
Mtunzi: Ally Mbetu
SEHEMU YA TATU
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
“Walianza upelelezi wa chinichini na kumjua mpenzi wangu ambaye walimbana kwa kumpeleka polisi ili awajulishe nilipo. Mwanzo aligoma kutokana na masharti niliyompa kama wazazi wangu watamuona asikubali. Mpango wetu ulikuwa kuishi pamoja nami nilitaka yeye asirudi tena kule.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
SASA TUENDELEE...
“Lakini kwa vile familia yake ipo kule walifanikiwa kumpata na baada ya kumbana sana aliwaleta hapa. Kama utakumbuka siku waliyokusanyana kuja kwangu ilikuwa baada ya kumtuma mtu kwa siri bila kujua ninapofanyia kazi zangu na kuamua kukusanyana kuja hapa ili nikubali kurudi nyumbani.
“Basi walipofika kila mmoja ooh, Monika umefanya vibaya kuondoka nyumbani wakati unafahamu kila kitu. Niliwaeleza siwezi kuumia mimi wakati wenyewe wanakula maisha, kama hivyo basi kidonda changu achukue mtu mwingine. Hakuna aliyekuwa tayari kuchukua ugonjwa wangu.
“Nilijua mkuki kwa nguruwe ila kwa binadamu mchungu, mwisho wa yote walikubali niendelee na kazi zangu kwa makubaliano nisitembee na mwanaume au kukitibu kidonda. Niliwakubalia ili kuwaridhisha kuwa nitafanya kama wanavyotaka. Lakini sikuwa tayari kukubaliana na ujinga wao tena.
“Nami nilikuwa na hamu ya kuwa na mwanaume ambaye muda ule alikuwa akija mara moja na wakati huo ndiyo alikubali kuhamia kwangu kabisa.
“Baada ya kuondoka niliendelea na mpenzi wangu ambaye muda huo nilikuwa nakaa naye nyumba moja, kupika na kupakua, sasa hivi yupo kwenye mihangaiko yake muda wake wa kurudi ni saa moja usiku. Ila jumapili huwa haendi popote.
“Tangu nihamie huku siku hizi nakwenda kanisani kama kawaida, ajabu ya Mungu kidonda kilianza kupona chenyewe bila kukiwekea dawa. Kumbe kidonda changu kilivyokuwa kikipona na mambo yalibadilika katika utajiri wa familia yetu. Matatizo yalitawala kwa maduka kuibiwa vitu vyote bila kujua tatizo ni nini.
“Kama kawaida walirudi kwa mganga na kuelezwa kuwa nimeishapona pia ninaendeleza kufanya uchafu katika mali ya familia yangu. Walijikusanya kama ilivyo kawaida na kuja kuniomba niokoe mali ya familia, niliwaeleza katu sitakubali kufanya tena ujinga ule.
“Baada ya juhudi zote kushindikana baba aliniapia mwaka huu siumalizi lazima nitakufa. Nilimhakikishia yeye si Mungu, kama kufa nitakufa kwa amri ya Mungu. Wote waliondoka vichwa chini wakiamini wanarudi katika maisha ya kawaida, tokea siku hiyo sijawaona tena na maisha yangu yanaendelea kama kawaida na muda si mrefu nawe utapata mjomba.”
“Dada una mimba?”
“Ndiyo mdogo wangu.”
“Mmh, Mungu mkubwa.”
“Basi mdogo wangu siri uliyokuwa huijui ndiyo hiyo, nasikia sasa havi mambo yote hayaendi vizuri kabisa na wamechanganyikiwa.”
“Ni kweli dada sasa hivi kila siku baba analalamika na kusema angekuwa na uwezo angekuulia mbali.”
“Sasa aniue kwa sababu gani? Kwa watoto wa mzee Makumiyane ni mimi peke yangu? Niliwaeleza mmoja ajitoe akichukue kidonda change lakini kila mmoja alikaa nyuma kukikimbia kidonda. Basi mdogo wangu nikifa leo ujue nimekufa kwa kukikataa kidonda.
“Siogopi kufa hata siku moja, kila kiumbe kitakufa! Kama nitakufa kwa kukataa kidonda nipo tayari, ila namuomba Mungu aniue baada ya kumzaa mwanangu ili niache jina langu,” dada alisema huku machozi yakimtoka, moyo wangu uliingia baridi ya woga wa ajabu kwa yote niliyoelezwa na dada juu ya siri nzito ya utajiri wetu iliyokuwa ikibebwa na kidonda cha dada.
Kingine kilichonitisha kilikuwa kusikia kuwa dada eti atakufa baada ya kukikataa kidonda. Machozi ya dada yaliniumiza sana moyo wangu na kumuonea huruma.
“Dada kwa nini usikubali kuliko kukubali kufa?”
“Masalu wewe hujui lolote katika maisha, lakini unakumbuka haya niyasemayo hata kama nikifa leo utayakumbuka maneno yangu. Kwa vile wote wameshazaa na kufanya mapenzi hawawezi kupatwa na kidonda. Wasiwasi wangu kikitoka kwangu kinaweza kurudi kwako.”
“Ha! Dada mbona unanitisha.”
“Kutokana na siri ya kidonda niliyoelezewa na baba, nakumbuka nilimuuliza kwa mfano nikifa itakuwaje? Alinieleza itabidi atafutwe aliye safi ndani ya familia. Nilimuuliza tena ni kwa mwanamke tu? Alinijibu ni kwa mtu yoyote mwanamke au mwanaume aliye msafi, unafikiri nani atakayekichukua kidonda changu kama si wewe?”
“Mimi sikubali.”
“Masalu huna jeuri ya kumbishia baba.”
“Nitahamia kwako.”
“Uhamie wapi nami umesikia lazima nitakufa?”
“Huwezi kufa dada, ni vitisho.”
“Hata nisipokufa siwezi kukukubali tena hicho kidonda kisicho na faida zaidi ya mateso.”
****
Kwa kweli sikuweza kumshawishi dada kutokana na msimamo wake mkali, jioni ilipofika niliagana na dada kwa kupanda daladala mpaka nyumbani. Nilipofika nyumbani nilikuwa na mawazo mengi juu ya maneno ya dada ambayo sikuamini kama yana ukweli wowote, nilipinga kuwa utajiri wetu si kupitia kidonda chake. Nilipoangalia hali ya maisha yetu ilikuwa ya kawaida tofauti na kauli ya dada ya kusema sasa hivi maisha ni magumu upande wa familia.
Chakula tulikula kama kawaida ambacho kwa kweli hakikuwa na hadhi ya utajiri uliotuzunguka. Lakini kwa muda ule sikushtuka kutokana maisha yale ndiyo yaliyokuwa ya kawaida ya siku zote. Japo kwa mbali nilijawa na maswali iweje nyumbani maisha yetu ya kawaida.
Kingine ambacho alikisema dada kiliniingia akilini kilikuwa kwa mama kuamka kila siku asubuhi na kwenda kulima wakati baba alikuwa na pesa nyingi. Kingine nilichokubaliana na dada ni mama kuokota kuni na kuja kupikia wakati dada zetu wanatumia majiko ya umeme na gesi.
Lakini kitu ambacho sikukubaliana naye ni imani za kishirikina kwanza maisha yetu yanategemea ushirikina wa kidonda chake. Katika akili yangu niliamini kidonda cha dada hakikuwa kimepata tiba sahihi. Lakini baada ya kupata tiba sahihi kilipona. Niliamini dada alitaka kunijengea uadui na wazazi ili niwaone ni watu wabaya wasiofaa.
Sikutaka kumuamini dada zaidi ya kuona anataka kunipotosha, lakini siri ile nilibaki nayo moyoni sikutaka kumwambia mtu. Siku zilizidi kukatika nami niliendelea na masomo kama kawaida. Pamoja na kuyapuuza ya dada na kuyaona kama ya uchonganishi lakini kuna vitu vilikuwa vikitia wasiwasi. Kuna siku nilimsikia baba akimwambia mama kwa sauti iliyoonesha hawakuniona kutokana na kiza kilichokuwepo.
“Mama Monika nimempa mpa muda mwanao wa kutosha, litakalotokea tusilaumiane.”
“Sasa mimi nitafanyaje kama mwenyewe hajihurumii.”
“Hali ni mbaya tukiendeleza huruma tutaadhirika.”
“Baba Monika mimi mwenyewe nilikwenda kwa Monika, lakini kiburi kimemjaa tena amekosa hata heshima kujua anazungumza na mama yake.”
“Mganga amenipa mwezi huu mwisho la sivyo kihame kwa mwingine.”
“Unafikiri kitaenda kwa nani?”
“Hilo suala tutalizungumza baada ya kushindikana kabisa.”
“Yaani Monika kanichanganya sana.”
“Basi uamuzi ni huo sina mwingine.”
“Utakavyokuwa mimi tena simo kayataka mwenyewe.”
Mazungumzo ya baba na mama kumhusu dada Monika yalinishtua sana na kujiuliza baba alikuwa anataka kufanya nini? Nilijiuliza au ndiyo niliyoelezwa na dada Monika juu ya kumlazimisha aendelee kuwa na kidonda na kama kikihama kitaenda kwa nani?”
Pia nilijiuliza mama alikuwa na maana gani kusema yakimkuta dada Monika hayumo ni mambo gani hayo. Nilijikuta nikiingiwa na wasiwasi wa maneno ya dada Monika kuwa baba alimtishia maisha kuwa kama akikataa kuendelea kuwa na kidonda hatadumu lazima atakufa.
Nilijikuta nikikosa raha na kutamani kwenda kumuomba dada akubali kuliko kutokewa na balaa lile. Kwa mbali nilijikuta njia panda kuamini kuwa kidonda cha dada ndicho kilikuwa kikifanya tuwe matajiri. Nilitamani nizungumze na mama kuhusu kujua baba alikusudia kufanya nini kwa dada.
Japo niliogopa kuulizwa nimejuaje, lakini nilipanga siku ya pili sitakwenda shule na kumfuata mama shambani kumuuliza kuna kitu gani dada Monika anataka kufanyiwa baada ya kukataa kuwa na kidonda kile. Usiku kwangu ulikuwa mzito sana niliota mambo mazito ambayo yalinitisha na kunifanya niamke saa nane za usiku na kukesha bila kulala.
Niliota familia yetu ikifanya sherehe kubwa huku dada Monika akiwa amekufa na mwili wake haukuwa na mguu mmoja uliokuwa ukivuja damu, ule mguu uliokuwa na kidonda. Damu ya dada Monika ndugu zetu walikuwa wakinywa kwa furaha. Niliamka na kukaa kitandani nikitweta. Nilijiuliza ndoto ile ina maana gani.
Baada ya muda usingizi ulinipitia, muda haukupita niliota ndoto nyingine mbaya, niliota nimeoza mguu sehemu ya ndani na kuanza kutoka funza, ajabu ndugu zangu walifurahia kama ndoto ya mwanzo ya kufurahia kifo cha dada Monika kwa kumla na kunywa damu yake.
*****
Nilishituka usingizini na kuogopa kulala tena mpaka asubuhi, asubuhi nilisingizia naumwa. Sikwenda shule, nilitoka ndani na kwenda kulala sebuleni ili kuogopa kuota ndoto za kutisha. Sebuleni nilipolala sikuota ndoto mpaka nilipoamka kujiandaa kwenda kwa mama shamba baada ya kufungua kinywa.
Nilioga na kufungua kinywa kisha nilielekea shambani kwa mama ili nikamuulize kuna kitu gani dada Monika anataka kufanyiwa na baba, kama kumuua ningepinga kwa nguvu zangu zote.
Nilikwenda hadi shambani na kumkuta mama akiwa katikati ya kilimo, sikumsemesha kitu, nilijiuliza iweje tuwe na pesa majumba na magari mama ateseke kiasi kile. Nilizidi kuingiwa na wasiwasi juu la mambo yaliyokuwa yakifanyika.
Baada ya muda nilimwita mama, aliponiona alishtuka na kuniuliza.
“Masalu kuna usalama?”
“Upo mama.”
“Si unaumwa, umekuja huku kufanya nini?”
”Kuna kitu nataka kuuliza mama.”
“Kitu gani?”
Mama alisema huku akiweka pembeni jembe na kunifuata nilipokuwa nimesimama.
“Masalu una nini mwanangu?”
“Mama jana nimeota ndoto mbaya sana.”
“Ndoto gani mwanangu?”
“Kuhusu dada Monika.”
“Monika! Ndoto inahusu nini?”
Nilimhadithia ndoto niliyoota, mama alishtuka na kutulia kwa muda kisha alisema kwa sauti ya chini.
“Sasa wewe wasiwasi wako nini?”
“Mama kuna maneno nilizungumza siku moja na dada Monika kuhusu baba kumtishia kifo na kunieleza kama akifa nijue baba ndiye aliyehusika.”
“Masalu!” Mama alishtuka.
“Naam mama.”
“Mlifikia wapi mpaka mkazungumza hayo?”
“Kuna siku nilikwenda kwa dada Monika na kumuuliza sababu ya yeye kuhama nyumbani. Mama dada alinieleza mambo mengi ya kutisha sana lakini sikuyaamini.”
“Masalu alikueleza mambo gani Monika?”
Nilimuhadithia baadhi ya mambo kisha nilimueleza ya yeye kulima wakati tuna pesa.
“Eti mama hata kulima kwako amesema ni imani za kishirikina iweje tuwe na pesa wewe ulime wakati ungewalipa watu wakatulimia?”
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi