
Mtunzi: Halfani Sudy
SEHEMU YA PILI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Dr Yusha akatulia kwa sekunde kadhaa, ndipo aliposikia, kumbe mshereshaji wa sherehe alikuwa amemwambia akakate keki iliyokuwa mbele ili akamlishe mkewe, Nasra, wakati yeye alikuwa busy na simu.
"Ndugu bwana harusi tunaomba uje ukate keki na kwenda kumlisha mkeo mpendwa " Mshereshaji alikuwa anayarudia kwa mara ya tano maneno hayo.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
Wakati Dr Yusha akiwa mbali kwa mawazo, ya kumfikiria mgonjwa. Dr Yusha alikuwa anawaza, akakate keki ama aende Kivinje kumsaidia mgonjwa.
Alikuwa anafikiria kwa kina, kumlisha mkewe mpendwa Nasra ile keki tamu aende kuokoa uhai wa mgonjwa.
Nasra, mwanamke aliyekuwa anampenda kuliko kitu chochote hapa duniani alikuwa analia. Hakuelewa kabisa mumewe kakumbwa na nini.
Dr Yusha alinyanyua mguu wake wa kulia taratibu na kuelekea kwenye meza iliyowekwa keki, ghafla simu yake iliita tena….BALAA.
Dr Yusha alisita sasa, akakosa msimamo thabiti, akaanza kuitoa simu yake kwenye koti….
Akaiangalia simu yake. Ilikuwa namba ileile iliyompigia mwanzo, Dokta Yusha alijishauri kidogo, aipokee ama asiipokee….simu iliita mpaka ikakata. Akaitia tena mfukoni. Ukumbi mzima ulikuwa kimyaa, watu wote wakiwa hawaelewi kinatokea nini. Dr Yusha alipiga hatua nyingine ya kivivu kwa mguu wa kushoto kuifuata meza ya keki. Hatua ilivyotua chini, na simu iliita kotini.
Dr Yusha aliitoa kwa haraka.
Akaipokea.
"Uhai wa Mtoto wetu unakutegemea wewe, tunaomba uje kutusaidia baba" Ile sauti ya mwanzo sasa ilikuwa inalia. Sauti ile iliyosikika katika hali ya huruma ilipenya hadi katika moyo wa Dokta Yusha. Badala ya kuelekea kwenye keki, alielekea katika mlango wa ukumbi ule. Aliitafuta gari yake harakaharaka, akakumbuka funguo hakuwa nayo yeye. Alitafuta pikipiki ya kulipia (bodaboda).
"Kivinje faster" Alisema huku akiipanda.
Mwenye ile pikipiki hakuwa na cha kuuliza, aling'oa ile pikipiki kwa kasi, akaishika barabara inayoelekea Kilwa Kivinje. Jamaa alikuwa ' faster' kweli.
Dokta Yusha aliacha taharuki kubwa sana kule ukumbini. Watu wote walibaki midomo wazi, wengi wakiamini Dokta Yusha amechanganyikiwa. Kwa bahati mbaya hakutokea mtu hata mmoja aliyepata wazo la kumzuia Dokta Yusha. Ilikuwa ni kama ukumbi mzima wamepigwa na ganzi.
Nasra, mke wake kipenzi Dokta Yusha alikuwa hakamatiki, alikuwa hashikiki. Analia kwa sauti na kugaragara chini. Ama hakika kilimuumiza sana kitendo kile. Aliona amepata aibu, aibu mbele ya wazazi wake, aibu mbele ya rafiki zake, aibu aibu aibu. Kwa mara ya kwanza alimchukia Dokta Yusha, kwa moyo wake wote alimchukia mwanaume yule wa maisha yake.
Wazazi wa Dokta Yusha nao walikuwa katika hali ya huzuni na masononeko makubwa. Hakika mtoto wao aliwaaibisha sana, tena katika sherehe ya ndoa yake, mbele ya umati mkubwa. Sherehe ile ya ndoa, iliyotangazwa sana, iliyogharimu pesa nyingi sana, ilikomea kati, kwa bwana harusi kutokomea na pikipiki, kusikojulikana, balaa !
Dakika kumi zilitosha pikipiki aliyopanda Dokta Yusha kufika hospitali, Kilwa Kivinje. Dokta Yusha aliruka kabla ya ile pikipiki haijasimama na kukimbilia kuingia ndani ya hospitali ile. Akiacha yule dereva wa pikipiki hajamlipa. Sasa ule mshangao wa watu wa kule ukumbini, ulihamia kwa mwendesha pikipiki. Dokta Yusha alifika hadi wodini, alikuta hali ya wodi shwari, hakuna mgonjwa yeyote aliyekuwa mahututi. Alienda mapokezi, hakukuwa na mtu yeyote usiku ule, alijaribu kuipiga ile namba, ilikuwa haipatikani, Balaa!
Sasa ule mshangao aliowaachia watu kule ukumbini, mshangao alioondoka nao na kumletea mwendesha bodaboda, sasa ulimvaa mwenyewe kwa kasi. Hakumwona kabisa mmiliki wa ile sauti iliyompigia simu, pale hospitali.
TANO, ni miongoni mwa walinzi wa Don Genge. Yeye ndio alipewa kazi ya kusafisha njia, ili mpango wao uendelee kama ulivyopangwa. Kusafisha njia ilikuwa inamaanisha kung'oa magugu yote, ambayo yangeweza kuwa kikwazo kwa mpango wao. Mmoja wa gugu ambalo walipanga kuling'oa ni daktari huyu kijana.
Walipanga kumuuwa Dokta Yusha !
Ni Tano ndiye aliyepiga simu ile, lengo ni kumleta Kivinje ili amuue. Bila kujua Dokta Yusha aliingia katika mtego huo hatari. Tangu Dokta Yusha alivyowasiri kwa pupa na pikipiki, mpaka sasa, Tano alikuwa makini nae kila anapokwenda. Lengo ni kupata sehemu sahihi ya kuweza kumuuwa Dokta Yusha.
Baada ya Dokta Yusha kutomuona mgonjwa aliyeitiwa, na simu ya mtu aliyempigia kuzimwa. Alikaa chini na kutafakari kilichotokea. Kila kitu kilijirudia katika kichwa chake kama filamu, sasa akaona ukubwa wa kosa alilolifanya. La kukimbia katikati ya sherehe ya harusi yake. Ukubwa wa kosa uliongezeka zaidi kwa kuwa hakukuwa na mgonjwa kweli pale hospitali…
Dokta Yusha sasa alikumbuka hali atakayokuwa nayo mke wake kipenzi Nasra kwa tukio lile baya alilolifanya. Alikumbuka pia huzuni atakayokuwa kawaachia wazazi wake wapendwa kule ukumbini baada ya kuondoka bila kuaga. Alijiona kafanya kosa kubwa sana.
Ghafla, majimaji mepesi yalitiririka katika mashavu yake, Dokta Yusha alikuwa analia. Kwa kosa kubwa alilolifanya usiku ule.
Wakati Dokta Yusha akiwaza yale, na chozi la uchungu kumdondoka pale hospitali. Muuaji namba tano alikuwa hatua chache sana na pale alipokaa Dokta Yusha, akifikiria jinsi ya kumuua. Aliona kumuua kwa risasi itazua tafrani kubwa pale hosptali, alipanga kumuuwa Dokta Yusha kwa mikono yake ama kwa kisu. Alihisi njia hizo ni salama zaidi. Sasa alikuwa anasubiri Dokta Yusha afanye kosa lolote lile.
Kule Kilwa Masoko, hali ile ya taharuki na huzuni iliendelea mle ukumbini.
Baada ya saa moja watu wote waliamua kurudi majumbani kwao. Huku kila mmoja akiliongelea kwa aina yake tukio la kukimbia kwa bwana harusi katikati ya sherehe. Wapo waliolifanya kama hadithi nzuri ya kufurahisha, wapo waliolifanya kama hadithi mbaya ya kusikitisha na kuhuzunisha.
Watu wa mwisho kurudi nyumbani katika usiku ule wa sherehe ya harusi ni familia mbili zilizokumbwa na kisanga kile cha kuajabisha, familia ya Dokta Yusha na familia ya Nasra. Waliweka kikao kidogo mlemle ukumbini kulizungumzia tukio lile. Kikao kilichoisha bila maelewano yoyote. Walijaribu kumpigia Dokta Yusha, simu iliita tu bila kupokelewa. Sasa familia zile mbili wakiwa na Bi harusi walikuwa wanarudi nyumbani, katika gari mbili tofauti, wakiwa na huzuni na simanzi tele. Huku wanawake wachache ndani ya familia zile walikuwa wanalia, wakiongozwa vizuri na Bi harusi, Nasra.
Katika gari aliyopanda Nasra, kulikuwa na watu watano, Kulikuwemo na dereva, baba yake Nasra, mzee Mpaukha, mama yake Nasra, mama Mpaukha, na mpambe wa Bi harusi, rafiki yake kipenzi Nasra, Hasina Omary.
Dereva wa gari ile, alikuwa anaitwa Musa. Dereva wa siku nyingi sana wa familia ya mzee Mpaukha.
Musa alikuwa amelewa sana pombe, pombe ambayo aliinywa vilivyo na marafiki zake mle ukumbini. Pombe ilimfanya apoteze umakini pale katika sukani na kuleta balaa kubwa sana.
Walitoka vizuri pale ukumbini, lakini gari lilivyokamata lami mwendo ulibadirika. Musa akawa anaendesha gari bila umakini wowote, siku zote pombe haziongopi.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa makini na mwendo ule, wakati Musa alikuwa amelewa pombe, watu wengine wote waliobaki walikuwa wamelewa na kitendo alichokifanya Dokta Yusha kule ukumbini. Gari zima walilewa kwa aina mbili tofauti. Kila mmoja alikuwa amekaa mkao wa kuchoka katika siti yake.
Gari wakati inakata kona ya kuelekea nyumbani kwa mzee Mpaukha, dereva ilimshinda. Ilikuwa kona kali sana, iliyomshinda kabisa Musa, gari liliacha njia na kujisweka kwenye kapori kadogo….ilikuwa balaa !
Gari ilijipiga kwa nguvu sana katika mti mkubwa kule kwenye kapori. Kishindo kikuu kilisikika.
TANO, baada ya kushindwa mpango wake wa kumuua Dokta Yusha usiku ule. Alirudi mafichoni kwa wenzake kujipanga upya. Usiku wa siku uliofuata kundi lile hatari la SIX KILLERS walikuwa na kazi kuu mbili.
Kwanza Kuhakikisha utoaji wa mioyo kwa maiti zilizokuwepo katika chumba cha kuhifadhia maiti unafanyika bila wasiwasi wowote.
Pia kuhakisha Dokta kijana anayejifanya ana morali ya kazi, Dokta Yusha anauwawa.
Kwa kushirikiana na wale madokta wasiokuwa na maadili ya kazi waliamini watafanikiwa katika malengo yao hayo mawili.
Jioni ya siku ile familia ya Dokta Yusha, ilikwenda hospitali kuwaangaalia wenzao. Yalikuwa majonzi makubwa sana baada ya kusikia mama Mpaukha alikuwa amefariki. Na ndugu wengine wa Mzee Mpaukha nao waliwasiri, na waliamua kuuchukua mwili wa mpendwa wao usiku wa siku ile ili kwenda kufanya maandalizi ya mazishi.
Hadi muda huo, madaktari wakuu katika hospitali hiyo walikuwa hawajulikani walipo. Nia yao ilikuwa ni kukaa mafichoni muda mrefu ili idadi ya watu watakaofariki waongezeke, ili mradi wao wa kupata mioyo kumi na tano kila siku ukamilike. Walijua wasipokuwa kazini wao, wagonjwa wengi watakufa.
Saa nne kamili usiku, mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya ya Kilwa, ndugu Zaidi Kilumba, Daktari Mkuu wa upasuaji Dokta Sharifa Juma, Mkuu wa chumba cha upasuaji, Dokta Tamaa Karimu, wale manesi watano, na kundi zima la SIX KILLER waliwasiri katika eneo la hospitali ile, kwa magari aina mbili tofauti. Madokta na manesi walipanda gari yao na lile kundi hatari walipanda gari yao. Walitofautiana kufika eneo la hospitali kwa dakika kumi tu, wakitangulia wale madaktari. Walikuwa wamekuja kufanya kazi ya kutoa mioyo ya maiti, wakifuatiwa na gari la kundi la hatari la Six Killers waliokuja kulinda hali ya usalama pale hospitali, na kumuua daktari aliyeonekana kizuizi kwa kazi yao, Dokta Yusha.
Wale madaktari waliposhuka tu pale hospitali, walilakiwa kwa furaha na bashasha kubwa sana toka kwa Dokta Yusha. Lakini wao hawakuonesha kabisa sura za furaha, haikuwa kama ilivyo kawaida yao kila walipokuwa wanakutana hapo kabla. Madaktari wale walionesha sura zilizoonesha dharau na kiburi.
Madaktari wote watatu walikataa kushikana mkono na Dokta Yusha wakati wa kusalimiana ! Waliuacha mkono wa Dokta Yusha ukielea hewani.
"Hivi wewe hiki ni kituo chako cha kazi, au unataka kutuaminisha kwamba wanaopanga vituo hawana akili?" Dokta Sharifa alimuuliza swali kwa dharau Dokta Yusha.
Dokta Yusha hakujibu swali lile, alitumbua macho kuonesha mshangao wake. Aliwaangalia kwa zamu madaktari wale. Wote walionesha kutojari kabisa mshangao wake.
"Au unahamu…..?" Dokta Kilumba nae aliuliza swali lililoelea hewani, bila kutanabaisha Dokta Yusha alikuwa na hamu ya nini.
"Mbona siwaelewi ndugu zangu" Dokta Yusha aliongea kwa sauti ndogo iliyokuwa ikiashiria kutoelewa kinachoendelea.
"Naitwa Tamaa Karimu, unaitwa Yusuph Shaweji,
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi