Mtunzi: Nyemo Chilongani
SEHEMU YA PILI
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Utingo huyo alikuwa akifikiria ngono, ila kichwa changu kilikuwa kikifikiria utajiri tu ambao niliamini kwamba ningeweza kuupata baada ya kufika jijini Dar es Salaam.
Bado akili yangu ilikuwa ikimfikiriaMudi, alionekana kuwa mwenye furaha tele kwani alijua kwamba siku hiyo mambo yake yangekwenda vizuri kabisa.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
SASA TUENDELEE...
Nilikuwa na hofu, nilichokuwa nikikifikiria ni namna ya kumkimbia mara baada ya kufika Ifakara.
Safari iliendelea, hakukuwa na abiria aliyekuwa akizungumza kitu chochote kile, kila mmoja alikuwa kimya. Daladala iliendelea kwenda mpaka tulipokaribia Ifakara ambapo huko abiria wangeshuka na kuchukua mabasi makubwa kwa ajili ya kuvuka ya kuelekea Ruaha kisha kuvuka Mbuga ya Mikumi na hatimaye kuingia Morogoro Mjini.
Kutoka hapo kijijini Lupiro mpaka Ifakara tulitumia saa tatu njiani. Barabara haikuwa nzuri hata mara moja, ilikuwa mbaya iliyokuwa na mashimoshimo mengi. Mara baada ya kuingia Ifakara moja kwa moja nikateremka kutoka ndani ya gari huku tayari ikiwa ni saa mbili asubuhi.
Muda wote Mudi alikuwa akiniangalia kwa macho ya matamanio, alionyesha ni jinsi gani alikuwa na uchu na mimi. Sikutaka kujali sana, sikutaka kumtoroka japokuwa nilikuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Kumbuka kwamba sikuwa na fedha, nilikuwa na begi langu tu lakini nia yangu ilikuwa ileile ya kutaka kuingia ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mambo yangu na nipate fedha.
Wakati nikiwa nimekwenda pembeni na kujiinamia, akanisogelea na kuniambia niende nyumbani kwake ambapo wala hakukuwa mbali kutoka mahali hapo. Sikukataa, nilikubaliana naye na kuanza kuelekea huko. Njiani alinishika mkono kama mke wake, kwa kumwangalia, alikuwa mtu wa sifa, alitaka kuonekana kwamba alikuwa na msichana mrembo, mwenye mvuto kwani kwa umbo langu hasa nyuma, nilikuwa nimejazia sana.
“Hapa nimewaweza…” aliniambia huku akiachia tabasamu pana.
“Wakina nani?”
“Hawa watu, wanafikiri kwamba sisi wengine hatuna uwezo…” aliniambia.
“Uwezo gani?”
Hakutaka kunijibu swali hilo, akalipotezea kwa kuingiza stori nyingine kabisa, nilijua alichomaanisha ila sikutaka kujali, nilichokifanya ni kubaki kimya na kuelekea nyumbani kwake.
Baada ya muda fulani tukaingia katika nyumba moja iliyokuwa kuu-kuu, nje kulikuwa na kibaraza kilichoharibika, ukuta ulikuwa na rangi iliyopauka, mabati yake yalikuwa na kutu, kwa jinsi ilivyoonekana, ilionyesha kwamba mwenye nyumba hiyo hakuwa akiijali, inawezekana hakuwa na fedha za kuikarabati au aliiacha kwa makusudi yake.
Tukapiga hatua kwenye korido ambapo kulikuwa na wanawake wawili waliokuwa wakizongea mambo yao, walipomuona Mudi akiingia nami, niliona kabisa wakishtuka ila wakazuga kama hawakushtuka kitu chochote kile, wakaanza kuzungumza naye kwa utani mwingi.
“Naona leo umetuletea shemeji…” alisema mwanamke mmoja.
“Hahah! Ndugu yangu bwana…” alijibu huku akicheka.
“Eti ndugu yako! Undugu gani huo mpaka chumbani,” alisema mwanamke mwingine, Mudi hakutaka kuongea kitu kingine, akaongeza tabasamu na kisha kuingia naye chumbani.
Chumba chake hakikuwa kizuri sana, kilikuwa moja ya chumba kilichomilikiwa na mtu asiyekuwa na pesa kama nilivyokuwa. Kulikuwa na kitanda kidogo, godoro lililochakaa, ndani humo kulikuwa na vyombo ambavyo havikuwekwa katika mpangilio maalumu, yaani kwa kifupi hakikuwa kizuri.
“Karibu sana mrembo…” aliniambia huku akichgia tabasamu.
Kwa mara ya kwanza nikalala na Mudi, sikupenda kufanya hivyo lakini kiukweli sikuwa na jinsi. Sikuwa nikiifahamu historia yake kimapenzi, sikujua alikuwa na nani kabla yangu lakini kutokana na uhitaji niliokuwa nao, sikuwa na jinsi, kwa usiku huo alinifanya kuwa mke wake.
Asubuhi ilipofika, nilimwambia kwamba ningeondoka, japokuwa alining’ang’ania sana nibaki lakini nilikataa, nilimweleza wazi kwamba nilikuwa na safari ya kuelekea jijinii Dar es Salaam, sehemu ambayo sikuwa na ndugu hata mmoja.
“Kwa hiyo hauna ndugu?” aliniuliza.
“Ndiyo! Ila nakwenda kutafuta maisha…” nilimjibu.
Akanionea huruma, kiukweli macho yake yalionyesha jinsi gani hakutaka mimi niende huko lakini hayakunishawishi niendelee kubaki hapo Ifakara, iwe isiwe ilikuwa ni lazima niendelee na safari ya kuelekea Dar es Salaam, kama wazazi walishindwa kunizuia, basi niliamini hata huyo Mudi naye asingeweza.
“Una nauli sasa?” aliniuliza.
“Hapana! Sina nauli…”
Akaingiza mkono mfukoni mwake na kutoa kiasi cha shilingi elfu hamsini na kunipa. Sikufichi, wakati akitoa fedha ile nilimuonea huruma mno, alikuwa katika maisha ya shida, yeye mwenyewe alihitaji fedha sasa ilikuwaje anipe kiasi kikubwa cha fedha namna hiyo? Nilijisikia hukumu moyoni mwangu.
“Unanipa fedha zote hizi?” nilimuuliza kwa kushangaa.
“Usijali Zakia! Ninakupenda na ndiyo maana nimekupa kiasi hiki cha fedha, chukua tu, katafute maisha, naamini Mungu atakupigania. Ila kumbuka, kila hatua utakayopiga, kila pumzi utakayotoa, kila moyo wako utakapodunda, jua kuna mtu anaitwa Mudi, anaishi Ifakara na ananipenda sana na yupo tayari kwa lolote kwa ajili yangu,” aliniambia Mudi maneno ambayo yalinifanya nione ni jinsi gani alikuwa akinipenda.
Asubuhi ya siku hiyohiyo nikaondoka nyumbani kwake, akanisindikiza mpaka kituoni, hakutaka nilipe nauli, akamwambia utingo wa basi tulilokuwa tunataka kusafiri kwamba alikuwa mume wangu hivyo nisidaiwe nauli, hilo halikuwa tatizo kabisa.
Nikaingia na kutulia katika kiti cha dirishani, macho yangu bado yalikuwa yakimwangalia Mudi aliyekuwa nje. Kwa kumwangalia harakaharaka alionekana kuwa wa kawaida lakini ukweli ni kwamba alikuwa mtu mwenye majonzi sana, kila aliponitupia jicho dirishani, alitamani kuniambia nirudi niishi naye.
“Nitarudi na kukusaidia Mudi, hata iwe vipi, nitarudi kulipa fadhila,” nilijisemea huku basi likiwashwa na safari ya kuelekea Ruaha kisha Morogoro Mjini kuanza.
Siku hiyo nilikuwa na mawazo tele, nilikuwa njiani kuelekea Ruaha ambapo huko ningeteremka kisha kuchukua chumba na kesho yake kuendelea na safari ya kuitafuta Morogoro huku tukipita katika mbuga ya wanyama ya Mikumi.
Niliifikiria familia yetu, nilijua kwamba wazazi wangu walikuwa na mawazo tele, kitendo cha kutokuniona najua kiliibua maswali mengi juu ya mahali nilipokuwa lakini sikutaka kujali kwa kuamini kwamba wakati mwingine tunatakiwa kufanya maamuzi pasipo kuwasikiliza wazazi, kwani kama utawasikiliza, unaweza usifanikiwe hata kidogo.
Safari ya kutoka Ifakara kwenda Ruaha ilikuwa ndefu sana, njiani nililala na kulala, kila nilipoamka bado tulikuwa njiani. Nakumbuka siku hiyo tulitumia saa tano njiani, nilipofika Ruaha, sikutaka kuunganisha safari japokuwa kulikuwa na magari ya kwenda Morogoro, nikaenda kwenye nyumba ya wageni kupumzika.
Huko, hata usingizi haukunipata, nilikuwa na mwazo tele, wakati mwingine nilimfikiria Mudi, alionekana kuwa mwanaume mwenye mapenzi ya dhati ambaye hakutaka niondoke mikononi mwake lakini kutokana na kunikuta nikiwa safarini, hakuwa na budi kuniacha.
“Nikuletee nini dada?” aliniuliza dada wa mapokezi baada ya kumwambia kwamba nilihitaji chakula.
“Niletee chipsi kama zipo…” nilimwambia japokuwa sikuwa hata na hamu ya kula.
Nikaondoka na kuelekea chumbani, baada ya dakika kadhaa, dada yule akaja chumbani na kuniletea chakula hicho. Hata hamu ya kukila sikuwa nayo zaidi ya kukishikashika kisha kukiweka pembeni.
Maneno ya baba ya kunikataza kwenda Dar yakaanza kujirudia kichwani mwangu. Kwa kweli yalinigusa lakini sikuwa na jinsi, iwe isiwe ilikuwa ni lazima niondoke na kuelekea huko, na muda huo ndiyo nilikuwa njiani.
Usiku huo nikalala hapohapo na kesho asubuhi kuanza safari ya kuelekea Morogoro Mjini. Safari ilikuwa ndefu sana ila baada ya saa kadhaa tukafanikiwa kuingia Msamvu ambapo nikateremka, kabla ya kuondoka, kwanza nikaanza kuangalia kila kona.
Sikuwa nimewahi kufika mjini, kitendo cha kuona mazingira mazuri tofauti na kule kijijini nilipokulia, hakika ilinishangaza sana, nilipaona pale Morogoro Mjini kuwa sehemu nzuri sana, sikuwahi kuona maghorofa, kwa mara ya kwanza niliyaona, mambo mengi yaliyoonekana mbele yangu yalinishangaza mno.
“Dada unataka kwenda wapi?” aliniuliza mwanaume mmoja.
“Dar…” nilimjibu kwa kifupi.
“Mbona upo hapa sasa, twende, magari yale kule,” aliniambia mwanaume huyo.
“Kiasi gani?”
“Elfu kumi, unayo?”
“Ndiyo!”
“Basi twende…”
Mwanaume yule akachukua kibegi changu na kuanza kuelekea ndani ya basi moja, sikumbuki liliitwaje. Nikaingia ndani, akanipa mzigo wangu na kisha kutulia kitini. Sikuwa nikiamini kilichokuwa kikiendelea, eti Zakia mimi, leo hii nilikuwa njiani kuelekea Dar. Safari ikaanza.
Kumbuka kwamba sikuwa na ndugu yeyote ndani ya Jiji la Dar es Salaam, nilikuwa nikienda mimi kama mimi, sikujua ningefikia wapi lakini hamu yangu ilikuwa ni kufika ndani ya jiji hilo tu. Njiani, sikutaka kulala, nilikuwa macho japokuwa nilichoka sana, nilitaka kuona huko mwanzomwanzo wa jiji hilo kulionekanaje.
“Hivi Dar kuzuri?” nilijikuta nikimuuliza mwanamke niliyekuwa naye.
“Ndiyo! Kwani hujawahi kufika?”
“Hapana kwa kweli…”
“Una ndugu huko?”
“Hapana!”
“Eeeh! Sasa unakwenda kufanya nini?”
“Nakwenda kutafuta utajiri!” nilimwambia yule mama, kwa mbali akaonekana kushangaa.
“Unakwenda kutafuta utajiri?” aliuliza kwa mshtuko.
“Ndiyo!”
Hakuuficha mshangao wake, aliniangalia kwa macho yaliyoonyesha kuwa na maswali mengi mno, sikujua alijiuliza nini lakini hata kwa kuniangalia usoni, aligundua kwamba nilimaanisha nilichokuwa nikikisema kwamba nilikwenda Dar kutafuta utajiri tu.
Hakutaka kuniuliza swali jingine tena, akanyamaza na kuendelea na mambo yake huku nikipata muda zaidi wa kuangalia dirishani. Baada ya saa moja na nusu, nikahisi kwamba ndiyo nilikuwa nikiingia ndani ya jiji hilo, nyumba nzuri zilianza kuonekana, hisia zangu zikaniambia kwamba tayari tulikuwa tukiingia ndani ya jiji hilo.
“Ndiyo tumefika?” nilimuuliza baada ya ukimya mkubwa.
Japokuwa sikuwa nikipafahamu huko na wala kufika sikuwahi lakini nilikuwa na hamu kubwa ya kuliona jiji hilo. Kipindi cha nyuma nilipokuwa kijijini, kila mtu alitaka kwenda huko, hawakujali kama walikuwa na ndugu au la, walichokitaka ni kujiona wanaingia ndani ya Jiji la Dar es Salaam na kufanya biashara kwa kuamini watafanikiwa.
Baada ya dakika arobaini, basi likaanza kuingia ndani ya kituo kikubwa cha Ubungo, huko, idadi kubwa ya watu ilinishangaza, haikuwa kama Morogoro, watu walionekana kuwa wengi huku wengi wao wakionekana kuwa bize wakifanya mambo yao.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi
