Machapisho

BALAA (7)

Zephiline F Ezekiel
Jina: BALAA
Mtunzi: Halfani Sudy

SEHEMU YA SABA
ILIPOISHIA...
Dokta Yusha, aliikwepa ile ngumi, huku nae akipiga ngumi yake kwa nguvu iliyotua barabara katika mbavu za Tano!
Tano hakuamini kasi aliyoitumia Dokta Yusha kukwepa ngumi ile, pia hakuamini uzito wa ngumi wa Dokta Yusha, sasa tano akajua anapambana na mtu anayejua anachokifanya. Hakujiuliza tena, sasa aliamua kupiga mapigo ya kifo,

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
mapigo ambayo yakimgusa mpigwaji yanaondoka na roho yake….Balaa!
Tano alianza na teke lilikwenda kwa kasi kama umeme, teke liliombatana na uzito wa kilo kadhaa. Dokta Yusha aliliona teke lile, teke liliolekezwa shingoni kwa lengo ya kuondoka na shingo yake, aliinama kidogo, teke likapita, ila upepo wa teke lile ulimyumbisha Dokta Yusha na kumdondosha chini, akiwa amelala pale chali, tano aliruka juu na kushuka chini huku akiwa amekitanguliza kifuti cha mguu wake wa kushoto, kifuto kilichoelekezwa katika upande wa kushoto wa kifua dokta Yusha, pale unapokaa moyo!

Dokta Yusha alijisogeza kidogo pale chini akiwa amelala vile vile, na kifuti cha dokta Yusha kutua katika lami, nguvu iliyoambatana na kifuti kile, na kutua kwenye lami ngumu, goti la Tano liligeuka palepale!
Tano alitoa ukelele mkubwa sana. Dokta Yusha alisimama na kwenda pale alipolala Tano huku akiwa amelishikia goti lake.
Dokta Yusha alijisachi mfukoni, na kutoa simu yake ya mkononi. Aliitafuta namba ya OCD ya kilwa, na kumpigia. Alimuelekeza kila kitu kilichotokea pale barabarani, na OCD alimwambia kwamba watafika askari pale baada ya muda mfupi.

Tano hakuwa na ujanja wowote, alikaa pake huku akilia, akisubiri hatma yake, mambo yalikuwa yameshaharibika.

Baada ya muda mfupi gari la polisi lilifika, likiwa na askari polisi sita waliovaa sare zao safi za jeshi la Polisi, wakiwa imara na bunduki mkononi kila mmoja. Walimbeba Tano na kumpakia nyuma ya gari ile ya Polisi. Dokta Yusha alipanda mbele ya gari ile, na safari ya kuelekea kituo cha polisi Masoko ilianza.

Dakika kumi zilitosha kuwafikisha askari wale wakiwa na Tano wa Six Killers katika kituo cha Polisi cha Masoko. Askari wawili walimshusha Tano msobemsobe, hawakujari kabisa makelele yake aliyokuwa anayapiga kutokana na maumivu akiyoyapata kutoka na maumivu ya kwenye goti. Kwa bahati mbaya askari wale hawakuwa na huruma kwa Tano, kwa kuwa hawakuwahi kufundishwa kumuonea huruma Mhalifu katika mafunzo huko chuoni Moshi.
Tano aliingizwa ndani ya kituo cha Polisi tayari kwa kuanza kuhojiwa.

Na alivyowekwa tu katika sakafu ya Polisi alikumbana na maswali mfululizo toka kwa askari wale. Kila askari alikuwa anauliza swali lake kwa sauti kubwa na ukali.
Tano alihisi kama wanampigia kelele, hakujibu kitu, alinyamaza kimya!

Dokta Yusha yeye aliitwa ofisini kwa mkuu wa upepelezi Wilaya. Alieleza kila kitu kilichotokea tangu alipopokea ile simu ya Mwanasheria mlevi. Simu iliyomtaarifu juu ya msiba wa Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, nae kuamua kwenda kilwa Masoko kwenye msiba.

Dokta Yusha alivyomaliza maelezo yake tu hapohapo wakatumwa askari kwenda kumkamata Mwanasheria. Mkuu wa upelelezi wa wilaya alihisi Mwanasheria mlevi anahusika na mbinu zile chafu!
Askari walewale waliomleta Tano waliingia tena kazini kumtafuta Mwanasheria mlevi popote alipo

Mwanasheria bado alikuwa kilabuni, hana hili wala lile. Alikuwa anakunywa pombe huku akiongea neno kila linalomjia kichwani mwake. Bila kujua kama askari sita wenye silaha walikuwa njiani wanaelekea pale kilabuni kumkamata yeye, akituhumiwa kupanga mauaji ya Dokta Yusha! Ghafla! Vumbi lilitimka pale kilabuni, gari ya Polisi lilifunga breki kali sana! Askari walikuwa wameshuka kabla hata ya breki ile. Walishuka kwa mbwembwe na bunduki zao mikononi. Walevi walitimka mbio, pombe zote ziliwatoka vichwani. Mwanasheria mlevi hakusogea hata hatua moja, alikuwa ameshazungukwa na askari polisi watatu.

Midomo ya bunduki ikielekezwa kichwani kwake! Mwanasheria hakuwa jasiri kama Dokta Yusha, yeye alikuwa anatetemeka, hakuweza kuuzuia kabisa mkojo usimtoke. Kuelekezwa bunduki kichwani kwake? Alikosa la kusema, askari walimuamuru asimame, na kumuelekeza pa kuelekea, ndani ya gari ya Polisi. Alifika ndani ya gari, na kukaa chini bila kuambiwa..machozi yalimtoka na kudondoka katika sakafu ya bodi ya gari ile. Askari hawakulijari lile chozi, hawakuwa na muda wa kulijari chozi la Mhalifu, walidandia gari na kuondoka kwa kasi kubwa sana, safari kituo cha Polisi Masoko. Laiti wangemjua Mwanasheria mlevi… Walipofika kituo cha Polisi, Polisi hawakuuliza, ilikuwa ni mateke, ngumi na vifuti kwa Mwanasheria mlevi.

Polisi walikuwa wanampiga Mwanasheria bila kujua kwanini wanampiga, na Mwanasheria nae hakujua kwanini anapigwa! Mwanasheria alipoteza fahamu kituo cha Polisi. Wote wawili Tano na Mwanasheria walipelekwa kituo cha afya Masoko, chini ya ulinzi mkali sana wa askari Polisi. Kama ilivyo kawaida katika hospitali nyingi Tanzania, wahalifu huwa hawapati huduma nzuri pindi wanapoumwa. Labda kwa kuwa wanakuwa hawana wauguzi wa kuwapa pesa wagonjwa( hongo). Hali hiyo iliwakuta Tano na Mwanasheria pale kituo cha afya Masoko. Waliachwa wamelala katika vitanda vyao wakiwa na pingu zao mikononi. Saa kumi na mbili jioni, Mwanasheria alizinduka, ni kudra za Mungu tu ndizo zilimuasha.

Mwanasheria hakupata huduma yoyote ile pale kituo cha afya. Mwanasheria aliamka na maneno yake, Mwanasheria aliamka na lawama za kutosha, lawama kwa Polisi, lawama kwa Serikali, lawama kwa mfumo mzima wa nchi, lakini lawama hazikusaidia, ukweli ulibaki palepale, Mwanasheria alikuwa amelala kitandani akiwa hoi bin taaban na pingu zake kitandani ! Tano wa Six killers naye alikuwa katika wakati mgumu sana, mguu wake ulikuwa umeumia vibaya sana, alikuwa anagugumia kwa maumivu. Lakini hakuwa na jinsi, alikuwa amelala katika kitanda kidogo cha kituo cha afya akiwa dhooful hali, huku akiwa hana namna ya kuwapigia wenzie ili awataarifu kwamba alikuwa mahali pale, kwa kuwa simu yake ilikuwa katika kituo cha Polisi.

Kundi la Six Killers walikutana kwa kikao cha dharura. Kikao kilichokuwa kinaongozwa na Don Genge mwenyewe, kikiwa na ajenda kuu mbili. Ajenda ya kwanza ilikuwa ni makabidhiano ya mioyo kumi na tano iliyopatikana kwa siku ile ya pili. Mambo yalienda sawa, na Dokta Sharifa alikabidhi deli kubwa jekundu lenye mioyo kumi na tano. Ajenda ya pili, ilikuwa inahusu kutoonekana kwa Tano. Masaa zaidi ya sita, Tano alikuwa hajaonekana, na simu yake ilikuwa haipatikani! "Hii ni siku ya tatu ya Mpango huu, kwa asilimia 90 mpango wetu umeenda sawa, lakini Kwa bahati mbaya sisi hatufanyi kazi kwa asilimia 90. Huwa tunafanya kazi kwa asilimia 100, au zaidi ya hizo ikiwezekana. Tano hajulikani alipo, na hizo ndio asilimia 10 tulizozipoteza. Natoa masaa mawili, Tano akiwa hai au amekufa mwili wake uwe hapa!. Baada ya masaa hayo mawili, tutaenda kutoa mioyo tukiwa na Tano kama atabahatika kuwa hai, mmebaki wa tano, hakikisheni mnarudi na Tano! Mnaweza kwenda…" Six killers walitoka mle ndani kwa lengo kuu moja, kwenda kumtafuta muuaji aliyepewa namba Tano.

Mbili alitoka nje, na kukutana na Sita. Walijipanga vizuri kwenda kumtoa Tano katikati ya maaskari wawili wenye bunduki!

Askari hawakuwa kizuizi kabisa kwa Mbili, bunduki hazikuwa tishio kabisa kwa Mbili. Alipewa namba mbili katika kundi la Six killer's kwa kuwa alikuwa mahiri kuliko wanakikundi wanne waliobakia. Wakiwa na Sita, walijiandaa kwa uvamizi.

Kule ndani Mwanasheria alikuwa anaendelea kuongea kama ilivyo ada yake. Askari Polisi walijaribu kumnyamazisha bila mafanikio yoyote. Kilabu sasa kilihamia katika kituo cha afya. Makelele yale yale ya Mwanasheria yalichangia kwa kiasi kikubwa kupunguza umakini kwa askari wale wawili. Wote walikuwa wanajitahidi kumnyamazisha Mwanasheria na kusahau kabisa suala la ulinzi.

Mbili na Sita walikuwa nje ya wodi ile. Walisikia kila kitu kilichokuwa kinaendelea kule ndani. Walijipanga vizuri.

Moja, mbili taaaaa…..wote kwa pamoja waliukumba ule mlango wa wodi kwa kutumia miili yao ya kimazoezi na wote kujikuta wako ndani. Kila mmoja kwa namna yake na bastola zao mkononi.

E bwana weee!

Mbili alijiviringisha kwa mtindo wa sarakasi na kujificha nyuma ya kitanda alicholala Tano huku akibonyea kidogo ili kile kitanda kimfiche, Sita nae alijiviringisha kwa kasi na kumfikia moja kwa moja askari mmoja na kumkaba shingoni, huku akimtumia kama ngao!
Huku bastola yake ikimtazama yule askari mwengine. Askari wote wawili waliwahiwa vizuri sana. Yule askari aliyepigwa kabali ilinasa kisawasawa, alijaribu kujitoa bila kutegemea, huku yule askari mwengine aliyeoneshwa bastola hakuwa na lolote la kufanya, alibaki ameganda kama sanamu. Six Killers walihamishia balaa wodini.

Ghafla! Yule askari aliyesimama alijishika kifuani, kulikuwa na majimaji mekundu, damu! Bastola ya Mbili yenye kiwambo cha kuzuia sauti ilikuwa imefanya kazi iliyotumwa. Yule askari aliyesimama alikuwa amepigwa risasi takatifu ya kifua. Aliyumba kidogo huku akipiga kelele, na kudondoka chini mzimamzima kisogo kikitangulia kufika chini !
Askari alikuwa mfu zamani sana kabla hata hajaigusa sakafu ya hospitali.

Sita naye aliongeza nguvu katika ile kabari, yule askari alikosa pumzi, nguvu zikamuishia, alilegea. Sita alimuachia yule askari, akadondoka chini. Vitendo vyote vilivyokuwa vinatokea Mwanasheria mlevi na Tano walikuwa wanashuhudia kila kitu, kimyakimya.

Wakati Tano akiufurahia ujio wa watu wale wawili aliokuwa anawafahamu vizuri sana, Mwanasheria mlevi alikuwa katika mshangao mkuu, hakutegemea wala kuelewa kinachotokea mle ndani wodini.

Mbili na Sita walikisogelea kitanda alicholala Tano. Waliliangalia lile jeraha kubwa la Tano pale mguuni, wote walimuonea huruma. Walimbeba na kutokomea nae kusikojulikana!

Baada ya robo saa kutokea kwa tukio lile, mganga wa kituo cha afya Masoko aliingia katika wodi ile.
Mganga alikutana na Balaa !
Miili ya askari wawili ilikuwa imelala chini, ikiwa haina uhai. Na mwili wa mgonjwa mmoja ukiwa haupo huku mwili wa Mwanasheria mlevi ukiwa juu ya kitanda, ukiwa umeloa jasho, hakika Mwanasheria aliyaona matukio ambayo hakutegemea kuyaona katika maisha yake. Alikuwa anatetemeka huku anatoa jasho!

Daktari hakuamini kabisa madhara yaliyotokea mle wodini. Alijishika kichwa huku akipiga kelele za kuomba msaada. Ndani ya dakika chache manesi na baadhi ya watu waliokuja pale hospitali walijaa katika wodi ile. Kila mmoja alistaajabu kilichotokea mle ndani, ilikuwa ni balaa !

Nesi mmoja alipiga simu kituo cha Polisi kuwataarifu juu ya mauaji yale.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni