
Mtunzi: Nyemo Chilongani
SEHEMU YA SABA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Mzee yule hakutaka kujibu kitu, bado alikuwa akinishangaa, kwake nilionekana kuwa kama kituko fulani hivi. Akatuambia kwamba alikuwa akiiuza kwa shilingi milioni themanini kwa kuwa alitaka kuondoka hapo na kwenda kuishi Mbagala, maisha ya mjini eti yalimchosha.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
“Mbona nyingi sana?” nilimuuliza mzee huyo.
“Si unaona Juma! Nilikwambia umeniletea mhuni unabisha! Sasa milioni themanini ina wingi gani?” aliuliza baba mwenye nyumba.
Maneno yake yalinikera sana, nilitamani ninunue nyumba yake na nimnunue mpaka yeye mwenyewe. Ila pamoja na kuumia hivyo, sikutaka kuonyesha hasira zozote zile zaidi ya tabasamu pana.
“Basi sawa! Nitakulipa hizo milioni themanini,” nilimwambia ili kuepusha maneno.
Nilichomwambia ni kutaka kuona hati ya nyumba hiyo. Hilo halikuwa tatizo, akamuita mtoto wake wa kike aliyeitwa Zamaradi ili alete hati ya nyumba.
Kwanza hiyo sauti ya huyo Zamaradi ilivyoitikia, jinsi ilivyosikika masikioni mwangu, nikajua tu kwamba huyo angekuwa bonge moja la demu.
Baada ya sekunde kadhaa, kweli hati ikaletwa, huyo Zamaradi nilipomuona, alikuwa bonge la demu. Mtu mzima udenda ukanitoka, shetani aliyekuwa ameniacha, akanirudia na kunipa mtego mkubwa.
“Hapa hatoki mtu,” nilijisemea.
Nikabaki namwangalia tu Zamaradi mpaka akashtuka kwamba nilikuwa namkodolea macho. Akayageuza macho na kuniangalia, mtoto jicho kama kala kungu, macho yalirembulika mpaka nikachanganyikiwa.
“Mzee mimi ndiye nataka ninunue hiyo nyumba,” nilimwambia mzee huyo pasipo kutarajia.
“Haina shida. Usiwe na hofu kijana. Ni milioni themanini tu,” aliniambia.
“Hakuna shida nitalipia,” nilisema na Zamaradi kuondoka hapo.
Unajua kwa nini nilisema hivyo? Ni kwa sababu Zamaradi alikuwepo hapo. Yaani kwa jinsi tulivyoonekana, dalali alionekana kama mnunuaji na mimi nilionekana kama dalali.
Nikaichukua ile hati na kuiangalia, kulikuwa na jina la huyo mzee. Niliporidhika nikampa. Kichwa changu kilikuwa kikifikiria kuhusu Zamaradi tu, alikuwa demu bomba ile kinoma, akili yangu iliniambia kwamba piga ua lazima nikaongee naye lakini si kuvumilia kubaki sebuleni hapo.
Kwa kuwa huyo mzee hakuwa na nguvu sana, nikamwambia ninahitaji kwenda chooni kujisaidia, niliamini kwamba angemuita Zamaradi kumpeleka mgeni kwenda huko, na mimi ningefanya yangu.
Kweli bwana! Akamuita msichana huyo na kumwambia anipeleke chooni. Mungu anipe nini tena? Nikasimama na kuanza kwenda huko huku tukiwaacha wao sebuleni pale.
Nilibaki nyuma ya Zamaradi huku nikimwangalia alivyoumbika. Jamani Mungu fundi, acheni masihara. Mpaka leo ninaamini kuna watu aliwaumba akiwa kwenye mood nzuri sana, na wengine aliwaumba kwa kuwaambia “Na nyie kaijazeni dunia tu manake hakuna namna.”
Ila kwa mtoto kama Zamaradi, nikahisi kwamba Mungu alisubiri siku ya wikiendi, ambayo hana kazi nyingi, siku aliyokuwa na furaha na kuanza kumtengeneza huyu mtoto. Yaani alikamilika kila idara kiasi cha kuedelea kunitoa udenda.
“Zamaradi!” nilimuita, nilishindwa kuvumilia, akageuka na kuniangalia.
“Abee bosi!” aliitikia, nikaachia tabasamu.
“Mungu fundi sana, anajua kuumba si mchezo!” nilimwambia.
“Kwa nini?”
“Umeumbika mno, u mzuri mpaka unaboa. Hebu naomba namba yako ya simu kwanza,” nilimwambia.
Mtoto alishasikia mimi ndiye niliiyetaka kununua nyumba yao, nilishatamba pale sebuleni, ataachaje kunimba namba, akanipa na kuniambia nimbipu manake alihisi asije akawa amekosea, nilivyofanya hivyo ikaita.
“Nakupenda sana,” nilimwambia, sikutaka hata kujivunga.
“Mh! Jomoniiii! Hebu nenda chooni kwanza.”
“Sijabanwa na haja nilitaka tu kuongea na wewe,” nilimwambia.
Mwenyewe akafurahi. Hapo ndipo nilipoamini kwamba mimi ni rijali, yaani sijui ilikuwaje ila nikajikuta nipo karibu naye na kuanza kubadilishana mate.
Pesa! Pesa! Pesa! Aliyezianzia Mungu anamuona, sijajua alikuwa na lengo gani kwenye dunia hii. Yaani ndiyo kwanza Zamaradi aliniona kwa mara ya kwanza, hakunijua nilikuwa nani lakini alivyonipokea mikononi mwake, kama mpenzi wake ambaye aliishi naye kwa miaka kumi.
“Nakupenda sana,” nilimwambia kwa sauti ndogo ambayo niliamini kuwa itampagawisha.
“Nakupenda pia!”
Baada ya hapo nikajiweka sawa na kurudi sebuleni na kuanza kuendelea kuongea nao. Tulikubaliana malipo kufanyika kesho, tena cash, hivyo tukaondoka.
Nilienda kuchukua chumba hotelini, nilipoingia tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumpigia simu Zamaradi, alinipagawisha mno na kuanza kuonja utamu wa pesa.
“Bebi! Nimekumiss sana,” nilimwambia.
“Kweli jamaniiii!”
“Ndiyo! Mwili wako una joto tamu sana, yaani nilivyokukumbatia , nilihisi raha kama nimeona mlango wa pepo. Zamaradi, unaufanya moyo wangu udunde, ndum ndum ndum....” nilimwambia.
“Jamaniiiiii”
“Wewe u mzuri mno, una tabasamu zuri, una meno mazuri, macho ya goroli, Zamaradi, umeumbika, unajua kucheka, una sura ya kitoto, umejazia, Zamaradi, hakika hakuna mwanaume anayeweza kukuacha akikupata,’ nilimwambia kwa kumchombeza.
“Jamaniiiii! Nasikia aibu huko!” aliniambia kwa kasauti kake ka kubembeleza.
“Zamaradiiiiiiii....nipo radhi nikose kila kitu, yaani pesa, kuingia peponi, nikose furaha lakini nisikukose wewe, ni mwanamke wa kipekee sana, ni mwanamke unayehitaji kuwa na furaha muda wote, unahitaji kutabasamu, kujaliwa, kusikilizwa, ni mwanamke unayetakiwa kuwa kwenye ulimwengu wako wa kipekee, Zamaradi, katika dunia hii hakuna mwanamke mzuri kama wewe,” nilimwambia, nilimsifia sana.
“Jamaniiiiiiiiiii” aliniambia, nahisi muda huo alikuwa aking’ata kidole chake.
“Zamaradi mpenzi, naomba ufungua mikono yako, unikumbatie, nikubusu, nikuonyeshee jinsi ulimwengu wa mapenzi ulivyo, nikaribishe mpenzi, nionje radha ya mate yako kwa mara nyingine, Zamaradi, kuwa mama wa watoto wangu,” nilimwambia kwa sauti ile tamu kabisa.
“Kwani hujaoa bebi?”
“Ningeoaje na wakati sikuwa nimeonana nawe? Zamaradi! Be mine mamiiiiii, unautetemesha moyo wangu....let me love you senyorita,” niliendelea kumchombeza.
Siku hiyo ndiyo nikaamini kwamba na mimi mkali kwenye maneno matamu, nilimfanya Zamaradi ajisikie kuwa mwanamke mzuri kuliko Mila Kunis, nilimwaminisha kwamba moyoni mwangu hakukuwa na yeyote yule.
Siku hiyo nilikesha nikiongea naye tu. Sijui alikuwa na bwana au peke yake, kitu nilichokuwa nikikiangalia ni mimi kuwa naye tu. Nakumbuka siku hiyo nililala majira ya saa saba na asubuhi nikapanga kwenda benki.
Ilipofika, nikachukua begi langu na kwenda benki kwa lengo la kuchukua pesa hizo. Nilihitaji kuchukua milioni tisini kwani nilijua kungekuwa na dharura.
Sikutaka kwenda na dalali, nilikwenda peke yangu. Niliingia benki nikiwa na begi langu lililokuwa na nguo ndani, unajua kwa nini? Kwa sababu ya kubadilisha.
Nilijua kwamba unapotoka kuchukua pesa nyingi benki na unapotoka, huwa kuna watu wanakufuata kwa ajili ya kukuua na kukuibia pesa, sasa kwa sababu nilikuwa mjanja, nilitaka niwachezee mchezo mpaka washangae.
Nilihitaji kiasi hicho cha pesa, niliambiwa nisubiri wakati wakiendelea kufanya process za mimi kupata kiasi hicho cha pesa. Baada ya saa moja, nikapewa na kuanza kuondoka.
Hapo benki, unapotoka, kwa kuwa ipo kwenye ghorofa refu, kabla ya kwenda nje kuna lifti, hivyo nilichokifanya ni kwenda kwenye lifti kama ninataka kwenda juu, humo ndani, nikabadilisha nguo zangu na kuchukua zilizokuwa kwenye begi, nikavaa na kofia kabisa kisha kuteremka kutoka kwenye lifti na kuchukua nyingine, nikaanza kushuka.
Nilitoka huku nikiwa na muonekano mwingine kabisa. Kwa kawaida sehemu hiyo si ya kupaki bodaboda, ila kwa mbali niliwaona vijana wawili, walikuwa na elementi, walisimama pembeni ya bodaboda yao huku wakiangalia kule kwenye jengo lile la benki, nikajua tu kwamba walitonywa kuna mtu ametoa milioni tisini hivyo walitakiwa kunifanyia uninja, kumbe hawakujua kama mimi mwenyewe nilikuwa ninja.
Nikawaacha wakiendelea kumsubiri mtu aliyevalia suruali ya kitambaa na fulana nyekundu, kumbe huyu aliyetoka ambaye alivalia pensi ya jinsi, fulana ya bluu na kofia nyeusi na kubeba begi ndiye mtu ambaye walitakiwa kumfuata, ila kwa kuwa hawakugundua kutokana na maelekezo waliyopewa kuwa tofauti na jinsi nilivyokuwa, nikawa huru kuondoka bila kufuatwa na yeyote yule.
Siku hiyohiyo nikamtafuta dalali na kumwambia kuhusu mzigo niliokuwa nimechukua, hakukuwa na kitu cha kupoteza kwani siku zote pesa ni mwanaharamu kwa sababu unaweza kujiona tajiri asubuhi lakini wakati wa adhana ya Magharibi ukawa masikini wa kutupwa.
Tulipofika nyumbani kwa akina Zamaradi, baba yake akaitwa na kumlipa pesa zake na hatimaye kuinunua nyumba hiyo. Kiukweli haikuwa nzuri sana kama nilivyowaeleza lakini niliamini kwamba baada ya kuwa nayo basi ningeweza kuirekebisha na kuwa moja ya nyumba nzuri sana hapa Dar es Salaam.
Wakati hayo yote yakiendelea sikuwa nimemuona Zamaradi, wakati mwingine nilijiongelesha kwa sauti kubwa ilimradi tu anisikie na kama alikuwa chumbani aje sebuleni lakini wapi.
Tulifanya biashara kwa amani kabisa na hivyo kuhitaji mwezi mmoja kwa ajili ya kujiandaa kuondoka mahali hapo. Hilo halikuwa tatizo lakini pia nikamwambia dalali kwamba nilihitaji kununua kiwanja maeneo ya Goba kwani pia nilitaka nishushe mjengo mkubwa wa kuanza maisha yangu.
Ngoja nikwambie kitu. Nilikuwa na pesa, tena nyingi mpaka wakati mwingine nilitamani sana kuombwa na mademu hivyo hii nyumba ya Sinza nilitaka niirekebishe ili iwe inatumika kwa ajili ya kulala na warembo tu, halafu ile ya Goba ambayo ningeijenga iwe ya mwanamke mmoja tu ambaye angekuja na kuwa mke wangu.
Tulipoondoka tu, nikampigia simu Zamaradi na kuongea naye, nilimwambia kwamba nilitoka kwao, aliniambia kuwa alikwenda kwa mama yake mdogo aliyekuwa akiishi Temeke ila angerudi muda si mrefu.
“Nije nikufuate?” nilimuuliza.
“Wapi? Huku Temeke?”
“Yaap!”
“Nimetoka! Sasa hivi nipo hapa Veta!” alinijibu.
“Hebu naomba uteremke hapo Ilala Boma mamii!”
“Wewe upo hapo?”
“Hapana ila nitafika kabla yako!” nilimwambia harakaharaka.
“Halafu!”
“Nataka tukae hapo Lamada tuongee kidogo,” nilimwambia.
“Sawa love.”
Akakata simu, nilihisi mwili wangu kama ukimwagiwa maji ya baridi, sikuamini mtoto angenikubalia kirahisi namna ile, nguvu ya pesa ilikuwa kubwa kupita kawaida.
Haraka sana nikaelekea kwenye kijiwe cha bodaboda na kutaka kuchukua moja ya kuniwahisha haraka sana kwani kutoka hapo Veta mpaka Ilala hakukuwa mbali, kazi kwangu kutoka huku Sinza mpaka hapo Ilala.
“Oya! Nataka unipeleke Ilala Boma,” nilimwambia dereva mmoja.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi