BABA KIUMBE WA AJABU (14)

Zephiline F Ezekiel
Mtunzi: Ally Mbetu

SEHEMU YA KUMI NA NNE
TULIPOISHIA...
Niliamini ndoto ile iliashilia kifo cha baba lakini kubadilika kwa umbile la ajabu lilikuwa likiashiria nini?

Lakini sikutaka kuamini moja kwa moja kutokana na kauli ya mganga kuwa baba yangu atakufa kama nikikutana kimwili na mpenzi wangu na sharti lile nililitekeleza.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

SASA TUENDELEE...
Niliamini huenda ile ni ndoto ya kawaida tu wala haihusiani na ukweli wowote, kutokana na kutoelezwa chochote na mganga juu ya kupata ndoto yenye kiashirio.

“Vipi Masalu?” Sauti ya mpenzi wangu ilinishtua nikiwa katikati ya dimbwi la mawazo.

“Aah… safi tu,” nilijibu huku nikijitahidi kuficha kilicho moyoni mwangu.

“Safi, mbona umeamka na kukuona ukitupa mikono kama unazungumza na mtu kuna kitu gani kimekusibu?”

“Mmh! Kweli nimeona ndoto moja imenitisha sana.”

“Ndoto gani?”

“Nimeota nyumbani ndugu zangu wanalia baba akiwa amelala kitandani, lakini kitu cha ajabu amegeuka kiumbe cha ajabu chenye kutisha.”

“Sasa wasiwasi wako nini? hiyo si ndoto tu?”

“Huenda baba amekufa.”

“Masalu si ulielezwa atakufa kama tukikutana kimwili?”

“Ndiyo, hata mimi nashangaa.”

“Kwani mganga alikueleza nini juu ya njozi utakayoota?”

“Hakunieleza chochote.”

“Sasa wasiwasi wako nini?”

“Kwa vile baba hali yake ilikuwa mbaya, ndoto hii imenitisha sana.”

“Masalu acha kujitia presha bure, maisha ya baba yako yako mikononi mwako.”

“Mmh! Sawa, lakini niliingiwa na wasiwasi mkubwa.”

“Lala mpenzi.”

“Nashukuru kwa kunipa moyo.”

“Nipo hapa kwa ajili hiyo.”

“Asante mpenzi wangu kwa kunijali sina cha kukulipa.”

“Cha kunilipa baada ya kupona ni ndoa tu.”

“Omba jingine hilo umepata. ”

Niliagana na mpenzi wangu kila mmoja alilala, usingizi haukuchelewa kunichukua, haikuchukua muda mrefu njozi ilijirudia, tena safari hii niliwasikia wakilia huku wakitupia shutuma zao kwangu kuwa mimi ndiye chanzo cha kifo cha baba.

Nilishtuka tena kitandani na kuwasha taa, mpenzi wangu naye alishtuka na kuhoji kwa nini nimeamka tena.

“Masalu, vipi mpenzi wangu?”

“Mmh!” niliguna tu.

“Mbona sikuelewi?”

“Mmh! Ndoto bado inaning’ang’ania.”

“Umeota nini tena?”

“Bado kifo cha baba kinaendelea na safari hii nimewasikia mama na ndugu zangu wakinishutumu ndiye niliyesababisha.”

“Lakini bado itakuwa ni njozi tu kwa vile mawazo yako yote umeyahamishia huko.”

“Kwa hiyo nifanyeje?”

“Hebu iache njozi iishe wala usiamke.”

“Mmh! Ngoja nijaribu.”

Nilirudi kulala tena, ajabu nililala mpaka asubuhi bila kuota tena, mpenzi wangu ndiye aliyeniamsha.

“Masalu.”

“Naam.”

“Vipi upo sawa?” 

“Nipo sawa, vipi?” 

“Naona leo umelala sana.”

“Kwa muda huu ni saa ngapi?”

“Mmh! Ni saa tatu na nusu.”

“Ooh! Leo nimelala sana.”

“Inawezekana ni kutokana na kuamkaamka usiku kutokana na njozi ulizoota.”

“Na kweli.”

“Vipi uliota tena?”

“Sikuota, nimelala vizuri.”

“Unaona wasiwasi wako tu, njozi zingine hutokana  na mawazo ya mtu.”

“Ni kweli, lakini ziliniweka kwenye hali mbaya kwa vile kama kweli baba atakufa ndugu zangu hawatanielewa.”

“Wasikuelewe vipi?”

“Si nitaonekana mimi ndiye niliyemuua.”

“Masalu acha kujitoa akili, ulikwenda sehemu gani kumroga baba yako?”

“Sijaenda popote.”

“Sasa?”

“Si inaonesha kuwa uchawi umewarudia.”

“Hukuwaroga?”

“Ndiyo.”

“Sasa wewe unaogopa nini?”

“Mmh! Suala la kuua si la kawaida.”

“Wangekuua wewe lingekuwa la kawaida au umefurahia kuuawa kwa dada yako Monika?”

“Swali gani hilo, hujui nilivyoumizwa na kifo cha dada yangu?”

“Sasa inakuwaje unaogopa vifo vya watu mnajua kabisa hawana nia nzuri na wewe?”

“Basi tuachane na hayo, tuoge tukapate chai.”

Niliamka kitandani na kwenda kuoga, baada ya kuoga tulikwenda kupata kifungua kinywa kilichokuwa mlemle kwenye hoteli tuliyokuwa tumepanga. 

Wiki ilikatika tukiwa tumejificha na mpenzi wangu, hata simu niliamua kuizima ili kuondoa usumbufu wa ndugu zangu. Siku moja asubuhi tukiwa mgahawani tukipata kifungua kinywa niliamua kuwasha simu. Utafikiri kuna mtu alikuwa akisubiri kwa hamu nilipowasha tu simu iliingia. Kuangalia ilionesha namba ya kaka yangu, niliiangalia kwa muda bila kupokea mpaka ikakatika. Haikupita muda simu iliita tena alikuwa dada nayo niliiangalia bila kuipokea.

“Masalu mbona hupokei simu?”

“Achana nao.”

“Kina nani?”

“Si hawa wapuuzi.”

“Ndugu zako?”

“Ndiyo.”

“Hebu pokea uwasikilize kwa vile hujui wanataka nini?”

“Achana nao najua wanataka kunijua nilivyo.”

“Masalu si umeambiwa kuwa sasa hivi mtu hakusogelei, wasiwasi wako nini?”

“Sina wasiwasi ila sipendi kuwasikiliza kwa vile hakuna jipya la kuniambia.”

“Wasikilize.”

“Sitaki, wale sio watu siwezi kuwasikiliza watu wabaya kama wale.”

Mara simu ya mpenzi wangu iliita aliipokea na kuzungumza.

“Eeeh...Ndiyo...Shikamoo mama...Ndiyo...Hapana...Lini?..... Leo...Sawa nitamwambia....nitakujulisha....Hapana tupo Mwanza...Sawa mama nitamwambia....Haya mama.”

Baada ya kukata simu alinigeukia na kunitazama kwa muda.

“Vipi kuna usalama?”

“Kiasi.”

“Kuna tatizo nyumbani kwenu?”

“Hapana, kwenu.”

“Kwetu kuna tatizo gani?” nilishtuka.

“Ndoto yako imekuwa na ukweli.”

“Ina maana baba amefariki?”

“Ndiyo, inaonekana hata ndugu zako walikuwa wakikutafuta kukupa taarifa.”

“Mmh! Sasa itakuwaje?”

“Mmh! Kazi ipo nataka nikueleze kitu kimoja kabla ya kufanya lolote turudi kwanza kwa mganga.”

“Kweli hilo wazo zuri. “

“Vipi mbona unanyanyuka?”

“Mambo yameharibika, japo alinitenda vibaya lakini kifo cha baba yangu kimeniuma sana.”

“Utafanyaje imeshatokea!”

“Lakini mganga si alisema mpaka tukikutana kimwili! Sasa imekuwaje?”

“Ndiyo maana nikasema twende kwanza tukamuulize kabla hatujafanya lolote.”

“Naona tusipoteze wakati.”

“Subiri basi tumalize kunywa chai.”

“Chai haipandi tena,” nilisema huku nikinyanyuka kwenye kiti.

“Pole mpenzi wangu.”

“Bado sijapoa, kifo cha baba kimeniuma sana,” nilijikuta nikidondokwa na machozi.

“Pole mpenzi,“ mpenzi wangu alinisogelea na kunibembeleza, kitu kile kiliniongeza uchungu moyoni na kuangua kilio cha sauti kilichowashangaza waliokuwepo hotelini. Ilibidi mpenzi wangu anipeleke chumbani.  

                                                               *****

Nilipofika hotelini niliendelea kulia kwa sauti ya chini huku mpenzi wangu akiendelea kunibembeleza. Pamoja na yote niliyotendewa na baba, lakini kifo chake kiliniuma sana. Niliweka pembeni ubaya wake na kuyakumbuka mapenzi yake kwangu kipindi chote cha kukua kwangu.

Nilijua kilichomponza baba yangu ni tamaa ya mali ambayo masharti yake yaliiathiri familia yetu. Nikiwa bado nimeinama nikiendelea kumlilia baba yangu, mpenzi wangu aliniuliza:

“Kwa hiyo utakwenda kwenye msiba?”

“Hata sijui nifanye nini?”

“Lakini jambo hili ni zito si la kukurupuka.”

“Ni kweli, najua kabisa kifo cha baba ndugu zangu wanajua mimi ndiye mhusika mkuu. Unafikiri nikienda itakuwaje kama siyo kutiana aibu msibani?”

“Lakini kwa nini tusirudi kwa mganga ili atueleze tufanye nini?”

“Lakini si mganga alisema mpaka tukutane kimwili, sasa nini kilichomuua baba yangu?”

“Masalu swali hilo mimi siwezi kukujibu.”

“Basi twende kwa huyo mganga.”

Tulikubaliana kwenda kwa mganga kumpa taarifa ya kifo cha baba, tulipofika tulikuta watu wengi, hivyo ilitupasa kusubiri zamu yetu japo niliamini itatuchukua muda mrefu kuonana na mganga. Hatukuwa na budi kusubiri, lakini mganga alipita na mgonjwa akienda naye nyuma ya nyumba, nilijua anakwenda kumfanyia matibabu.

Baada ya dakika kama ishirini alirudi peke yake na kuniona, alionesha ishara ya kuniita. Nilinyanyuka na kumfuata ndani ya kilinge cha kutibia, baada ya kukaa alisema:

“Vipi, mbona umerudi mapema?”

“Baba amefariki jana.”

“Sasa tatizo nini?”

 Swali la mganga lilinishangaza, baba yangu amefariki yeye haoni tatizo.                 

“Si ulisema mpaka tukutane kimwili ndipo baba angefariki, au hata kulala chumba kimoja?”

“Masalu sijakueleza hivyo kuwa muelewa, nilikueleza mpaka mkutane kimwili si kulala chumba kimoja.”

“Sasa kifo cha baba yangu kinatokana na nini?”

“Kwa amri ya Mungu.”

“Si ulisema mpaka tukutane kimwili?”

“Eeh, lakini na Mungu ana nafasi yake, huamini kuna kifo?”

“Naamini.”

“Sasa?”

“Lakini ndugu zangu waliniomba niokoe hali ya baba, kama amekufa bila mimi kufika si nitaonekana ndiye niliyechangia.”

“Huo ni wasiwasi wako, baba yako amejiua mwenyewe kwa msaada wa ndugu zako.”

“Una maana gani kusema hivyo?”

“Baada ya kushindwa kukudhuru walijaribu uchawi mmoja ambao ni mbaya kuliko kitu chochote. Ule ukifanyiwa huchukui muda lazima ufe, baada ya kuonekana hujali na unajiamini waliamua jambo moja, kukufutilia mbali. Kama si kinga niliyokufanyia sasa hivi ungebaki jina.”

“Ni uchawi gani?” Kauli ya mganga ilinitisha.

“Kweli ndugu zako wamekupania vibaya, uchawi uliofanywa ni wa kinyonga, anakamatwa kinyonga mzima anapasuliwa na kuchunwa ngozi. Kisha ngozi yake inawambwa na kupakwa dawa huku likinuizwa jina lako. Ngozi ikikauka na wewe uhai huna.”

“Du!” Nilishtuka.

“Ndiyo walivyofanya, kazi hiyo ilifanywa saa sita usiku ili asubuhi ukiamka ukutwe umekufa. Baada ya kutega uchawi wao walikwenda kulala huku mganga akiwahakikishia kuwa asubuhi wakiamka watasikia habari za kifo chako.

“Lakini ilikuwa tofauti na walivyo fikiria, kinga niliyokuwekea ilifanya kazi, nilikueleza kila watakachokufanyia kitawarudia. Uchawi uliotaka kukuua ndiyo uliomuua baba yako. Ndio maana nilikuambia kifo cha baba yako alijitakia mwenyewe akishirikiana na ndugu zako.”

“Unataka kuniambia bila kinga nisingeiona leo?”

“Hilo ni jibu uliza swali.”

“Kuhusu kwenda msibani itakuwaje?”

“Ukitaka nenda hawawezi kukufanya lolote.”

“Hatuwezi kutiana aibu kuwa mimi ndiye niliyemuua baba?”

“Wataanzia wapi, kwa kitendo walichokitenda jana usiku na leo kukuona hai wamezidi kuchanganyikiwa. Kama wangejua kama ni mimi ndiye niliyekukinga, basi wangenipa pesa nyingi ili wakupoteze.”

“Kuna umuhimu wa kuongeza kinga mwilini maana kama kinyonga kashindwa lazima wataendelea kutafuta kitu kingine,” nilijikuta nikijihami baada ya kuona vita iliyopo mbele na ndugu zangu ni nzito.

“Kijana kama kinyonga ameshindwa hakuna kitu chochote kitaweza japo kwa dawa yangu walikuwa wakijisumbua, uchawi ule ni mbaya sana.”

“Kwa hiyo unaniambiaje?”

“Ondoa wasiwasi, chochote kitakachokupata si mkono wa mtu bali amri ya Mungu.”

“Nashukuru mzee wangu.”

“Basi ondoa hofu hakuna chochote kitakachokukuta, kila atakayekugusa kitamrudia.”

Niliagana na mganga kisha nilimpitia mpenzi wangu na kurudi hotelini kujiandaa na kwenda msibani.

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni