SHEREHE KUZIMU (19)

Zephiline F Ezekiel
Mtunzi: Frank Silaa

SEHEMU YA KUMI NA TISA
ILIPOISHIA...
Ilikuwa siku moja ya jumamosi usiku wa manane ambapo Vivian alifunga safari kutokea kuzimu kwenda duniani kumchukua mama Nelson kusudi akaliwe nyama kuzimu.

KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA NAYO...
Alifanikiwa kwa asilimia mia moja kutekeleza adhima yake ya kumtoa mama wa mume wake kafara. Sherehe kubwa ilifanyika ambapo nyama na damu ya mama Nelson ilishambuliwa kuzimu.

**********

Palipokucha siku ya jumapili, nyumbani kwa mama Nelson palikuwa na ukimya mzito. Milango na madirisha ya nyumba ilikuwa imefungwa. Taa zote za nje zilikuwa zinawaka. Muda ulizidi kusonga wakati ukimya nao ukizidi kuendelea kuchukua atamu katika nyumba ile ya kisasa, aliyokuwa amejengewa na kijana wake. Ilipofika mida ya saa tano asubuhi mama mmoja wa jirani (mama Kitomari) ambae ni rafiki wa mama Nelson. Aliamua kupitia nyumbani kwa mama Nelson akitokea kanisani ili aweze kufahamu kilichokuwa kimemkwamisha kwenda ibadani. Alipofika kwa mama Nelson alikuta taa za nje bado zinawaka hadi muda ule.

Haikuwa kawaida kwahiyo aligonga mlango kwa mda mrefu ili aweze kufunguliwa lakini jitihada zake ziligonga mwamba kwasababu hakufanikiwa kufunguliwa. Alichukua simu yake ya mkononi na kumpigia kwa mara kadhaa lakini simu iliita upande wa pili bila kupokelewa. Alipata wazo la kwenda kugonga dirisha ya chumba chake akiamini pengine labda bado alikuwa amelala lakini wazo hilo nalo halikuzaa matunda. Baada ya jitihada za muda mrefu alikata tamaa na kuamua kuondoka kwenda nyumbani kwake akiamini kwamba ataendelea kumtafuta kwa njia ya simu. Nelson nae alizoea kumpigia mama yake simu mara kwa mara kumjulia hali.

Jumapili usiku Nelson alipokuwa sebuleni kwake akiangalia runinga alimkumbuka mama yake kwahiyo alichukua simu yake na kujaribu kuwasilina na mama yake. Simu iliita upande wa pili bila kupokelewa, Nelson alikata tamaa ya kuendelkea kumpigia mama yake simu kwa kuwaza huwenda atakuwa ameshalala. Nelson aliamua kumwandikia mama yake ujumbe mfupi wa maandishi kumtakia usiku mwema.

“Uwe na usiku mwema mama. Nakupenda sana.” huo ndio ujumbe mfupi aliouandika Nelson kwa mama yake baada ya kuhisi atakuwa usingizini. Alifanya hivyo kusudi mama yake atakapoamka na kukutana na missed call yake ajue kwamba alimpigia kumtakia usiku mwema.

Siku iliyofuata wakati Nelson alipokuwa kazini kwake, alikumbuka kwamba jana yake alimpigia simu mama yake lakini hakufanikiwa kumpata kwahiyo alijaribu kumpigia kwa mara nyingine tena kwasababu alikuwa amemisi sauti ya mama yake. Kwa zaidi ya mara tano alimpigia mama yake bila mafanikio ya kumpata hewani. Simu iliita hadi ikakata. Alijaribu kuwaza mama yake amekumbwa na tatizo gani tangu jana yake hapokei simu yake lakini kichwa chake kilishindwa kupata jibu la kueleweka. Alisubiri baada ya masaa mawili akajaaribu kumpigia tena simu mama yake kwa mara kadhaa lakini bado haikupokelewa. Alipata wazo la kujaribu kuwasiliana na mjomba wake ili aweze kumuuliza kama amewasiliana na mama yake katika kipindi kifupi kilichopita.

“Shikamoo mjomba.”

“Marahaba Nelson, hujambo?”

“Sijambo bwana, nimejaaribu kumpigia mama simu tangu jana usiku lakini simu yake haipokelewi. Vipi wewe umewasiliana na mama tangu jana?” Nelson aliitikia salamu, nakujieleza na kisha akamalizia kwa kumuuliza mjomba wake swali.

“Hapana, mara ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa siku ya jumamosi, tena yeye ndiye alinipigia kunijulia hali.” Maneno ya mjomba hayakuleta matumaini katika moyo wa Nelson kwasababu hata yeye alizungumza na mama yake kwa njia ya simu siku hiyohiyo ya jumamosi.

“Sasa itakuwaje anko?” Nelson aliuliza swali.

“Kwa sasa nipo kazini kwangu, kibaya zaidi leo sipo na gari langu kwasababu ningekufuata hapo kazini kwako halafu tungeongozana kwenda kwa mama kuangalia amekumbwa na tatizo gani.”

“Kuhusu suala la usafiri ondoa shaka tutatumia gari langu.”

“Basi hakuna tatizo, njoo sasahivi nipitie hapa kazini kwangu ili tuweze kwenda pamoja.”

Harakaharaka Nelson alifuata utaratibu wa kuomba ruhusa kazini na baada ya muda mfupi aliondoka katika eneo lake la kazi na kuelekea ofisini kwa mjomba wake kumchukua ili waweze kwenda katika safari waliyokuwa wameipanga.

Baada ya dakika kumi Nelson alimchukua mjomba wake kazini kwake na kuanza safari ya kuelekea maeneo ya kambi ya chupa madukani ambapo ndipo alipokuwa akiishi mama Nelson. Dakika ishirini baadae Nelson aliegesha gari lake nje ya nyumba ya mama yake. Baada ya kushuka kwenye gari walipokelewa na harufu kali mithili ya panya alieoza. Hakuna aliyeonekana kujali ile harufu mbaya ambayo ilikuwa kero katika pua zao, walihisi labda kuna mzoga uliokuwa karibu. Jambo lililowashangaza ni kwamba taa za nje bado zilikuwa zinawaka hadi wakati ule. Waligonga mlango wa mama yake kwa muda bila mafanikio yeyote. Nelson pamoja na mjomba walikwenda kwenye nyumba ya jirani kuulizia kama walikuwa na habari za mama yao.

“Karibuuu.” Sauti ya kike ilisikika ndani ikiwakaribisha baada ya kubisha hodi katika nyumba ya jirani.

Nelson na mjomba walijieleza kwa jirani yule ambae Nelson alifahamiana nae kipindi ambacho alikuwa anajenga ile nyumba kwaajili ya mama yake. Kilichowasikitisha zaidi pamoja na kuongeza mashaka makubwa ndani ya mioyo yao ni maelezo ambayo walielezwa na huyo jirani wa mama Nelson.

“Kiukweli huyu mama tangu jumapili hatujamwona. Kwa mawazo ya harakaharaka tukafikiri labda alipata safari ya ghafla iliyopelekea hadi akasahau kuzima taa za nje.” Jirani alizungumza.

“Kwahiyo zile taa za nje zilikuwa zinawaka tangu jumapili?” Mjomba aliuliza kwasababu Nelson alihisi kuishiwa nguvu ghafla kutokana na maelezo aliyoyasikia kutoka kwa mama Kitomari.

Nelson na mjomba walipata wazo la kwenda kupasuka kioo cha chumba alichokuwa analala mama yake ili waweze kuchungulia ndani. Mjomba alichukua jiwe kubwa na kubamiza katika kioo cha chumba cha dada yake na kukisarambatisha. Kitendo cha kioo kupasuka kilisababisha ile harufu mbaya waliyokuwa wanaivuta tangu walipofika pale nyumbani kuongezeka kwa kiasi kikubwa ,ambayo ilipelekea wazibe pua zao kwa vidole. Baada ya pazia kusukumwa pembeni Nelson pamoja na mjomba walirefusha shingo zao na kuchungulia ndani ya chumba na kuuona mwili wa mama Nelson ukiwa umelala chali kitandani huku ukiwa umevimba sana.

Kwa mwonekano na harufu kali iliyokuwa inatoka chumbani mle iliashiria kwamba mama huyo tayari alikuwa ni marehemu. Nelson alianza kuangua kilio kisichokuwa na mfano. Kilio cha Nelson kilisababisha majirani wamiminike kwa wingi pale nyumbani kwa mama yake. Majirani waliingia kibarua cha kuanza kumbembeleza Nelson ambaye alikuwa akimwaga machozi kwa masikitiko makubwa. Mjomba alijitahidi kujikaza kiume lakini nae alishindwa na kujikuta akiangua kilio vilevile. Muda huohuo simu ilipigwa katika kituo kidogo cha polisi kilichopo maeneo ya Ngulelo. Ndani ya muda mfupi gari la jeshi la polisi lilifika katika eneo la tukio na kukuta umati mkubwa wa watu ukiwa umekusanyika katika nyumba ya mama Nelson. Polisi walivunja mlango na kuutoa mwili kisha kuupeleka mwochwari. Msiba uliwekwa nyumbani kwa Nelson.

Kiukweli Nelson alikonda ghafla, kutokana na pengo kubwa alilolipata katika maisha yake. Hakutegemea mama yake atamuacha mapema kiasi kile katika dunia hii iliyojaa shida nyingi na mateso. Alitamani laiti baba yake angekuwa na ushirikiano mzuri na yeye pengine ingemfariji angalau kidogo. Vivian alionekana kusikitika sana alipopata taharifa za kifo cha mama mkwe wake. Alilia sana lakini machozi yake yalikuwa ni ya kinafiki kwasababu yeye ndiye alifanya mauwaji hayo. Nelson alilia hadi machozi yakamkauka. Wakati mwingine fahamu zilikuwa zinampotea Nelson kwasababu ya kulia sana. Ingawa watu wengi walijitahidi kumfariji na kumtaka ajikaze kiume lakini aliona hawakuwa wakifahamu machungu makubwa yaliyopo ndani ya mtima wake.

Kifo cha mama yake kilikwenda kutonesha majeraha makubwa yaliyokuwa ndani ya moyo wake ya kupotelewa na watoto wake wawili katika kipindi kifupi kilichokuwa kimepita. Mipango ya mazishi ilipangwa. Maafikiano yalifanyika kwamba mama huyo atakwenda kuzikwa katika makaburi ya nyumbani kwao mkoa wa Kilimanjaro.

Kwasababu mwili ulikuwa umeshaharibika sana siku ya tatu safari ya kusafirisha maiti kutokea mkoa wa Arusha kwenda mkoa wa jirani ilianza mapema saa kumi na mbili. Ndugu jamaa na marafiki walijitokeza kuusindikiza mwili kwenda mkoa wa jirani. Kosta nne zilikodiwa kwaajili ya kubeba watu waliojitokeza kuisindikiza familia ya Nelson kwenda mazikoni.

***********

Usiku wa kuamkia siku ya safari kulifanyika kikao kikubwa na cha muda mrefu kuzimu. Vivian aliagizwa kusababisha ajali ambayo itamuuwa mtumishi wa Mungu mchungaji Eugin Alivin ambaye kesho yake atakuwa katika msafara wa kwenda mazikoni. Mchungaji huyo amekuwa akiharibu vikao vingi vilivyokuwa vikifanyika kuzimu mara kwa mara kwa njia ya maombi. Malikia aliona endapo mchungaji huyo atauwawa basi wataishi kwa amani sana. Malikia alimuahidi Vivian kumpandisha cheo maradufu endapo atafanikiwa kutekeleza zoezi hilo gumu. Vivian alikubali kuitoa roho ya mchungaji wakati watakapokuwa safarini kurejea arusha kutoka kwenye mazishi mkoa wa Kilimanjaro.

***********

Marafiki wengi wa Nelson pamoja na wa mjomba waliamua kuunga msafara kwa magari yao binafsi kuelekea katika shughuli ya maziko. Magari yaliyokuwa katika msafara yalitembea kwa mwendo wa taratibu, kiasi kwamba wakati mwingine katika baadhi ya maeneo palitokea msongamano mkubwa wa magari. Watu wengi walibahatika kuuona msafara ule uliokuwa unausindikiza mwili kwenda kuzikwa walishikwa na butwaa kwasababu hawakuwahi kuona msafara mkubwa wa magari kama ule wa siku ile. Nelson alikwa mtu wa watu ndio maana watu wengi walionekana kumpenda. Mvua ilikuwa ikinyesha sana. Ilisababisha asubuhi ionekane kama vile jioni kwasababu wingu lilikuwa limefunga sana.

kila mtu alionekana kuvalia makoti makubwa kwasababu hali ilikuwa ni ya ubaridi sana siku ile ingawa kipindi cha baridi kilikuwa kimeshapita. Wakinamama walijitanda kanga tatu tatu kutokana na baridi kali iliyokuwepo siku hiyo. Kila mtu alikuwa aking’ata meno kutokana na baridi ilivyokuwa ikipenyeza katika ngozi ya miili yao. Kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inazidi kunyesha ilisababisha msafara uzidi kwenda kwa mwendo wa taratibu sana. Vivian alikuwa katika gari moja ambayo ilikuwa imebeba watu wa familia.

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi

Chapisha Maoni