KITABU CHA SHETANI (1)

0
Mtunzi: Aziz Hashim

SEHEMU YA KWANZA
Manyunyu ya mvua yalikuwa yakiendelea kudondoka taratibu kuashiria kumalizika kwa mvua kubwa iliyonyesha mfululizo usiku kucha. Tofauti na siku zote, watu walikuwa wachache sana barabarani japokuwa tayari kulishapambazuka. Ubaridi ulioambatana na mvua hiyo, ulimfanya kila mmoja kutamani kuendelea kuvuta shuka na kuuchapa usingizi.

“Hee! Tayari ni saa moja? Mungu wangu, nitachelewa kazini,” Edmund Katera ‘Mundi’, kijana mdogo aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni kubwa ya mawasiliano ya Hashcom Mobile kwenye kitengo cha Teknolojia ya Mawasiliano (Information Technology) alikurupuka kutoka usingizini na kukimbilia kwenye kabati lake la nguo kwa lengo la kuchukua taulo.

Harakaharaka akatoka mpaka nje na kuchukua ndoo ya maji ya kuoga huku mswaki ukiwa mdomoni, akatembea kwa hatua za haraka mpaka bafuni ambapo alijimwagia maji bila kujali ubaridi uliokuwepo asubuhi hiyo kutokana na mvua iliyokuwa inaishia.

Muda mfupi baadaye, tayari alikuwa amerejea chumbani kwake, akavaa na baada ya dakika chache, alikuwa ameshajiandaa, akajitazama kwenye kioo kikubwa cha ‘dressing table’ iliyokuwa ndani ya chumba chake na baada ya kuridhishwa na mwonekano wake, alitoka na kufunga mlango wa nyumba aliyokuwa anaishi, akatoka na kuianza safari ya kuelekea kazini.

Kwa jinsi barabarani kulivyokuwa na matope na foleni kubwa ya magari barabarani kutokana na mvua hiyo kama ilivyo desturi ya Jiji la Dar es Salaam hasa nyakati za mvua, ukizingatia kwamba tayari alikuwa nyuma ya muda kutokana na kuchelewa kuamka, hakuwa na ujanja zaidi ya kukodi bodaboda.

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

TUENDELEE...
“Naenda Bamaga, Mwenge.”

“Buku nne tu mwanangu.”

“Aaah! Buku nne mi sina, nitakupa buku mbili jero.”

“Unaua mwanangu, ok poa twenzetu,” dereva wa bodaboda alimwambia Edmund ambaye bila kupoteza muda, alikwea kwenye bodaboda na safari ikaanza. Dereva huyo wa bodaboda akawa anapenya kwenye foleni, wakati mwingine akilazimika kupita katikati ya magari yaliyokuwa yamefungana kwa lengo la kumuwahisha mteja wake sehemu aliyokuwa anaenda.

Hata hivyo, haraka hizo zilienda kuishia eneo la Sinza Afrika Sana ambapo magari kutoka kila upande, yalikuwa yamefungana eneo hilo lililokuwa na makutano ya barabara nne, moja inayotokea Shekilango, nyingine inayotokea kwenye taa za kuongozea magari za Bamaga, inayotokea kituo cha polisi cha Mabatini na ile iliyokuwa inatokea Mwenge kwa kupitia ofisi za TRA.

Kwa jinsi magari hayo yalivyokuwa yamefungana, haikuwa rahisi hata kwa mwenda kwa miguu kukatisha katikati ya magari hayo, manyunyu ambayo yalikuwa yamepungua yakaanza kuongezeka na kusababisha kero kubwa kwa wasafiri waliokuwa wakitumia bodaboda, akiwemo Edmund ambaye tayari shati lake nadhifu alilokuwa amelivaa lilianza kulowa.

“Pipiiii! Pipiiii... Poooopooo!” milio ya honi nyingi za magari iliendelea kusikika eneo hilo, kila dereva akijiona yeye yupo sahihi isipokuwa wengine ndiyo wanavunja sheria za barabarani, hali iliyosababisha taharuki kubwa eneo hilo.

Ilibidi Edmund aanze kumshinikiza dereva wake afanye kila linalowezekana kuhakikisha wanajinasua eneo hilo kwani ukiachilia mbali ukweli kwamba alikuwa anaendelea kuloa, alikuwa pia anaendelea kuchelewa kazini.

Wakati dereva wa bodaboda akihangaika kuitoa pikipiki pale ilipokuwa imezingirwa na magari, kwa bahati mbaya alijikuta akilikwangua gari lililokuwa nyuma yao na kulibonyeza eneo kubwa na kukwangua rangi.

“Mungu wangu, tumeharibu gari la watu,” alisema dereva wa bodaboda huku akiendelea kuhangaika kutafuta upenyo wa kukimbia kabla mwenye gari hajashuka lakini alikuwa amechelewa kwani mwenye gari alishashtukia kwamba amegongwa na bodaboda.

Msichana mdogo mwenye umri wa kati ya miaka ishirini na mbili hadi ishirini na tano, mrefu wastani, mwenye umbo lenye mvuto wa aina yake, akiwa amevalia mavazi ya kisasa kama mtu anayefanya kazi kwenye ofisi moja kubwa mjini, chini akiwa amevaa suruali nyeusi ya kitambaa iliyomshika kisawasawa maungo yake makubwa na shati jeupe nadhifu, usoni akiwa amevaa miwani ya kisasa ya rangi nyeusi, aliteremka kwenye gari la kifahari, Jeep Grand Cherokee la rangi ya fedha na kuzunguka upande ule bodaboda iliyokuwa imembeba Edmund ilipokuwa.

“You stupid poor boys, do you know how much it cost to buy this type of car?” (Nyie wavulana maskini wapumbavu, mnajua inagharimu kiasi gani kununua gari kama hili?) alisema msichana huyo kwa jazba huku akivua miwani yake aliyokuwa amevaa, akainama kuangalia pale dereva wa bodaboda alipoligonga gari lake wakati akirudi nyuma.

Kwa kuwa Edmund na dereva wake ndiyo waliokuwa na makosa na ni kweli kwamba waliharibu gari hilo ambalo hata wangeambiwa walipe gharama za kutengeneza sehemu waliyoigonga hawakuwa na fedha, ilibidi waufyate mkia. Wakawa wanatazamana huku kila mmoja akijisikia aibu kubwa kutokana na jinsi msichana huyo alivyokuwa akiendelea kuwachambua, akichanganya lugha, Kiingereza cha Kimarekani na Kiswahili.

“Please forgive us ladyboss, its just an accident,” (Tafadhali tusamehe bosi, ni ajali tu) alisema Edmund, kauli iliyomfanya yule msichana amgeukie na kumtazama kwa jicho la ukali.

“Ajali? Unazijua ajali wewe? Mtazame kwanza, nikikwambia ulipe gharama za uharibifu alioufanya huyo maskini mwenzio utaweza? Go to hell! (Nenda kuzimu!)” alisema msichana huyo kwa hasira, kauli iliyomfedhehesha mno Edmund.

Tayari madereva wa magari mengine walikuwa tayari wameteremka kwenye magari yao na kuanza kumsihi msichana huyo awasamehe Edmund na dereva wake. Kwa nyodo na dharau akageuka na kuanza kutembea kuelekea kwenye gari lake huku akiivaa miwani yake. Akaingia kwenye gari na kukaa nyuma ya usukani.

Edmund aliyekuwa ameshuka kwenye bodaboda, aliendelea kulitazama gari lile, hasa pale bodaboda yao ilipopagonga. Akiwa anaendelea kushangaa, aliona kitu chini kwenye lami chini ya gari, bila kuonekana na mtu yeyote akainama na kukiokota.

Ilikuwa ni simu ya kisasa iliyokuwa imedondoka chini, bila hata kuuliza akajua kwa vyovyote lazima yule msichana aliiangusha alipoinama kuangalia gari lake. Tayari askari wa usalama barabarani walikuwa wameshafika eneo hilo kusaidia kufungua njia ambayo ilikuwa imefungwa na magari yaliyofungamana kila upande.

Wakati Edmund akiwa bado anajishauri kama amrudishie msichana yule simu yake au la, tayari barabara ilishafunguliwa na magari yakaanza kuondoka kwa kasi. Akashuhudia yule msichana naye akibadili gia kwenye gari lake la kifahari na kuondoka kwa mbwembwe za hali ya juu.

“Oyaa twende mwanangu!” dereva wa bodaboda alimuita Edmund kwa sauti ya juu ambayo ilimzindua kutoka kwenye hali aliyokuwa nayo, akaiweka simu hiyo mfukoni na kusogea hadi pale dereva wa bodaboda alipokuwa anamsubiri, akapanda na kuendelea na safari.

Kwa kuwa eneo hilo halikuwa mbali na ofisini kwao, dakika chache baadaye tayari walishawasili Bamaga, akashuka kwenye bodaboda na kumlipa dereva fedha zake kisha akaanza kutembea harakaharaka kuelekea kazini kwao huku akiwa anaendelea kutafakari juu ya tukio hilo lililotokea muda mfupi uliopita na jinsi alivyotolewa nishai na msichana yule mrembo.

Kila alipokuwa akikumbuka jinsi msichana huyo alivyowatolea maneno ya shombo, Edmund au Mundi kama wengi walivyozoea kumuita, alijikuta akipandwa na hasira kali ya maisha.

Aliamini umaskini wake ndiyo uliosababisha msichana huyo amtusi kwani kama angekuwa tajiri, na yeye angekuwa akiendesha gari lake, tena la kifahari kuliko la msichana huyo na kamwe asingekumbana na dharau kama hizo.

Edmund alishusha pumzi ndefu na kuwasha kompyuta yake aliyokuwa anaitumia kazini, akatoa kitambaa na kuanza kujikausha maji ya mvua iliyomnyeshea huku kichwa chake kikiwa bado hakijatulia.

Dakika chache baadaye, aliinuka sehemu anayokaa siku zote kazini na kwenda kutengeneza kahawa kwani baridi aliyokuwa anaisikia asubuhi hiyo, ukichanganya na kipupwe (AC) ya ofisini humo, alijiona kama mwili wake unaganda.

Akarudi kwenye kiti chake akiwa na kikombe cha kahawa, akakaa na kuanza kuchangamsha tumbo huku bado akionesha kutotulia kiakili.

“Mundi vipi mwanangu? Mbona leo hata salamu hakuna? Yaani umefika kimyakimya na kula bati kama hujatuona wanao,” Clarence, mfanyakazi mwenzake na Edmund, waliyekuwa wakifanya kazi kwenye kitengo kimoja cha Teknolojia ya Mawasiliano (IT) kwenye Kampuni ya Hashcom Mobile, alimuuliza Edmund baada ya kumuona hayuko kwenye hali yake ya kawaida.

Swali hilo lilimzindua Edmund kutoka kwenye lindi la mawazo, ikabidi aanze kuvunga na kusingizia kwamba mvua iliyomnyeshea asubuhi hiyo wakati akienda kazini ndiyo iliyosababisha akili zake zihame. Wakaendelea kuzungumza mawili matatu kisha Edmund akatulia tena. Ni hapo ndipo alipokumbuka kwamba mfukoni alikuwa na kitu cha thamani.

Akaingiza mkono na kutoa simu kubwa ya kisasa iliyokuwa mfukoni, kwa mara nyingine akaitazama na kujikuta akishusha pumzi ndefu. Ilikuwa simu ya thamani kubwa mno ambapo kwa makadirio yake ya harakaharaka, aliamini dukani lazima itakuwa inauzwa zaidi ya shilingi milioni mbili.

“Duh! Mundi umenunua iPhone 6? Umepata wapi hela mwanangu? Hizo simu za washua, wewe maskini mwenzangu umeipata wapi?” Clarence alimuuliza Edmund kwa masihara baada ya kumuona akiitazama simu hiyo.

Wafanyakazi kadhaa waliokuwa wamekaa jirani naye, waliacha kila walichokuwa wanakifanya na kumsogelea, kila mmoja akitaka kuiona simu hiyo ambayo kwa kipindi hicho ndiyo ilikuwa ikiongoza kwenye soko la simu kwa kuwa na bei ya juu na ubora kuliko simu zote.

“Hebu tuone? Hebu na mimi niione?” wafanyakazi kadhaa walikuwa wakigombea kuishangaa simu hiyo. Wakati wao wakigombea simu hiyo, akili ya Edmund ilikuwa mbali kabisa, akiendelea kumfikiria yule msichana na jinsi alivyomdhalilisha mbele za watu.

Baada ya muda, Edmund aliichukua simu hiyo na kuanza kuikagua vizuri, akagundua kuwa ilikuwa imefungwa kwa namba maalum (security codes).

Kwa kuwa alikuwa na uelewa mkubwa wa namna ya kuchezea simu na kompyuta, muda mfupi baadaye alifanikiwa kuifungua simu hiyo, juu kabisa akakutana na picha ya msichana yule aliyemtoa nishai, jambo lililomfanya awe na uhakika kwamba ni kweli ile simu ni yake na aliiangusha pale alipoikuwa anaangalia jinsi gari lake la kifahari lilivyogongwa na bodaboda.

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)