
Mtunzi: Aziz Hashim
SEHEMU YA TISA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
“Sasa itakuwaje na umeshasema kila mwanaume anayejaribu kufanya naye mapenzi ni lazima afe?” Edmund aliuliza huku akionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka majibu. Licha ya yote yaliyotokea, alishindwa kuuficha ukweli uliokuwa ndani ya moyo wake kwamba anampenda sana msichana huyo.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
“Jiandae kufa,” alisema mganga huyo huku akiangua kicheko cha kizee, Edmund akajiinamia chini.
“Ipo njia moja tu ya kuwasaidia wote wawili lakini ni ya hatari sana, hata mimi sipendi kumuona akiendelea kuua watu wasio na hatia, natamani nimuone akiwa na mume anayempenda, ajenge familia na hatimaye atulie lakini siyo rahisi,” alisema mganga Shiwinga, kauli iliyomfanya Edmund ainuke pale alipokuwa amejiinamia na kumsogelea mganga akitaka kujua ni mbinu gani hiyo ya kuwasaidia.
“Inabidi Samantha atolewe nguvu za giza na tego aliloingiziwa mwilini mwake tangu akiwa mtoto lakini suala hilo ni lazima yeye mwenyewe aridhie kwa sababu litakuwa na madhara makubwa kwake na kwa familia yake.
“Lakini pia baba yake hatakiwi kabisa kujua kwa sababu anaweza hata kutupiga risasi wote, Samantha ndiyo kitega uchumi chake,” alisema mzee Shiwinga na kumfanya Edmund ashushe pumzi ndefu na kujishika shavu.
Alizama kwenye dimbwi la mawazo, akawa anatafakari mambo mbalimbali yaliyotokea, akawa anajiuliza kama inawezekana msichana huyo akatolewa nguvu mbaya zilizopandikizwa ndani ya mwili wake na akawa binadamu wa kawaida.
Hofu ya kifo ilimfanya amuogope mno Samantha, akaendelea kutafakari kwa muda mrefu bila kupata majibu. Hakuna kitu kilichokuwa na maana kwake zaidi ya uhai wake kwani mpaka muda huo ilikuwa ni miujiza ya Mungu tu ndiyo iliyomfanya awe hai.
“Mbona umekuwa kimya kiasi hicho?”
“Babu sidhani kama nitaweza kuwa na amani na Samantha. Moyo wangu unamuogopa mno hata kama ni yeye ndiye aliyeniokoa,” alisema Edmund na kumfanya mganga Shiwinga aachie tabasamu.
“Siyo kazi nyepesi, moyo wako umeshaingiwa na hofu, ni binadamu anayeweza kuzitawala hisia zake pekee ndiye anayeweza kuuona upendo wa kweli alionao Samantha na kumsaidia kutoka kwenye shimo la mauti aliloishi kwa kipindi kirefu tangu akiwa mdogo.”
“Kuzitawala hisia? Ndiyo kufanya nini?”
“Namaanisha mtu anayejitambua, anayefahamu yeye ni nani na kwa nini yupo duniani ndiyo anayeweza kuishinda hofu ya kifo. Mtu akishaishinda hofu ya kifo anaweza kuzitawala hisia zake na anaweza pia kuwasaidia wengine wenye uhitaji,” alisema mganga Shiwinga na kumfanya Edmund akune kichwa kwani kimsingi hakuwa amemuelewa.
“Kwa hiyo unataka kusema inabidi nijifunze uchawi?”
“Uchawi? Sijazungumzia suala la uchawi hapa, nazungumzia elimu ya utambuzi. Haina uhusiano wowote na uchawi.”
“Lakini nimewahi kusikia kuwa waganga na wachawi peke yao ndiyo wanaoweza kuishinda hofu dhidi ya kifo.”
“Tangu uzaliwe umesikia mambo mengi sana yasiyo sahihi, ni jukumu lako kuutafuta ukweli kwani ndiyo kitu pekee kitakachokuweka huru. Hata vitabu vya dini vinazungumzia suala la kuutafuta ukweli, mimi siyo muumini lakini nayafahamu vizuri maandiko matakatifu,” alisema mganga Shiwinga huku akiendelea kumuandalia Edmund dawa.
Maelezo yake yalimfanya Edmund aanze kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. Alitamani kumuuliza maswali mengi sana mganga huyo lakini alishindwa hata aanzie wapi.
Mganga Shiwinga ni kama alielewa kilichokuwa kikipita ndani ya mawazo yake, akamwambia asiwe na wasiwasi akimaliza kumuandalia dawa atamjibu maswali yote aliyokuwa akihitaji majibu.
Kazi ya kuandaa dawa iliendelea ambapo baada ya kumaliza, mganga huyo alimnywesha Edmund huku nyingine akimpaka kwenye jeraha lake. Kutokana na ukali wa dawa hiyo, Edmund alianza kuhisi usingizi mzito, mzee huyo akamuandalia sehemu ya kupumzika ambapo muda mfupi baadaye alipitiwa na usingizi.
***
Saa chache baada ya Samantha kuondoka pamoja na baba yake na dereva wao, mganga Shiwinga alishtuka kusikia mlio wa pikipiki ikija kwa kasi nyumbani kwake, akabaki anajiuliza maswali yaliyokosa majibu kwani haikuwa kawaida kwa wagonjwa wake kwenda kwake kwa kutumia aina hiyo ya usafiri.
Akatoka nje na kusimama juu ya jiwe kubwa, akawa anatazama kule mlio ule wa pikipiki ulikokuwa unatokea. Muda mfupi baadaye, tayari pikipiki hiyo ilikuwa imeshafika, akabaki amepigwa na butwaa kumuona Samantha akishuka kwenye bodaboda na kufungua pochi yake, akatoa fedha na kumpa yule dereva wa bodaboda kisha harakaharaka akaondoka na kumuacha mganga Shiwinga akiwa bado amepigwa na butwaa.
“Samantha! Imekuwaje tena?” aliuliza mganga Shiwinga kwa mshangao, msichana huyo akatembea harakaharaka mpaka pale alipokuwa amesimama.
“Nataka kumuona Edmund, nataka kuhakikisha kama yupo salama,” alisema Samantha huku akionesha kuwa na hofu kubwa.
Ilibidi mganga Shiwinga amtulize na kumtoa wasiwasi, akamuingiza ndani ya kibanda chake na kwenda kumuonesha Edmund ambaye alikuwa amepitiwa na usingizi mzito. Samantha akashusha pumzi ndefu na kumgeukia mganga.
“Nashukuru kwa msaada wako babu, sina imani na baba najua anaweza kufanya kila kinachowezekana kumuondoa duniani Edmund, naomba usinisaliti,” alisema Samantha huku akilengwalengwa na machozi.
Mganga huyo akamhakikishia kwamba asiwe na wasiwasi, na yeye akaanza kumuuliza kilichotokea kwani hakutarajia kumuona muda huo hasa baada ya kuwa amefuatwa na baba yake akiwa na jazba kali.
“Tumeenda naye mpaka nyumbani lakini nikafanya ujanja na kuondoka bila mtu yeyote kujua. Wanajua nipo chumbani kwangu nimelala. Muda si mrefu baba atajua Edmund mahali alipo kwa sababu nimemuacha akiandaa rada zake za kichawi kwa ajili ya kuanza kazi ya kumtafuta, anataka kumuua,” alisema Samantha huku akihema kwa nguvu.
“Usiwe na wasiwasi, hakuna rada zinazoweza kunasa chochote kinachoendelea hapa nyumbani kwangu, mimi ndiyo Shiwinga mwenyewe kutoka Lyamba Lya Mfipa, niamini,” alisema mganga huyo huku akijipigapiga kifuani kwa kujiamini.
Samantha alikaa kwenye kiti cha miguu mitatu na kuanza kuzungumza na mganga huyo ambaye alimueleza kilichoendelea baada ya yeye kuondoka.
“Nataka kujua kuhusu msimamo wako, huyu kijana wa watu anaonesha kuwa na hofu kubwa juu yako na mimi sitaki kuja kuonekana nimemsaliti, nataka uniambie unafikiria nini juu yake.”
“Kama nilivyokudokeza babu, mi nampenda Edmund na nataka kujenga naye familia. Wewe ni shahidi, sijawahi kumpenda mwanaume yeyote zaidi yake, naomba unisaidie babu.”
“Mimi sina tatizo, cha msingi ni utayari wako mwenyewe kwa sababu ili uweze kuwa naye, inabidi ukubali hizo nguvu za giza ndani ya mwili wako zitolewe, jambo ambalo baba yako hawezi kulifurahia hata kidogo.”
“Babu nimeshakwambia, nimechoka kuwa mtumwa wa baba, nimechoka kuwa kaburi la wanaume, na mimi nina haki ya kupenda na kupendwa! Nampenda Edmund na nipo tayari kufanya chochote kwa ajili ya penzi lake,” alisema Samantha kwa msisitizo huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.
“Una uhakika na unachokisema?”
“Nina uhakika wa asilimia mia moja, mimi nimeshakuwa mkubwa babu, isitoshe Mungu kanijalia urembo, kwa nini niendelee kuishi maisha ambayo siyataki? Nataka kuwa mke wa Edmund,” alisema Samantha kwa sauti ya juu ambayo ilimfanya Edmund aliyekuwa amelala, kuzinduka na kuyasikia maneno hayo.
Akawa anajihisi kama yupo ndotoni kwa sababu hakutegemea kwamba Samantha anaweza kurudi kwa mganga muda huo, harakaharaka akainuka pale alipokuwa amelala.
Akajaribu kusimama lakini kutokana na dawa alizopewa na Mganga Shiwinga, Edmund alijikuta akianza kupepesuka mithili ya mlevi, akagonga vyombo vilivyokuwa pembeni na kuwashtua Samantha na Mganga Shiwinga.
Akiwa bado anapepesuka, harakaharaka Samantha aliinuka na kumkimbilia, akawahi kumdaka na kumvutia kifuani kwake.
“Samantha! Ni wewe?”
“Ni mimi Edmund, najua huwezi kuamini lakini ndiyo hivyo, nimerudi kwa ajili yako,” alisema Samantha huku akizidi kumbana Edmund kwenye kifua chake kizuri, akamtazama Edmund kwa macho yake yaliyokuwa mithili ya mtu anayesikia usingizi, Edmund akashindwa kuzizuia hisia zake na kujikuta mapigo ya moyo wake yakianza kwenda mbio.
Ni kweli alikuwa anaumwa na dawa alizopewa na mganga Shiwinga zilimlevya sana lakini kitendo cha kukumbatiwa na Samantha, kilimfanya ajihisi kama tayari ameshapona. Wakabaki kutazamana usoni huku kila mmoja akizisikiliza pumzi za mwenzake.
“Nakupenda sana Edmund, sijawahi kupenda kama ninavyokupenda wewe, tafadhali naomba nisamehe kwa yote yaliyotokea,” alisema Samantha kwa sauti ya kudeka huku akianza kulengwalengwa na machozi, Edmund hakumjibu kitu zaidi ya kumbusu kwenye paji lake la uso, kitendo kilichomfanya msichana huyo mrembo asisimke mwili mzima.
Mganga Shiwinga aliyekuwa amesimama hatua kadhaa akiwatazama, aliishiwa cha kuzungumza, kwa akili za kiutu uzima ikabidi akohoe kidogo na kutoka nje, akawaacha wawili hao bado wamegandana kama ruba.
“Niambie kama umenisame...” alisema Samantha lakini alishindwa kumalizia kauli yake, wawili hao wakajikuta wamegusanisha ndimi zao na kuanza kuelekea kwenye ulimwengu wa tofauti, kila mmoja akionesha kuwa na hisia nzito juu ya mwenzake.
Muda mfupi baadaye, walijikuta wakiwa juu ya kitanda cha kamba alichokuwa amelala Edmund muda mfupi uliopita. Usingeweza kudhani kwamba Edmund alikuwa anaumwa kwa jinsi alivyoonesha ushirikiano.
Kama isingekuwa nguvu za giza zilizokuwa ndani ya mwili wa msichana huyo, huenda wawili hao wangefika mbali zaidi na kuvuka mipaka lakini Edmund alipokumbuka kilichotokea mara ya mwisho alipojaribu kukutana kimwili na Samantha, alijikuta akiwa mpole ghafla.
“Kweli unanipenda Samantha?” aliuliza Edmund kwa sauti ya chini, msichana huyo akaitikia kwa sauti ya kunong’ona na kumueleza Edmund kwamba anajishangaa nini kilichomtokea kwa sababu hajawahi kuhisi hali hiyo hata siku moja tangu azaliwe.
“Babu Shiwinga amesema hatuwezi kuwa pamoja kutokana na nguvu zako vinginevyo nitapatwa na madhara makubwa zaidi.”
“Hata mimi nimezungumza naye na kuna mambo tumeshakubaliana. Nimechoka kuwa mtumwa Edmund, na mimi nataka nijisikie kama mwanamke niliyekamilika, nipo tayari kwa chochote,” alisema Samantha kwa sauti iliyoonesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.
“Edmund! Muda wa kunywa dawa umefika,” mganga Shiwinga alikatisha mazungumzo ya wawili hao, wote wakajivuta kichovu na kuamka huku Samantha akiendelea kuonesha waziwazi hisia nzito za kimapenzi alizokuwa nazo kwa Edmund.
“Na wewe Samantha inabidi urudi nyumbani ili baba yako asije akashtukia, inabidi ujue namna ya kula na kipofu,”
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)