Mtunzi: Hassan S. Kajia
SEHEMU YA KWANZA
JOHN AMIGOLAS YUKO MAHABUSU BAADA YA KUKUTWA AKIWA NA MWILI WA MFANYABIASHARA MAARUFU, GULAM, MARA BAADA YA KUPIGWA RISASI NA MAJAMBAZI AMBAO WALIMVAMIA NA KUCHUKUA PESA ZAKE ZOTE NA KUKIMBIA NAZO HUKU WAKIMPIGA RISASI NA KUMUUA. JOHN ANASHIKILIWA NA POLISI.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
ASUBUHI ya siku hiyo John alikuwa amesimama peke yake.nywele zikiwa timtim huku amepauka baada ya muda mrefu wa kutokuoga na mgomo wa kutokujishughulisha na chochote hadi atakapopata hatma ya jambo lililomleta hapo.
Mawazo yalikuwa yakimwandama baada ya usingizi wa mang’amung’amu ambao alikuwa hajauzoea. Hakuna aliyejali. Labda kwa kuwa hawakupewa taarifa juu. Juu ya hali aliyonayo. Hakuna aliyejua ni nini kilichomkumba.
Alipiga ndoo teke. Ndoo iliyokuwepo karibu na sehemu aliyokuwa amelala. Sababu za yeye kuwepo hapo pamoja na ndoo havikumwingia akilini. Alivuruga kitanda na kukaa chini huku akiwa ameshika kichwa chake.
Hasira zilikuwa zimempanda sana John ambaye alikuwa mahabusu kwa wiki moja sasa bila ya kupewa dhamana. Aliumia zaidi baada ya kuona hakuna msada wowote na kwamba alidhaniwa kwamba yeye ndiye aliyemuua mfanyabiashara mmoja wa magari.
Hiyo ni baada ya polisi kumwona yeye kwani ndiye aliyekutwa katika eneo la tukio pasipo kuwepo mtu mwingine. Eneo ambalo damu zilikuwa zimetapakaa baada ya watu wenye silaha kumvamia mfanyabiashara aliyekuwa tayari amekufa akiwa amelala chini.
Mfanyabiashara huyo, Gulam alikuwa akielekea benki kuweka fedha zake na mara alijikuta akiishia mikononi mwa watu wanne waliokuwa na bastola. Walimvamia na kumwibia hela zote na kisha kumuua. Watu hao walifanikiwa kukimbia na gari yao aina ya Mark II pasipo kukamatwa.
Katika kuwahi kumwokoa, John alikuta yule mfanyabiashara tayari ameshakata roho. Alijaribu kuwaita watu ili kusaidiana lakini baada ya mlio wa risasi kusikika watu walitawanyika na hivyo John alibaki pale peke yake hadi polisi walipofika dakika chache.
John alikuwa na bastola yake ambayo aliitoa mara tu baada ya kusikia mlio ule na kuishika. Hali hiyo alipelekea polisi kumkamata kwa kumshukia kwamba ni yeye aliyefanya mauaji yale baada ya kukutwa.
Bastola aliyokuwa nayo alikuwa akiitembea nayo siku zote kwani alikuwa na kibali cha kuimiliki. Wakati wa tukio hakuweza kuonyesha kibali na hivyo alifungwa pingu katika mikono yake.
Sasa aliishia mikononi mwa polisi kwani majambazi wale walifanikiwa kutoroka na pesa za mfanyabiashara yule. Alijaribu kujielezea kwamba siye yeye aliyefyatua risasi ile lakini polisi hawakumwelewa. Alipelekwa kituo cha polisi cha kati kwa ajili ya mahojiano na kupisha uchunguzi.
Gari lake aina ya Land Cruiser V8 liliachwa karibu na benki ambapo mauaji yalitokea. Hakujali na wala hakuwajulisha ndugu zake walifate. Aligundua kwamba alikuwa amelifunga vizuri na hivyo alielekea polisi.
*****
John hakujua lililoendelea nyumbani kwao kwani alijua si rahisi ateseke mahabusu wakati Mzee wake anaweza kumwekea dhamana akawa huru. Akiwa bado kituoni ndani, siku inayofuata alipata taarifa juu ya kifo cha Mzee wake Amigolas. Baba yake mzazi. John alichanganyikiwa sana hadi kupoteza fahamu.
Hakuwa amemini kama ni kweli baba yake amefariki dunia. Baadhi ya askari walimsaidia kumpepea hadi akazinduka, alizinduka akiwa hajitambui vizuri. Bado alikuwa haamini kama ni mzee Amigolas aliyefariki.
"Amigolas, baba... Amigolas...baba," ndio majina yaliyokuwa yakitajwa na John siku nzima. Hakujua juu ya familia yake kwani taarifa zilizokuja zilikuwa za baba yake kuuliwa.
Polisi walimwonea huruma lakini asingeweza kuachiwa kwenda kuona hadi uchunguzi wa tukio lake utakapokamilika.
Hakuna mtu aliyejua lolote kuhusu John kwani siku hiyo ndo siku ambayo nyumbani kwa kina John palipata pigo kubwa sana. Ni siku hiyohiyo John alikuwa aachiwe huru baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa si yeye aliyeua.
“John aachiwe huru,” mkuu wa kituo alitoa kauli hiyo baada ya kupiga simu na kuongea na Afande Mushi.
"Naomba hilo file la John Amigolas, anatakiwa aje aweke saini. Na umtoe huko ndani. Taarifa kutoka kwa mkuu zinasema kwamba si yeye aliyeua. Afande Nicco, kamtoe huko aliko umlete hapa," Afande Mushi alitoa amri na kusisitiza kwa afande Nicco ambaye alileta faili la John na kwenda kumtoa. Alikabidhiwa vitu vyake na kuruhusiwa japo alikuwa akionekana kutojitambua.
Alitoka nje ya Kituo cha polisi. Aliangalia uelekeo na kwanza alitaka kulifuata gari lake. Alitaka kujua ni kina nani waliotekeleza mauaji kwa baba yake na ni kwa sababu gani. Gari lake lilikuwa limeshaletwa hadi kituoni. Aliingia na kuwasha.
Aliifuata Barabara ya Uhuru kuelekea Hospitali ya Mount Meru, hospitali kubwa jijini Arusha. Alijua kwamba mwili wa baba ake utakuwa umehifadhiwa huko. Hakutaka hata kurejea kwanza nyumbani kwani angechelewa kupata uthibitisho kwa kuona kweli mwili uliopelekwa hospitali ni wa baba yake Mzee Amigolas.
Alifika hospitali na kukuta umati wa watu ukiwa unafuatilia juu ya maiti zilizoingizwa hospitalini hapo asubuhi. Alisikia tu minong’ono ya watu ambao walikuwa wakisikitika kutokana na kuona maiti zikiingizwa na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti.
Alisogea na kukutana na mmoja wa majirani zao ambaye alishirikiana na polisi kuzileta maiti hospitali hapo.
"Gaudence, ni...ni kweli maiti iliyoletwa ni ya baba yangu, tafadhali naomba niambie, we ni kama ndugu yetu. Tafadhali Bwana Gaudence,” John alikuwa akimuuliza Gaudence ambaye ni mmoja wa majirani zao huku akilia kwani alijua kuwapo tu kwa Gaudence hospitalini hapo kunadhihirisha ya kwamba mzee Amigolas amefariki kweli.
"Pole sana John, ni kweli na si baba tu, wameuliwa pia ndugu zako pamoja na mama yako Magdalena.”
"Unasemaje?” John aliishiwa nguvu na kukaa chini huku akilia. Gaudence alimsaidia kumwinua na kumpeleka katika gari lake alilokuwa amefika nalo hospitali.
“Usilie bwana John. Jikaze….hii ni kazi ya Mungu. Tuko pamoja.”
“Ina maana na wadogo zangu Isack, Neema na Jenipha?”
“Ndiyo John, wameshapelekwa chumba cha maiti, tunachosubiria ni taarifa za polisi kama watu waliowaua wanajulikana na itatangazwa pia katika vyombo vya habari baada ya uchunguzi,” Gaudence alimwambia John ambaye muda wote alikuwa amejiinamia huku akilia.
Aminata alikuwa ameshafika hospitali. Alikuwa anazunguka huku akifatwa na waandishi wa habari, alikuwa akielekea ndani kuonana na daktari mkuu wa hospitali hiyo. Baada ya muda alirudi akiwa anaangaza huku na huko. John alimtazama. Alihisi kukumbuka kitu lakini machungu ya kumpoteza mzee wake hayakumpa nafasi ya kutafakari lililotokea.
Aminata alimfuata baada ya kujua kuwa ni John. Alimfuata ili kuthibitisha.
"Habari yako kaka?” Aminata alimsalimia John ambaye alikuwa akimwangalia muda wote.
“Salama tu dada, karibu,” John alipata picha juu ya Aminata, alikumbuka kwamba alishawahi kumwona akiwa ameongozana na polisi wakati akikamatwa na baada ya hapo hakumwona tena hadi alipoachiwa huru.
“Inawezekana huyu ni mpelelezi,” aliwaza John huku akimwangalia Aminata aliyekuwa tayari amefika alipokuwa John.
“John, nadhani ndiyo wewe,” Aminata alimuuliza John jina lake kama kuthibitisha kweli alikuwa ndiye John mtoto wa Amigolas.
“Yes, ndiyo mimi. Kuna tatizo na mimi dada,” John hakuelewa Aminata alichomaanisha. Ndiyo kwanza ametokea mahabusu na sura ya Aminata aliikumbuka tayari. Hakujua Aminata alikuwa anashida gani na yeye.
"Nahitaji ushirikiano wako, baada ya kumaliza mazishi naomba unitafute,” Aminata alimaliza kuongea na kuondoka kulifuata gari lake. Aliwasha na kuondoka. John aliachwa na maswali kichwani. Alitakiwa amtafute Aminata baada ya mazishi ya ndugu zake.
*****
Taarifa za vifo zilimfikia Antony ambaye alikuwa nchini Kenya. John ambaye ni pacha wake, alimfahamisha na hivyo Antony alipanga kurudi kumzika baba yake pamoja na ndugu zake. Maumivu yalikuwa makubwa sana kuwapoteza.
Baada ya siku mbili Antony aliwasili akitokea Nairobi nchini Kenya ambako alikuwa akifanya shughuli zake za biashara huko. Mzee Amigolas alikuwa amefungua maduka makubwa ya vitu mbalimbali vya umeme na nguo za kifahari. Maduka hayo yalisimamiwa na Antony.
Antony aliungana na ndugu zake katika mazishi huku akiwalilia sana. Ulikuwa ni msiba mzito sana kwa John na Antony ambao walibaki wenyewe. Antony alilia sana. Hakuamini macho yake kwa kuwapoteza watu wake wa karibu. Watu wengi walifika nyumbani kwa marehemu Mzee Amigolas. Na hii ni kutokana na kuwa maarufu kutokana na biashara zake.
Mzee Amigolas alikuwa ni mfanyabiashara maarufu wa madini aina ya Tanzanite. Alimiliki mgodi mkubwa wa madini hayo huko Mererani. Alikuwa ni tajiri mkubwa sana ambaye kutokana na utajiri wake na umaarufu wake, aliweza kushirikiana na matajiri wenzake kusafirisha madini nje ya nchi na kuyauza.
Utajiri wake ulijulikana kwa watu wengi. Alikuwa amewekeza kwa kujenga nyumba nyingi na hoteli mbalimbali mkoani Arusha pamoja na mikoani kama Dar ea Salaam. Pia maduka makubwa ya biashara nchini nan je ya nchi. Alikuwa ana nyumba kubwa sana maeneo ya Njiro aliyoishi pamoja na familia yake.
Alimuoa Magdalena na kufanikiwa kupata watoto watano yeye na pacha wake Antony, Isack, Neema pamoja na Jenipha.
Nyumba yake ilikuwa kubwa sana na yenye ulinzi mkali sana. Alimiliki magari mengi ya kifahari ambayo yalitumiwa zaidi na watoto wake. Watoto wake wawili mapacha John na Antony walikuwa wakisimamia baadhi ya biashara za baba yao. Antony ambaye ndiye aliyekuwa mdogo. Alikuwa akisimamia biashara za baba ake nchini Kenya. Wadogo zao Isack, Neema na Jenipha walikuwa wakisomea nchini Uingereza. Waliishi huko na mama yao Magdalena.
Hadi mauti yanawakuta, walikuwa likizo kwa ajili ya sikukuu ya Chrismass na Mwaka Mpya. Hawakuwa na taarifa juu ya kuvamiwa usiku kwani wauaji walianza kuwaua walinzi wawili pamoja na mbwa wao kwa kuwapiga risasi kabla ya kufanikiwa kuingia ndani. Hakuna aliyesikia sauti ya risasi kwani walikuwa wameweka viwambo vya kuzuia sauti isitoke. Na huo ndiyo ukawa mwisho wa kuonana na ndugu zake ambao wote waliuliwa.
Hakuna taarifa za kukamatwa kwa wahusika japo polisi walikuwa wakiendelea na uchunguzi. Alitaka kumuuliza John kaka yake kama alikuwa akijua lolote linaloendelea kuhusiana na vifo hivyo.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi