BABA KIUMBE WA AJABU (5)

Zephiline F Ezekiel
Mtunzi: Ally Mbetu

SEHEMU YA TANO
TULIPOISHIA...
“Nalo hilo alilizungumzia, ila wamemtesa sana mke wangu mpaka kifo chake. Kibaya wamemuua hata mtoto wangu aliyekuwa tumboni bila kosa, yaani siamini familia yako kuna na roho mbaya kiasi hicho. Kama mtu kawapatia utajiri akisema amechoka na yeye anataka maisha yake kuna ubaya gani?”

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

SASA TUENDELEE...
Maskini shemeji yangu alizungumza huku akitokwa na machozi, nilijikuta nikitokwa na mimi machozi bila kupenda.

“Masalu familia yenu haifai, unafikiri maisha ya kuongozwa na nguvu za kishirikina mwisho wake nini? Haya sasa wamemuua Monika nani atafuata na kwa taarifa kidonda alichokikataa dada yako kitahamia kwako. Kabla ya kufa kaitaja familia yenu wote kuwa wanagombania roho yake kasoro wewe pake yako na kuonesha jinsi gani huhusiki na mateso ya mke wangu.”

“Mungu wangu!”

“Huo ndio ukweli wenyewe, hujiulizi kwa nini mama yako bado analima kama sio ushirikina, hivi baba yako hana pesa ya kuwapa watu walime na mama yako na utu uzima wake apumzike?”

“Anaweza.”

“Kama anaongeza majumba na magari kwa nini mama yako usipumzike, hebu angalia ndugu zako wakubwa. Nao wana roho ya tamaa ya mali kushindwa kumuonea huruma mama yenu. Nasikia ndani mwenu kuna chumba kisichofunguliwa, unajua kuna nini?”

“Hata sijui!”

“Kwa taarifa yako kuna maiti ya mtoto mchanga ambayo kila baada ya siku tatu hupakwa mafuta ili isiharibike.”

“Shemuuuu! Umejuaje?” Nilishtuka kusikia habari zile, chumba alichokisema kweli kilikuwepo ambacho sikuwahi kukiona kikifunguliwa.

“Dada yako Monika alikuwa na siri nzito moyoni mwake, nyingine alisema hawezi kuniambia labda ungekuwepo kabla ya kufa kwake.”

“Sasa yeye alijuaje kama kuna maiti ya mtoto?”

“Mara nyingi kazi ile aliifanya yeye, baba na mama yenu. Hakuna mtu mwingine aliyeruhusiwa kuifanya.”

“Mmh! Maiti ya mtoto wa nani?”

“Kama una kumbukumbu, nasikia mtoto wa kwanza wa dada yako ambaye ndiye aliye na pesa kuliko wote alimtoa mtoto wake kafara ili kuongeza utajiri.”

                                                                *****

Kauli ile ilinirudisha nyuma na kukumbuka miaka sita iliyopita dada mkubwa alifiwa na mwanaye lakini mazishi yake sikuyaelewa japo msiba ulikuwa nyumbani. Kingine kilichonifungua macho hakikuwa na tofauti na msiba wa Monika kilikuwa cha kifamilia tena ya ndani hata wanandugu hawakujulishwa. Taratibu nilianza kufunguka akili na kuamini kila lililosemwa na Monika lilikuwa na ukweli mkubwa.

“Asante shemu kwa kunifumbua macho,” nilimshukuru ili tuagane, nilipotaka kuondoka aliniuliza kitu.

“Masalu unataka kuniambia hukuwa na habari Monika amekufa au ulitaka kunitega akili?”

“Shemu, huwezi kuamini kila dakika nimekuwa nikichanganyikiwa juu ya taarifa za msiba wa dada Monika. Kweli niliuona mwili ukiteremshwa kwenye gari. Lakini tokea hapo sikuweza kujua nini kilichoendelea mpaka leo hii.”

“Ulipouliza walikujibu nini?”

“Sijauliza bali nilifanya upelelezi wangu, kila kona nilifika lakini sikupata kuona chochote.”

“Ulichunguza nini?”

“Sehemu za makaburi au kupata taarifa kama hajafa yupo wapi?”

“Una uhakika Monika hakuzikwa?”

“Nina uhakika.”

“Basi kuna sehemu wamemuweka, isiwe naye wamemuweka kwenye hicho chumba na kumpaka mafuta?”

“Mmh! Sijui.”

“Unaweza kuingia?”

“Mmh! Nitajitahidi kuhakikisha napata ukweli.”

“Basi utakachokipata usikose kunijulisha.”

“Nakuahidi kukuletea kila kitu.”

“Haya shemu kwaheri.”

“Ya kuonana.”

Niliagana na shemu na kurudi zangu nyumbani, nilizidi kuchanganyikiwa na maneno ya pande mbili juu ya ukweli juu ya kifo cha dada Monika. Moyoni niliapa nikipata muda lazima mama ataniambia ukweli.

Siku zilikatika bila kujua taarifa za uhakika kuhusiana na habari tata juu ya kifo cha dada Monika ni kweli amekufa? Kitu ambacho moyo wangu haukukubaliana nacho. Uvumilivu ulinishinda, siku moja nilimfuata mama shambani kutaka kujua ukweli wa dada Monika. Kama kawaida yangu nilidanganya naumwa.

Baada ya kuondoka na kuniacha nyumbani na mfanyakazi, majira saa nne asubuhi nilikwenda hadi shamba. Nilimkuta mama akipiga jembe kama hana akili nzuri. Moyoni nilimuonea huruma jinsi alivyohenyeka japo tuna pesa, kila dakika niliyakumbuka maneno ya dada Monika kuwa maisha yetu yanaongozwa na ushirikina.

Nilimwita mama ambaye alishtuka kuniona, niliamini kabisa alijiandaa kutokana na kumuuliza maswali mazito siku ya kwanza.

“Wee Masalu mbona huku si unaumwa?”

“Kidogo nimepata nafuu.”

“Haya ulikuwa unasemaje?”

“Kuna kitu mama kinanisumbua kila siku naomba msaada wako kwani naweza kuwa chizi.”

“Wee mwana mbona una mambo kuna nini tena?”

Mama alisema huku akiweka jembe pembeni na kunifuata nilipokuwa nimesimama.

“Masalu kuna nini tena?” Mama aliniuliza huku akifuta jasho kwenye paji la uso kwa mkono.

“Mama toka kifo cha dada Monika kuna mambo yamekuwa yakinichanganya na kunifanya kila siku nisijielewe.”

“Masalu mambo gani tena mwanangu kila siku huishi vioja?”

“Kuhusu dada Monika.”

“Monika kafanya nini tena?”

“Mama ni kweli dada Monika amefariki?”

”Masalu wewe si mtoto mdogo sasa, kila mtu anajua Monika amefariki wewe ukiwemo.”

“Mamaa, kama dada Monika amefariki mbona sikuona mazishi wala kaburi lake.”

“Masalu uyaone hayo ili yakusaidie nini?”

“Mama unajua majirani wanatusema vibaya toka taarifa za kifo cha dada Monika.”

“Nani aliwaambia Monika amekufa?”

“Mamaa, kwani kifo cha dada Monika kilikuwa cha siri?”

“Hata kama sio cha siri sio lazima wajue.”

“Hivi mama watu wakiniuliza dada Monika yupo wapi mimi niwajibu nini?”

“Wanyamazie usiwajibu chochote.”

“Lakini mama, kumbe hata yule shemeji aliyekuwa anakaa na dada Monika mlimfukuza asihudhurie mazishi?”

“Ahudhurie ametoa kiasi gani cha pesa kwa dada yako, zaidi ya kutuchanganya kifamilia?”

“Lakini mama tuachane na hayo, kaburi la babu na bibi nalifahamu, kaburi la kaka mkubwa nalifahamu. Makaburi yote yanayotuhusu nayafahamu na kila mwisho wa mwaka huenda kuyazuru familia yote na pia huenda kila mwezi kusafisha na kuyaweka katika hali ya usafi. Lakini kaburi la dada Monika lipo wapi, japo sikuhudhuria mazishi yake?”

“Masalu, wee mtoto mdogo hujui lolote, elewa kuwa dada yako Monika amefariki.”

“Mama, bado hayajaniingia akilini.”

“Masalu hebu niondokee, nilifikiri jambo la maana kumbe ni upumbavu,” mama alisema huku akijiandaa kurudi shambani.

“Mama unaniona mtoto lakini mambo yetu yote yapo hadharani.”

“Mambo gani?” Mama alishtuka na kunigeukia ili kutaka kujua.

“Dada Monika alinieleza mengi kuhusiana kifo chake alichotishiwa na baba kwa ajili ya kukikataa kidonda na kunitisha kidonda kile kitahamia kwangu.”

“Masalu nikueleze mara ngapi kuwa dada yako Monika alikuwa muongo aliyetaka aonekane alichokifanya ni sahihi cha ukosefu wa adabu?”

“Lakini mama mbona mengi aliyonieleza yanatokea? Uongo wake ni nini?”

“Kama nini?”

“Kuhusu wewe kuteseka na kilimo wakati familia ina uwezo mkubwa?”

”Kulima si kujitesa bali kujipa mazoezi.

“Mama, juzi uligombana na baba akikulazimisha uje shamba wakati ulikuwa hujisikii vizuri hata juzi uliniambia hukulala kutokana na maumivu ya mgongo. Mama naona umejisahau pale uliponiambia kuwa baba atakuua kwa vitu vya kulazimishana, bado tu unasema mazoezi. Mama unaweza kuona mnafanya siri lakini kila kitu kipo wazi. “Unaweza kuona watu wapo kimya, lakini kuna maneno mengi sana juu ya kifo cha dada Monika, hakina tofauti na kifo cha mtoto wa dada Mihayo.”

“Masalu! Hakina tofauti ya nini?”

“Wanasema hata mtoto wa dada Mihayo alipokufa hakuzikwa.”

“Hakuzikwa alifanywa nini?” Maskini mama aliniuliza huku macho yakimtoka pima na kijasho chembamba kilimvuja.

“Eti wanasema kile chumba ambacho hakifunguliwi ndani kuna maiti ya mtoto ambayo huwa mnaipaka mafuta kila siku ndicho chanzo cha dada Mihayo kuwa na utajiri mkubwa kuliko wenzake.”

“Wee mtoto, haya yote umeyasikia wapi?” Mama alishtuka.

“Shemeji aliniambia kuwa kabla dada hajakata roho alimueleza mambo mengi juu ya ushirikina wa familia yetu kutumia kidonda chake kujipatia utajiri na hata alipotoka nyumbani kukataa kuendelea na kidonda ilisababisha kifo chake.”

“Masalu! Alimueleza kuwa kwenye chumba hicho kuna maiti ya mtoto?”

“Ndiyo, tena alimueleza kuwa watu waliokuwa wakiipaka maiti ile mafuta ni wewe baba na yeye dada Monika.”

“Mungu wangu, kayasema hayo Monika?”

“Na wasiwasi mwingine wanasema maiti ya dada Monika huenda nayo haikuzikwa imefichwa kwenye chumba kile cha siri.”

“Ooh… Mungu wangu …Ooh moyo wangu,” mama alisema huku akishikilia kifua na kuanguka chini. Nilipojaribu kumuamsha hakuamka, nilipiga kelele kwa majirani wa shamba la pili. Sauti yangu iliwakusanya watu ambao walifika na kumpa huduma ya kwanza mama aliyekuwa amepoteza fahamu.

Alipopata fahamu aliwaomba wampe msaada wa kumrudisha nyumbani, jirani yetu mama Kusekwa alimsindikiza mama hadi nyumbani. Tulipofika alituacha na yeye kurudi shambani. Nilijawa na wasiwasi huku nikijilaumu kwa kumueleza mama mambo ambayo niliyaona mazito.

Nikiwa pembeni ya mama aliyekuwa bado amejilaza kwenye zulia huku akipuliziwa na upepo wa feni aliniita:

“Masalu.”

“Naam mama.”

“Kuna mtu aliuliza sababu ya kuanguka kwangu?”

“Ndiyo mama.”

“Uliwajibu nini?”

“Niliwaeleza kuwa ulianguka ghafla.”

“Hawakukuhoji zaidi?”

“Hawakunihoji zaidi ya kukupa huduma ya haraka.”

“Ooh, afadhali.”

“Unajisikiaje kwa sasa?” Nilimuuliza mama kwa huruma.

“Mmh, sijambo kidogo ila nakuomba tuliyozungumza yote usimwambie mtu.”

“Sawa mama.”

Nilimkubalia ili tu kuiacha siku ile ipite pia kutokana na hali yake, lakini bado sikupata jibu la dada Monika amekufa kweli, japo shemeji alinihakikishia amekufa. Na kama amekufa amezikwa wapi au ndiyo yaleyale niliyoelezwa kuwa mwili wake umefichwa ndani.

Moyoni nilibakia njia panda kutaka kujua ukweli kuhusu dada Monika, nilipanga kama mama atashindwa kunieleza basi nitamvaa baba na ukali wake ili nijue amekufa au mzima na kama amekufa amezikwa wapi.

Sikutaka kuliulizia jambo lile haraka kutokana na hali ya mama, niliamua kukaa kimya, lakini moyoni sikuwa na raha kutaka kujua ukweli wa kifo cha dada Monika. Siku moja asubuhi kabla ya kwenda shule mama alinifuata chumbani kwangu na kunieleza nisiende shule kuna sehemu anataka kunituma.

Nilibadilisha nguo zangu za shule na kuvaa za nyumbani, wakati huo alikuwa akijiandaa kwenda shambani. Lakini siku ile hakuwahi kama ilivyo kawaida yake. Tuliondoka nyumbani pamoja kuelekea shambani, baada ya muda wa chai, kutoka nyumbani mpaka shambani ni mwendo wa dakika 45.

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni