CHUZI NDIO HILO, HAKUNA KUONJA (2)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA PILI
ILIPOISHIA...
“Sawa,” alikubali mama Shua huku akigeuka kulala sawasawa…

“Humu ndani kuna mpangaji kama sisi…”

“Ndiyo…”

“Sasa nataka kusema kuwa, tupo familia mbili tofauti…”

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI

ENDELEA...
“Ni kweli mume wangu…”

“Sasa msimamo wangu ni huu. Kila familia ibaki kuwa kivyake. Sitapenda kuona mazoea yoyote kati ya familia yangu na yule bwana, nadhani nimesikika.”

“Nimekusikia mume wangu. Lakini ina maana hata salamu nisimpe?”

“Salamu mpe. Sitaki mazoea yale ya ndani kabisa, sipendi hata kusikia.”

“Nimekuelewa mume wangu.”

“Ndiyo hivyo basi.”

***

Asubuhi kulikucha, Shua alitoka uani akiwa hajavaa nguo. Musa alikuwa uani wakati huo na mama Shua alikuwa akitoka chumbani kwenda uani…

“He! We Shua kwa nini unatembea bila nguo?” mama yake alimjia juu japo Shua hakuwa mtoto mwenye kujitambua…

“Ha! Mchumba unanidhalilisha bwana, hujavaa nguo?! Basi sitakuoa,” alisema Musa akimtania mtoto huyo ambaye hajui lolote…

“Unaona sasa, unakosa mchumba hivihivi mwanangu?”

Musa alikwenda kuoga, akarudi kujiandaa. Mama Shua naye alijiandaa. Kwenye kutoka, baba Shua alisimama nje. Kwa hiyo Musa alipotoka alikuwa kasi kuashiria anawahi. Mama Shua alipotoka yeye, mumewe alimsemesha maneno mengi yaliyomfanya apitishe dakika tano nzima.

Alifanya hivyo ili kumpa Musa nafasi ya kufika mbali ili mama Shua akitoka wasiongozane.

Mama Shua alipotoka, alikimbia, baba Shua akamuuliza…

“Mbona unakimbia? Unamuwahi nani?”

“Jamani baba Shua kwani we’ huoni kwamba nimechelewa mume wangu?”

“Sasa ndiyo ukimbie? Si utembee kwa haraka tu. Unakimbia kama vile kuna mtu anakusubiri?”

“Mh! Baba Shua bwana. Mbona umekuwa hivyo mume wangu?” alihoji mama Shua huku akiangalia simu yake…

“Unachati na nani na we unasema umechelewa kazini?”

“Baba Shua, sichati na mtu. Nimeangalia tu simu.’’

Mbele ya safari akiwa ameshapotea machoni mwa mume wake, mama Shua alimtumia meseji Musa…

“Umeshatimua?”

“Niko barabarani tayari. Vipi? Kwema?”

“Kwema. Ah! Mista alinipotezea dakika kidogo, ndiyo nafika kituoni.”

“Pole sana. Baadaye basi nitachati na wewe.”

“Sawa, usijali.”

***

Musa alipofika kazini alimsimulia mfanyakazi mwenzake, aitwaye Miayo kuhusu mama Shua na akaomba ushauri…

“Musa, huyo mwanamke anakutaka. Hilo liko wazi kabisa. Lakini sasa mwepuke. Unajua mke wa mtu ni sumu inayoua mara moja?”

“Ndiyo, lakini sasa Miayo, si anajileta mwenyewe?”

“Musa….ulitaka ushauri au ulitaka nikuunge mkono?”

“Nilitaka ushauri.”

“Ndiyo huo nimekupa. Utajaza mwenyewe.”

Waliachana na kila mmoja akaendelea na kazi. Kichwani, Musa aliazimia kutembea na mama Shua. Kwanza alimwona ni saizi yake licha ya kwamba yeye alishapata mtoto mmoja huyo Shua…

“Nikishinda mara moja tu si mbaya. Lakini lazima nicheze naye mechi. Mtu anajikomba mwenyewe, mi kosa langu nini sasa?” alijiuliza, akajipa ujasiri.

Akiwa kwenye kuwaza hayo, mara meseji ikaingia, Musa akaifungua haraka sana…

“Vipi, umekula?” ilitoka kwa mama Shua…

“Haya sasa! mambo kama haya ya kuulizana kama nimekula halafu nimwache? Aaa! Wapi! Hata shetani atanicheka,” alisema moyoni Musa.

“Ndiyo nataka nitoke nikale, karibu sana,” alijibu Musa... “Kale bwana! Mwili haujengwi kwa simenti wala matofali, unajengwa kwa misosi mbalimbali. Mimi ndiyo natoka kula naingia job sasa.” “Poapoa.” Moyoni mama Shua alijua wazi kwamba, anatengeneza msala kati yake na mumewe. Alijua mumewe akibaini ukaribu wake na mpangaji huyo patachimbika. Tangu afunge ndoa na mumewe huyo haijawahi kutokea wakatibuana kuhusu mapenzi au uaminifu. “Mh! Yaani baba Shua akijua tu, imekula kwangu. Mbona atanitoa roho!” alisema moyoni mama Shua huku akijipanga kwamba, kuanzia siku hiyo aanze kuidhibiti simu yake kwa kiwango cha kimataifa ili mumewe asije akaidaka na kukutana na uozo wake na Musa.

***

Ilikuwa saa tisa na nusu, mama Shua alimtumia meseji Musa... “Mimi natoka job now . Wewe je?” “Hata mimi mama. Ndiyo niko nje hapa.” “Kituo wapi?” aliuliza mama Shua... “Mh! Nataka nipite Morocco nikapige kituo pale Makumbusho.” “Nije nikujoini?” “Mh! Utaweza?” “Naweza, kwa nini nisiweze? Kwani kuna kikwazo gani?” “Njoo.” “Poa.” Musa aliendesha gari huku mawazo yake yote yakiwa kwa mwanamke huyo. Na yeye alianza kuweka akili sawa kwamba, wanakokwenda lazima hakutakuwa na mwisho mzuri... “Lakini yule ni mke wa mtu. Hivi tunaweza kuwa kwenye uhusiano kwa muda gani bila mume wake kujua?” alijiuliza Musa huku mikono ikiwa kwenye usukani. Alifika Makumbusho, akatafuta baa nzuri na kukaa hapo.

Alimtumia meseji mama Shua ya kumwelekeza... “Poapoa. Na mimi ndo’ nashuka hapa kituoni,” alijibu mama Shua. Kwa uelewa wake, mama Shua alikwenda moja kwa moja hadi kwenye baa hiyo na kuungana na Musa. Kabla hajakaa, alivuta kiti, akamsogelea Musa, akampiga busu... “Mmwaaa...” Musa alishtuka kidogo, akataka kukwepa lakini aliogopa kumtia aibu mgeni wake huyo. Kikubwa alichokiwaza yeye ni kwamba, mbona hakuna mawasiliano ya kimapenzi? Sasa mabusu yanatokea wapi tena! “Mmmm...asante sana,” alisema Musa huku akitegesha shavu waziwazi ili apigwe busu hilo. Mama Shua alikaa. Akamwangalia Musa kwa macho ya kulegea kama vile ndiyo yupo eneo la tukio. “Vipi, pole na kazi,” alisema mama Shua... “Nimepoa, pole na wewe.” “Hata mimi nimepoa.”

***

Kule nyumbani, baba Shua aliwahi kurudi na kushangaa siku hiyo, mkewe amechelewa na wala hajatoa taarifa yoyote. Alishika simu na kumwendea hewani... “Haloo,” alipokea mama Shua baada ya kumtahadharisha Musa kukaa kimya, mumewe anapiga... “Huko wapi, mbona umechelewa?” “Niko kwenye daladala baba Shua.” “Uko kwenye daladala! Mbona nasikia muziki? Siyo baa hapo?” “Hapana, sema tu daladala linapita nje ya baa moja hapa.” “Wapi?” “Eee...eee...Makumbusho.” “Yaani upo mahali hupajui sawasawa mpaka unajifikiria?” “Jamani baba Shua, mbona hivyo?” Baba Shua alikata simu. Mama Shua alikaa sawasawa, akamwangalia Musa kama anayesema... “Mbona hunitongozi?” “Vipi, mista nini?” “Ah! Ana mchecheto kama nini!” “Wahi basi, mimi bado nipo.” “Kweli, ngoja nipande basi hapa.” Musa alimkatalia kupanda basi, akampa pesa achukue Bajaj ili awahi... “Ooh! Jamani! Asante! Sasa itakuaje?” “Si tutawasiliana.” “Ukija home nishtue basi.” “Ili tuchati?” “Eee.” “Wee! Unataka kupigwa wewe.” “Hakuna. Ila we ukifika nishtue tu.” “Poa.”

***

Baada ya kufika nyumbani, mama Shua alimpandishia mume wake... “Yaani wewe unataka hata kama nachelewa dakika kumi nikwambie? Mbona una wivu wa kijinga sana wewe baba Shua?” Baba Shua hakuwahi kusikia maneno kama hayo kutoka kwa mkewe, alikazia macho simu yake... “Mama Shua...” “Nini?” “Leo unanijibu hivyo mimi?” “Ah! Umenikera sana baba Shua ndiyo maana.” “Ndiyo unijibu hivyo mama Shua?” “Nisamehe kama umekereka baba Shua.” “Unajua umechelewa kwa muda gani?” “Nusu saa tu.” Baba Shua aliinyakua simu ya mkewe na kukimbia nayo mpaka chumbani...

Mama Shua alitoka mbio kumfuata nyuma yake huku akimsema vibaya kwa kitendo chake hicho...

“We baba Shua ndiyo nini hivyo? Baba Shua bwana, nipe simu yangu.”

“Aha! Kumbe hii simu ina mambo yako ndani siyo?” aliuliza baba Shua kwa sauti iliyojaa hasira...

“Wala hakuna kitu kama hicho.”

“Sasa kwa nini unaing’ang’ania kama haina mambo mabaya?”

“Si yangu lakini! Kwani mimi nimeitaka simu yako?”

“Shika yangu hiyo. Kaa nayo na mimi nakaa na yako.”

Mama Shua alikumbuka kuwa, kila meseji aliyoipokea kutoka kwa Musa aliifuta na hata zile alizokuwa akituma yeye pia alizifuta. Kwa hiyo akawa hana wasiwasi kwa hilo, bali wasiwasi wake ni kuhusu Musa kama atatuma meseji wakati simu anayo mume wake...

“Haya kaa nayo...kaa nayo...” alisema mama Shua huku yeye akiisusa simu ya mume wake.

Baba Shua alikaa kitandani na kuanza kusoma meseji mbalimbali za mkewe, alizotumiwa na alizotuma. Hakuona ya mapenzi. Akaanza kusachi majina yaliyoseviwa, akatafu ta jina la Musa, kumbe mkewe alimsevu Musa kwa jina la Karibu Mgeni. Akimaanisha Musa alihamia pale muda si mrefu.

Wakati baba Shua amekazana kusaka herufi M, K ya karibu aliipa kisogo na hivyo kumnusuru mkewe katika mtego mbaya wa usaliti.Mama Shua akawa hachezi mbali na mumewe. Alikuwa akijifanya kupanga nguo kwenye kabati huku muda mwingi alimkazia macho mumewe ili aone kama atabadilika uso ajue tayari amekumbana na meseji ya Musa.

***

Musa alipomaliza bia zake nne kwenye baa hiyo aliondoka. Safari yake ilikuwa ni kurudi nyumbani. Aliwaza kumtumia meseji mama Shua lakini moyo ukasita, akakumbuka mazungumzo yake na mwanamke huyo wakiwa wanaagana pale baa...

“Basi ukifika nyumbani nishtue.”

“Ngoja nikifika ndiyo nitamshtua,” alisema moyoni Musa akiwa tayari barabarani.

Ile anaingia tu, anakutana na mama Shua. Mama Shua akamsogelea kwenye sikio na kumwambia...

“Usitume meseji mpaka nianze mimi.”

Musa alikubali kwa kutingisha kichwa tu huku akimtumbulia macho mwanamke huyo.

Mama Shua alirudi tena chumbani. Mumewe akampa simu yake...

“Huna namba ya huyu kijana mgeni?”

“Sina.”

“Haya.”

***

Saa moja jioni, baba Shua alipata wageni wawili anaofanya nao kazi. Kwa hiyo mama Shua akapata nafasi ya kukaa chumbani akiwa na shughuli zake na akatumia nafasi hiyo sasa kuwasiliana na Musa...

“Mambo? Sikuwa na simu mimi ndiyo maana muda ule nikakwambia usitume meseji mpaka nianze mimi. Niambie.”

Musa aliisoma meseji ile na kumjibu kwa kifupi sana...

“Miss u.”

“Miss u 2. Umelala?”

“Hapana,” Musa akamjibu.

“Unafanya nini?” Mama Shua akamtumia meseji ya kumwuliza.

“Nipo baa ya nyuma huku nimekuja kula mishikaki mara moja.”

“Mh! Jamani! Umenitajia mishikaki, mate kinywani yamenijaa.”

“Nikuletee?”

“Utaweza kweli?”

“Nitaweza. Si nikifika naiweka sehemu nje halafu nakujulisha!”

“Sawa, niletee hata miwili.”

“Mitamu sana. Miwili haitoshi, nakuletea mitano.”

“Du! Haya, sawa. Asante sana.”

Musa aliagizia mishikaki sita. Akafungiwa kwenye mfuko wa rambo.

Lakini mama Shua akakumbuka kwamba, akiletewa hiyo mishikaki atailia wapi? Maana mume wake akiona atamuuliza alikoitoa kwa usiku ule. Lakini pia kumkataza Musa asinunue aliona atatoa picha mbaya, akaacha. Liwalo na liwe.

Musa alipofika nje, akauweka mfuko wa rambo juu ya meza ya plastiki iliyochoka, kwenye kona kabisa ya nyumba, akamtumia meseji mama Shua...

“Mzigo wako upo kwenye meza ya plastiki nje kwenye kona.”

Mama Shua alitoka haraka,

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni