Machapisho

BALAA (21)

Zephiline F Ezekiel
Jina: BALAA
Mtunzi: Halfani Sudy

SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA
ILIPOISHIA...
Hakujua kabisa alikuwa karibu na mtego. Karibu na hatari! Dokta Kilumba alikuwa anawindwa na wawindaji mahiri sana. Kwa bahati nzuri siku hiyo kulikuwa na 'disco' ndani ya ukumbi wa Masoko by night. 'Disco' ambalo lilikuwa na faida kubwa sana kwa Dokta Yusha na Mwanasheria mlevi

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Wingi wa vijana wacheza 'disco' waliozagaa pale nje iliwafanya wasionekane na Dokta Zaidi Kilumba. Hadi kibanda cha vocha kinafungwa Dokta Kilumba alikuwa bado anapata ulabu na kina Dokta Yusha wamejificha palepale. Usiku mnene Dokta Kilumba aliinuka pale katika kile kiti chake alichokalia. Alipepesuka kidogo kutokana na pombe, kisha akakaa sawa. Akapiga hatua za taratibu kutoka katika uwanja wa baa ile. Alifanya yote hayo huku akitazamwa kwa umakini na macho manne. Mhudumu wa baa ya Masoko by night alimkimbilia Dokta Kilumba alitoka kule nje.

Dokta Kilumba alikuwa anapepesukia nje bila kulipa bia alizokunywa pale baa. Mhudumu alipomfikia na kumueleza, Dokta Kilumba hakuwa mbishi. Alitia mkono mfukoni na kumlipa Mhudumu hela yake. Baada ya kumlipa Mhudumu yule, Dokta Kilumba akapiga hatua zake za kilevi, huku akiyumba, hatua za kilevi zilizomfikisha Dokta Kilumba hadi katika gari yake ndogo, Toyota corolla. Kwa bahati mbaya kabisa, Dokta Yusha na Mwanasheria mlevi hawakuwa wamejiandaa kwa jambo hilo. Walitegemea Dokta Kilumba ataondoka kwa miguu. Wao hawakuwa na usafiri wa aina yoyote ili kumfatilia Dokta Kilumba.

Wakiwa pale nyuma ya kibanda cha vocha walimshuhudia Dokta Kilumba akipanda gari lake taratibu na kuiongoza gari yake upande wa bandarini (custom). Dokta Yusha na Mwanasheria mlevi walibaki wakiikodolea macho ile gari aliyopanda Dokta Kilumba ikishika kasi katika barabara ya lami. Kichwani mwa Dokta Yusha alikuwa anawaza wafanye nini ile Dokta yule mwanaharamu asiwapotee katika upeo wa macho yao. Alitafakari harakaharaka bila kupata jibu. Aliamua kushauriana na Mwanasheria, Dokta Yusha alipoangalia pembeni pale alipokuwa Mwanasheria, hakuwepo! Alikuwa amebaki peke yake amejibanza pale katika kibanda cha vocha.

Alipoangalia ile barabara alikoelekea Dokta Kilumba, kwa mbali, usawa wa baa ya Makondeko alimuona Mwanasheria akiwa kwa juu ya pikipiki aina ya boxer akielekea upande uleule alikoelekea Dokta Kilumba. Taa zilizokuwa zinawaka pale baa, zilisaidia Dokta Yusha amtambue vizuri Mwanasheria mlevi. Alipigwa na butwaa! Mwanasheria mlevi juu ya pikipiki? Dokta Yusha alipigwa na butwaa. Hakuelewa kabisa Mwanasheria mlevi alikuwa ametoka saa ngapi pale nyuma ya kibanda cha vocha walipokuwa wamejificha. Dokta Yusha pia alipigwa na butwaa, hakuwa anaamini kabisa kama Mwanasheria mlevi angeweza kuendesha pikipiki. Tena kwa kasi namna ile. Yalikuwa maajabu hasa! Aliwaza hayo kwa muda mfupi, Dokta Yusha nae hakutaka kuzubaa, akajua kazi sasa imeiva, ni kuipakua tu. Alimuita dereva pikipiki za

 kukodi harakaharaka, akapanda nyuma na kumuelekeza kwa kidole kuwa aifate pikipiki aliyokuwa anaendesha Mwanasheria mlevi. Sasa watu wawili wakiwa katika pikipiki mbili tofauti walikuwa wanamfukuzia mtu mmoja, Dokta Zaidi Kilumba. Safari ya Dokta Zaidi Kilumba iliishia katika nyumba ya kulala wageni ya Mjaka. Nyumba safi na ya kisasa ya wageni iliopo katika mtaa wa Tanesco. Dokta Kilumba aliingia ndani, na moja kwa moja alielekea chumbani kwake. Baada ya kubadili nguo na kuoga, dokta Zaidi Kilumba alilala, bila kujua hatari iliyokuwa inamfata nyuma yake. Mwanasheria mlevi nae alipaki nje ya nyumba ile ya kulala wageni, lengo la mwanasheria lilifanikiwa kwa asilimia mia moja, yeye alikuwa anataka kujua mahali anapoishi dokta yule kwa kipindi kile.

Na alifanikiwa. Mwanasheria mlevi alitabasamu peke yake alivyokumbuka jinsi alivyoparamia pikipiki ya watu kule Masoko by night, baada ya mwenye pikipiki kuiacha ikiwa na funguo yake, sijui alijisahau ama alikusudia, Mwanasheria hakutaka kujua. Alifikiria pia jinsi mshangao atakaopata mwenye pikipiki, baada ya kurudi na kutoikuta pikipiki yake pale alipoiacha. "Kwa vyovyote atadhani kaibiwa, nitamrejeshea lakini" Mwanasheria akasema kwa sauti ndogo na kujijibu mwenyewe. Dakika mbili baadae pikipiki aliyopanda Dokta Yusha nayo iliwasili. Dokta Yusha alimlipa yule dereva pikipiki pesa yake. Baada ya dereva pikipiki kuondoka.

Mwanasheria ndiye alikuwa wa kwanza kuiona pikipiki ile toka mahali alipokuwa, alifurahi alivyoona abiria wa pikipiki ile ni rafiki yake kipenzi, dokta Yusha. Alimfata dokta Yusha aliyekuwa anazubaazubaa tu. Baada ya kuonana. Walikumbatiana kwa furaha. "Kazi nzuri Mwanasheria" Dokta Yusha alimpongeza Mwanasheria. "Ndio majukumu yangu haya Dokta, usihofu" Mwanasheria mlevi nae alijibu kiuhakika. Dokta Yusha na Mwanasheria mlevi walijipanga kwa ajili ya uvamizi. "Sasa mwanasheria tutaingiaje hapa" Dokta Yusha aliuliza huku akimwangalia Mwanasheria mlevi usoni. "Hapa inabidi tujifanye Wateja, ndo njia pekee ya kuingia humu" Mwanasheria mlevi alijibu kwa kujiamini. "Halafu" Dokta Yusha aliuliza tena. "Tukishapewa chumba tutajua jinsi ya kufanya humohumo ndani" Mwanasheria alijibu.

"Sawa Mwana" Dokta Yusha na Mwanasheria walienda mapokezi kwa lengo moja tu, la kupata chumba ili wawe karibu na Dokta Zaidi Kilumba. Walifika mapokezi, walikutana na mhudumi wa kike, aliwahudumia vizuri. Mwanasheria na Dokta Yusha wakakodi vyumba viwili. Chumba alichopewa Mwanasheria na chumba alichopewa Dokta Yusha vilikuwa vinaangaliana. Kila mmoja aliingia katika chumba chake. Baada ya kama dakika tatu Mwanasheria mlevi alitoka katika chumba chake ns kwenda kugonga katika mlango wa chumba cha Dokta Yusha. Dokta Yusha alienda kumfungulia, walikaa ndani na kuanza kupanga mambo yao. "Sasa tutajuaje chumba alichpanga yule mwanaharam?" Dokta Yusha aliuliza katika hali ya udadisi mkubwa. "Dokta Kilumba yupo chumba namba 8" Mwanasheria alijibu katika hali yake ileile ya kujiamini.

"Umejuaje Mwanasheria kama Dokta Kilumba yuko chumba namba nane?" Dokta Yusha aliuliza huku akiwa amemkazia macho Mwanasheria mlevi. "Nilichungulia katika daftari pale mapokezi wakati tunaandikiashwa" Dokta Yusha sasa alitokea kumhusudu sana Mwanasheria mlevi. Hakukuwa na umbali mkubwa sana kati ya chumba namba nane alichokuwemo Dokta Kilumba na chumba namba kumi na tatu walipokuwepo watu hawa wawili, Mwanasheria mlevi na Dokta Yusha. Kulikuwa na tofauti ya vyumba kama vinne hivi ili kufika katika chumba alichokuwa amepanga Dokta Kilumba.

"Tutaingiaje sasa chumbani kwake?" Dokta Yusha aliuliza huku akimwangalia Mwanasheria mlevi usoni. "Tutagonga tu mlango" Mwanasheria mlevi alimjibu Dokta Yusha kwa kifupi. "Je akiuliza nani anagonga akiwa bado hajafungua mlango?" Dokta Yusha aliuliza tena. "Tutasema Mhudumu" Mwanasheria mlevi alikuwa anajibu majibu mafupi huku akiwa na uhakika tele. "Ahaaa..poa twende tukajaribu" Dokta Yusha alikubaliana na Mwanasheria mlevi, bila ya kudadisi sana. Usiku uleule wa maneno Dokta Yusha na Mwanasheria mlevi walitoka katika, chumba namba kumi na tatu, walichopanga na kwenda chumba namba nane, chumba alichokuwa amepanga hasimu wao, adui yao, Dokta Kilumba.

Kule ndani Dokta Kilumba baada ya kwenda kujimwagia maji, sasa alikuwa amekaa katika shuka nyeupe iliyokuwa imetandikwa juu ya kitanda kikubwa, ndani ya nyumba ile ya kulala wageni ya Mjaka. Dokta Kilumba alikuwa akisubiri ujio wa mgeni, mwanamke baamedi aliyekubaliana kwenda kustarehe nae alivyokuwa kule baa. Dokta Kilumba akiwa kule baa, alipatana kwa siri, kwenda kufanya mambo ya siri. Alikuwa Baamedi wa Masoko by night, aitwaye Glad na alikuwa amemuelekeza namba ya chumba alichofikia, pia alikuwa ameshampa hela ya usafiri wa kumfikisha pale, na sasa alikuwa anamsubiri tu ili aje kupewa huduma ya siri atakayoilipia.

Dokta Kilumba hakutaka kufatana nae wala kukaa nae karibu Glad baamedi, alikuwa anaogopa kuchafua taswira yake ya heshima mbele jamii. Ingawa Alice alikuwa mwanamke mrembo sana, lakini kutokana na kazi aliyokuwa anaifanya (Ya ubaamedi) Dokta Kilumba aliiona kama kazi ya dharau, kazi ambayo yeye kama Dokta anayeheshiwa hakustahili kuambatana na mwanamke wa aina hiyo. Tena akielekea nae katika nyumba ya kulala wageni. "Ngongongo" Mara mlango wa chumba alichokuwa Dokta Kilumba uligongwa, na Dokta Kilumba bila kufikiria alinyanyuka pale kitandani kwa mbwembwe bila tahadhari yoyote na kwenda kuufungua ule mlango.

Katika akili ya Dokta Kilumba alikuwa anajua yule mwanamke aliyeongea na kule baa, Glad baamedi, mwanamke aliyekubaliana nae kule katika baa ya Masoko by night ndiye alikuwa anagonga mlango muda ule. Dokta Kilumba aliusogelea ule mlango bila wasiwasi wowote. Akiwa amejifunga taulo jeupe safi kiunoni, huku juu akiwa kifua wazi. Alipofungua tu mlango alikutana na Balaa! Alipigwa na dhoruba kali sana. Alijikuta amesukumwa kwa nguvu na kifua cha kiume cha Dokta Yusha, msukumo ambao ulimrudisha ndani kwa kasi na kumdondosha chini moja kwa moja.

Dokta Kilumba hakujiandaa kabisa na tukio lile, alitegemea kukutana na kukumbatiwa na kifua laini cha mrembo Glad, lakini kwa bahati mbaya kabisa alikutana na kitu tofauti, alikutana na kifua kigumu cha kiume, kifua cha Dokta Yusha. Baada ya anguko lililotokana na msukumo wa kifua cha dokta Yusha. Kwa mwendo wa taratibu dokta Yusha alimfata Dokta Kilumba pale chini. Wakati Dokta Yusha akimfata Dokta Kilumba pale chini, Mwanasheria mlevi alibaki pale mlangoni, alikuwa anafunga mlango wa chumba kile cha kulala wageni kwa ndani. Mambo yote hayo yalifanyika kwa muda mfupi sana, na kwa umakini mkubwa pia.

Dokta Kilumba alibaki ametumbua macho pale chini, sakafuni. Kichwani mwake yalikuwa yanapita maswali mengi sana, bila ya kuwa na majibu. Ingawa Dokta Kilumba alikuwa anawafahamu vizuri watu wale wawili lakini Dokta Kilumba hakujua kabisa watu wale wametokea wapi baada ya kutoweka kwa muda mrefu, na wamekijua vipi chumba chake. Dokta Kilumba hakupata muda wa kutafakari zaidi, Kofi la nguvu la mkono wa kulia toka kwa Dokta Yusha lilitua katikati ya uso wa Dokta Kilumba.

Dokta Kilumba aliona vimulimuli. Kilikuwa kitendo cha ghafla sana na Dokta Kilumba hakutegemea kabisa kufanyiwa vile na Dokta Yusha. Hali ilikuwa tete mle ndani kwa upande wa Dokta Kilumba. Vijana wale wawili makini walikuwa wamembana Dokta Kilumba kisawasawa. Mwanasheria mlevi nae alitoka pale mlangoni na kusogea pale walipokuwa Dokta Yusha na Dokta Kilumba. Siku hiyo Mwanasheria alikuwa hajatia hata tone moja la pombe,

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni