Mtunzi: 2jiachie
SEHEMU YA KWANZA
“Wewe una hoja Martha, kumbe unajua chakula kizuri...nikuambie kitu mke wangu.”
Martha alipoisoma meseji hiyo, akaguna kwanza, akamjibu”
“Mh! Nimekuwa mkea mara hii jamani?”
“Kwani umeboreka kukuita hivyo?”
JIACHIE MWENYEWE SASA…
Martha hakujibu haraka, Roi akawa na presha kubwa ya kutaka kuiona meseji iliyofuatia msichana huyo angejibu nini...
“Si vibaya ila....”
“Ila nini tena?”
“Basi tuyaache kwanza.”
“Sawa, nahitaji nikuone leo jamani,” aliandika Roi.
“Leo?”
“Ndiyo! Mbona umeshtuka hivyo mke wangu?”
“Kwa leo hapana.”
“Mpaka lini?”
“Labda siku nyingine.”
“Ndiyo nataka kuijua hiyo siku nyingine.
“Ila si nimekwambia nitakwambia jamani!”
“Basi sawa, hakuna tatizo.”
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
ENDELEA...
Katika kila hatua aliyokuwa akipiga, Roi alijiona kuwa mshindi, uzuri wa Martha ulikichanganya kichwa chake mpaka kufikia hatua ya kumuona mjinga mwanaume aliyezaa naye na kisha kuuacha mzigo mzuri kama ule ukiondoka zake...
Siku hiyo alifanya kazi harakaharaka, kitu pekee alichokuwa akikihitaji ni kutaka kuzungumza na msichana huyo tu. Alipomaliza kazi zake, akaondoka. Ilipofika usiku kama kawaida yake akachukua simu yake na kumtumia meseji.
“Jamaniiiiiii....” alianza kumchokoza...
“Nini tena kababaaaa?”
“Hata kunikumbuka!”
“Nilikuwa bize kidogo.”
“Naomba nikupigie basi niisikie sauti yako.”
“Nipo kwenye kelele, nitakushtua.”
“Sawa.”
Roi akabaki akiwa na presha kubwa, kila wakati alipokuwa akimkumbuka Martha, mwili wake ulikuwa unamsisimka kupita kawaida. Hakujua kama alikuwa amempenda mwanamke huyo au alimtamani, lakini kila wakati alihisi kuwa na hamu ya kutaka kuwasiliana naye....
Alisubiri meseji ya Martha mpaka zilipopita dakika thelathini, akasikia mlio wa meseji, kwa haraka sana huku akiwa na presha tena akikenua meno yake akaiwahi simu, akaichukua na kufungua meseji. Hakuwa Martha, alikuwa rafiki yake Sudi ambaye alimshtua kwenda kuchukua hela yake aliyokuwa akimdai....
“Mjinga kweli huyu mtu, watu tupo kwenye presha, yeye anatushtua tu, na hiyo hela abaki nayo,” alisema Roi kwa hasira na kumalizia na msonyo mkubwa. Baada ya hapo, wala hazikupita dakika nyingi, Martha huyo simuni....
“Nipigie sasa,” ilisema meseji aliyotuma Martha.
Roi hakutaka kupoteza muda, alijiona kama angechelewa vile, kwa haraka sana akaanza kumpigia Martha simu, ikapokelewa, Roi akashusha pumzi ndefu na nzito.
“Mambo,” ilisikika sauti nyororo ya Martha....
“Poa, mzima mke wangu...”
“Mi mzima sijui wewe kababaa.”
“Nipo poa. Nimekumisi sana wangu, unanibania kweli kukuona,” alisema Roi.
“Unasema kweli?”
“Ndiyo. Nimekukumbuka mno. Nataka nikuone, lini utakuwa tayari?”
“Sijajua, nina kazi zinanibana sana kwa sasa.”
“Kwa hiyo hatutaweza kuonana?”
“Nitaangalia.”
“Ushaanza.”
“Nimeanza nini tena?”
“Tangu siku ile umesema utaangalia, huko kuangalia hakuishi tu?”
“Hahaha! Sawa, nitakujibu kesho, usijali.”
“Sawa. Ila nikwambie kitu?”
“Niambie tu.”
Una sauti nzuri sana, nampa pongezi mama aliyekuzaa, hata Mungu kakupendelea sana,” alisema Roi, sauti yake ilisikika kimahaba....
“Hahaha! Nashukuru jamaniiii...”
“Upo wapi sasa hivi?”
“Nipo kitandani, nimejiachia tu.”
“Upo na nani?”
“Peke yangu, halafu kuna kibaridi, si unajua mvua zinazoendelea, natamani ningekuwa na mtu hapa,” alisema Martha maneno yaliyompagawisha Roi...
