NYUMBA ILIYOJAA DHAMBI (6)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA SITA
ILIPOISHIA...
Nilimwambia kuhusu kile kilichotokea usiku wa siku ile, watu wale walitumwa kwa sababu walikosa walichokuwa wakikifuata kwa baba yake ila sikumwambia ni kitu gani, nikaongezea kuwa kulikuwa na walinzi wenzangu ambao waliuawa na bila shaka watu wale ndiyo waliokuwa wamewaua kwa sababu niliwasikia wakiongea kuhusu hilo.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Ilikuwa ni stori fupi lakini iliyomsisimua mno. Akanisogelea na kunibusu shavuni, yaani hilo busu likanipa nguvu ya ajabu kupita kawaida. Kuanzia siku hiyo akaanza kuja hospitalini hapo kuniona akiwa na ndugu zake wengine ambao walinionyeshea thamani kwa kuwa niliyaokoa maisha ya baba yao.

Kichwa changu kilikuwa kikifikiria kuhusu ile almasi iliyokuwa chumbani kwangu, nilitamani sana niiuze, nipate mamilioni na kuendelea na maisha yangu. Nilikaa hospitalini hapo kwa wiki moja huku Nurat na mama yake wakigharamia matibabu, na nilipopata nafuu, nikaruhusiwa kuondoka.

Nilipofika nyumbani kwangu, sikutaka kukaa humo, nilipekua nilipoificha almasi ile, nikaichukua na kuondoka zangu. Kumbuka sikuwa na pesa lakini ilikuwa ni bora kukaa mitaani, niteseke nikitafuta duka la almasi kuliko kubaki mule chumbani kwani niliamini kwamba vijana wale wangefika na kuniua kama walivyokuwa wakipanga.

Maisha yakawa mtaani. Sikumwambia Nurat kuhusu maisha hayo, nilijua kwamba angenitafutia chumba kitu ambacho sikutaka kabisa kuona kikitokea.

Niliamua kufanya hivyo makusudi kabisa, unajua watu wa mitaani hawafuatiliwi kwa kuwa wanaaminika kwamba hawana pesa wala kitu chochote kile cha thamani na ndiyo maana na mimi nikajifanya kuwa mtu wa huko.

Nusrat alipotaka kuonana nami, nilitafuta sehemu ya kawaida na kuonana naye huku nikimwambia kwamba kulikuwa na kazi nafanya ambayo iliyaendesha maisha yangu.

“Pole sana! Ila nitakusaidia,” aliniambia kwa sauti ya chini.

“Nitashukuru mno. Naweza kuuliza swali?” nilimuuliza.

“Uliza tu!”

“Nina lengo la kwenda Shinyanga kuchimba dhahabu ila tatizo ni moja tu, kama nikipata dhahabu huko nitakwenda kuiuza wapi?” nilimuuliza makusudi, nilihitaji kujua kuhusu hilo.

“Kule huwa kuna makampuni, hutakiwi kutoka nayo!”

“Najua! Tufanye nimefanya magumashi, nikafanikiwa kutoka nayo, niende wapi?’ nilimuuliza.

“Kwenye maduka ya kuuza dhahabu na almasi!”

“Sonara?”

“Hahaha! Hebu acha hizo. Nenda hata Posta, kuna duka moja pale linanunua vitu hivyo, ukipata niambie nikupeleke,” aliniambia Nurat.

Nilikuwa makini kumsikiliza, aliniambia mambo mengi pasipo kugundua kwamba nilikuwa na almasi ndani. Tuliongea mambo mengi siku hiyo na akaamua kuondoka zake huku akiniachia kiasi cha shilingi elfu hamsini kwa ajili ya matumizi yangu.

Mpaka siku hiyo sikuwa nimemwambia lolote lile, nilihofu moyoni mwangu, nilimwangalia jinsi alivyokuwa, mtoto wa Kiarabu, mzuri, mwenye shepu bomba, halafu nikajiangalia na kapuku mimi, nilivyokuwa kituko, yaani niligundua kabisa nisingeweza kufanikiwa kuwa na mtoto mzuri kama yeye.

Siku iliyofuata tu nikaondoka na kuelekea huko Posta kulitafuta duka hilo. Almasi hiyo nilikuwa nayo, nilivalia suruali yangu ya jinsi, kwa ndani nilifunga kamba fulani ambayo niliiunganisha kwenye kitambaa cha peke yake na kuiweka ile almasi.

Sikutakiwa kumwamini mtu yeyote yule, na hata nilivyokuwa nikitembea, sikuwa nikijiamini hata kidogo. Nilifanikiwa kufika kwenye hilo duka, nikaingia ndani, nikamkuta mzee wa Kihindi na vijana wawili, nikawasalimia na kuomba kuuliza.

“Kuna nini?” aliniuliza yule mzee.

“Nataka niuze mali yangu!” nilimwambia.

“Mali gani?” aliniuliza.

Sikumjibu, nilibaki nikimwangalia. Wote watatu walinikodolea macho, mzee huyo alijua kwamba najishtukia, akanichukua na kunipeleka ndani ya chumba kimoja, tukakaa na kuanza kuzungumza.

Nilimwambia ukweli kuhusu ile almasi, akahitaji nimuonyeshee, nikafanya hivyo, alishtuka, hakuamini kama ningekuwa na almasi kubwa kiasi hicho.

“Umeipata wapi?”

“Nimeitoa mgodini. Mimi ni mchimbaji, zali tu limeniangukia,” nilimwambia.

“Hii ni kubwa sana. Nikupe kiasi gani?” aliniuliza, najua alihitaji kujua uwezo wangu wa kugundua kuhusu madini.

“Wewe una kiasi gani?”

“Milioni mia tano?” aliniambia, nikashtuka lakini nilijua yeye ni mfanyabiashara, kiasi hicho kilikuwa kikubwa kwangu lakini kwake, kulingana na mzigo, kilikuwa kiasi kidogo mno.

“Duuh!” nilitoa mguno.

“Niambie hata sasa hivi nakupa!”

“Yaani nikuuzie kwa milioni mia tano! Mzigo huu? Mzee unazingua,” nilimwambia, sikutaka kubaki hapo, nikairudisha na kusimama kutaka kuondoka.

“Sasa mbona unaondoka? Usifanye hivyo, rudi tuongee,” aliniambia huku akinishika mkono, alijua tu kwamba nilitaka kwenda kwenye duka jingine.

“Mzee unazingua, halafu unaniona mimi wa kuja, bora niende kwenye duka la mzee Sunil atanipa kiasi kinachostahili,” nilimwambia, hilo jina lenyewe nililitunga hapohapo.

“Hakuna! Hii biashara! Basi niambie nikupe kiasi gani.”

“Hapana nahitaji 1.2 B,” nilimwambia.

“Bilioni 1.2?” aliniuliza kwa kushtuka.

“Mzee! Nakuuzia almasi kubwa, sikuuzii dhahabu. Ndiyo maana nilisema kama hutaki acha niondoke nikale bilioni mbili,” nilimwambia kwa kujiamini.

Mpaka hapo niliweza kumdanganya kwa muonekano wangu, sikwenda kimama, nilikwenda kama mtu ambaye nilijua sana madini. Mzee akaniambia ukweli tu kwamba kwa ile almasi niliyokuwanayo, gharama yake ilikuwa ni shilingi bilioni 1.5 ila kama ningependa nimuuzie hiyo bilioni moja ili akiiuza apate faida ya milioni mia tano.

“Yaani upate nusu yangu? Hapana! Weka bilioni moja pointi mbili, kama hutaki naondoka,” nilisema huku nikiinuka na kuufungua mlango.

“Subiri kwanza!” aliniambia.

Ilikuwa ni kama utani lakinid ndiyo tukawa tunazungumzia pesa nyingi. Akaingia kwenye chumba fulani na aliporudi alikuja na chombo fulani cha kuangalia kama ile ilikuwa almasi kweli ama la. Akaipima, mzigo ulikuwa wenyewe. Akatoa tabasamu pana, nikajua tu kuwa aligundua ina thamani sana, ila kwa kuwa na mimi sikujua kitu, nikaona poa tu, hata nikipigwa, kwani nilinunua?

Akakubaliana nami na kunichukua kuelekea benki kufungua akaunti na kuniingizia kiasi hicho cha pesa. Zilikuwa pesa nyingi mno, nilichanganyikiwa, sikuamini kama mimi, Edward nilikuwa na pesa hizo kwenye akaunti yangu.

Nilichokumbuka ni watoto wazuri, si walinikataa, wakajiona wao ndiyo wao, si waliniambia mimi kapuku, sina pesa, halafu yule Issa si alitembea na demu wangu, halafu hakukumbuka kama ana wadogo zake, na huyohuyo Issa naye ana demu wake aliyetaka kumuoa, sasa nitaanza nao hao kwanza, halafu ndiyo nitadili na wengine, kuhusu huyo demu wake, hata kama amemuoa, nitatembea na mkewe kulipa kisasi, pesa ndiyo itaongea lugha tamu ya kumshawishi.

Nilikuwa bilionea, tena mkubwa, ilikuwa ni vigumu kuamini kama nilikuwa na kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia mbili kwenye akaunti yangu. Sikuamini kama ni mimi kweli ndiye nilikuwa na kiasi hicho cha pesa.

Niliondoka Posta huku nikiwa makini kuliko siku zote katika maisha yangu. Nilihisi kama ningegongwa na gari na hivyo kupoteza kiasi changu chote hicho kilichokuwa benki.

Nilitembea kwa tahadhari sana na si hivyo tu, yaani siku hiyo hata daladala sikupanda kwa kuhisi kwamba ingeweza kupata ajali, abiria wote wakafa nikiwemo mimi.

Yaani niliogopa kufanya mambo mengi, nilikuwa natembea tu kurudi mtaani lakini sikutaka kupita barabarani kwani bado mawazo ya ajaliajali yalikuwa yakinijia kichwani mwangu.

Nilikuwa bilionea lakini nilivyokuwa nikitembea nilionekana kama sina pesa. Kichwani mwangu kulikuwa na picha za wanawake wengi wazuri, niliwakumbuka marafiki zangu walipokuwa wakiniambia kuhusu mademu wakali waliokuwa wakipatikana katika klabu za usiku, achana na hao, niliwakumbuka wale mademu wakali waliokuwa wakionekana kwenye video nyingi za hapa Bongo, yaani kwa akili yangu, nilitaka nilale na wote hao.

Niliondoka mpaka mtaani, nikatulia kwanza na kuanza kuyafikiria maisha yangu, sikuamini kama kweli nilifanikiwa kuwa na kiasi hicho cha pesa. Nilitaka nikachukue kidogo kwa ajili ya kwenda kutumia.

Nilikuwa na kadi yangu ya ATM, kutokana na ushindani mkubwa wa kibenki, kipindi hicho ulipokuwa unajisajili tu na kupata akaunti yako ulikuwa ukipewa kadi yako hapohapo na si kama zamani ambapo ulitakiwa kusubiri kwa wiki nzima.

Nilikwenda mpaka kwenye mashine ya ATM iliyokuwa Sinza. Niliwaona watu wakiwa wamepanga mstari wakiingia kwa zamu kuchukua pesa. Nilitamani nisimame na kuniambia wanipishe kwani mimi nilikuwa na pesa zaidi yao wote, hata ukizichanganya wasingeweza kunifikia.

“Jamani! Mpaka pesa ziishe humo!” nilisema kwa hasira mpaka jamaa aliyekuwa mbele yangu kuanza kucheka.

Zamu yangu ilipofika, nikaingia kwenye kibanda kile. Tangu nizaliwe sikuwahi kuingia sehemu kama hiyo lakini sikutaka kupata maelekezo kwa mtu yeyote yule kwa kuwa sikutaka watu wajue kama nilikuwa na kiasi hicho cha pesa.

Nilifuata maelekezo na hatimaye kuchagua lugha ya Kiswahili na kutoa kiasi cha shilingi milioni mbili na kuondoka zangu. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kununua simu ya kupangusa kisha kuanza kuulizia kuhusu nyumba.

Kwanza sikutaka kufikiria kuhusu biashara, makazi yalikuwa bora kabisa. Niliulizia madalali, hatimaye nikakutana na mmoja na kumwambia hitaji langu la nyumba.

“Unataka nyumba ya kiasi gani?” aliniuliza.

“Yoyote nzuri! Kwanza zinapatikana?” nilimuuliza.

Dalali yule hakuniamini, kwa jinsi nilivyoonekana na kumwambia kwamba nilitaka kununua nyumba vilikuwa vitu viwili tofauti. Nilichoka, sikuwa na nguo mpya, yaani kwa akili yangu ilivyokuwa, nilianza kununua simu kabla ya nguo.

“Twende huku tajiri,” aliniambia japokuwa bado hakuonekana kuniamini.

Tulikwenda mpaka kwenye nyumba moja kubwa. Ilikuwa Kijitonyama, haikuwa nzuri sana lakini kwa kuwa nilikuwa na pesa, nilijua ningeirekebisha na kuifanya nitakavyo.

Nikapelekwa mpaka ndani na kuonana na mwenye nyumba, dalali akaanza kuongea naye na kumwambia kwamba mimi ndiye nilikuwa mteja pekee niliyepatikana.

Mwenye nyumba akaniangalia, alionekana kunishangaa, ilikuwaje niwe na pesa za kununua nyumba na wakati muonekano wangu tu nilikuwa kama fukara fulani hivi.

“Huyu ndiye anataka kununua nyumba?” alimuuliza dalali huku akionyesha mshangao.

“Ndiyo!”

“Acha masihara!”

“Huyu ndiye bosi. Niambie, kiasi gani?” alisema dalali.

Mzee yule hakutaka kujibu kitu, bado alikuwa akinishangaa, kwake nilionekana kuwa kama kituko fulani hivi. Akatuambia kwamba alikuwa akiiuza kwa shilingi milioni themanini kwa kuwa alitaka kuondoka hapo na kwenda kuishi Mbagala, maisha ya mjini eti yalimchosha.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni