JAMANI DADA MARTHA... LOOO! (12)

Zephiline F Ezekiel
Mtunzi: 2jiachie

SEHEMU YA KUMI NA MBILI
ILIPOISHIA...
Waliingia ndani watatu, wale wapangaji wawili na Martha.

Mama Anna aliwakaribisha kwa mbwembwe akijifanya mama mwenye nyumba huku Roi akionekana kukosa amani...

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Karibuni jamani...karibuni sana,” alikaribisha mama Anna kwa sauti ya ‘mimi ndiye mmiliki halali wa mwanaume huyu’, yaani Roi sasa.

“Tunashukuru sana,” waliitikia wale wapangaji wawili kasoro Martha ambaye yeye alifikia kuweka begi chini kisha akamwambia Roi...

“Ungeangalia kama nguo zako zote zipo maana nimehakikisha siachi nguo yako hata moja.”

“Naamini zote zipo bila hata ya kuhakikisha,” alisema Roi kwa sauti iliyojaa dharau, mkono mmoja ulipita kiunoni kwa mama Anna huku mkono mwingine ukishughulika na rimoti ya televisheni.

Bila kukaa, Martha akageuza kutoka lakini kabla hajafika mlangoni, ikasikika hodi...

“Hodi,” hodi hiyo ilipigwa huku aliyepiga akisukuma mlango kuingia sebuleni.

Roi alishtuka sana, akatumbua macho huku akisimama na kusema...

Mama Neema...mbona umekuja bila taarifa mke wangu? Umeona sasa umenikuta katika mazingira tata. Lakini kifupi hapa hakuna mwanamke wangu mama Neema.”

Kauli ya Roi ilimshtua sana mama Anna, Martha mwenyewe na wale wapangaji wawili…

“Ha! Mpenzi wangu, kumbe wewe una mke?” aliuliza mama Anna kwa sauti yenye mshtuko…

“Wewe. Mimi ni mpenzi wako tangu lini? Acha uzushi? Eti Martha, huyu mama Anna ni mpenzi wangu?” Roi aliomba huruma ya Martha ili kuokoa ndoa yake.

Mama Neema ni mke wa Roi. Alikwenda masomoni Uingereza kwa mwaka mmoja na muda huo ndiyo alikuwa amerudi rasmi. Neema alipelekwa kusoma kwa babu yake.

“Mi mwenyewe nimeshangaa. Kwani we mama Anna, Roi ni mpenzi wako?” aliuliza Martha huku akianza kujisikia furaha kwa anguko la mwanamke huyo aliyempindua yeye.

Mama Neema alifika kukaa kwenye kochi kubwa huku akimshangaa mume wake na ugeni ule. Alitaka kujua…

“Baba Neema hawa wote ni akina nani na wamefuata nini hapa nyumbani?”

“Mama Neema wewe ndiyo kwanza umefika. Ungetulia kwanza basi. Umekuja na begi hilo moja tu?”

“Nina mizigo mingi ipo kwenye gari nje,” alijibu mama Neema kwa sauti iliyojaa hasira.

Roi alisimama na kutoka nje. Alishusha shehena ya mizigo huku moyo ukiwa kasi. Alijua kimenuka…

“Eti nyie ni akina nani?” mama Neema aliwauliza kwa mpigo huku akimwangalia mmoja mmoja.

“Mimi naitwa Martha. Ni rafiki wa Roi,” alisema Martha huku akiogopa. Mama Neema akamwangalia mama Anna kama anayesema ‘na wewe?’

“Mimi naitwa mama Anna. Roi nii…niii…mimi sikujua kama Roi ana mke.”

“Nimekuuliza wewe nani, siyo Roi ana mke au hana,” alikuja juu mama Neema huku akionekana kutaka kusimama kumfuata mama Anna…

“Mimi pia ni rafiki yake wa karibu tu,” alijibu haraka mama Anna.

Wale wapangaji wengine walijitambulisha kwa haraka huku wakisimama kutaka kuondoka. Mizigo iliingia ndani, Roi alisaidiwa na vijana wa mtaani.

Mama Neema aliwazuia wote kutoka mpaka Roi arudi na kuzungumza naye kuhusu wao. Walikaa kinyonge.

Baada ya utulivu, Roi alirejea na kukaa…

“Baba Neema naomba utambulisho wa hawa watu wote humu ndani,” alisema mama Neema kwa sauti yenye hasira…

“Wote ni marafiki zangu. Wametoka kumoja na wataondoka pamoja.”

“Kwa nini huyu alikaa jirani na wewe kiasi kile?”

“Nani, huyu? Huyu aliamua tu.”

“Lakini mwenyewe si alisema we ni mpenzi wake?” alihoji mama Neema.

Roi alitulia akiashiria hana cha kujibu…

“Nyie malaya, nawaomba muondoke sasa hivi la sivyo nitampiga mtu risasi,” alisema mama Neema.

Akina Martha walitoka mbio, mlangoni waliminyana kila mmoja akitaka kuwa wa kwanza kutoka nje.

Wakiwa nje ya geti kuu, mama Anna alimuomba msamaha Martha…

“Martha ndugu yangu. Mi naomba nisamehe sana. Ni kweli nilikuingilia kwenye penzi lako. Sikujua kama Roi yuko vile. Nisamehe sana ndugu yangu. Nimejifunza kwamba, kila binadamu na riziki yake. Roi alikuwa riziki yako. Mimi nikaingilia kati,” alisema mama Anna huku akimwangalia Martha…

“Mh! Yaani wewe unamwomba samahani mwenzako kwa sababu kule kumeharibika siyo? Kwa nini usingemwomba sahamani jana au juzi?” mmoja wa wale wapangaji aliingilia kati…

“Eti!” mwenzake alidakia.

Walimnanga mama Anna kama si wao waliokuwa wakimuunga mkono na kumficha Martha kwamba wanajua.

“Sikiliza mama Anna. Kwanza sipokei msamaha wako. Pili, uache unafiki wako. Kilichokufanya uniombe msamaha ni baada ya kujua Roi kumbe ana mke. Usingejua je? Yaani we mwanamke mimi nimekushangaa sana. Umekuwa ukinila hivihivi najiona,” alisema kwa ukali Martha…

“Siyo hivyo Martha. Jamani msinielewe vibaya. Mambo mengine yanafanyika ili mtu ujifunze. Naamini hata kilichotokea nyumbani kwa Roi kimekuwa cha makusudi ili mimi nijifunze. Please nisamehe sana Martha,” alisema mama Anna kwa sauti ya unyonge huku akimtangulia mbele na kuonesha ishara ya kutaka kupiga magoti huku akifunga mikono…

“Oke, sawa. Sasa niambie ukweli…”

“Niko tayari Martha,” alisema mama Anna…

“Wewe na Roi mmeanzia wapi na lini mpaka mkawa wapenzi?”

Japokuwa mama Anna alikuwa tayari kujibu maswali kama alivyosema mwenyewe, lakini swali hilo lilikuwa gumu sana kwake. Ikabidi adanganye…

“Sikia Martha. Mimi na Roi tunajuana zamani sana. Tena sana. Kwa hiyo alipokuja kwako ikawa kama tunakumbushia tu,” alisema mama Anna…

“Muongo huyu Martha. Alichukua namba za simu palepale nyumbani. Siku ile wakati shemeji anatoka kuoga ndiyo akachukua, wakaanza mawasiliano. Na alisema nia yake mpaka akupindue,” alisema mmoja wa wale wapangaji.

“Sawa jamani. Martha ni kweli walichosema hawa. Mimi nilijua nikikwambia hivyo utazidi kuumia wakati mtu mwenyewe haunaye tena. Nisamehe sana.”

Martha aliamua kumsamehe mama Anna huku akimwonya kutorudia tabia hiyo kwa watu wengine kwani si njema…

“Yaani kama utakuja kumfanyia hivi mtu mwingine yeyote yule, ujue maisha yako yatakuwa mabaya sana mama Anna. Nakwambia mimi,” alisema Martha.

Wale wapangaji wengine pia wakamzodoa mama Anna na kumwambia ana tabia mbaya. Hata wao wamejifunza kuwa naye mbali. Hata hivyo, mama Anna aliahidi kubadilika kanzia siku hiyo.

MWISHO

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni