JAMANI DADA MARTHA... LOOO! (11)

Zephiline F Ezekiel
Mtunzi: 2jiachie

SEHEMU YA KUMI NA MOJA
ILIPOISHIA...
Martha alipojitokeza, mama Anna alishtuka, akapunguza sauti huku akisema...

“Basi tufanye kesho baby wangu, usiku mwema.”

Martha alipita bila kusema kitu kwa mama Anna, akazama ndani na kumpa Roi vocha ya buku,

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
akabaki na ya buku kuingiza kwenye simu yake.

***

Ilikuwa saa saba usiku, Martha alichelewa kupata usingizi kwa mawazo kuhusu kutaka uhakika wa kuwepo kwa mawasiliano kati ya mama Anna na jamaa yake, Roi...

“Hivi kama ni kweli nichukue hatua gani?” alijiuliza moyoni Martha...

“Na yale mazungumzo ya kwenye simu ya mama Anna muda ule mbona ni kama alikuwa akiwasiliana na Roi?”

Ghafla alipata wazo, alitoka kitandani huku macho yake yakitua kwa Roi. Alipobaini anauchapa usingizi mzito, aliifuata simu yake, akaichukua na kwenda nayo sebuleni.

Aliikuta simu hiyo haina ‘password’ kwa hiyo akaingia ndani moja kwa moja kwenye kiboksi cha meseji...

“Baby, unajua wakati tunaongea ghafla akatokea demu wako, ndiyo maana nikakuaga.”

Meseji hiyo ilitoka kwa mama Anna kwenda kwa Roi. Martha aliishiwa nguvu, nusura aanguke. Akaendelea kusoma nyingine...

“Basi usiku mwema baby. Nimekumisije jamani!”

Roi naye akajibu...

“Mimi je? Natamani kesho ifike haraka tukutane unikate kiu yangu. Lala salama mpenzi wangu nikupendaye.”

Martha alisimama, akamwomba Mungu kwanza kisha akajipa moyo na ujasiri wa hali ya juu. Akatuma meseji kwa mama Anna...

“Baby...”

Ingawa ilikuwa usiku sana, Martha akaamini atajibiwa, lakini hakujibiwa, akatuma nyingine...

“Jamani baby, naomba nije kwako basi, nimekumisi kweli mwenzio.”

Dakika zilikatika, hakupata jibu. Akazifuta meseji zake hizo mbili na kuamua kurudi chumbani kulala. Alitamani sana kumwamsha Roi ili ambane kuhusu meseji hizo lakini akajivumilia. Aliirudisha simu mahali alipoichukua na kulala.

***

Kulikucha, Martha aliamka na kuanza kufanya kazi za ndani lakini siku hiyo hakumwamsha Roi mpaka alipoamka mwenyewe.

Roi, kabla hajatoka kitandani, aliichukua simu na kuangalia meseji, akakutana na meseji ya mama Anna ikiomba radhi...

“Baby samahani, ulipotuma meseji usiku nilikuwa nimelala fofofo mwenzako. Halafu uliposema umenimisi unataka kuja ulikuwa unamaanisha au utani tu? Bibiye ungemwachaje kitandani peke yake?”

Roi alishtuka sana. Akaangalia kama alituma meseji amesahau, hakuona meseji yoyote. Akahisi huenda meseji hiyo ya mama Anna ilimfikia yeye kwa bahati mbaya tu, akamuuliza…

“Sweet, meseji hii ya nani?”

Akajibiwa…

“Ya nani kwani darling. We unadhani inaweza kuwa ya nani zaidi yako jamani? Au unanituhumu kwamba nina mchepuko?”

“Mh!” Roi aliguna kwanza. Akakaa kitandani na kufikicha macho. Bado aliamini mama Anna anajitetea tu…

“Mimi nilikutumia meseji wewe ya kukutaka nije kwako?”

“Ndiyo. Kwani si imekuja kwa namba yako baby! Acha hizo bwana.”

Roi alitoka kitandani, akasimama na kujishika kichwa. Mapigo ya moyo yakamwenda kwa kasi ya ajabu.

Aliizima simu, akaenda kuoga. Aliporudi alivaa kisha akamuaga Martha kwamba anaondoka…

“Baadaye baby.”

“Poa sweetheart,” Martha alimjibu kama hakuna lolote jambo ambalo lilizidi kumchanganya Roi.

Hatua kumi hazikufika baada ya kutoka na gari, Roi alimtumia meseji mama Anna akimtaka akae sehemu nzuri anataka kumpigia simu…

“Piga tu baby, niko chumbani bado nimelala. Kwani we umeshatoka kwenda kazini?”

Roi hakujibu meseji ya kuulizwa kama ameshatoka kwenda kazini. Alichofanya yeye alimvutia uzi moja kwa moja…

“Yes baby, niambie,” alipokea mama Anna kwa sauti iliyojaa kudeka kimahaba…

“Hivi ulichosema ni kweli au utani?” aliuliza Roi…

“Kwamba?”

“Kwamba nilikutumia meseji ya kutaka nije kwako?”

“Khaa! Jamani! Sasa …kwanza nikuulize baby, kwani jana ulilewa?”

“Sikulewa. Hata wewe unajua sikulewa.”

“Sasa kwa nini usijue kama ulinitumia meseji mimi mke wako?”

“Sijatuma meseji ya hivyo kwako. Imeingia saa ngapi?”

“Mh! Hujatuma? Ilikuwa usiku kama saa saba hivi.”

“Kweli?”

“Kweli baby.”

“Meseji ngapi?”

“Mbili.”

“Zilisemaje?”

“Ya kwanza uliita baby…ya pili ukasema jamani baby, naomba nije kwako basi, nimekumisi kweli mwenzio.”

Roi alikosa nguvu, kidogo aiingize gari kwenye mtaro. Ni Mungu tu alimsaidia…

“Mimi siamini mpaka nizione hizo meseji kama kweli zimetoka kwenye namba yangu ya simu.”

“Ina maana huamini?”

“Siamini.”

“Nije ofisini kwako muda huu?”

“Itakuwa vizuri aisee. Njoo,” alisema Roi.

Roi alimwelekeza mama Anna ofisini kwake akimsisitizia kwamba aende na Bajaj, yeye atalipa.

***

Mama Anna naye alianza kuingiwa na wasiwasi. Alijua kama Roi hakutuma meseji zile basi aliyetuma ni Martha. Alitungua taulo, akavaa, akatoka kwenda uani kwa sababu mbili. Kwanza akamwone Martha anafananaje! Sura yake inasema kwamba kuna donge moyoni au kawaida. Pia, akaoge tayari kwa kwenda mjini kazini kwa Roi.

Hakumwona Martha zaidi ya wale wapangaji wenzake wawili…

“Jamani kimenuka,” alisema Martha.

“Ki nini?”

“Martha alichukua simu ya jamaa yake usiku akanitumia meseji mimi.”

Wale walishtuka sana…

“Kwa hiyo wewe ukajibu nini?”

“Sikujibu, nilikuwa nimelala.”

“Loo! Sasa?”

“Hata sijui, naoga nakwenda kazini kwake muda huuhuu.”

Mama Anna mpaka anaondoka, hakuonana na Martha. Alifuata maelekezo mpaka akafika ofisini kwa Roi.

Kitu cha kwanza, Roi aliomba simu ya mama Anna na kuangalia meseji. Kweli zilitoka kwenye simu yake…

“Daa! Hatari. Hizi alituma Martha kweli. Na kama alituma yeye ina maana kwamba aliziona meseji zote za awali ambazo mimi nilikutumia,” alisema Roi akiwa tayari na macho mekundu.

“Sasa itakuaje?” alihoji mama Anna…

“Hamna jinsi.”

“Jinsi ipo.”

“Ipi?”

“Akikuuliza mwambie mimi ni dada yako.”

“Ah! Kwa zile meseji halafu niseme wewe ni dada yangu, inakuja kweli?”

“Inakuja. Huna utetezi mwingine kwa siku ya leo. Lakini pia si ulisema unataka kumwacha Martha uwe na mimi tu, yameishia wapi mpaka unakuwa mwoga?” aliuliza mama Anna kwa sauti iliyojaa ujasiri wa hali ya juu.

“Ni kweli, lakini si katika mtindo wa kukuta meseji zako kwenye simu yangu. Nilitaka iwe amani tu.”

“Ameshakuta sasa, itakuaje?”

“Hata sijui.”

“Ndiyo ujue sasa. Mimi nakushauri jambo moja mpenzi wangu.”

“Lipi hilo baby?”

“Mimi na Martha wajina wangu, nani unampenda zaidi?”

“Martha wewe.”

“Basi mtumie meseji kwamba umeamua kuwa na mimi, hivyo jioni utakwenda kuchukua nguo zako tu.”

“Mh! Atakuibulia ugomvi wewe.”

“Mimi nipo tayari.”

Wakati wakizungumza hayo, mara Martha akaingia…

“Anhaaa! Mungu kweli mkubwa. Leo nimeamini. Kumbe hii ndiyo biashara yenu siyo?” aliuliza Martha kwa sauti yenye kujiamini...

“Hebu kaa kwanza hapo,” alisema Roi huku akitetemeka. Mama Anna alitetemeka lakini si sana.

Martha alivuta kiti, akakaa na kusema...

“Unasemaje wewe mwanaume mwenye majina mengi. Maana nimesikia una majina kama matatu hivi wewe peke yako. Kila mtu mtaani anakufahamu kwa jina lake.”

Roi alishtuka kusikia hivyo. Kwani ni kweli mtaani ana majina mengi...

“Mh!” aliguna Roi huku akimtumbulia macho ya aibu Martha. Lakini hakujibu hoja ya kuwa na majina mengi.

“Sikia nikwambie baby wangu Martha. Huyu si mpenzi wangu, ni sista‘angu ila sijawahi kukwambia,” alianza kusema Roi...

“Mimi dada yako mimi?” mama Anna alikuja juu kumuuliza Roi...

“Aaa! Jamani dada Martha...looo! yaani unanikataa kaka yako hivihivi naona jamani?”

“We wajina...sikia, mimi si dada yake wala yeye si kaka yangu. Mipango yetu ni kufunga ndoa. Huyu si wa kumtegemea wewe kwani mapenzi yake ameyahamishia kwangu...we ulie tu,” alisema mama Anna kwa macho yaliyokosa aibu.

Martha alidondoka palepale, akapoteza fahamu, hali ikawa tete. Roi huku akiogopa, alimtupia lawama mama Anna...

“Unaona sasa? Kwani kulikuwa na ulazima gani wa kumwambia wewe. Si ningemwambia mimi mwenyewe...

“Na haikuwa lazima kumwambia sasa hivi, hata nyumbani ningemwambia...”

“Baby, mimi tatizo langu sipendi kukatishakatisha. Niko moja kwa moja sana. Nisamehe kwa hilo. Ndiyo maana nilikuuliza awali unampenda nani. Mtu akifiwa hakuna haja ya kufichaficha, ni kumwambia tu ili kama kulia alie,” alisema mama Anna.

Roi na mama Anna walimzoa Martha na kumkimbiza hospitali ambako alilazwa. Mama Anna aliwapa taarifa wale wapangaji wengine kuhusu kuugua ghafla kwa mwenzao huyo.

***

Ilikuwa saa kumi na mbili jioni, Martha alikuwa kwake baada ya kutoka hospitali. Wapangaji wenzake waliingia kumpa pole kasoro mama Anna tu ambaye muda huo alikuwa nyumbani kwa Roi...

“Pole mwaya! Yaani tuliposikia umelazwa tukashangaa sana. Da! Sasa tatizo lilikuwa wapi Martha?” mpangaji mmoja alimuuliza...

“Jamani ni hadithi ndefu sana. lakini kifupi nilikuwa sijui kama jamaa yangu anatoka na mama Anna. Nilihisi wakati f’lani nikafuatilia, jana usiku nikanasa meseji zao za mahaba.

“Leo asubuhi nikasema niende kazini kwake kufika namkuta mama Anna ndani. Yeye jamaa yangu akasema mama ni dada yake, japo nilijua ni uongo, lakini mama Anna mwenyewe akanipasulia kwamba wao si ndugu bali ni wachumba na wanatarajia kufunga ndoa hivi karibuni,” alitiririka Martha...

***

Kule nyumbani kwa Roi, mama Anna alimtaka Roi amruhusu awaite wale wapangaji wenzake wawili ili awatambulishe rasmi kwake...

“Aaaa...eeee...oke, waite basi,” alisema Roi ambapo awali alianza kwa kutaka kukataa.

“Mbona baby kama unasita? Au mipango yetu imekufa nini?” aliuliza mama Anna...

“Aaa! Noo...iko palepale. Basi waite.”

Mama Anna alimpigia simu mmoja wa wapangaji wenzake, akampa maelekezo ya namna ya kufika hapo.

Wakati wanaondoka, wakamuaga Martha...

“Basi twendeni wote na mimi nataka kupeleka nguo za Roi.”

Wale ilibidi wamjulishe mama Anna kwanza ambapo naye alikubali bila kumuuliza Roi...

“Aje tu, hakikisheni amebeba hizo nguo za Roi ili asije kupata kisingizio kingine baadaye,” alisema mama Anna.

Wakati anazungumza hivyo, Roi ndiyo akasikia na kuhoji ni nini, mama Anna akamwambia, Roi akatingisha kichwa tu kukubaliana naye.

Kutoka moyoni mwake, Martha alishakubaliana na hali iliyotokea, akajilaumu sana kwa uamuzi wake wa kung’ang’ania yeye na Roi wasiwe kaka na dada na badala yake wawe wapenzi...

“Ningeusikiliza moyo siku zile haya maumivu yalikuwa yanakwepeka,” alisema moyoni wakiwa wanakaribia nyumbani kwa Roi yeye akiwa kiongozi maana alishafika.

Waliingia ndani watatu, wale wapangaji wawili na Martha.

Mama Anna aliwakaribisha kwa mbwembwe akijifanya mama mwenye nyumba huku Roi akionekana kukosa amani...

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni