
Mtunzi: Ally Mbetu
SEHEMU YA SITA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Nilibadilisha nguo zangu za shule na kuvaa za nyumbani, wakati huo alikuwa akijiandaa kwenda shambani. Lakini siku ile hakuwahi kama ilivyo kawaida yake. Tuliondoka nyumbani pamoja kuelekea shambani, baada ya muda wa chai, kutoka nyumbani mpaka shambani ni mwendo wa dakika 45.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
SASA TUENDELEE...
Tulikwenda huku tukizungumza, mama aliniulizia habari za shule, nilimuelezea maendeleo yangu japo hakuwahi hata siku moja kushika madaftari yangu kuyaangalia.
Katika kumbukumbu zangu nilielezwa kuwa mama aliishia darasa la sita baada ya kupewa ujauzito na baba kisha kumtorosha. Taarifa hizo alinipa marehemu ambaye sina uhakika kama kweli amekufa au maiti yake imefungiwa katika chumba kisichofunguliwa.
Dada Monika alinieleza kuwa mama yetu alitengwa na familia yake baada ya kubebeshwa ujauzito na baba na kutoroshwa. Kitendo kile ndicho kilichofanya mama aishi maisha ya peke yake bila ndugu, ndugu yake mkubwa alikuwa baba kitu kilichofanya amnyanyase kwa kujua hana pa kwenda.
Sababu ile ndiyo iliyomfanya mama aishi kama mtumwa kwa vile kila alipofanya kosa baba alimtishia kumfukuza. Kwa kweli kitendo cha baba nilikiona cha kikatili sana, kila dakika nilijikuta nikimchukia baba kwa roho mbaya ya kuitesa familia yake kwa ajili ya mali.
Niliamini mateso ya muda mrefu na shuluba zote, baada ya kupata utajiri wa kushirikina, basi alitakiwa mama atulie na kufaidi matunda ya uchawi wao. Lakini imekuwa tofauti mama kila kukicha amekuwa mtu wa kusurubika. Kilichonishangaza ni ndugu zangu kushindwa kumsimamia mama na kumpunguzia mateso ya kulima na kupasua kuni. Kila nilipomtazama mama yangu roho iliniuma na kujiapiza kama Mungu atanisaidia kupata kazi na kuwa na maisha mazuri basi nitamuondoa kwa baba.
Moyoni nilijiapiza kutokubali kuishi maisha machafu ya ndugu zangu ya kutoa familia zao kwa ajili ya kafara ya hatari na kujiona kama wataishi milele. Nilijiuliza dada Mihayo atamwambia nini mwanaye mbele ya Mungu, aliyemtoa kafara kwa ajili ya utajiri na baadaye kuendelea kumtesa kwa kumlaza kwenye chumba?
****
Kuna kitu alinieleza dada Monika juu ya mama na kuniomba nimchunguze, nakumbuka siku hiyo alinieleza:
“Masalu, mama yetu anaishi maisha ya mateso makubwa sana, baba ni shetani asiyefaa mbele ya jamii. Nataka nikueleze kitu kimoja ambacho mimi wananikataza. Kwa taarifa yako nilikatazwa kulala na mwanaume lakini baba ana mwanamke kamjengea nyumba ya gharofa moja.”
Dada Monika aliendelea kunieleza jinsi watu wanavyotumia pesa huku mama akiteseka, alinieleza:
“Mdogo wangu familia yetu yote tutateketea kwa moto wa kiama, hebu ona maisha ya mama yanalingana na utajiri tulionao? Hata kama kuyumba hatuwezi kuishiwa kiasi cha kutisha, sawa na tembo kuugua maralia hawezi kukonda kama mbwa.
“Masalu, sema tu mama mbishi, nilimueleza mapema tuondoke pamoja ili aepukane na maisha ya mateso, lakini mama kama amerogwa na baba haelewi hasikii. Hivi kweli mama yetu ni wakuvaa kandambili za kufunga na kamba?” Nakumbuka siku hiyo dada Monika alizungumza huku akibubujikwa machozi.
Mama anateseka dada Mihayo anamhonga bwana wa pembeni gari, Masalu inauma lakini sina uwezo. Kama kidonda hiki angekuwa nacho mtu mwingine na mimi kuwa na uwezo wa dada Mihayo hata kwa kutoa kafara ya mtoto mama yangu angeishi kama malaika.
Lakini sina uwezo, hata hiki kidogo ninachokipata nikimpelekea mama hatakitumia zaidi ya kugeuzwa ndondocha na baba.”
Kila nilipoyakumbuka maneno ya dada nilijikuta nikitokwa na machozi. Nilikumbuka neno moja ambalo dada Monika alinieleza nilifanyie kazi, aliniambia:
“Masalu, mchunguze mama muda mwingi akiwa peke yake mkono huwa shavuni, na kama utamfuatilia kwa muda baada ya kutoa mkono shavuni hutikisa kichwa na kufuta machozi. Katika maisha yetu toka tupate utajiri wa kishirikina furaha ya mama imetoweka, kutabasamu kumekuwa kama ajali lakini kulia kumekuwa kitu cha kawaida.
Mara nyingi mama amekuwa kila akiwa peke yake kanga huwa mkononi ili kufuta machozi. Vitu vile nilivifanyia kazi na kumueleza dada Monika yote aliyonieleza ni kweli. Aliniuliza swali lingine:
“Masalu umeshawahi kumuona mama akivaa nguo mpya?”
“Hapana,” nilimjibu.
“Hebu jifikirie mama yetu ni wa kuvaa nguo zilizoachwa na wanaye?”
“Nilikuwa sijui.”
“Kama hujui, hata macho yako hayaoni? Masalu sasa hivi wewe si mtoto unaona vitu ambavyo baadaye vinataka majibu kwa kile ulichokiona.”
“Huwezi kuamini dada nilikuwa kama nimefungwa akili, unachonieleza sasa hivi ndiyo kama kwangu kunapambazuka baada ya kukaa gizani kwa muda mrefu. Kama usingenieleza haya ningekufa kibudu.”
Niliamini kabisa kama dada Monika kweli amekufa, basi alikuwa amekufa na mengi moyoni sawa na samaki mwenye mengi ya kuzungumza lakini kila alipofumbua mdomo maji yalimjaa mdomoni. Kama alivyonieleza shemeji kabla ya kufa kutokana na maelezo yake mengi angenieleza mengi mazito.
****
Tulipofika shambani mama hakuonesha kama anataka kulima, aliniweka chini ya mti huku akionekana mwingi wa mawazo. Baada ya ukimya mfupi mama aliniita jina langu.
“Masalu.”
“Naam mama.”
“Najua umesikia mengi juu ya maisha yetu, lakini hakuna ukweli kwa yote uliyosikia nakuomba uwapuuze, sawa baba.”
“Lakini mama mbona yote niliyoelezwa yana ukweli.”
“Ukweli upi?
”Mama kwanza naanza na wewe, toka nipate akili sijawahi kukuona ukifurahi, kila siku mtu wa masikitiko na kutokwa na machozi.”
“Ha! Masalu umejuaje?”
“Mama dada Monika kanieleza mambo mengi sana ambayo niliyafanyia kazi na kuupata ukweli juu yako.”
“Ukweli gani?”
“Kuhusu muda mwingi kuweka mkono shavuni na kutokwa na machozi, nilikufuatilia bila wewe kujijua na kuupata ukweli, pia uvaaji wako wa nguo mama toka nipate akili sijakuona ukivaa nguo mpya au nzuri, pia mama hebu angalia ndala zako. Kwa maisha tunayoishi wewe si wa kuvaa ndala za kufunga na waya.”
Niliposema vile mama alijiangalia kama hakujua alichokivaa wakati wa kutoka nyumbani.
“Mama najua yote haya yanatokea kwa ajili ya nini.”
“Kwa ajili gani?”
“Haya ni mateso anayokupa baba, baada ya kutengwa na ndugu zako, na chanzo cha yote ni yeye. Kutokuwa na ukaribu na familia yako, katumia ni fimbo ya kukuadhibia. Hivi mama hata wanao wengine wanajijali wao na kukusahau , bila wewe wangeijuaje dunia?
“Mama maisha haya unayoishi siyo mazuri, nilisikia eti baba alikutishia maisha kama utataka mambo makubwa. Haya ndiyo aliyoyakataa dada Monika kidonda akitunze yeye wengine wale maisha mazuri. Matokeo yake mnaamua kumuua na kuificha maiti yake.”
“Masalu nani kaificha maiti ya Monika?”
“Ipo wapi?”
“Masalu swali gani hilo, kila anayekufa si huzikwa?”
“Mbona mtoto wa dada Mihayo hakuzikwa?”
“Masalu una uhakika gani?”
“Dada Monika hakunificha yote nisemayo ni yeye aliyeniambia ni mengi sana nayajua kuliko mtu mwingine.”
“Masalu yote usemayo ni kweli, nakuomba usimwambie mtu yoyote habari hizi.”
“Kama ni kweli naomba kuanzia leo kazi ya kulima aachiwe mtu mwingine, uvae nguo nzuri ili ulingane na utajiri wa familia yetu.”
“Masalu hilo haliwezekani.”
“Kwa nini?”
“Baba yako ataniua, naomba mwanangu yote unayoyaona yaache kama yalivyo, na ukizidi kumchokonoa anaweza kukuua.”
“Kama alivyomuua dada Monika?”
“Usiseme hivyo Masalu.”
“Mama tunafichana nini? Hivi utajiri ndiyo unaotufanya tukose huruma kwa wenzetu?”
“Masalu nakuomba usichimbe sana.”
“Hapana mama, huwezi kujua sasa hivi tunaonekana vipi mbele ya macho ya watu, kwa taarifa yako inasemekana Monika hajazikwa amewekwa ndani kwa imani za kishirikina.”
“Nani kasema?”
“Aliyekuwa akikaa na dada Monika ndiye anayeeneza habari hizi.”
“Yeye kajuaje?”
“Mama ina maana ninapozungumza na wewe unakuwa wapi? Nilikueleza kuwa kabla ya kufa dada Monika alimpa siri kubwa ya maisha yetu na sababu ya kifo chake. Pia alimueleza kuwa alikuwa na siri nzito ambayo asingemwambia mtu zaidi yangu mimi.”
“Mmh, sasa huyo kijana kinamhusu nini kututangaza vibaya?”
“Kinachomuuma ni kumuulia mtoto wake asiye na hatia.”
“Hivi baba yako akijua kuwa ndiye anayetutangaza vibaya kwa watu kutakuwa na usalama kweli?”
“Atamfanya nini?”
“Masalu wee acha baba yako hana dogo, anaweza hata kumkata kichwa.”
“Akimuua atapata faida gani? Si ndiyo atakuwa anaongeza chuki kwa watu?”
“Masalu mwanangu, kwa umri wako hata nikueleza kitu hutanielewa, nakuomba kila ulilosikia liache lilivyo, wewe bado mtoto mdogo litakuchanganya.”
“Sawa nimekuelewa, ila naomba ukweli wa jambo moja.”
“Jambo gani?”
”Kuhusu ukweli wa dada Monika.”
“Ukweli upi?”
”Ni kweli amekufa?”
“Ndiyo.”
“Amezikwa wapi?”
“Mmh! Si makaburini.”
“Makaburini gani?”
“Kwa kweli siwezi kujua makaburi gani sikwenda kuzika.”
“Mama kuna makaburi tofauti na tuliyoyazoea?”
“Hakuna.”
“Na misiba yote huanzia kanisani kisha kupelekwa kuzikwa?”
“Ndiyo.”
“Sasa msiba wa dada Monika mliupeleka kanisa gani?”
“Masalu hata ukijua itakusaidia nini? Aliyekufa amekufa huwezi kumfufua.”
“Hata kama siwezi kumfufua, dada Monika ndiye kipenzi changu, kaburi lake kwangu ni kielelezo cha kumuona kipenzi changu.”
“Masalu nakuomba suala hilo uachane nalo.”
“Yote nitaachana nayo si la dada Monika.”
“Masalu ukitaka kujua mengi utakosana na baba yako.”
“Kwa hiyo ukweli dada Monika maiti yake haikuzikwa?”
“Masalu nakuomba mwanangu chondechonde achana na hayo ili maisha yako yawe salama.”
“Kwa hiyo nikitaka kujua baba ataniua?”
“Hawezi kukuua ila utakuwa matatizoni.”
“Mmh! Sawa mama,” nilikubali kwa shingo upande kutokana na kuonekana kumuweka mama katika wakati mgumu.
Sikutaka kumsumbua sana mama yangu kutokana na maelezo ya dada Monika, kila nilipomtazama nilimuonea huruma. Nilimuahidi mama toka moyoni mwangu sitaulizia lolote kuhusiana na dada Monika wala kitu chochote kuhusiana na familia yetu.
Kauli yangu ilimfurahisha mama na kuonekana hawezi kuamini nilichokisema.
“Kweli Masalu.”
“Kweli mama, nakupenda sana mama yangu.”
“Asante Masalu, nakuomba kila unachokijua huenda hata mimi mama yako sivijui kwa vile baba yako alimpenda sana Monika hata siri zingine sizijui ambazo alikueleza wewe na pengine kabla ya kufa angekueleza,” maskini mama yangu alisema huku akitokwa na machozi, kitu kilichozidi kuniumiza nami machozi yalianza kunitoka kwa mbali.
“Nimekuelewa mama yangu, nimekuelewa sina budi kukusikiliza.”
“Asante Masalu, siku zote niliamini wewe na Monika ndiyo watoto wangu wanaonijali,
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi