
Mtunzi: Ally Mbetu
SEHEMU YA KUMI NA SITA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
“Japo unakuhusu lakini mazingira yake hayakuwa mazuri.”
“Yawe mazuri vipi ikiwa aliyekufa ni mzazi wangu?”
“Sawa mzazi wako lakini unajua kifo chake kilitokana na nini, Na dada yako baada ya kifo cha baba yenu maneno aliyokuambia,
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
SASA TUENDELEE...
sasa nini kigeni kwako?”
“Nimekuelewa, lakini watanitambua.”
“Masalu jambo hili linahitaji utulivu, nakuomba tuondoke hapa twende sehemu yoyote ili upate utulivu wa moyo.”
“Nashukuru kwa kunipa moyo na kuwa mtu wangu muhimu.”
“Najua upo katika kipindi kigumu hivyo nahitaji kuwa karibu yako na kuhakikisha hupati mawazo mabaya. Nina imani utavuka kipindi hiki kigumu.”
“Nashukuru sana, sasa tutakwenda wapi?”
“Twende Musoma au Shinyanga.”
“Mi nafikiri Musoma panafaa.”
“Vipi kuhusu duka linaendelea?”
“Hata najua.”
Kwa kweli nilijibu nikiwa sijui nini kinaendelea, muda mwingi nilifikiria maisha yangu kuliko biashara kilichokuwa kikinisaidia ni pesa kidogo zilizokuwa kwenye akiba yangu pia mpenzi wangu naye alichangia kwa kiasi kikubwa kutokana na uwezo wa familia yake.
“Nakuomba kitu kimoja, funga duka kisha tuondoke, na msiba ukiisha usifanye biashara yoyote bila kumshirikisha yule babu. Si alikuambia biashara zenu zinaendeshwa na kidonda chako na maiti ya dada na mtoto wa dada yako?”
“Na kweli basi nitampigia simu anayetunza funguo za duka ili asilifungue tena.”
“Sio alifungue anaweza kuombwa funguo na dada zako na kufanya jambo lolote dukani kwako wale sasa si ndugu bali maadui zako.”
“Na kweli wacha nimwambie aniletee funguo kabisa.”
“Hilo ndilo jambo muhimu.”
Nilimpigia simu anayetunza funguo za duka ili asifungue pia aniletee funguo. Alikubali ataniletea baada ya kutoka msibani, lakini nilimuomba aniletee muda ule, alikubali na kuniahidi kuniletea baada ya muda mfupi. Tulikubaliana na mwenzangu baada ya kupata funguo za duka tuondoke mchana ule kwenda Musoma.
Kwa vile safari ilikuwa ya kuchukua hata wiki mpenzi wangu alirudi kwao kuchukua nguo za kuvaa na kuniacha nikijiandaa. Muuzaji wangu aliniletea funguo na kushangaa kuniona nipo nyumbani badala ya msibani.
“Bosi mbona haupo msibani?”
“Nitakuja baadaye.”
“Sawa lakini nimeacha maandalizi ya mwisho kwenda kuzika.”
“Nakuja muda si mrefu.”
“Haya wacha niwahi.”
Tuliagana na kuniacha nikimsubiri mpenzi wangu ambaye alikuja baada muda si mrefu. Tuliongozana hadi Buzuruga na kukata tiketi ya basi la Musoma, tulifika Musoma jioni na kupanga tatika Hoteli ya Orange Tree iliyokuwa ipo katika hali nzuri, tulipanga pale kwa wiki nzima nikiwa nimezima simu ili kujiepusha na maneno ya ndugu zangu.
Kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu kuogopa kufanya mapenzi na mpenzi wangu nikihofia kusababisha kifo cha baba tuliweza kufanya mapenzi bila hofu ya kila kitu huku mpenzi wangu akifurahia starehe ya siku ile huku akiniahidi nifanye haraka kumuoa.
Nilimuahidi kufanya vile baada ya matatizo kutulia kwa kuonesha mapenzi ya dhati kwangu kipindi chote cha matatizo. Kipindi nilichopitia kama mwanamke asiye na mapenzi ya dhati lazima angenikimbia lakini wa kwangu hakunikimbia zaidi ya kunipa moyo.
Baada ya wiki tulirudi Mwanza na kwenda moja kwa moja kwa mganga, baada ya kuniona alinieleza hali ilivyokuwa juu ya mipango ya ndugu zangu.
“Kijana japo ndugu zako walijaribu kutaka kukuangamiza lakini matokeo yao ni kufilisika kwa kasi ya ajabu, aibu itakayowakuta juu yako watakuja kukuomba msamaha. Ulichokifanya ni kitu cha busara sana kama ulivyonieleza mawazo yote kakupa mpenzi wako nina imani hiki ni kipindi cha kukaa pamoja na kupanga maisha yenu.
“Kuhusu duka nilitalifanyia zindiko kuhakikisha ndagu ya familia haikupati, na kazi hii itafanyika usiku huu. Tutaondoka pamoja hadi kwenye duka lako tutaingia ndani na kuua uchawi ambao ungeweza kupoteza mali yako yote iliyo humo ndani.”
Nilikubaliana na mganga usiku nimfuate na gari, nilimueleza mwenzangu na kurudi kwenye hoteli yetu. Majira ya saa tano usiku tulimfuata na kwenda moja kwa moja kwenye duka, alifanya zindiko lake kisha tulifungua duka, alifanya dawa zake kisha tulimrudisha na sisi kurudi hotelini kulala mpaka siku ya pili.
Tangu siku ile niliendelea na biashara zangu kama kawaida huku sehemu kubwa ya mambo yangu nikiwashirikisha marafiki zangu na upande wa mpenzi wangu ambao waliahidi kunisimamia katika mambo yangu yote.
Nilishukuru Mungu biashara zangu zilikwenda vizuri tofauti na ndugu zangu ambao walianguka anguko la aibu. Sikuwaonea huruma kwa vile hawakuwa watu wema kwangu. Pamoja na ubaya wao wote taarifa za kufilisika kwa haraka sikuzifurahia.
Dada mkubwa alianza kuchanganyikiwa na kutembea akizungumza peke yake, watu wa karibu waliniomba niinusuru aibu ya familia. Katika mtu aliyeniuma alikuwa mama yangu mzazi ambaye siku zote aliona aibu kwa niliyotendewa na baba na ndugu zangu na yeye kukaa kimya.
Nilijiuliza nikimfuata nyumbani na kuwakuta na ndugu zangu ambao walinigeuza mchawi itakuwaje? Taarifa za kusikitisha zilisema sehemu kubwa za maduka zimefilisika na wafanyakazi wengine wamekimbia na pesa baada ya malimbikizo ya mshahara.
****
Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya kushindwa kulipa mikopo mikubwa ya benki kufikia hatua ya kufilisiwa vitu vyao kwa kupigwa mnada zikiwemo nyumba na magari. Ilibidi ndugu zangu warudi kuishi nyumba ya wazazi ambayo siku zote haikufanyiwa ukarabati. Kila aliyenielezea anguko la familia yangu huku wakiishi maisha ya kubahatisha aliniomba niinusuru kutokana na maisha yangu kuwa na uafadhali mkubwa.
Taarifa za utajiri wa ndagu zilisambaa kila kona kama moto kwenye majani makavu ambao uliipaka matope mazito familia yetu. Kilichowashangaza watu wengi ni anguko la familia yangu lakini upande wangu mambo yaliendelea kuninyookea.
Niliamua kumchukua mama yangu na kukaa naye, kila tulipokuwa wawili mama alitumia muda mwingi kuniomba msamaha kutokana na yote waliyonitendea. Nilimueleza mama sitaweza kumlaumu ila sitawasamehe ndugu zangu.
“Mwanangu Masalu nakuomba nipo chini ya miguu yako wasamehe ndugu zako, hali yao ni mbaya sana.”
“Mama siwezi kuwasamehe mpaka nakufa.”
“Nakuomba nipo chini ya miguu yako tunaadhirika.”
“Mama kama ningekufa angewasamehe nani?”
“Ni kweli walikuwa na dhamira mbaya kwako lakini ilikuwa ni shinikizo la baba yako.”
Pamoja na mama kunibembeleza sikuwa tayari kuwasamehe ndugu zangu, muda ulikatika huku nikiendelea na maisha yangu huku nikiishi nyumba moja na mpenzi wangu Mary, baada ya mama kuwepo pale nilipanga mipango ya ndoa kwa kuamini msimamizi yupo.
Siku moja nikiwa mjini nilishtuka kumuona dada yangu akiwa nusu uchi huku akiomba kwa watu, muonekano wake alionekana mtu aliyerukwa na akili. Nilipatwa na mshtuko wa ajabu na moyo kuniuma, nilibakia nikimtazama kwa muda huku machozi yakinitoka.
Kwa vile nilikuwa ndani ya gari nililipaki gari pembeni na kujikuta nikilia kwa uchungu huku nikisikia sauti ya mama kuwa niwasamehe ndugu zangu. Taratibu donge la kisasi liliyeyuka moyoni mwangu na kuamua kusikiliza kilio cha mama yangu juu ya ndugu zangu. Lakini sikuwa na jibu la moja kwa moja, niligeuza gari na kwenda kwa mganga Pasiansi kuulizia kama nitaweza kuwasaidia ndugu zangu.
Nilipofika kwa mganga nilikuta watu wengi kama kawaida, aliponiona pamoja na kuwa na watu wengi kwa vile alinizoea alinipa upendeleo. Nilipofika aliniuliza:
“Vipi una shida gani?”
Nilimweleza ombi la mama kuwasamehe ndugu zangu na hali ya dada yangu, baada ya kunisikiliza kwa kina mganga alisema:
“Nimekuelewa, hakuna tatizo lolote kama wewe utakubali kuwasamehe ndugu zako.”
“Na kuhusu dada yangu?”
“Alichotaka kukufanyia ndicho kilichomrudia lakini kama umemsamehe kazi ya kumtibu si ngumu.”
“Nimemsamehe kwa vile kisu kimegusa mfupa.”
“Basi mleteni hapa apate tiba.”
Baada ya makubaliano na mganga nilirudi nyumbani na kumueleza mama kuwa nipo tayari kuwasamehe ndugu zangu na kumtibu dada, mama alifurahi sana. Niliwatuma watu wamkamate dada ambaye nilimpeleka kwa mganga, kutokana na tatizo lake alikaa wiki moja na kurudi katika hali ya kawaida. Baada ya kupona mama alimueleza kuwa mimi ndiye niliyemsaidia baada ya kuugua wendawazimu.
Nilimueleza mama akimtoa kwa mganga amrudishe nyumbani kwangu, jioni niliporudi nyumbani nilimkuta na mama wamekaa sebuleni wakitazama runinga. Aliponiona naingia alinikimbilia na kunipigia magoti kuniomba msamaha.
Nilimuwahi kumnyanyua na kumweleza yaliyopita yamepita ni wakati mwingine wa kujipanga upya na kujenga familia iliyo imara. Maneno yangu yalimliza dada yangu na kujikuta akisema:
“Sasa tungekuuwa tungepata faida gani, nani angetusaidia kama hivi?”
“Dada yamekwisha naomba ya zamani tuyasahau.”
”Ni kweli kaka lakini ulichonifanyia Mungu pekee atakulipa.”
“Amina.”
Baada ya kumrudisha dada nilifanya utaratibu wa kuwakusanya ndugu zangu, baada kuwakusanya. Tulikaa kikao cha kifamilia kuondoa tofauti zetu huku ndugu zangu wakitokwa na machozi kwa yote waliyoyafanya. Nilimshukuru Mungu kuturudisha katika mapenzi ya awali nami niliwaheshimu kama ndugu zangu japo hawakuwa na kitu. Nilijitahidi kuhakikisha kila ndugu yangu anakuwa na maisha mazuri baada ya Mungu kuniangazia mafanikio.
Leo hii ninavyomalizia kutoa ushuhuda huu, kila ndugu yangu ana duka lake japo si kubwa kama enzi za baba la kutumia ndagu ya kidonda. Lakini maisha yaliendelea huku tukimalizia siku zote za maisha kurudi kwa Mungu ili atuongoze na kutuepusha na maisha machafu.
Maisha sasa hivi ni mazuri huku Mary akiwa mke wangu wa ndoa, japo inauma baada ya mama yangu kufariki miezi minne baada ya ndoa yangu. Nitaendelea kumuombea mama yangu kipenzi Mungu ampe mapumziko ya milele. Pia baba yangu japo alikuwa chanzo cha matatizo kwenye familia.
Naamini Mungu ni mwenye huruma hivyo atamsamehe kwa kujua udhaifu wa sisi wanadamu. Namalizia kwa kuwaomba wote tumtangulize Mungu kwa kila kitu ili tusiishi maisha ya mashaka kwa kuwategemea miungu watu. Mungu anatupenda tumtegemee yeye siku zote.
MWISHO
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi