MAUAJI YA KASISI (26)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA
ILIPOISHIA...
“Ok, Una akili sana Kamanda, siwezi kupata mtu kama wewe tena katika ofisi yangu. Sikiliza, baadae nitakupigia simu tuonane.” Baada ya mazungumzo machache kati yao waliagana na kuondoka kila mtu na hamsini zake.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Ndani ya ofisi za AGI Int’, Gina alikuwa ameandaa bonge la keki na mvinyo wa kutosha kusherehekea kurudi salama kwa boss wake Kamanda Amata. Walipongezana wakiwa wawili tu, wakikata keki na kunywa mvinyo kwa fujo kiasi. Wakiwa katika hali hiyo ndipo simu ya Kamanda iliita kwa fujo, “Aaaaaaa nani tena huyo?” Gina aliuliza kwa sauti ya kilevi. “Madam S” Kamanda Amata akajibu na kuiweka ile simu sikioni.

“Unikute hapa katika ofisini kwangu mara moja,” na ile simu ikakatika, Kamanda Amata akashusha ile simu na kuitia mfukoni, mara Gina akamvamia na kumkubatia kwa nguvu, “Kamanda, sikjawahi kukwambia jamani, mi nakupenda, unioe, uwe mume wangu,” Gina alilalama akiwa kalewa chakari, chezea Dompo wewe! “Hebu toa ulevi wako Gina,” Amata aling’aka lakini Gina bado alikuwa kamng’ang’ania sasa akitaka kumpa ulimi, Amata akamuweka kwenye kiti.

“Wewe, uwe na akili, umelewa wewe, mi naenda kwa Madam S kaniita,” Amata alimwambia Gina, “Tunaenda wote,” Gina nae akaliunga. Dakika chache tu ziliwachukua kuwasili katika ofisi ya Madam S iliyopo mkabala na jengo la hazina, akaingia getini na kuegesha gari panapotakiwa, aliteremka na kumuacha Gina akiwa anakoroma garini, tayari alibebwa na usingizi mzito. Akajiweka tai yake vizuri kisha akajitupia koti lake na kuziendea ngazi zinazoingia katika ofisi hiyo, akiwa mlango wa kwanza alikutana na mtua mmoja ambaye alimjua vilivyo ni mwenzake wa idara ya usalama wa taifa lakini vitengo tofauti akiwa kakunja sura hata hakumsalimu, Kamanda aliponyosha mkono kumsalimi hakupokelewa, akaona isiwe shida alimpita na kuingia ofisini kwa Madam S.

“Karibu Kamanda,” Madam S alimkaribisha huku amesimama badala ya kukaa.

“Asante Madam kwa kunikaribisha katika ofisi yako tukufu ambayo sikutegemea kuiona tena,” Kamanda Amata alizungumza akiwa siriasi kabisa.

“Kamanda Amata, kutokana na mchango wako mkubwa katika kuliokoa Taifa, na kutatua migogoro mizito na mikubwa ambayo ama ingelipoteza Taifa au maisha ya wananchi, maamuzi ya kikao cha watu wa idara ya usalama kimeamua kikushushe cheo kutokana na kutoitilia umakini nafasi uliyopewa na kudharau amri au maamuzi ya wakubwa wako, hivyo umeshushwa cheo na kubadilishiwa kitengo, kutokana na hilo kuanzia sasa ofisi yako ya kazi itakuwa Ikulu, kuratibu na kuhakikisha usalama wa msafar wa Mheshimiwa Rais pindi awapo nje ya jengo la Ikulu.” Madam S alimtazama Kamanda Amata usoni hakuona dalili ya tabasamu wala chuki kutoka kwa mpiganaji huyo. Kwa kuwa yeye kupata nafasi hiyo alikuwa ametokea katika jeshi la polisi kitengo cha CID alitoa heshima ya kijeshi kwa Madam S ya kuonesha amekubaliana na uamuzi huo bila ubishi.

Madam S akamkabidhi barua maalu yenye mhuri wa serikali kuthibitisha hilo pamoja na muhtasari wa kikao, akavipokea na kuvibana kati mkono wake wa kulia. Madam S akamtazama tena Amata, “ Kamanda Amata, kutokana na kuwa idara ya usalama imekosa mtu wa kuishika nafasi yako mithili ileile ya jinsi ulivyokuwa ukifanya kazi kwa makini na akili nyingi, ukiwa tayari kufa kwa ajili ya Taifa lako au kwa ajili ya wanyonge, imeonelewa tukurudishie cheo chako cha Tanzania Secret Agency namba 1 kwa muda usiojulikana mpaka itakavyoamriwa vinginevyo,” Madam S alimtazama tena Kamanda usoni akakutana na sura ileile ya ukakamavu. Akachukua beji maalum ya utambulisho kwa watu wote wa usalama wa Taifa na kuipachika katika upande wa kushoto wa ukosi wa koti lake, beji ambayo ilichukuliwa wakatia alipofikishwa hospitali Muhimbili akitokea Kenya. Madam S akamkabidhi kikasha kimoja kilichofungwa kwa utepe mwekundu.

Akakipokea akaukata utepe na kukifungua ndani, bastola aina ya Walther PPK (PPK ni Polizei Pistole Kriminal-The Criminal Police Pistol), pembeni ya bastola hiyo kulikuwa na kiwambo chake cha sauti. Chini ya hicho kikasha kulikuwa na bahasha ndogo, akaichana na kuifungua, ilikuwa tiketi ya ndege kwenda Ujerumani, alipochambua vizuri akakutana na picha ya Bill Van Getgand, juu yake imeandikwa ‘WANTED’ yaani ‘ANATAFUTWA’ halafu chini yake wameorodhesha mashirika mbalimbali ya kijasusi ambayo yanamtafuta jasusi mwenzao aliyehasi huko KGB na kuingia kwenye mikono ya uhalifu wa kimataifa.

“Kamanda Amata, sasa unaenda kufanya kazi ngumu ambayo shirika la letu la ujasusi japo halitambuliki hivyo kimataifa linakutuma, Safari njema.” Madam S alimaliza na kuketi tena katika kiti chake. Akili ya Kamanda Amata ilianza kufanya kazi ndani ya muda mdogo akiikabili kazi hiyo ngumu na ya hatari ambayo hakujua wapi itaishia. Alimtazama madam S kwa tuo. “Keti chini kamanda,” Madam S alimwambia Kamanda Amata wakati mlango ukifunguliwa na jamaa mmoja akiingia na sanduku moja dogo la chuma, akakaribishwa na kuketi katika kiti kingine pembeni ya kamanda Amata. Kamanda Amata alielewa kinachotakiwa kufanyika, walihitaji kuiridisha ile microchip ya GPS ambayo huweza kumfanya aonekane popote alipo.

Yule daktari akatoa mashine Fulani na kumfanyia vipimo vichache ikiwamo presha ya damu na vitu vingine, kisha akachukua kitu kama sindano iliyounganishwa na bomba kabisa ambapo ndani yake kuna hiyo microchip, akamdunga sehemu Fulani ya msuli wake wa mkono juu ya kiwiko na chini ya bega akasukuma kama anavyosukuma dawa katika sindano ya kawaida, ile microchip ikasafiri katik ule msuli na kujikita ndani kabisa, baada ya hapo akafungwa bandeji na kupewa dawa Fulani za vidonge za kutumia.

Wakati huohuo mlango ukafunguliwa na Chiba akaingia ndani akiwa na begi lake ambalo daima hupenda kutembea nalo, akatoa kompyuta yake ndogo lakini yenye kazi nyingi za kijasusi, akaiweka mezani na kuiwasha kisha akaanza kuingiza namba Fulani Fulani, waya mmoja akaupachika katika sehemu ile aliyohisi ile chip imetuama, ikashikiwa kwa ile bandeji na waya mwingine wenye kitu kama kibanio mwishoni ukabanwa katika kidole gumba cha mkono mwingine, kisha Chiba akawa akifanya kazi katika kompyuta yake.

“Ok, kila kitu tayari,” akasema huku akimtoa zile nyaya zote. Kisha akaingiza mkono katika upande mwingine wa lile begi lake, “Hii hapa saa ya kutumia Kamanda, saa hii ina uwezo wa kukata chuma cha aina yoyite kwa kutumia nishati ya infrared ambayo imekwishawekwa ndani yake, ina uwezo wa kutuma fax fupi na pia inatambua hatari ya mlipuko mahala popote ambapo umetegwa. Uwe mwangalifu kijana,” Chiba alimaliza maneno yake huku akimpigapiga mgongoni.

“Kamanda!” Madam S aliita, “Nimekupigania sana mwanangu, nenda kafanye kazi, nakuomba usichezecheze na wasichana hawa huko, ujue kwamba Bill ni jasusi, si ajabu akawa anajua safari yako yote hata sasa, nimemaliza kwa heri,” Madam S alimaliza na kuagana na Kamanda Amata akabaki na Chiba ofisini.

Kamanda Amata akashuka ngazi na kuiendea gari yake ambako alimkuta Gina bado kalala akikoroma. Akaingia na kuwasha gari akaondoka zake mpaka nyumbani kwake Kinondoni, hakuwa na muda wa kutosha alipanga vitu vyake vichache, akakusanya silaha zake zote za siri na kuzificha panapostahili katika kijibegi chake cha mgongoni ambacho ni yeye tu aliweza kujua kipi kiko wapi na wapi kiko kipi, wakati lile sanduku lilikuwa na nguo na zana ndogondogo. Alijiangalia kwenye kioo cha chumbani mwake na kujiuliza aingie vipi Ujerumani, mkimbizi? Mfanyabiashara, mtalii, muandishi wa habari au vipi, akapata jibu, akafungua kabati na kuchukua bunduki yake ya kisasa kabisa, iliyotengenezwa kwa mfano wa camera kubwa ya picha mnato lakini ndani yake ilikuwa na uwezo wa kubeba risasi ishirini na nane za bastola aina ya Smith and Wesson.

Alipohakikisha kila kitu kipo sawa, akatulia juu ya kitanda huku mawazo yote yakiwa juu ya Bill, kila akikumbuka kitendo alichofanyiwa na Bill alijikuta hasira zikimpanda maradufu, aliamua kumfungia kazi kikweli, ‘ulimwengu utatambua kuwa Bill kauawa na mkono wa Amata, sitaiacha roho yake ipotelee jela wala kwenye mikono ya nani, mi sijui nitakapomuona tu uso kwa uso ama zake ama zangu’ yalikuwa ni mawazo yaliyopita katika kichwa cha Kamanda Amata muda huo. Usingizi ulimpitia na ndoto mbaya zikamuandama, mara anakabwa mara anakimbizwa mara anatumbukia kwenye shimo, basi shida tu.

Kengele ya saa ya mezani ilimuamsha ilikuwa yapata saa nne usiku, alikurupuka na kuingia bafuni akaoga harakaharaka na kujiandaa, alipoenda mutazama Gina, alimkuta bado yuko hoi kwa usingizi akamuandikia ujumbe na kuufutika mahali alipolala kisha ye akachukua gari yake na kuondoka zake kuelekea JNIA tayari kwa safari.

Majira ya saa saba usiku, ndege kubwa ya sirika la Qatar Airways au kama wanavyoliita dege lenye hadhi ya nyota tano liliiacha ardhi ya Dar es salaam na kukata anga kuelekea Doha ambako abiria wangebadilisha ndege ili kuendelea na safari zao. Kamanda Amata alitulia kitini katika behewa hiyo ya VIP akiwa kanyoosha miguu kwa raha zote akipata raha kwa kuwatazama warembo wa Qatar waliokuwa wakijipitisha pitisha na kuumuuliza hili au lile. Akili na mawazo yake tayari yalikuwa yamejipanga kimchezo huo wa hatari ambao unamkabili mbele yake ambao alipenda aufanye kwa siri na kwa muda mfupi.

ACHEN – UJERUMANI

ANDREAS Schurmann alimtazama Bill Van Getgand, hakummaliza, mtu huyo mnene, mwili jumba lakini mwepesi kwenye mapambano alikuwa ameketi mbele ya tajiri huyo, tajiri anayejulikana sana katika mji wa Achen na pembezoni. Ilkuwa ni siku moja tu baada ya Bill kuwasili katika jumba hilo la kifahari lililojengwa katika eneo la Mausbach. Jumba la bei mbaya ambalo hakuna asiyelijua katika mji huo.

“Nini kilikuwa kinakushinda siku zote kupata kitu kidogo kama hiki Bill?” Don Andreas alimuuliza Bill huku akimmiminia bia aina ya Pilsner, bia bora Ujerumani.

“Hata huko nilikoipata usifikiri kazi ilikuwa rahisi, imebidi kumwaga damu,” Bill alijibu huku akiinua glass yake na kuiweka mdomoni kabla hajamiminia kinywaji kilichomo ndani yake, akabeu kidogo, “Imebidi tumwage damu, hakukuwa na jinsi,” alimalizia kusema. “Usijali, maadam tumepata tunachotaka basi,” Don Andreas akamtia nguvu kwa maneno hayo.

“Hii mali yetu kaka, aliwekeza baba wa babu yetu, alikuwa na makusudi mazima juu yake,” Andreas aliendelea kuongea huku akiigeuzageuza ile monstrance mikononi mwake,

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni