BALAA (1)

Zephiline F Ezekiel
Jina: BALAA
Mtunzi: Halfani Sudy

SEHEMU YA KWANZA
KILWA KIVINJE, mwaka 1989.

Ilikuwa tarehe kumi na tano, mwezi wa nne, mwaka elfu moja mia tisa themanini na tisa. Ilikuwa usiku wa manane, usiku wenye kiza kinene, usiku ulioandamana na mvua kubwa sana, na radi iliyotoa sauti kali na za kutisha sana pamoja na miale yenye mwanga wa kuogopesha.

Usiku huo ulikuwa ni usiku muhimu sana, kwa Don Genge pamoja na kundi lake hatari sana. Usiku huo wa tarehe 15 mwezi wa 4 mwaka 1989 katika chumba cha kuhifadhia maiti, katika hospitali ya wilaya ya Kilwa, maarufu kama Kinyonga, iliyopo katika mji wa Kilwa Kivinje, mkoa wa Lindi, kulikuwa na mkutano wa siri.
Don Genge akishirikiana na madaktari mahiri wa hospitali ya Kinyonga, pamoja na manesi wenye roho nyeusi, roho mbaya kabisa, roho zisizokuwa na chembe ya huruma hata kidogo, roho zinazojari pesa na kusahau utu, walikuwa wanaendelea na kikao chao cha Siri, kilichofanyika katika chumba cha siri, kikiwahusisha watu wanaojua kutunza siri.

Katika kikao hiko cha Siri. alikuwepo Don Genge mwenyewe ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao, Dokta Zaidi Kilumba, mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dokta Sharifa Juma, daktari bingwa wa upasuaji wilayani Kilwa, Dokta Tamaa Karimu, daktari aliyekuwa ndiye mkuu wa chumba hiko cha kuhifadhia maiti, kulikuwepo pia na watu sita, walinzi wa Don Genge, walikuwa walinzi mahiri, walinzi makini, wenye kujua kupigana aina zote za mapigano.

Walinzi waliopitia vyuo mbali mbali duniani, waliojifunza aina mbali mbali za kuuwa na kufuzu kwa kiwango cha juu sana, waliopitia mateso makubwa sana katika mafunzo hayo, mateso ambayo si rahisi kuvumilika kwa binadamu wa kawaida, ndio, walipitia mateso katika mafunzo, mateso ambayo yamewafanya wawe imara sana leo hii, kutokana na mateso hayo sasa wana uwezo mkubwa sana wa kutesa, kumtesa mtu yeyote yule na kusema chochote watakachomuuliza, hata kama aliapa kiapo cha damu kutosema, vijana hao sita walikuwa wanajulikana kama SIX KILLERS, na majina yao walipewa kwa namba, kulikuwa na one, two mpaka six, namba zilizotolewa kutokana na ubora wao katika mapigano, ubora wao katika kujua mambo.

Katika kikao hiko cha siri walikuwepo pia manesi watano, manesi ambao walikuwa na umuhimu mkubwa sana katika mpango huu wa siri, manesi walioapa kuzitunza siri, kuzitunza siri vifuani mwao zikatulia tuli katika mioyo yao mibaya.

Ulikuwa mkutano muhimu sana kwao, labda ungeweza kufanyika sehemu nyingine tofauti na chumba hiki cha kuhifadhia maiti. Lakini sehemu zingine zote waliona siyo sahihi kwao, wakihofia siri zao kuwa hadharani. Waliamua kufanya kikao chao hiki katika chumba hiki, wakiamini ni sehemu salama sana, chumba ambacho kingekuwa ndio ofisi yao ya muda katika kutekeleza mambo yao hayo ya kinyama, mambo ya siri sana, yaliyohitaji sehemu ya siri na kuhusisha watu wenye kujua kutunza siri kama hawa.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
"Naamini wote tumekula kiapo hapa, kile kiapo kinaitwa kiapo cha moto, kiapo kisichofutika hata mmoja wetu atakapokufa. Kiapo kile tulichokula inamaana tutaitumikia kazi hii katika siku zote za maisha yetu, na hata tukifa. Kazi tulionayo ni nyepesi, na kwa kuwa nyinyi ni watu makini naamini itakuwa nyepesi zaidi. Kazi yetu ni kuhakikisha hakuna maiti inayoenda kuzikwa kaburini kutoka katika hospitali hii ikiwa na moyo, lazima tuhakikishe kila maiti inayotoka katika chumba hiki, cha kuhifadhia maiti haina moyo.

Kwa siku tuna mkataba wa kupeleka mioyo ya watu kumi na mbili. Najua ni idadi ndogo sana hiyo, kwa hospitali kubwa kama hii, hospitali inayohudumia wilaya nzima.
Wote tunajua maiti zote za hospitali hii zinapitia humu, na ndio maana Dr Tamaa Karimu ukajumuishwa katika mpango huu" Mwenyekiti Don Genge aliacha kuongea, alitulia ili Kuhakikisha kila neno aliloongea linapenya na kunasa vizuri katika vichwa vya watu wale. Mle ndani kulikuwa kimya, kulikuwa na utulivu mkubwa sana, baada ya kimya cha kama dakika moja Don Genge aliendelea.

"Lakini inawezekana ikatokea siku hawajafariki watu kumi na mbili, na hivyo tukashindwa kupata idadi ya mioyo tunayoihitaji, Dr Zaidi Kilumba ndio maana ukajumuishwa katika jopo hili, wewe ni mganga mkuu katika hospitali hii, lakini kazi yako hapa itakuwa ni Kuhakikisha mioyo tunayoihitaji inapatikana kila siku, na ikiwezekana izidi, kazi yako kama mganga mkuu ni Kuhakikisha watu kumi na mbili au zaidi ya kumi na mbili wanakufa kila siku katika hospitali yako, isipofikia idadi hiyo itabidi uhakikishe unawauwa wewe, hapa sitaki kukufundisha utawauwa vipi, wewe ni daktari, kwa kuwa unajua kuwatibu, bila shaka na kuuwa unajua pia" Alipofika hapo Don Genge alitulia tena. Ili maneno hayo yazame na kujikita vizuri katika bongo za watu wale.

Baada ya muda mfupi aliendelea tena.
"Najua kazi hii inahitaji kufanya upasuaji, kuzipasua maiti ili kutoa hiyo mioyo inayohitajika, Dr Sharifa Juma ndio maana upo hapa, kazi yako ni Kuhakikisha unazipasua maiti kumi na tano kila siku na kuzitoa mioyo. Najua kazi yako ni ngumu na inahitaji wasaidizi, ndio maana kuna hawa madada watano, watakusaidia kila utakapohitaji msaada." Don alitulia tena, Akafungua chupa yake ya maji na kunywa funda tatu kwa pupa, bila kujari kama alikuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti. Kuingia tu katika chumba kile kulihitaji ujasiri mkubwa, hili la kunywa maji lilihitaji uwe kichaa kidogo. Chumba cha maiti chenye harufu ya ajabu ya dawa zilizopuliziwa maiti ili zisiharibike halafu unywe maji, ama hakika zilihitaji ukichaa, ukichaa kama wa Don.

"Kanuni za kazi hii ni mbili tu, kutunza siri na ushirikiano. Kila mmoja wetu lazima atunze siri, huu ni mpango hatari kwa hiyo unahitaji usiri mkubwa mno, pia lazima tushirikiane ili kuweza kufanikisha Mpango huu, ushirikiano uwe ndio nguzo yetu kuu. Bila ushirikiano hakuna litakalofanyika. Mwisho kabisa, tutahakikisha akaunti ya kila mmoja wenu inajazwa pesa nyingi sana kila siku mtakapotukabidhi mzigo wetu. Pesa ambazo hamjawahi hata kuwaza kuwa nazo, hapo sisemi sana, mtajionea wenyewe…"

Alipofika hapo Don Genge alitulia, alitembeza macho yake taratibu kwa kila mtu mle ndani. Wote walikuwa kimya, Don Genge alivua miwani yake, akaanza kuipangusa vumbi kwa kutumia shati, ingawa haikuwa na vumbi hata kidogo. Wanajopo wote walimwangalia Don Genge, sasa ilikuwa zamu yake kuangaliwa.
"Nadhani tumeelewana" Don alisema huku akiendelea kuifuta miwani yake.
"Ndio" Wanajopo wote waliitikia. Kila mmoja kwa sauti yenye hisia tofauti. Wengine hisia za uwoga na wasiwasi, wengine hisia za majonzi, wengine hawakuwa na hisia yoyote, wao waliona wanaenda kufanya jambo la kawaida tu.

"Good, napenda sana watu majasiri kama ninyi, hii nchi imeshaoza, kila mmoja anakula kutokana na urefu wa kamba yake. Acha viongozi wafisadi kwa kupitia mikataba wanayosaini, mikataba ya kijinga kama ya chifu Mangungo. Nasi lazima tufisadi kwa nafasi yetu. Nchi haina mwenyewe hii, kila mmoja anakula anapopata nafasi ya kula" Don aliongea maneno hayo ili kuhalalisha wanachotaka kufanya. Wote mle ndani walisahau kwamba, ubaya haulipwi kwa ubaya, njia bora ya kulipa ubaya ni kumfanyia wema kwa aliyekufanyia ubaya, ili nafsi imsute, ili ajifunze.
Kikao kilifungwa saa tisa alfajiri. Kila mmoja alitoka katika kikao kile na dhamira moja tu, Kuhakikisha mioyo kumi na tano inapatikana kila siku, kwa njia yoyote ile.

Yusuph Shaweji, alikuwa ni daktari kijana sana katika kituo cha afya Kilwa Masoko. Marafiki zake walizoea kumwita Dr Yusha, wakichukua herufi ya kwanza ya jina lake, na herufi ya kwanza ya jina la baba yake.
Dr Yusha alikuwa daktari mwadilifu sana, mwadilifu kwa madaktari wenzake, mwadilifu kwa wagonjwa. Alikuwa ni daktari mwenye weledi na kazi yake. Daktari mwenye kuheshinu miiko na maadili ya kazi yake.

Usiku ule wa tarehe 15/ 4/ 1989, wakati Don Genge, madaktari pamoja na manesi wa hospitali ya wilaya ya Kilwa Kivinje, wakipanga mpango wao ule hatari, Dr Yusha alikuwa katika ukumbi wa Sillent in, katika sherehe ya ndoa yake, baada ya kufunga ndoa mchana wa siku ile. Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa Dr Yusha kutimiza ndoto ile adhimu katika maisha yake, ndoto iliyodumu katika moyo wake kwa muda mrefu sana. Kuoa ilikuwa ni ndoto yake, kumuoa Nasra, Ilikuwa ni ndoto yake kubwa sana.

Wakiwa katikati ya sherehe, katikati ya furaha, wakati Mc wa sherehe ile akitangaza kuwa ulikuwa wakati wa kulishana keki maharusi, ndipo Dr Yusha akipoisikia simu yake ikiita kwa mbali katika mfuko wa koti lake.

Katikati ya sherehe ya ndoa yake Dr Yusha aliitoa simu yake.

"Haloo Dr, mwanangu anaumwa sana, nahitaji msaada wako sana" Bila salamu sauti ilianza kuongea, Ilikuwa ni kama sauti ya kizee ama sauti ya mtu aliyechoka kutokana na madhila makubwa. Sauti ikiyotoka kwa hisia kali, ikiomba msaada.
Pamoja na kelele za muziki pale ukumbini, pamoja na kelele za watu pale ukumbini, lakini sauti ile iliyochoka ilipenya japo kwa shida katika spika ya simu ya Dr Yusha, na kutua kwa shida vilevile katika sikio lake la kushoto la Dr Yusha.

"Upo wapi?" Dr Yusha aliuliza kwa sauti kubwa kidogo.
"Hospitali Kivinje"
"Ngoja nimpigie Dr Kilumba, tuone atawasaidiaje?"
"Dr Kilumba na Dr Tamaa wote tumejaribu kuwapigia, hawapatikani kwenye simu zao kaka yangu" Ulikuwa mtihani mkubwa sana kwa Dr Yusha. Pamoja ya kuwa hospitali ya Kivinje hakikuwa kituo chake cha kazi, lakini alijiona ana dhima ya kusaidia wagonjwa popote pale. Sasa alikuwa anawaza, aendelee na sherehe ya ndoa yake au aende Kivinje kumsaidia mgonjwa.
"Nakuja baada ya nusu saa" aliijibu ile simu.

Mtihani mwengine ukafata, atatokaje katika ukumbi ule ilhali yeye ndiye bwana harusi. Upande mwengine wa shilingi maadili ya kazi na kiapo cha udaktari vilikuwa vinamsulubu kwa zamu.
Dr Yusha aliamua kwenda kumsaidia mgonjwa kwa njia yoyote ile.
Aliangaza mle ukumbini, alipigwa na butwaa, ukumbi mzima ulikuwa unamwangalia yeye. Ukumbi ukimshangaa. Dr Yusha akatulia kwa sekunde kadhaa, ndipo aliposikia, kumbe mshereshaji wa sherehe alikuwa amemwambia akakate keki iliyokuwa mbele ili akamlishe mkewe, Nasra, wakati yeye alikuwa busy na simu.

"Ndugu bwana harusi tunaomba uje ukate keki na kwenda kumlisha mkeo mpendwa " Mshereshaji alikuwa anayarudia kwa mara ya tano maneno hayo.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni