KITABU CHA SHETANI (1) Jina: KITABU CHA SHETANI Mtunzi: Aziz Hashim SEHEMU YA KWANZA Manyunyu ya mvua yalikuwa yakiendelea kudondoka taratibu kuashiria kumalizika kwa mvua kubwa iliyonyesha mfululizo usiku kucha. Tofauti na siku zote, watu walikuwa wachache sana barabarani japokuwa tayari kulishapambazuka. Ubaridi ulioambatana na mvua hiyo, ulimfanya kila mmoja kutamani kuendelea kuvuta shuka na kuuchapa usingizi. “Hee! Tayari ni saa moja? Mungu wangu, nitachelewa kazini,” Edmund Katera ‘Mundi’, kijana mdogo aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni kubwa ya mawasiliano ya Hashcom Mobile kwenye kitengo cha Teknolojia ya Mawasiliano (Information Technology) alikurupuka kutoka usingizini na kukimbilia kwenye kabati lake la nguo kwa lengo la kuchukua taulo. Harakaharaka akatoka mpaka nje na kuchukua ndoo ya maji ya kuoga huku mswaki ukiwa mdomoni, akatembea kwa hatua za haraka mpaka bafuni ambapo alijimwagia maji bila kujali ubaridi uliokuwepo asubuhi hiyo kutokana na mvua iliyokuwa inaishia. Muda mfupi baadaye, tayari a…