Mtunzi: Omary John Mndambi
SEHEMU YA NNE
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Nilianza kupiga hatua kwenda pembeni ya barabara nitafute sehem yenye kivuli nikae lakini kila nilipokuwa nakata hatua nilikuwa najisikia unyonge sana, miguu ilianza kuwa mizito huku nikisikilizia maumivu ya lile kofi nlilopigwa na Yule konda.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
Jua lilikuwa kali sana na tayari nilikuwa nasikia kiu mno, sehemu hii ilikuwa ni vichaka tupu na hakuna gari iliyokuwa inasimama kwani hakukuwa na kituo wala nyumba za watu.
Nilipiga macho mbele nyuma na pembeni nikashuhudia vichaka vya miti mikavu kuonyesha kuwa hii sehemu hakukuwa na makazi ya watu, sikuona hata dalili ya mtu kupita isipokuwa magari yaliyokuwa yanapita kwa kasi sana.
Katika hali ambayo sikuitegemea nilishuhudia majimaji yakishuka kwenye mashavu yangu nikaaanza kuyafuta, kumbe yalikuwa ni machozi.
Nilikuwa najihisi hali ya upweke sana, nilijiona kutengwa na wanaonijua na wasio nijua, mbaya zaidi sehemu hii sikuijua, nilitamani bora ningebaki kule kwa Bibi kwani nilianza kukosa matumaini ya huko niendako.
Baada ya kukosa kivuli niliamua kutembea taratibu kuifwata barabara, jua kali lilinichoma huku nikiwa sioni hata mtu wa kuongea nae, isipokuwa ngedere ambao walikuwa wengi wakikimbizana vichakani, nilipomkumbuka Yule nyoka aliyenitemea mate kule mlimani nilianza kuogopa nikijua kuwa kwa eneo nililopo inawezekana pia kuna chatu kabisa.
Sikuogopa kifo, nilikuwa tayari kwa lolote mbele yangu kwani maisha yangu tayari ni ya mitihani, pamoja na ujasiri niliojivika bado nilikuwa namwamgikwa na machozi usoni, ilifika hatua nikawa nalia kwa kwikwi kabisa kwani nilikuwa najisikia unyonge, upweke na nilikuwa na njaa na kiu.
Nilitembea kwa zaidi ya lisaa limoja lakini sikuona nyumba wala kituo lakini ghafla nilipokunja kona niliona gari aina ya Semi trela likuwa limeinama upande wa pembeni ya barabara. Nilijikuta nikipata matumaini mapya kwa kuona tu watu.
Pembeni ya lile gari nilimuona jamaa mmoja ameshikilia dumu la maji ya Uhai la kama lita kumi hivi anajimiminia kinywani, kwa kiu niliyokuwa nayo nilijikuta nayamezea mate yale maji, asikwambie mtu kiu inatesa kuliko njaa ya chakula.
Nilitamani nimfwate hata nimpokonye yale maji lakini nikaamua kumfwata kistaarabu.
“Broo naomba maji kidogo nina kiu sana”
“we fala nini, unadhani hapa mtoni, hata salam hutoi unataka maji tu…kwendaaaa mse..ge wewe”
Kitendo cha Yule jamaa kunijibu vile nilijikuta nikimwagikwa na machozi kama chem chem, sikuweza kugeuza shingo yangu niliangua kilio kama nimefiwa, sikuwa naigiza, nilijikuta tu nafsi yangu ikitaka kulia, nilijaribu kujizuia lakini sikuweza kila nilivyokuwa nakata hatua ndio kilio kiliongezeka.
Hatimaye miguu haikunyanyuka tena nikakaa chini huku kilio kikiongezeka mara dufu, nilishtuka nikishikwa bega, nilipotupa macho yangu nikakutana nayule jamaa aliyenifukuza.
“We dogo una nini”
Alivyoniuliza lile swali ndio alizidisha machungu yangu kwani nilijikuta unyonge ukizidi na hali ya kutengwa ikanisononesha zaidi. Hapa ndipo niligundua kuwa kumbe ukitaka mtu anaelia anyamaze hutakiwi kumbembeleza, ukimbembeleza utamliza zaidi.
“Dogo hebu simama basi, mbona sikuelewi”
Yule konda alizidi kuniongelesha huku wale wenzie wakija usawa ule tuliopo, nilitaka nisimame lakini miguu ilikuwa imenyong’onyea kwa uchovu wa kutembea kuanzia kule mlimani lakini pia machungu yaliyokuwepo moyoni.
“Siwezi kusimama broo, niacheni tu muendelee na mambo yenu”
“Tukuacheja dogo hebu simama uje hapa”
Nilishikwa mkono nikanyanyuliwa huku akiwa amepitisha mkono wake kwenye bega langu na kufanya kama amenikumbatia huku akiniongozea kwenye gari.
Tulizunguka nyuma ya gari ambapo kulikuwa na kivuli cha gari kisha akatoa maji kwenye dumu na kumimina kwenye chupa tupu ya litamoja na nusu kisha akanipa.
Kwa kiu niliyokuwa nayo niliyapokea yale maji lakini koo langu halikuruhusu kupitisha maji,, kulikuwa na kitu kama fundo limenikaba, nilijikaza sana na mwishowe nikafanikiwa kunywa yale maji.
Niliyanywa yote mpaka yakaisha, yalipoisha tumbo likaanza kuniuma nikajua kuwa ni kwasababu nimekaa na kiu mda mrefu alafu nikanywa maji kwa pupa.
Halikuuma sana, lilipoa kisha Yule jamaa akanipa keki za kwenye pakti na juisi, nilipokea nikanywa pia haraka haraka.
Alianza kunihoji mambo mengi na mimi sikusita nilimueleza kila kitu nikamuoana akisikitika sana ila akaniambia.
“ wala usijali, we komaa tu maisha nikutafuta na siku zote mtafutia juani hulia kivulini, usichoke.”
………………………
Ilikuwa ni usiku wa saa kumi tukiwa tunakatiza mto wami tuko ndani ya semi trela scania lililobeba cemet likielekea Mbeya.
Sehemu hii ya dereva ilikuwa inatosha kukaa watu watatu lakini kuna chemba iko kwa juu kidogo ambayo ina kitanda, walininitaka nipande nilale nami sikusita kwani nilikuwa nimechoka sana.
Nilishtuka nikiamshwa nishuke, nilipokata jicho kulikuwa kumepambazuka, hapa tulikuwa kwenye mizani ya challinze na gari lilikuwa linaacha njia ya dar es salaam likielekea mbeya hivyo ilibidi mimi kushuka hapa.
Yule Konda alinishika mkono akaniambia nimfwate, tulielekea kwenye zile ofisi za mizani tukaingia ndani, Yule konda aliwasalimia wale jamaa wa pale mizani kisha akamuulizia jamaa mmoja aliyemtaja kwa jina Mapunda.
“Mapunda saivi yuko Mikese Morogoro, amehamishwa, kama unaenda huko utakutana nae pale”
Yule konda aliachana nao akaniambia tuondoke.
“Yani huyu Mapunda angekuwepo angukusaidia sana, ni mshkaji wangu sana”
Aliniongoza mpaka kwenye Coaster iliyokuwa inaenda Dar es salaam kisha akanipakia. Nilipokaa kwenye kiti alimuita konda wa ile Coaster na kumlipa nauli yangu kisha akaja na kunipa shilingi elfu tatu.
Alinipa namba zake za simu akaniambia nikifika Dar nimtafute, aliniaga akaondoka zake na muda sio mrefu gari ile nayo ikaondoka.
Miaka mitano baadae nilipata taarifa zilizonihuzunisha kuwa Yule jamaa alifariki kwa kukanyagwa na ile Scania alipokuwa anarekebisha kitu chini ya uvungu wa gari ambalo liliserereka na kumpondaponda na kufariki hapohapo, roho iliniuma sana na namuombea maisha mema huko aliko.
Gari liliingia Ubungo mida ya saa sita mchana, niliangaza macho pale Ubungo sikuelewa A wala B, Bahati nzuri kulikuwa na vibanda vya kupigisha simu kila kona, watu waliofika ama kuishi dar kwa siku za nyuma kidogo watakuwa mashuhuda wa hili.
Nilikifwata kibanda kimoja kilichokuwa na msichana mrembo nikamuomba huduma ya simu akaniambia ni shilingi elfu moja kwa dakika, nilimlipa kisha nikampa namba akaipiga.
Hapa nilikuwa nampigia rafiki yangu niliyesoma nae msingi japo alinitangulia lakini alikuwa rafiki yangu sana.
Wakati huu yeye alikuwa anasoma Mlimani Chuo kikuu. Aliniuliza niko wapi nikamwambia niko Ubungo.
“Uko Ubungo upande gani”
“Kaka sielewi chochote hapa mimi ni mgeni”
“Mpe huyo mwenye simu hapo kibandani”
“Eee unaona hilo Bango hapo la BUZZ ni Bomba, …kwa pembeni kuna mabasi ya kwenda Morogoro, Dodoma na Mbeya, njoo hapa kibanda changu kiko kwa jirani tu”
Ndani ya dakika sihirini nilimuona Joshua akija pale akiwa ameongozana na Rafiki yake mmoaja, nilishangaa sana kumuona akiwa vile, alikuwa amependeza sana na kunawiri mno, alikuwa mweupe siku zote lakini saivi weupe wake ulizidi na alikuwa amenona mno, alikuwa amevalia kisasa sana na kuonekana kijana wa mjini wakati tulikuwa tunacheza nae mpira wa manailoni kwenye Vumbi.
Alinifwata akanikumbatia tukasalimiana fresh sana, tulipiga story mbili tatu kisha akaniambia tuondoke, wakati tunaondoka Joshua alirudi kwa Yule dada akampa mkono akiwa anamuaga.
“Dada kwaheri sana, naondoka lakini ntakukumbuka daima, mgeni wangu umemkaribisha vizuri kaniambia na soda ulimpa bure kabisa, hakika wewe ni wife material, hivi umeolewa? Hebu chukua hii namba na wewe unipe yako…”
Joshua aliongea maneno mengi sana huku dada wa watu akijitahidi kuutoa mkono wake lakini Joshua alikuwa kaung’ang’ania vilivyo.
Walipeana namba za simu kisha tukaondoka, tilikunja kona mbili tatu huku nikishuhudia magari mengi yanavyopita kwa kasi huku wenyeji wakionekana hawayaogopi kabisa.
Tulipanda Daladala zilizokuwa zinaenda Mwenge zikipitia Chuo kikuu cha Dar es Salaam kisha hatimaye tukawa kwenye hosteli anazoishi Joshua.
Jambo la historia kwangu ni kwamba hii ndio ikawa siku yangu ya kwanza kupanda lifti, japo hata nilipopanda sikujua kuwa ile ndio lifti. Niliona tu tukiingia kwenye gorofa refu mno alafu tukaingia kwenye kijichumba kidogo ambacho kilijifunga milango na nikaona Joshua akibonyeza vitufe flani na hatimaye tukajikuta ndani ya sekunde ile milango ikifunguka tena kisha tukatoka.
Nilibaki na maswali kichwani kuwa tuliingia hapa kufanyaje na hatukikaa wala kufanya chochote, nilipojikuta naona mji wa Dar es salaam kwa chini nikajua tuko juu ghorofani na lazima ile ilikuwa ni lfti
Maisha ya pale Mlimani yalinivutia sana, yalikuwa ni maisha yasiyokuwa na stress hata kidogo, nilijikuta nikimtamania Abeid kuwa mwanafunzi wa chuo.
Kilikuwa na mazingira mazuri, mahusiano yalikuwa poa sana na zaidi wanafunzi wa pale walikuwa wanaishi kijamaa sana, utani na masihara mengi yalisababisha wawe wanacheka mara kwa mara.
Nilittamani angalau na mimi ningekuwa mwanafunzi pale lakini ilikuwa haiwezekani kwa wakati ule.
Usiku ulipoingia tulilala japo kwa kuchelewa kwani watu walikuwa hawaishiwi na story, mara wengine wanaangalia movie kwenye tv na PC zao ili mradi kila mtu alikuwa huru kufanya anachotaka.
Kulipokucha asubuhi niliamshwa nikaenda kuoga nikapiga na mswaki kisha tukaenda canteen kwa ajili ya kunywa chai.
Binafsi nilikunywa chai ya maziwa na vitumbua vitatu kisha tukarudi hostel, ukweli ni kwamba nilikuwa na nguo chache sana na zilikuwa za kishamba, sikufanana na watu walionizunguka pale chuoni nikaamini ule msemo wa Kuku mgeni ………
Abeid aliliona hili akanipa flana yake na pensi na sendoz akaniambia nivae tutoke, siku hii ilikuwa ni jumapili hivyo hakuwa na vipindi vya darasani.
Tulitoka akanizungusha maeneo mbalimbali ya jiji la dar es salaam, kuanzia kariakoo, Mnazi Mmoja, Posta mpaka Baharini tukapanda pantoni mpaka kigamboni.
Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuiona bahari…asante sana Abeid, nakuombea Mungu akuzidishie mafanikio kwenye ualimu wako uje kufika mbali zaidi ya hapo ulipo.
……………………..
Ilikuwa ni jumatatu tuko na Abeid tunaelekea Posta karibu kabisa na BoT ambapo ziko ofisi za wizara ya Mambo ya Ndani nikimtafuta Yule niliyeambiwa nijitambulishe kwake anisaidie kupata nafasi ya mafunzo ya uaskari.
Abeid alikuwa ni mjanja sana maana kwa jinsi tulivyofika pale wizarani na maswali tuliyoulizwa na wale walinzi basi ningekuwa peke yangu ningesharudi kwa kuogopa lakini tofauti ni kwamba Abeid kila alipokuwa anajibiwa vibaya yeye alikuwa anatabasamu na kuonyesha kutoshtuka.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)