“Nielekeze nije.”
“Mmh! Hapana. Usiku sana sasa hivi!”
“Si nachukua bodaboda tu...”
“Hapana bwanaaaa, usiku ushaingia,” alisema Martha, wakati akiongea na Roi kipindi hicho, tayari mwanaume huyo alishainuka kitandani, alikuwa akivitafuta viatu vyake kwa kuona kwamba angekubaliwa kwenda...
“Sawa. Basi tutazidi kuwasiliana.”
“Hakuna tatizo kababaa...”
Roi akakata simu, alikuwa hoi bin taabani, alipojiangalia, hakujiona kama alikuwa vizuri, akainuka pale alipokuwa na kwenda bafuni kuoga. Sauti ya Martha iliutetemesha moyo wake, mwili wake ulisisimka sana...
Kila alipokuwa akizungumza naye alichanganyikiwa zaidi mpaka kufikia kipindi akawa halali vizuri kwa kumkumbuka msichana huyo...
“Yaani simuelewielewi, anaingia bandani, anatoka, anaingia, anatoka, ila poa tu, akiingia tena, nafunga banda,” alijisemea Roi huku akijiandaa kulala na kichwa chake kikiwa kimechanganyikiwa kwa mwanamke huyo.
“Yaani simuelewielewi, anaingia bandani, anatoka, anaingia, anatoka, ila poa tu, akiingia tena nafunga banda...”
“Martha...Martha...anaonekana ni mwanamke mwenye kujitambua. Inaonekana ameshaumizwa sana sasa machale yanamcheza namna ya kumkubali mtu,” alisema moyoni Roi akiwa amelala anaangalia juu...
“Da! Iko siku lakini...naweza kusema atakuwa wangu lakini kumbe ana mwingine ndiyo maana anaingia na kutoka.”
***
Kwa upande wake, Martha kule kwake alikokuwa alikuwa amelala huku akiwaza...
“Mh! Roi bwana. Anaonekana ananitaka, lakini mimi siwezi kwa kweli. Nimeshalizwa sana tu. Wanaume wa siku hizi ndivyo walivyo,” alisema moyoni Martha, akajikuta akishika simu na kumtumia meseji Roi...
“Baba!”
Roi alikuwa anaangalia muziki kupitia runinga, meseji ya Martha ikaingia, akaisoma...
“Nikwambie kitu baba?”
Roi aliachia tabasamu, akaamini kwamba anachotaka kukisema Martha ni kwamba amekubali wawe na uhusiano, akamjibu...
“Niambie baby wangu...”
“Unanipenda?”
“Sana!”
“Kweli?”
“Kweli kabisa.”
“Mimi naomba...tena naomba sana baba, tuwe kaka na dada.”
Roi alikuwa peke yake lakini aliguna kwanza, akaangalia kulia na kushoto kama aliyeamini kwamba, kuna mtu anamwona alivyong’onyea...
“Sawa,” alijibu Roi meseji kwa ufupi sana...
“Loo! Asante God...sasa naweza kuwa huru na wewe kama kaka yangu...nakupenda sana kaka, nitakuheshimu na kukuthamini. Nimetokea kukupenda sana Roi, amini hivyo.
“Kifupi mimi sina kampani yoyote ile, wewe ndiyo utakuwa kampani yangu kama kaka.”
“Usijali sista...hata mimi nakupenda sana kama dada yangu, nitakuheshimu na kukuthamini,” alijibu Roi.
Baada ya hapo, waliagana kwa ajili ya kulala...
“Bro, usiku mwema, Mungu akulinde...”
“Na wewe sista. Mungu akutangulie, ulale salama chini ya ulinzi wake.”
“Asante kaka...”
***
Kulikucha, Martha ndiye alikuwa wa kwanza kumtumia meseji Roi...
“My love bro.”
Mlio wa meseji ndiyo uliomwamsha Roi kutoka usingizini, akaisoma meseji hiyo na kuijibu...
“Yes darling sista.”
“Umeamkaje my sweethaert kaka?”
“Niko vizuri my baby sister. Wewe je?”
“Mimi pia...niko njiani bro nakwenda job. Leo tunaweza kuonana?”
“Hakuna tabu sista.”
“Oke...basi kazi njema na wewe bro wangu, nakupenda sana.”
“Nakupenda sana pia sista.”
***
Jioni walipomaliza kazi, walikwenda kukaa baa ya Ground Pub! Waliipenda pub hiyo kwa sababu ilikuwa inauza pweza na supu yake ‘mchuzi wa pweza’ na wakazi wengi wa Jiji la Dar walipenda kwenda kukaa hapo jioni.
Wakiwa hapo, Martha alimtumia meseji Roi...
“Sweetheart bro!”
Roi baada ya kuisoma meseji hiyo alianza kuweweseka akitingisha kichwa na kuachia tabasamu. Kuitwa sweetheart bro alihisi mwili kusisimka kimahaba..!
“Duu! Huyu Martha huyu...sijui! Huu ni usista kweli au kuna lingine?” alijiuliza mwenyewe, akamjibu...
“Darling sista!”
“Wapi?”
“Nipo hapa Ground Pub Sinza...wewe je?”
“Mimi ndiyo natoka. Je, tunakutana?”
“Yes! Njoo hapa, si unapajua?”
“Yes! Nikifika hapo?”
“Ukifika nipigie.”
Roi alipomaliza kuzungumza na Martha aliwaambia wenzake...
“Jamani...jamani...sikieni...”
“Vipi?” walimuuliza...
“Kuna mgeni wangu anakuja hapa, anatokea Kariakoo.”
“Ni shemeji yetu au?” aliuliza Julio...
“Acha maswali mengi wewe, mtamuona hapahapa akifika.
Lakini Roi akatumia nafasi ile kuwasimulia kisa chake na msichana huyo. Aliwasimulia ishu yote kuhusu Martha walivyokutana, walikofikia na wanakoelekea...
“Aaah! Mtu kama huyo bwana ngumu sana kumwelewa. Hapo unatakiwa kujiongeza katika kila neno lake. Pengine yeye yupo siriasi kwamba anataka wewe uwe kaka yake halafu wewe unawaza mapenzi, utamboa” alisema Julio...
“Hakuna, huyo ameshaingia laini, hapo Roi ni wewe tu,” alisema Pauli wakiwa tayari wapo kwenye moja baridi, moja moto.
Walibadilishana mawazo kuhusu Martha mpaka wakafikia hatua ya kuachana na mazungumzo hayo, wakahamia kwenye mambo mengine.
Baada ya nusu saa, simu ya Roi iliita...
“Jamani huyo, ameshafika...halooo sista...”
“Ee... nimefika hapa barabarani.”
“Ngoja nimtume mhudumu akufuate.”
“Poa.”
Roi alimpa simu yake mhudumu mmoja wa baa hiyo aende nayo barabarani...
“Ukifika pale piga namba hii, utakutana na dada mgeni wangu mmoja mlete hapa,” alisema Roi, mhudumu akaondoka na simu.
Baada ya dakika mbili, mhudumu aliongozana na Martha mpaka alipokaa Roi na marafiki zake. Kazi ikawa, Martha akae wapi sasa? Akae kwenye kiti cha jirani na kaka yake, Roi au?
“Karibu hapo,” alisema Roi akimtengea kiti Martha ili akae jirani na yeye.
Martha siku hiyo alivaa suruali ya jinzi iliyomkaa sawasawa kwa kumbana, alionekana ni mwanamke mwenye kujiamini sana. Ongea yake, tazama yake ilimfanya kila mmoja kati ya Roi mwenyewe, Pauli na Julio kujua kuwa, Martha ni mwanamke...
“Bro,” Martha alituma meseji palepale kwenda kwa Roi...
“Sema sweet sista.”
“Mimi nina majina mawili. La kwanza, Martha. La pili ni Liz. Lakini jina ambalo limezoeleka sana ni Liz. Kwa hiyo kuanzia leo nitapenda uniite Liz na achana na jina la Martha.”
Roi alipoisoma meseji hiyo aliona sawasawa tu. Atumie jina la Martha, atumie la Liz sawa, kwake majina yote yalikuwa ni mazuri...
“Poa sista, love u sana...”
“Love u too.”
Mazungumzo kati ya Roi na marafi zake yaliendelea huku Liz akiwa ametulia kimya pembeni kwenye kiti akiwasikiliza. Ilifika mahali, Roi akawaomba watulie ili atoe utambulisho...
“Jamani...jamani...” Roi alisema kwa maana ya kuomba utulivu...
“Sema kaka...”
“Huyu anaitwa Liz, ni dada yangu kipenzi,” alisema Roi huku akimshikashika begani dada yake huyo...
“Kumbe hapa Dar upo na dada yako? Sisi tulikuwa hatujui,” alisema Julio...
“Hata mimi nimeshangaa sana,” alidakia Pauli huku wote wakimkaribisha Liz tena na tena...
“Asanteni jamani, nashukuru sana.”
Baada ya utambulisho huo, mazungumzo ya wote yalikata, sasa ikawa wote wako na simu zao. Kila mmoja alituma meseji alikokujua yeye...
“Bro!” alituma Liz kwa Roi...
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi