitaka kuingia Hospitali ya Mwananyamala.

Harakahara dereva akaanza kuhangaika kugeuza gari na kusababisha madereva wenzake wawe wanampigia honi kwa fujo kwani alikuwa akisababisha foleni. Hatimaye akafanikiwa kugeuza na kuelekea kule lile gari lilikoelekea huku baba yake Samantha akimsisitiza kuongeza mwendo.

Kwa mbali wakawa wanaliona gari hilo ambapo walipotazama namba waligundua kuwa ndiyo lenyewe, mzee huyo akawa anamhimiza dereva kuhakikisha anaongeza kasi mpaka alifikie.

***

Samantha akiwa anakanyaga mafuta na kusababisha gari liwe linaenda kwa kasi kubwa, alishtuka zaidi baada ya kuona gari la baba yake nalo likigeuza na kuanza kumfuata kwa nyuma. Akazidi kuchanganyikiwa, akawa anaendelea kuendesha gari kwa kasi huku akitazama nyuma kwa kupitia vioo vya pembeni, akaona gari la baba yake likizidi kuongeza kasi, hofu ikazidi kumjaa.

Japokuwa barabara ilikuwa na magari mengi, Samantha alizidi kuongeza kasi, akawa anazipita daladala kwa namna ambayo ilikuwa rahisi sana kusababisha ajali, muda mwingine akawa analazimika ‘kutanua’ na kutoka nje ya barabaraba, madereva wengine wakawa wanapunguza mwendo ili kuepusha ajali.

Japokuwa kulikuwa na matuta makubwa kwenye eneo la Mwananyamala Komakoma, Samantha aliyapita bila kupunguza mwendo hata kidogo na kusababisha gari liruke juu na kuzua taharuki kwa watumiaji wengine wa barabara, dakika chache baadaye akawa ameshapotea kabisa eneo hilo.

“Ongeza mwendo! Inawezekanaje akushinde wakati wewe umesomea udereva? Nitakufukuza kazi.”

“Lakini mzee, hili gari lipo chini na huwezi kupita kwa kasi kwenye matuta haya makubwa kama yeye alivyofanya, tutaharibu gari au tutapata ajali,” dereva alijitetea lakini utetezi wake haukuwa na maana kwa mzee huyo ambaye tayari kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka.

Akamlazimisha dereva kusimama haraka, akateremka na kukaa mwenyewe nyuma ya usukani, akaondoa gari kwa kasi lakini tayari alishachelewa kwani Samantha alishapotea kwenye upeo wa macho yao, walipofika eneo la Kinondoni Studio, kwenye makutano ya Barabara za Mwananyamala na Kawawa, walishindwa kuelewa kama Samantha ameelekea kulia au kushoto, wakajikuta wakikwama.

***

Baada ya kuendesha gari kwa kasi kubwa, akinusurika kupata ajali mbaya zaidi ya mara nne, hatimaye Samantha aliwasili Mlingotini, Bagamoyo, nyumbani kwa mzee Tenson Shiwinga, mganga wa baba yake ambaye alizoea kumuita babu.

Akafunga breki kali na kusababisha gari liseleleke na kutoa mlio uliomshtua Mzee Shiwinga ambaye alikuwa ndani ya kibanda chake cha miti, udongo na makuti, akatoka akiwa amejifunga shuka jekundu na kupigwa na butwaa kumuona Samantha akishuka kwenye gari huku akihangaika kumteremsha mtu ambaye ilionesha wazi alikuwa hajitambui.

“Babu nahitaji msaada wako, nisaidie niko chini ya miguu yako.”

“Samantha? Kuna nini tena mjukuu wangu? Baba amekutuma?”

“Hapana babu, nisaidie kwanza nitakueleza kilichotokea. Huyu ni mchumba wangu nataka umsaidie kumtoa sumu, nimemng’ata kwa bahati mbaya, fanya kila liwezekanalo akipona nakuahidi nitakupa zawadi kubwa sana,” alisema Samantha huku machozi, jasho na kamasi vikimtoka kwa wakati mmoja.

Mzee Shiwinga alimtazama Samantha usoni na kugundua kuwa alikuwa analia, akawa hana namna zaidi ya kumsaidia. Akamsaidia kumbeba mtu huyo ambapo kutokana na jinsi mzee huyo alivyokuwa na nguvu licha ya umri wake mkubwa, alimbeba kwenye mikono yake na kutembea naye haraka kuingia ndani ya kibanda chake.

Samantha akawa anafuata kwa nyuma huku baibui aliyovaa akiiona kama mzigo, alitamani aivue na kuitupa mbali lakini haikuwezekana, akawa anaendelea kulia huku akimsisitiza mzee huyo kufanya kila linalowezekana kumsaidia kijana huyo.

Baada ya kumuingiza ndani ya kibanda chake kilichojaa matunguli, pembe, kwato, mikia na ngozi za wanyama mbalimbali wa porini, mzee huyo alimlaza juu ya ngozi ya chui aliyokuwa akiitumia kuwatibu wagonjwa wake, akachukua kibuyu kimoja na kukitingisha kwa nguvu kisha akakifungua ambapo kilitoa gesi kama soda inayofunguliwa.

Akanywa dawa zilizokuwa ndani yake kisha akaanza kumnywesha mgonjwa wake kwa kutumia mdomo huku mkono mmoja akiutumia kufungua bandeji kwenye jeraha la kung’atwa lililokuwa shingoni. Baada ya kumnywesha, alichukua kibuyu kingine chenye dawa na kumwagia juu ya jeraha, akaanza kuliminyaminya huku akitamka maneno ambayo Samantha hakuyaelewa.

Sekunde chache baadaye, mganga huyo alitoka mbio na aliporejea alikuwa na majani kadhaa mkononi ambayo aliyatafuna harakaharaka na kuanza kumtemea mwili mzima.

”Anaitwa nani?”

“Edmund!” alisema Samantha huku akijifuta machozi, mganga huyo akaanza kulitaja jina la Edmund huku akichanganya na maneno mengine ambayo hakuyaelewa, akaendelea kuchakarika, akitumia karibu vibuyu vyote vilivyokuwa na dawa, muda mfupi baadaye, wote walishtuka baada ya kusikia Edmund akipiga chafya mfululizo kisha akafumbua macho.

“Ooh! Edmund wangu jamani, siamini,” alisema Samantha na kuanza upya kuangua kilio huku akimkumbatia Edmund kwa nguvu. Bado Edmund alikuwa amepigwa na butwaa, akawa anashangaashangaa akiwa haelewi kinachoendelea.

“Sa...ma..ntha...” alisema kwa tabu huku akijaribu kuinuka lakini maumivu makali shingoni yakamfanya arudi tena pale chini.

“Ni..ni kime..tokea? Ha..pa ni wa...pi?” alihoji Edmund huku akiendelea kushangaa, maswali mengi yakipita ndani ya kichwa chake.

“Tupo kwa mganga Edmund, nisamehe kwa yote yaliyotokea, nitakueleza kila kitu kilichotokea,” alisema Samantha huku akiendelea kulia, ikabidi mganga amsogeze pembeni kwani bado alikuwa na kazi kubwa ya kuendelea kumhudumia, Samantha akakubali kusogea pembeni lakini bado alikuwa akiendelea kulia kwa uchungu.

Mganga Shiwinga aliendelea kumfanyia dawa Edmund na baada ya takribani saa mbili kupita, Edmund alikuwa na uwezo wa kuinuka mwenyewe na kukaa japokuwa bado alikuwa akilalamikia maumivu makali.

“Una bahati sana kijana, tayari ulishafariki, ni kama muujiza tu! Umshukuru sana Samantha kwani asingekuwahisha pengine tungekuwa tunaongea mengine hivi sasa,” alisema Mganga Shiwinga wakati akiendelea kumkanda Edmund jeraha lake.

“Samantha,” aliita Edmund, harakaharaka msichana huyo aliyekuwa amekaa juu ya kiti cha miguu mitatu akiwa amejikunyata, aliinuka na kumsogelea Edmund, akambusu kwenye paji la uso kisha akakaa juu ya ile ngozi aliyokuwa amekalia Edmund.

“Unajisikiaje mpenzi wangu?”

“Bado shingo inauma, hebu niambie nini kimetokea? Halafu kwa nini jana uliondoka ghafla nyumbani kwangu? Kwa nini uliniumiza shingoni kiasi hiki? Kwa nini... mbona sielewi kinachoendelea? Na hapa nimefikaje? Kwa nini mganga anasema nilikuwa nimeshakufa?” Edmund aliuliza maswali mengi mfululizo akionesha kuchanganyikiwa kabisa.

Samantha alishusha pumzi ndefu na kumuomba mganga atoke na kuwapisha ili wazungumze kwa uhuru zaidi, mganga Shiwinga akafanya kama alivyoombwa, Samantha akashusha tena pumzi ndefu na kumtazama Edmund usoni.

“Naomba unisamehe sana kwa kilichotokea Edmund, halikuwa kusudio langu. Najua itakuwa vigumu kuniamini lakini naomba uelewe kwamba nimelijua kosa langu na nimeamua kukulinda kwa sababu naamini wewe ndiye utakayenitoa kwenye hiki kifungo Edmund!

“Sijawahi kufurahia maisha hata mara moja, usinione niko hivi napata kila ninachokitaka ukajua nina furaha, nateseka sana mwenzio! Nipo chini ya miguu yako.

“Naomba uniahidi kwamba hata nikikuambia ukweli bado utaendelea kuwa nami na kamwe hutaniacha, nakupenda Edmund,” alisema Samantha huku akilia kwa uchungu mkubwa na kumlalia Edmund kifuani, machozi yakawa yanamtoka na kutiririka kupitia kona za macho yake mpaka kwenye mwili wa Edmund.

Kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa akilia kwa uchungu, kabla hata Edmund hajajua anataka kumwambia nini, kitendo cha kushtuka na kujikuta nyumbani kwa mganga wa kienyeji huku msichana huyo akiwa pembeni yake, kilimfanya aamini kwamba hawezi kuwa na nia mbaya naye.

Kwa taabu alinyanyua mkono wake mmoja na kumshika Samantha mgongoni, akampigapiga kama ishara ya kumbembeleza na kumwambia yupo tayari kumsikiliza na atakuwa naye kwa hali zote. Kauli hiyo ilimfurahisha mno Samantha, akambusu Edmund mdomoni na kuanza kumueleza kilichotokea.

Akamwambia kwamba baba yake anamiliki utajiri mkubwa lakini kwa njia zisizo halali na kwamba kwa kipindi chote cha maisha yake tangu azaliwe, Samantha ndiyo kichocheo cha utajiri huo.

“Sijakuelewa unamaanisha nini,” Edmund alimkatisha Samantha, ikabidi aanze kumfafanulia kila kitu kwa kina.

Akamueleza kwamba wazazi wake wamepata utajiri walionao kwa njia za kishirikina na kwamba walikuwa wakiwachukua watu misukule na wengine kuwatoa kafara kwa kumtumia Samantha ili utajiri wao uzidi kuchanua siku baada ya siku.

Licha ya kujitahidi kufafanua, bado Edmund alikuwa hamuelewi msichana huyo, huku muda mwingine akijihisi pengine yupo kwenye ndoto ya kutisha na muda mfupi baadaye atashtuka na kujikuta akiwa amelala chumbani kwake.

Samantha alikuwa na kazi ya ziada ya kumuelewesha Edmund, akamwambia kwamba tangu akiwa mdogo, wazazi wake walimpeleka kwa waganga waliomuwekea tego mwilini mwake kupitia sehemu zake za siri kwamba mwanaume yeyote atakayejaribu kufanya naye mapenzi, achukuliwe msukule au akatolewe kafara.

“Nimeshawaua wanaume wengi sana Edmund, hata wewe ilikuwa ufe kwa njia hizohizo, nimekuokoa kwa sababu kwa mara ya kwanza maishani mwangu nimetokea kukupenda Edmund,

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)

Chapisha Maoni