Machapisho

BALAA (8)

Zephiline F Ezekiel
Jina: BALAA
Mtunzi: Halfani Sudy

SEHEMU YA NANE
ILIPOISHIA...
Daktari hakuamini kabisa madhara yaliyotokea mle wodini. Alijishika kichwa huku akipiga kelele za kuomba msaada. Ndani ya dakika chache manesi na baadhi ya watu waliokuja pale hospitali walijaa katika wodi ile. Kila mmoja alistaajabu kilichotokea mle ndani, ilikuwa ni balaa !

Nesi mmoja alipiga simu kituo cha Polisi kuwataarifu juu ya mauaji yale.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Askari waliwasili baada ya muda mfupi sana, na kushuhudia unyama mkubwa waliofanyiwa askari wenzao. Huku Mwanasheria mlevi akiwa ni shuhuda pekee aliyeshuhudia kila kitu. Nusu saa baadae, kundi hatari la Six Killers walikutana tena na bosi wao. Ilikuwa ni furaha kubwa sana kwao, kuitekeleza kazi ile ya masaa mawili kwa nusu saa tu. "Hongereni sana vijana wangu, mmefanya kazi kwa haraka sana, ila sina uhakika kama mmeifanya kwa umakini ninaouhitaji" Don Genge alikuwa anaongea huku akiwaangalia Mbili na Sita usoni. "Hakika tumefanya kazi kwa umakini mkubwa mno Bosi" Mbili alijibu kwa kujiamini. "Mmeua watu wote waliowashuhudia? Kuanzia huyo askari aliyekupeni siri mahali alipo Tano, Mganga mkuu pamoja na huyo mgonjwa aliyelazwa pamoja na Tano?" Mbili na Sita waliangaliana usoni, waligundua kuwa walikuwa wamefanya kosa! "Tumefanya kosa, dakika kumi" Mbili alijibu kibabe. "Naongeza kumi na tano" "Sawa mkuu" Waliondoka. Walikuwa wamepewa dakika kumi na tano kuhakikisha yule askari aliyewapa siri, Mganga mkuu na Mwanasheria mlevi wanauwawa! Kundi zima sasa kasoro Tano tu walinyanyuka na kuingia tena kazini.

Dakika kumi baadae kundi zima la Six Killers lilikuwa limerejea tena. Wakiwa wamefanikisha kuwauwa watu wawili kati ya wale watatu. Askari na mganga mkuu walikuwa wameelekea kuzimu kwa mtindo tofauti, wakati yule askari aliuwawa kwa bastola nyumbani kwake, Mganga mkuu wa hospitali aliuwawa kwa kisu ofisini kwake. Wote wakiwa hawajawahi kutumia hata senti tano katika zile laki moja walizokuwa wamepewa. Tatizo lilikuwa kwa Mwanasheria mlevi, walienda mle wodini hawakumkuta yule mgonjwa, na kwa bahati mbaya hawakuwa wameishika kabisa sura yake. Lilikuwa kosa la kubwa sana walilolifanya wauaji wale wazoefu. Askari Polisi sasa walikuwa wanamlinda Mwanasheria mlevi kupita kiasi. Jeshi la Polisi hawakuwa wanajua kabisa kama kuna watumishi walihusika katika kutoa siri, na kupokea hongo kutoka kundi la Six Killers. Nusu saa baadae taarifa mbaya zikalifikia jeshi la Polisi. Taarifa mbaya za vifo ! Kifo cha Sajenti Alex Omolo wa kituo cha Polisi Masoko, na kifo cha daktari Mosha Gabriel, Mganga mkuu wa kituo cha afya Masoko. Askari walitapakaa mtaani kuwasaka watu waliowauwa Afande Alex Omolo na Dokta Mosha Gabriel.

Askari walifanya msako kimyakimya. Lakini ilikuwa kama wanawatafuta watu ambao hawakuwahi kuwepo duniani. Msako wao haukuwasogeza kabisa karibu ya Muuaji! Wakati askari wakimwagika kama njugu huko Kilwa Masoko kuwatafuta watu waliowauwa Afande Alex na Dokta Mosha, Kundi hatari la Six Killers walikuwa wapo njiani kwenye gari wakielekea hospitali ya wilaya Kilwa Kivinje huku wakilaumiwa vibaya mno na Don Genge kushindwa kumuua mgonjwa aliyewashuhudia wakati wanafanya mauaji. Ilikuwa ni lawama nyingi sana, kundi zima walikuwa kimya wakati Don Genge akifoka! "Six killers huwa hatufanyi makosa. Kosa lolote inamaanisha kujiweka katika hali ya hatari, na mipango yetu kukwama. Ona sasa, yule Dokta mpumbavu bado anaishi, yule mgonjwa mpumbavu bado anaishi. Ni makosa haya, Dokta mpumbavu anamfahamu Tano, Mgonjwa mpumbavu anawajua Mbili na Sita. Ni makosa makubwa sana, lazima wafe!" Kundi la Six Killers walimwacha Tano katika nyumba yao iliyokuwa kama kambi ya muda mfupi huko Ngome, akipatiwa matibabu na daktari waliyemkodi. Wao walikuwa wanaenda Kilwa Kivinje kufanya kazi yao hatari! Ya kutoa mioyo ya wagonjwa kumi na tano kama ilivyo ada.

Ingawa askari Polisi walimtaka Dokta Yusha akae pale kituo cha Polisi kwa usalama wake. Lakini Dokta Yusha hakukubali kabisa, Dokta Yusha alipinga katakata. Alikuwa anataka kutoka ili akamzike rafiki yake Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, pia alikuwa anataka arudi hospitali Kilwa Kivinje kuwaona wagonjwa wake. Polisi hawakuwa na jinsi, walimruhusu Dokta Yusha atoke pale kituo cha Polisi. Katika mtaa wa National, katika nyumba aliyokuwa anaishi Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa kulikuwa na umati wa watu mkubwa sana.

Watu wengi wakilia kwa uchungu mkubwa mno, msiba huu ulikuwa msiba mkubwa sana ndani ya Kilwa Masoko. Alivyotoka kituo cha Polisi, Dokta Yusha alienda moja kwa moja msibani. Alishiriki vizuri kwenye shughuli za mazishi. Hadi Mwanasheria alivyopumzishwa katika makazi yake ya milele katika makaburi ya Sanga. Baada ya mazishi, Dokta Yusha alielekea hospitali Kilwa Kivinje ambako kundi la Six killers Don Genge nao walielekea huko. Huko wakiwa na mikakati ya kumuua yeye na Mwanasheria mlevi. Kundi la Six killers walikuwa wamejipanga vizuri sana huko Kilwa Kivinje. Kutokana na kutokuwepo kwa Tano, ratiba zao zilibadirika kidogo.

Kazi ya kumuwinda Dokta Yusha sasa alipewa Sita. Huku waliobaki walikuwa wanalinda eneo la chumba cha kuhifadhia maiti ili operesheni yao ya kutoa mioyo iliyotarajia kufanyika usiku wa siku hiyo iende vizuri. Kwa bahati nzuri siku hiyo ilitokea ajari ya basi katika kijiji cha Somanga. Ajari ilioua watu thelathini na kujeruhi saba, Six killers walikuwa na uhakika wa kupata mioyo thelathini ambayo, mara mbili ya oda yao, bahati ilioje? Saa moja usiku Dokta Yusha alikuwa anaelekea Kilwa Kivinje. Kwenda kuwaangalia watu aliowapenda sana. Ambao sasa walikuwa wagonjwa, Mkewe kipenzi Nasra, rafiki wa mkewe, Hasina na mkwe wake. Njiani roho ilikuwa inamdunda sana, bila kujua kwanini hali ile ilimtokea.

Laiti Dokta Yusha angejua anayoenda kukutana nayo huko basi angeusikiliza moyo wake, Dokta Yusha alikuwa anaenda kwenye balaa kubwa sana! Na moyo wake uliligundua hilo mapema sana. Lakini hakuusiliza moyo wake, au labda hakuuelewa moyo wake unamaanisha nini? Nusu saa ilitosha kumfikisha Dokta Yusha Kilwa Kivinje. Na moja kwa moja alienda katika wodi waliolazwa wakina Nasra. Hali ya wagonjwa wale wawili ilikuwa vilevile. Mkewe kipenzi Nasra na rafiki wa mkewe Hasina walikuwa wamelala katika usingizi ule mbaya, usingizi nzito usiojulikana mwisho wake. Huku Mzee Mpaukha naye akiwa kalala kwa kujifunika nusu shuka safi ya hospitali, shuka iliiyoiashia kifuani, uso ukiwa wazi.

Dereva alikuwa amejifunika shuka la hospitali gubigubi sawa na mgonjwa mwengine aliyelala kitanda cha pili toka pale alikolala dereva. Kumbe jirani yule alikuwa ni Sita wa Six killers, akiwa amejificha kwa kujifunika gubigubi katika kitanda kimoja katika wodi ile. akiwa amepania kummaliza Dokta Yusha kabla hajaenda katika jukumu lake lengine la usiku ule. Dokta Yusha kama kawaida yake alienda kwenye kitanda alicholala mkewe kipenzi, Nasra, alimwangalia kwa muda mkewe, bado alikuwa katika hali ya kutia shaka. Alipiga hatua chache na kukisogelea kitanda cha Hasina, nae alikuwa taabani kwa ajari ile.

Alisogea tena hadi kitanda alicholazwa Mzee Mpaukha, Mzee Mpaukha alikuwa amelala, hakutaka kumsumbua, alimshuhudia akipumua vizuri. Alikiangalia kitanda alicholazwa dereva wa Mzee Mpaukha, alimwona amejifunika gubigubi. Alikisogelea taratibu kile kitanda, alikuwa anasogea Huku akiiona kuwa kitanda cha pili kutoka kitanda cha dereva Musa nacho kulikuwa na mgonjwa aliyejifunika gubigubi kama Musa, alipanga kwenda kumwangalia nae, bila kujua dhamira mbaya ya mgonjwa aliyelala kitanda kile. Kitanda kililaliwa na Sita wa Six killers. Na lengo lake kuu ni kumuuangamiza Dokta Yusha. Dokta Yusha alifika kitanda alicholazwa dereva Musa. Aliifunua lile shuka na kumwangalia Musa usoni.

Alistuka sana! Alikuwa daktari, na hakuhitaji kifaa chochote kile kutumia ili kumpima dereva Musa, macho ya kidaktari yalitosha kumwambia kwamba alikuwa anatazamana na mtu ambaye ameshafariki ! Nguvu zilimuisha Dokta Yusha. Kwa hali aliyomuacha nayo dereva Musa, haikumuingia akilini hata kidogo kama Musa angefariki, moja kwa moja alijua kwamba ameuliwa! Kwa jinsi hali aliyoiacha, angeamini kama mkewe Nasra ama Hasina wangekuwa wamefariki, maana ndio ambao walikuwa katika hali ngumu, lakini siyo dereva Musa. Dokta Yusha Alijua kwa vyovyote vile kuna mchezo mbaya ulikuwa unaendelea mle wodini. Kwa mwendo wake uleule wa taratibu alikuwa anakisogelea kile kitanda alicholazwa mgonjwa mwengine, ambaye nae alijifunika gubigubi, au pengine alifunikwa gubigubi baada ya kuuwawa kama dereva Musa.

Bila kujua kitanda alichokuwa anakisogelea ndio kitanda alicholala Sita. Muuaji hatari toka kundi la Six killers, ambaye ndiye alimuua dereva Musa kwa kumnyonga shingo muda mfupi uliopita. Dokta Yusha alikifia kile kitanda ambacho alilala mtu hatari sana. Aliishika ile ncha ya shuka taratibu na kuanza kumfunua yule mgonjwa. Hamadi! Dokta Yusha alikuwa anatazamana na mdomo wa bastola. Moyo wa Dokta Yusha ulipiga kwa kasi sana. Kilikuwa ni kitendo cha ghafla ambacho hakukitegemea kabisa. Sita wa Six killers alinyanyuka pale kitandani na kukaa kitako. "Hongera sana Dokta Yusha, uko vizuri sana, tumeona ulichomfanyia Tano,

hongera Dokta Yusha" Sita alikuwa anaongea huku akiipangusa vumbi bastola yake kwa kutumia shuka la hospitali. "Mwisho wako umefika Dokta Yusha, nakuuwa! Ndio nitakuuwa baada ya mateso kidogo lakini" Sita aliongea kwa kujiamini sana. Dokta Yusha aliamua kutulia, alijua kuwa na wasiwasi hakutomsaidia, aliamua kuwa makini ili ajue anatoka vipi katika kisanga kile kipya. "Unaona wagonjwa wako wote wamelala, sipendi tuwasumbue, tutoke humu ndani kimyakimya nikakusulubu huko nje, sitaki niwamalize hawa kwa ujinga wako" Sita alimtahadharisha Dokta Yusha.

Dokta Yusha hakuwa na jinsi, aliongoza mwenyewe mlangoni, huku akifuatwa na Sita wa Six killers na bastola yake. Wakiwa wameongozana walifika nje, Dokta Yusha alisimama akisubiri maelekezo toka kwa Sita. "Elekea chumba cha kuhifadhia maiti" Sita alitoa maelekezo kwa sauti ya chini. Bila kujishauri Dokta Yusha alielekea katika chumba cha kuhifadhia maiti, huku akifuatwa nyuma na Sita. Dokta Yusha hakuwa anajua balaa alilokuwa anaenda kulishuhudia katika chumba cha kuhifadhia maiti. Waulikuta mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti upo wazi. Waliingia ndani. Hali aliyoikuta Dokta Yusha mle ndani ilimstua sana! Aliona maiti zimelazwa bila mpangilio mle ndani, tena sakafuni. Maiti zenye majeraha ya kutisha sana, ambayo ni ngumu kutazamwa na macho ya kawaida. Aliangalia watu aliowakuta mle ndani,

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni