Machapisho

BALAA (9)

Zephiline F Ezekiel
Jina: BALAA
Mtunzi: Halfani Sudy

SEHEMU YA TISA
ILIPOISHIA...
Waulikuta mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti upo wazi. Waliingia ndani. Hali aliyoikuta Dokta Yusha mle ndani ilimstua sana! Aliona maiti zimelazwa bila mpangilio mle ndani, tena sakafuni. Maiti zenye majeraha ya kutisha sana, ambayo ni ngumu kutazamwa na macho ya kawaida. Aliangalia watu aliowakuta mle ndani,

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
wote wakiwa makini na shughuli zao za kinyama, walikuwa hawamwangalii kabisa yeye. Macho ya Dokta Yusha yalitua kwa Dokta Sharifa, daktari wa kike alikuwa makini bila wasiwasi wowote, akiishughulikia maiti iliyolazwa juu ya meza mbele yake.

Macho ya Dokta Yusha yalitua kwa Dokta Sharifa, daktari wa kike alikuwa makini bila wasiwasi wowote, akiishughulikia maiti iliyolazwa juu ya meza mbele yake. Dokta Yusha aliitazama kwa makini ile maiti akitaka kujua Dokta Sharifa alikuwa anaifanyia kitu gani. Bila wasiwasi wowote Dokta Sharifa alichomeka kisu kwa nguvu kidogo kifuani kwa yule maiti aliyekuwa amelazwa katika kitanda kilichokuwa mbele yake.

Mwili wa Dokta Yusha ulimsisimka kwa hofu na woga, alifumba macho ili asiushuhudie unyama ule. Alipofumbua macho aliona moyo wa yule maiti ukiwa mkononi mwa Dokta Sharifa ! E bwana eee! Nesi mmoja alienda pale kwenye meza iliyolazwa maiti akiwa na deli jekundu, ule moyo ukawekwa humo. Na Dokta Sharifa alianza kuushona ule mwili. Dokta Yusha sasa alikumbuka, alikumbuka kuhusu kile kidonda alichokutwa nacho mama Mpaukha kifuani. Kumbe mama Mpaukha alifanyiwa mchezo huu mbaya, mama Mpaukha naye alitolewa Moyo! Hasira zilimpanda Dokta Yusha, mishipa ya kichwa ilimsimama huku machozi yalikuwa yanamtiririka bila kupenda.

Alitamani awauwe watu wote waliokuwemo mle ndani, lakini hakuweza, atawauwa vipi ilhali yeye ndiye aliyekuwa katika hatari zaidi ya kuuwawa! Chozi la Dokta Yusha lilimsha shangwe mle ndani. Watu wote walikuwa wanamcheka Dokta Yusha alivyokuwa analia. Dokta Yusha alijiona kama yupo katikati ya mashetani wenye roho mbaya. Alipangusa machozi kwa kutumia kiganja chake cha mkono wa kushoto. Aliwaona manesi wawili wakichagua maiti nyingine pale chini, ilikuwa mithili ya wanunuzi wakichagua nguo katika soko la Tandika. Wakaipata maiti wakiyoitaka. Wakaibeba na kuipeleka kwenye ile meza iliyokuwa mbele ya Dokta Sharifa.

Dokta Sharifa aliendelea na kazi yake huku akitabasamu. Kwa mara nyingine tena, daktari katili wa kike Sharifa Juma alichomeka kile kisu chake kifuani mwa ile maiti mwengine. Aliifanyia kama alivyoifanyia ile maiti ya awali. Safari hii Dokta Yusha alithubutu kuangalia, aliangalia kila hatua ya kikatili iliyofanywa na mabaradhuli wale. Alibaki anatikisa kichwa tu kwa masikitiko. Hakutegemea kabisa kama kitendo kile cha kikatili kinafanywa na daktari wa kike anayeheshimika zaidi wilayani Kilwa, Dokta Sharifa. Ama hakika hali ilikuwa ya kusikitisha sana. Dokta Yusha aliangalia upande wake wa kulia, alimwona Dokta Zaidi Kilumba akiwa ametulia tuli kitini. Akitabasamu huku akimwangalia Dokta Yusha kwa dharau.

"Una dhamana kubwa sana Dokta Kilumba, umeaminiwa na Taifa kuiongoza hospitali hii, kuwahudumia wananchi maskini, tena wagonjwa. Kinachofanyika hapa siyo haki Dokta Kilumba. Ndio! Hii siyo haki kabisa Dokta, kwanini unafanya hivi vitu ? Kumbuka maadili ya kazi ya udaktari, Kumbuka kiapo ulichoapa Dokta, kinafanana na kinachofanyika hapa Dokta?" Dokta Yusha alisema kwa hisia na uchungu mkubwa sana. "Hahaha eti maadili ya kazi, hahaha eti kiapo cha udaktari, kiapo cha udaktari nd'o nini, kwa taarifa yako hii kazi tumelipwa hela nyingi sana! Tofauti na hizo zinazowafanya madaktari wagome kila siku.

Unazungumzia maadili ya kazi, hivi kuna maadili mbele ya pesa?" Dokta Kilumba alikuwa anaongea akiwa amekaa palepale katika kiti, anaongea bila wasiwasi wowote. "Mtalipa Dokta kwa huu unyama mnaofanya hapa, naapa mtalipa!. Hata mkiniua mimi kizazi kijacho kitakuja kulipa damu za watu hawa wasio na hatia!" Dokta Yusha munkari ulianza kumpanda. "Tulipe damu gani Dokta Yusha wakati hawa wameshakufa, hizi ni maiti Dokta?" "Usibishane nae, yeye tunamtoa moyo leo akiwa anajiona. Ili tulipe vizuri hizo damu anaozisema huko mbinguni kama kupo!" "Mletee hapa!" Sita akamshika mkono na kumvuta. Kumpeleka pale alipo Dokta Kilumba.

Alipofikishwa pale ndipo Dokta Yusha alimuona mtu mwengine kabisa, ambaye hakuwa amemuona pindi alipoingizwa mle ndani. Na hakuwa amemuona kabisa katika maisha yake. Mzee mwenye sura ya kikorofi, alikuwa na sharubu mithili ya Karl Peter's 'mkono wa damu'. Mzee mwenye mwili uliojengeka kimazoezi, mrefu sana, kwa majina alikuwa anaitwa Don Genge. Dokta Yusha alidhani ile sauti ya kuitwa imetoka kwa Dokta Kilumba, la hasha. Haikuwa hivyo, kumbe alikuwa ni jasusi Don Genge mwenyewe. "Hahaha hiki ndio kifaranga kinachowasumbua?" Don Genge aliuliza kwa kejeli huku akiubinua kwa juu mdomo wake mpana.

"Ama kweli maajabu hayana mwisho duniani. Wewe ndio umemvunja goti komando Tano? Kwa nguvu gani ulizonazo mpumbavu wewe, kwa akili gani ulizonazo mjinga wewe? Don Genge alikuwa anauliza maswali bila ya kusubiri majibu toka kwa Dokta Yusha. Kamtie kwenye gari tuondoke nae kambini tukaone uwezo wake mpaka Komando Tano ashindwe kumkamata na kuambulia kuvunjwa goti." Kwa haraka Sita alimsukasuka Dokta Yusha na kumpeleka kwenye gari. Gari aliloingizwa dokta Yusha ni yale magari yenye bodi zenye visanduku nyuma. Mara nyingi hutumika katika mahospitali kusafirishia dawa. Kundi la Six killers nao walikuwa wanautumia gari aina hiyo kusafirishia mioyo. Na leo hii gari hiyohiyo ilitumika kama mahabusu inayotembea kwa Dokta Yusha.

Ndani ya kile kisanduku kulikuwa na giza totoro, pia kulikuwa na joto sana, maana hakukuwa na uwazi wa kupitisha mwanga wowote katika kisanduku hiko. Kilikuwa kisanduku kidogo sana kilichompa shida sana Dokta Yusha. Ilimbidi ajikunje sana ili akae vizuri mle ndani ya gari. Hakukaa vizuri lakini alikaa. Baada ya nusu saa alisikia kelele za miguu ya watu ikielekea pale kwenye gari aliyokuwa ndani yake. Mara alisikia mlango wa ile bodi ukifunguliwa. Ulifunguka. Yule jamaa aliyetambulika kwa jina la komando Sita aliingia na kuweka deli, deli la kuhifadhia mioyo ya maiti. Baada ya kuweka lile deli jekundu yule jamaa alitoka nje. Kile kisanduku kikafungwa tena. Giza likarejea kwa kasi! Akiwa kule nyuma ya gari alisikia gari likiwashwa.

Na safari ya kuelekea kusikojulikana ilianza. Gari lilitembea sana, takribani saa sita lilikuwa halijafika lilikokuwa linaenda. Dokta Yusha aliamini safari ile ilikuwa ni nje ya wilaya ya kilwa, au nje ya mkoa kabisa. Maana hakukuwa na sehemu ndani ya kilwa ya kutembea saa nyingi namna ile. Sasa alianza kulizoea giza, na kuyaona vizuri mandhari ya kule nyuma kwenye kisanduku. Kwenye sakafu ya gari ile, aliyaona madeli matatu yakiwa yamewekwa pamoja. Hakujua ni madeli ya nini, ingawa alihisi yatakuwa ya mioyo. Dokta Yusha hakutamani hata kuhangaika kuyafungua. Aliangazaangaza mle ndani ya gari, hakuona kitu kingine zaidi ya yale madeli mekundu.

Mara gari lilisimama, ishara kuwa lilikuwa limefika ilikokuwa inaelekea. Saa zaidi ya nane walizitumia barabarani. Ilichukua kama robo saa ndipo akaja kufunguliwa kule nyuma. Dokta Yusha akaona tena mwanga halisi wa dunia. Alishuka mwenyewe bila kuambiwa. Alikuwa amechoka sana kukaa mle ndani ya kisanduku. Joto kali ndani ya kisanduku na kukosa hewa kulimuadhibu barabara Dokta Yusha. Alishuka chini, alikutana na nyumba ndogo ya kisasa. Nyumba iliyonakshiwa kwa rangi ya bluu. Huku chini kukiwa na michirizi ya rangi nyeusi.

Juu iliezekwa na bati za vigae toka Afrika ya Kusini. Nyumba hiyo ilikuwa imezungukwa na ukuta mkubwa sana wenye rangi ya bluu pia. Ulikuwa ukuta mrefu ulioipita hadi nyumba yenyewe. Yaani kama mtu akiwa kwa nje ataishia kuuona ukuta tu. Hatuiona nyumba ile. Dokta Yusha aliingalia kwa makini nyumba ile huku akiangalia mandhari ya sehemu ile. Alikiri kuwa hakuwahi kufika hata siku moja mahali pale. Hakujua kabisa nyumba ile ilikuwa mahali gani ndani ya nchi ya Tanzania?

Sita wa Six killers alimshika mkono Dokta Yusha na kuizunguka nyumba ile kuelekea nyuma kwa kupitia mkono wa kushoto. Walipofika uwani Dokta Yusha macho yake yalitazamana na kibanda kidogo mithili ya stoo. Sita alifungua kile kibanda kwa funguo na kumsukumia Dokta Yusha mle ndani.

Kilikuwa ni kibanda kidogo kwa nje, na ndani pia. Dokta Yusha alisimama hatua kama mbili toka katika mlango wa kile chumba na kuanza kukiangalia. Kilikuwa ni chumba ambacho hakukuwa na kitu chochote zaidi ya kiti kimoja tu cha chuma. Kuta yake ilipakwa rangi nyekundu ambayo ilikuwa inaumiza macho ukiitazama muda mrefu.
Dokta Yusha alipiga hatua za taratibu kuelekea katika kile kiti. Alikuwa na lengo la kwenda kukikalia kiti kile. Maana hakukuwa na sehemu nyingine ya kukaa zaidi ya kwenye kile kiti. Alikikaribia kabisa kile kiti, alitaka kukaa lakini aligairi. Alikitilia mashaka kile kiti. Kwanini kile kiti cha bati kiwekwe katika chumba kile, ni kweli kimewekwa kwa lengo la kukalia tu? Au kuna lengo lengine, siku zote wasiwasi akili. Dokta Yusha hakukaa, alirudi kinyumenyume hadi ukutani. Akakaa chini taratibu huku akikiangalia kwa makini kile kiti cha chuma.

Dokta Yusha alikaa pale chini sakafuni huku akitafakari mustakabari wa maisha yake. Aliona mambo yamebadirika kwa kasi sana, tena yakianzia siku ya sherehe ya ndoa yake.
Aliwakumbuka wagonjwa aliowaacha hospitali. Mkewe kipenzi Nasra, rafiki wa mkewe, Hasina na mzee Mpaukha, alijua watakuwa katika hali ngumu sana kwa kutokuwepo yeye, pia alijua jinsi walivyoikaribia hatari ya kutolewa mioyo na wale mabaradhuli. Alimfikiria dereva wa Mzee Mpaukha, Musa akijua kwa vyovyote kwa sasa atakuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, akisubiri kutolewa moyo .

"Kwanini moyo? Itakuwa wanafanyia nini hiyo mioyo? Tena bila shaka mioyo ya maiti ndiyo inayohitajika ndio maana wameweka kambi hospitali tena katika chumba cha kuhifadhia maiti. Lazima nijue undani wa sakata lile, na Lazima nihakikishe watu hawa wenye nia mbaya wanafikishwa katika vyombo vya sheria" Dokta Yusha aliwaza hayo bila ya kujua yupo sehemu hatari kiasi gani, bila kujua atatoka vipi ili akawafikishe katika vyombo vya sheria ilihal alikuwa tunduni akisubiri adhabu yake, bila shaka adhabu ya kifo!

Wakati akiwaza hayo alisikia mlango ukifunguliwa kwa nje. Ukafunguka kidogo na mtu mpya alisukumwa kwa nguvu kuingizwa mle ndani. Dokta Yusha alimwangalia vizuri mtu yule walitambuana.

"Wamekuleta huku Dokta"

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni