CHUZI NDIO HILO, HAKUNA KUONJA (3)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA TATU
ILIPOISHIA...
Musa alipofika nje, akauweka mfuko wa rambo juu ya meza ya plastiki iliyochoka, kwenye kona kabisa ya nyumba, akamtumia meseji mama Shua...

“Mzigo wako upo kwenye meza ya plastiki nje kwenye kona.”

Mama Shua alitoka haraka,

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
akaenda nje kwenye meza na kuchukua mfuko kisha akasimama kulekule nje na kutumbukiza mkono mfukoni na kuchukua kipande kimojakimoja cha mshikaki na kukipeleka mdomoni. Mpaka akamaliza mishikaki yote sita.

Alirudi ndani akiwa anajifuta mkono huku akisahau kwamba, mishikaki inanukia...

“Mh! Nasikia harufu kama ya mishikaki,” alisema mgeni mmoja wa baba Shua wakati mama Shua akipita. Wote wakasema kweli.

***

Asubuhi kulikucha, Shua na mama yake walikuwa uani. Musa alipotoka kwenda kuoga akaanza kumtania Shua...

“Mchumbaaa...umeamkaje wewe mchumba?”

Shua aliachia tabasamu tu akiwa hana la kujibu...

“Mwambie nimeamka poa, sina hela ya nyama leo.”

“Sawa mchumba...nikupe shilingi ngapi ya nyama?”

“Mwambie elfu kumi.”

“E...fu ku...mi,” alisema kwa tabu Shua huku akiuma vidole. “Basi mchumba usiwe na wasiwasi , nikiwa natoka kwenda kazini nitakuachia.” “Mwambie ukaniachie pale dukani kwa Mangi,” alisema mama mtu... “Aachie kwa...Mangi,” alisema Shua kwa kufuata maelekezo ya mama yake.

¤¤¤¤

Musa aliingia kuoga. Baada ya dakika sita tu, akatoka. Alirudi chumbani kujiandaa, akatoka zake. Nje alimkuta baba Shua. Akamsalimia kwa furaha... “Mkubwa umeamkaje?” “Salama kaka, umeamkaje na wewe ?” “Niko fiti. Kumekucha.” Mara, mama Shua alitoka akiwa ameshajipigilia tayari kwa kutoka kwenda kazini... “Za asubuhi?” Musa alimsalimia mama Shua kama vile hawajuanagi... “Salama tu, umeamkaje anko?” “Ah! Kumekucha, nimeamka salama.” Musa aliondoka kwa kasi, nyuma baba Shua akaanza... “Kwani yule kijana ni anko wako?” “Kwa nini?” “Nimesikia umemsalimia ukisema ‘umeamkaje anko.’” “Ah! Baba Shua jamani. Basi nisamehe mimi...halafu nimechelewa, naondoka.” “Ngoja kwanza. Umechelewa kivipi? Unamuwahi nani? Mbona jana ulichelewa zaidi ya leo!” “Jamani baba Shua, kwani unataka kuniambia nini?” “Nakushangaa ukisema kwamba unaondoka. Au kuna mtu unamuwahi mahali?” “He! Mtu gani sasa jamani?” “Unamjua wewe .” “Wala hakuna mtu ninayemuwahi . Niamini baba Shua jamani.” Mama Shua aliondoka. Ilibidi atembee kwa mwendo wa polepole ili mumewe asimwelewe vibaya.

Akiwa anapita duka la jirani, akaitwa... “Mama Shua.” Aligeuka... “Kuna pesa nimeambiwa nikupe wewe ,” alisema muuza duka... “Na nani?” aliuliza mama Shua... “Kaka mmoja simfahamu.” “Shilingi ngapi?” “Elfu kumi.” “Ooo! Nimeshamjua. Asante sana,” alishukuru mama Shua. Hakuamini kama mazungumzo ya Musa na binti yake, Shua yalikuwa siriasi kiasi cha kuacha pesa dukani kweli. Yeye alijua wapo kwenye utani tu. Mbele, mama Shua alimpigia simu Musa... “Haloo...” “Nashukuru sana wangu. Kumbe ulifanya kweli? Mi nilijua unataniana na binti yangu tu...teh! Teh! Teh!” alisema na kucheka mama Shua... “Usijali my love, tupo pamoja.” “Poa, kazi njema.” “Poapoa.”

*****

Kama ilivyokuwa jana yake, mchana wa saa saba, mama Shua alimtumia meseji Musa... “Wangu umekula?” Muda aliijibu haraka sana meseji hiyo... “Yap! Wewe?” “Mimi ndiyo nakula sasa, njoo ule.” “Sina hela.” “Mimi ninayo.” “Teh! Teh! Endelea tu bhana, baadaye.”

***

Kwa kawaida, mama Shua hutoka kazini saa tisa na nusu. Siku hiyo ilipofika saa nane akamtumia meseji Musa... “Nimeboreka na kazi leo, natamani kwenda kupumzika mahali mpaka muda wa kazi ukiisha ndiyo nirudi nyumbani.” “He! Pole sana. Sasa ukapumzikie wapi, baharini?” “Hapana...” “Baa?” “Hapana, sitaki baa.” “Porini?” “Teh! Bhana mi sitaki utani wako. Porini kwani mi swala?” “Wapi sasa? Labda ukapumzikie gesti!” “Hayo maneno.” “Kwa hiyo unakwenda kupumzika gesti?” “Natamani iwe hivyo .” “Du! Hongera, mpaka nakutamani.” “Unanitamani nini sasa?” “Unavyopumzika na mimi ningekuwepo.” “Njoo.” “Kweli?” “Kha! Mbona hujiamini wewe !” “Oke utaniambia wapi upo!” “Poa.”

Muda huohuo mama Shua alikusanya vilivyo vyake na kubeba mkoba wake begani, akaaga kwamba anajisikia vibaya , hivyo anakwenda kupumzika. Aliingia katikati ya jiji na kusaka hoteli, akaipata. Alipolipia na kuoneshwa chumba, akamtumia meseji Musa... “Oya! Nipo Greenland Hotel. Rum namba 17.” “Naifahamu, nakuja mama. Da! Mwili mzima umesisima.” “Mwili umesisimka kisa nini?” “Si nakuja kupumzika na wewe . Najua nitapata joto lako, utanibusu midomo, utanivua shati...da!” Mama Shua alipokuwa akiisoma meseji hiyo, naye mwili ulimsisimka... “Da! Bwana Musa, njoo.”

*****

Baba Shua akiwa kazini kwake , alipokea barua iliyomtaka asafiri kwenda Arusha kikazi kwa siku saba... “Da! Jamani hakuna mtu mwingine anayeweza badala yangu?” alimuuliza bosi wake mmoja... “Hakuna. Kajiandae, kesho asubuhi unaondoka.”.

Kwa baba Shua, ni mara ya kwanza kuonesha kwamba hapendi kusafiri kikazi. Mara zote, amekuwa akifurahia safari hizo kutokana na kulipwa posho ya safari ambayo humsaidia.

Alibaki akijifikiria kiasi cha dakika tatu nzima na mabosi wake walionesha hawana habari naye tena.

Aliondoka akiwa mnyonge. Mawazo makubwa kwake ilikuwa ni jinsi gani atasafiri na kumwacha mkewe, mama Shua kwenye nyumba ile ambako kuna mpangaji mpya, kijana na mtanashati…

“Hivi kweli yule kijana hawezi kuniingilia kwa mke wangu?” alijiuliza baba Shua.

Aliwaza na kuwaza, ikafika mahali akakubali kwamba lazima asafiri kwani kazi ndiyo inamuweka mjini lakini huku moyoni akipanga kwamba, mkewe huyo atakwenda kumwacha kwa kaka yake…

“Mama Shua na Shua watakwenda kukaa kwa bro mpaka nirudi. Hii balaa,” aliwaza mwenyewe.

Alimtumia meseji mke wake…

“Mama Shua mimi kesho asubuhi nina safari ya kikazi, nakwenda Arusha kwa siku saba.”

“Mh,” aliguna mama Shua. Moyoni alifurahia sana, akasema…

“Kwa siku saba! Du! Nitafaidi sana na Musa.”

Palepale, badala ya kumtumia meseji mumewe kumjibu, alimtumia meseji Musa…

“Wangu, kuna uhuru f’lani unakuja mkubwa sana.”

Musa aliisoma meseji hiyo lakini hakuuelewa huo uhuru, akauliza…

“Upi huo wangu?” “Mista ana safari ya Arusha, atakaa kwa siku saba.”

“Du! Kweli huo ni zaidi ya uhuru,” alijibu Musa.

Baba Shua alishangaa kuona mkewe anachelewa kujibu meseji yake wakati si kawaida yake. Akampigia…

“Haloo,” alipokea mama Shua…

“Wewe vipi, umepata meseji yangu?”

“Nimepata mume wangu, nilikuwa bize kidogo, samahani,” alijibu mama Shua…

“Oke, basi endelea,” alisema baba Musa na kukata simu.

Mama Shua aliendelea kuchati na Musa…

“Kwa hiyo wangu angalia ni jinsi gani tutakuwa huru. Labda wewe ubanwe.”

“Mimi nibanwe na nani wakati nipo singo. Labda wewe…”

“Hata mimi nitabanwa na nani kama mume wangu hayupo. Labda wewe.”

Baada ya kuchati sana na Musa, mama Shua ndiyo akamgeukia mumewe…

“He! Siku zote hizo jamani! Si afadhali zingekuwa siku mbili au tatu tu! Loo!”

“Ndiyo hivyo, ndiyo kazi. Nitafanyaje sasa? Lakini itabidi we ukakae kwa bro, Buguruni,” meseji ya baba Shua ilisema hivyo. Mama Shua alishtuka kusoma meseji hiyo, akakosa raha. Akaiangalia simu yake kwa muda kama haamini kuwa ndiyo iliyoleta meseji ile.

Alichoka kabisa, hakumtumia meseji mume wake ya kumwambia sawa, wala hakumtumia meseji Musa ya mwendelezo wa kuchati kwao.

***

Muda wa kutoka kazini ulipofika, mama Shua aliondoka kimyakimya. Hakumjulisha Musa wala mume wake. Alifika nyumbani akiwa mpole. Furaha yake ilipotea…

“Kwanza baba Shua ye hakumbuki tu. Mke wa kaka yake hatupatani kama nini…sasa anaposema akaniache kule kwa siku saba anatafuta nini kwa yule mwanamke?”

Baba Shua aliporejea alimkuta mkewe amesharudi, akafurahi sana…

“Kumbe umesharudi mke wangu? Pole na kazi.”

“Nimepoa, lakini kichwa kama kinagonga kwa mbali.”

“Umekunywa dawa?”

“Bado, ila kikiendelea hivihivi nitakunywa.”

***

Mpaka usiku, mama Shua hakumtumia meseji Musa wala Musa mwenyewe pia hakumtumia meseji mwanamke huyo. Yeye alikuwa muoga wa kuanza…

“Mama Shua,” alianza kwa kuita baba Shua wakiwa tayari kitandani…

“Abee…”

“Kesho asubuhi ndiyo utakwenda kwa bro. Maana mimi nitaondoka saa kumi na moja na nusu.”

“Umeshaongea naye kwenye simu?” aliuliza mama Shua kabla hajamzungumzia mke wa kaka yake baba Shua…

“Sijampigia. Lakini ngoja nimpigie sasa hivi. Lakini sidhani kama kuna tatizo hata ukienda mwenyewe,” alisema baba Shua. Alichukua simu, akampigia kaka yake huku akiweka loud speaker…

“Shikamoo kaka…”

“Marhaba, za familia yako?”

“Njema tu. Sasa kaka kesho mimi nasafiri kwenda Arusha. Nitakaa kwa siku saba. Naomba familia yangu ije ikae kwako…”

“Mbona shemeji yako amesafiri leo. Amekwenda Morogoro na watoto. Nyumbani hakuna mtu, mimi nimekuja kikazi huku Rufiji.”

Baba Shua alishusha pumzi kwa nguvu…

“Ooo! Sikujua, basi sawa kaka. Nakutakia kazi njema.”

“Haya poa.” Baba Shua alikaa kimya kwa muda kisha akasema…

“Basi itabidi ubaki hapahapa lakini take care.”

“Usijali mume wangu.”

***

Saa kumi na moja na nusu ndiyo baba Shua aliondoka nyumbani kwa usafiri wa Bajaj hadi Ubungo.

Nyuma, mama Shua akamtumia meseji Musa…

“Jamaa ndo huyooo anaondoka zake.” Haikuchukuwa muda Musa akaijibu fastafasta. “Bado hata sijaenda kuoga niende kazini kwa hiyo vipi?” Akamtumia mama Shua kiuchokozi. “Unauliza virungu polisi, njoo!” Nyuma mama Shua alikuwa akijiamini kwa asilimia zote kuwa mumewe asingeweza kurudi kutokana na haraka aliyokuwanayo wakati anaondoka. Alichokifanya ni kumchungulia Shua kama hajashtuka kisha akajiweka sawa kwenye kochi na kumsubiri Musa.

¤¤¤¤¤¤¤¤¤

Mwendo wa nusu saa, baba Shua alikuwa katika foleni ya gari ya kuelekea kituo cha mabasi, Ubungo. Bajaj aliyokuwa ameipanda ilishindwa kujipenyeza kutokana na magari mengi kutanua barabarani na kushindwa kusonga mbele. “Unaweza kunirudisha tulipotoka?” aliongea baba Shua baada ya kugundua kafanya kosa kuchukua makaratasi muhimu ya kazini ambayo aliyahifadhi nyumbani

kwake. “Usijali bosi hapa tunatoka tu,” aliongea dereva bila kujua kama kuna kitu baba Shua amekisahau nyumbani, alichokuwa akijua ni kuwa anamchelesha kupanda gari. “Kuna kitu muhimu sana cha ofisini nimesahau kwangu, au chukua hela yako nirudi kwa bodaboda fasta,” aliongea baba Shua, kisha akashuka na kupanda bodaboda kuelekea nyumbani kwake.

**********

Kitendo cha kuingia na bodaboda nyumbani kwake,

kikamshtua Musa ambaye tayari alikuwa amejiandaa kudumbukia chumbani kwa baba Shua ili kumkabili mama Shua.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni