
Mtunzi: Juma Hiza
SEHEMU YA PILI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
"Amefanyaje?" aliniuliza Daniel kisha nikaanza kumsimulia kila kitu. Nilipomaliza kumsimulia nikamuona akivuta pumzi ndefu na kuziachia kwa pupa, kama ilivyokuwa kwa Baba yake na yeye pia hakutaka kuamini, kitendo cha kuwachanganya kimapenzi na Baba yake kilimuumiza mno.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
Nilishangazwa na maamuzi aliyoyachukua Daniel, hakutaka kuendelea kuushuhudia uchafu kama huo ukiendelea mbele yake, alichoamua kukifanya ni kuniambia kuwa siku hiyo ndiyo ulikuwa mwanzo na mwisho wa mapenzi yetu, hakutaka kusikia nikimuita mpenzi tena.
Niliumia sana baada ya Daniel kuchukua maamuzi hayo, mtu ambaye niliamini ndiye angeweza kuwa msaada wangu kwa wakati huo hakutaka kunisikia hata mara moja.
Maisha yalibadilika ndani ya nyumba, kila siku nilikuwa ni mtu wa kumuomba Mungu aninusuru na mabaya ambayo yangeweza kunitokea. Nilifahamu hapakuwa na amani tena, kuanzia Baba na Mtoto wote walikuwa na visasi juu yangu, hawakunitazama kwa macho ya wema tena, nilionekana kuwa mbaya tena adui mkubwa ambaye walitakiwa kuniepuka.
Vitisho havikuishia hapo, Mzee Gidion aliendelea kunitishia kuniua kila kukicha, wakati mwingine alikuwa akiniambia ni lazima niondoke katika nyumba yake nikiwa maiti ndani ya jeneza.
Wakati yote haya yakiendelea mke wake alikuwa hafahamu lolote, iliendelea kubaki siri katika moyo wangu mpaka pale nilipoanza kukosa uvumilivu, nilitishiwa sana, sikuwa na amani tena katika moyo wangu, uhuru wangu wote ulipotea, nilikuwa nikiishi maisha kama ya mfungwa aliyetoroka gerezani.
Wazo la kutoroka likanijia kichwani, nilichokuwa nikikiwaza kwa wakati huo ni kutoroka na kwenda mbali. Sikuwa mwenyeji wa jiji la Daresalaam, tangu nilipoweza kufika kwa mara ya kwanza maisha yangu yote yalikuwa ni ya kukaa ndani, labda siku moja moja za wikiendi niliweza kupata bahati ya kupelekwa katika fukwe za Coco ambapo hata njia ya kufikia huko nilikuwa siifahamu.
Nadhani unaweza ukaona ni kwa jinsi gani nilivyokuwa mgeni katika jiji hili. Wakati ambapo nilikuwa sifahamu mtaa hata mmoja tayari nilikuwa nimejiwa na wazo la kutoroka. Unafikiri nilifanikiwa katika mpango huu? Jibu ni hapana, niliendelea kujiuliza maswali ambayo yalizidi kuniumiza kichwa.
Ni katika kipindi hicho ambapo kumbukumbu za nyumbani kwetu zikaanza kunijia, nilipakumbuka mno, nilitamani kuambiwa kuwa nilitakiwa kurudi nyumbani kwetu lakini jambo hilo halikuweza kutokea hata mara moja.
Nitaishi maisha ya vitisho mpaka lini? Hili lilikuwa ni swali lililoniumiza usiku na mchana, nilikosa wa kumsimulia maisha niliyokuwa nikiyapitia kwa wakati huo.
Baada ya kupita mwezi mmoja huku nikiendelea kuishi maisha ya vitisho, siku moja majira ya usiku Mama Daniel aliniita na kuniambia kuwa alifahamu kila kitu kilichokuwa kikiendelea, aligundua kuwa nilikuwa nikitembea na mume wake jambo ambalo lilimuumiza mno.
"Mwajuma msaada wangu wote niliyokusaidia katika maisha yako leo umeamua kunilipa kwa kutembea na mume wangu kweli?" aliniuliza, wakati huo machozi yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake.
"Hapana Mama nili...." kabla sijamaliza kuzungumza alinikata kauli, nilishtukia nikipigwa kofi moja zito lililoniyumbisha, wakati nikiendelea kuugulia maumivu ya kofi, hakuishia hapo, alianza kunipiga kila sehemu ya mwili wangu huku akinilaani kwa kitendo nilichomfanyia. Nilipata maumivu makali mno, siwezi kuyaelezea maumivu niliyokuwa nikiyapa, nililia sana, nilimuomba kila aina ya msamaha lakini sikuweza kuambulia jibu lolote zaidi ya kipigo kikali kama cha mbwa koko na mwisho wa siku aliweza kunifukuza.
Nilifukuzwa kama mbwa usiku huo, nilitupiwa begi langu la nguo na kupewa kila kilichokuwa changu. Nililipwa pesa yangu ya mshahara wa mwezi uliyopita niliyokuwa nikidai pamoja na mwezi huo ambao niliweza kulipwa nusu yake.
Hakukuwa na mtu ambaye alinisaidia siku hiyo, nilionekana kuwa mbaya kupita kawaida, niligeuka kuwa adui. Kuna muda nikatamani nimwambie kila kitu kuhusu mume wake lakini nilikosa muda huo, tayari nilishafukuzwa na sikuhitajika tena kuwemo katika familia hiyo.
Sikujua nilitakiwa kwenda wapi usiku huo, nilipolifikiria hilo nikazidi kuchanganyikiwa.
Nilijutia mambo mengi mno lakini kubwa nililolijutia ni hili la kutembea na mume wa mtu, tamaa yangu ya pesa iliniponza na kuniweka katika wakati mgumu ambao sikutegemea kuupitia.
Machozi yalikuwa yakinidondoka muda wote, kila hatua niliyokuwa nikiipiga njiani nilipishana na watu wengi, baadhi yao walinishangaa kutokana na muonekano niliyokuwa nao, ulitosha kabisa kunielezea kuwa nilifukuzwa na muda huo nilikuwa katika safari nisiyoifahamu mwisho wake.
Nilitembea umbali mrefu sana mwisho nilichoka, sikuwa nikifahamu sehemu hiyo au mtaa huo niliyokuwepo uliitwaje.
Niliwaona wanaume wawili wakinifuata nyuma yangu, mwanzo sikutaka kuogopa kitu kwani kulikuwepo na watu wengi niliyopishana nao hivyo niliamini kuwa salama lakini nilipofika eneo hilo nilishangaa nikiwa peke yangu, hakukuwa na mtu niliyepishana naye zaidi yangu na hao wanaume wawili waliyokuwa wakinifuata.
Nilianza kuingiwa na wasiwasi baada ya kuwaona wakizidi kukazana kunifikia, moyo wangu ukalipuka paaa!! hofu ikanitawala, mapigo ya moyo wangu yakaanza kunienda kasi.
"Habari yako binti," alinisalimia mwanaume mmoja huku yule mwingine nikimuona akiangalia huku na kule, nilifahamu hawakuwa na nia nzuri na mimi. Hofu ikazidi kunitawala.
"Nzuri," nilijibu huku nikitetemeka.
"Mbona unaogopa usiogope sisi ni watu wazuri unaitwa nani?" aliniuliza yule mwanaume mwingine.
"Naitwa Mwajuma,"nilimjibu.
Walitazamana kisha wakapeana ishara fulani, sikujua walimaanisha nini ila nikashangaa wakinisogelea, ghafla! yule mwanaume wa kwanza akanirukia na kunikaba, nilishtukia nikipigwa na ubapa wa panga kwenye paja na kuambiwa nisipige kelele na endapo kama ningekiuka agizo hilo ningeweza kuuliwa, niliogopa mno, nilibaki nikiugulia maumivu ya ubapa wa panga pamoja na kabali niliyokuwa nimepigwa.
Yule mwanaume mwingine alianza kunisachi, akachukua simu, pesa pamoja na lile begi la nguo. Alipojiridhisha kuwa alifanikiwa kuchukua kila kitu changu alimpa ishara mwenzake na ndipo hapo alipoweza kuniachia.
"Sasa sikia wewe fala ukipiga kelele tunakuua, kaa kimya hivyohivyo," aliniambia kisha akanitukana tusi la nguoni.
Nikabaki kimya huku nikiendelea kuugulia maumivu niliyoyapata. Wale wanaume wakakimbia eneo hilo.
Wakati nikiendelea kuugulia maumivu huku nikiwa sijui nini nifanye mara akatokea mwanaume mmoja ambapo aliponiona alinifuata na kuniuliza nilikuwa na tatizo gani?
"Nimeibiwa kaka yangu, wameniibia," nilimwambia huku nikionekana kuchanganyikiwa.
"Embu subiri kwanza akina nani hao wamekuibia?" aliniuliza.
"Siwajui, siwajui kaka angu" nilimjibu huku nikianza kulia.
"Usilie sasa taratibu niambie kwanza unatokea wapi na unaitwa nani?"
"Naitwa Mwajuma nimetokea huko nilipokuwa nafanya kazi za ndani."
"Wapi?"
"Kijitonyama."
"Sasa huku umekuja kufanyaje?"
"Wapi?"
"Kwani unajua hapa upo wapi?"
"Hapana sijui kaka angu kwani hapa ni wapi?
" Tandale," alinijibu kisha akaanza kunionea huruma,
"Umesema umetokea Kijitonyama?'
" Ndiyo."
"Kwanini sasa wamekuruhusu kuja sehemu kama hii usiku?"
"Hapana nimefukuzwa," nilimjibu kisha akaonekana kunihurumia zaidi.
Mpaka kufikia muda huo nilikuwa bado sijalifahamu jina lake, alinitazama kama niliumia sana lakini hakukuwa na majeraha niliyoyapata zaidi ya kuugulia maumivu ya ndani kwa ndani. Hakutaka kuona nikiendelea kubaki eneo hilo kwani aliniambia mtaa huo palikuwa na vibaka wengi sana, hakuishia hapo alizidi kunipa sofa mbaya za mtaa huo hivyo kitendo cha mimi kuendelea kuwepo mahali hapo kingeweza kunihatarishia maisha yangu.
Baada ya kusikia kuwa nilifukuzwa na sikuwa na mahali pa kwenda usiku huo, alihitaji kunisaidia. Aliniambia alikuwa akiishi peke yake hivyo kama nisinge jali anichuke na kwenda naye kwake usiku huo.
Kiukweli sikuweza kumkubalia kirahisi, nilihofia mambo mengi mabaya ambayo angeweza kunifanyia lakini baada ya kunohakikishia kuwa ningekuwa salama na kuniondoa hofu ilibidi nimkubalie. Akanichukua na kunipeleka mpaka kwake.
Kilikuwa ni chumba kimoja, nilipofika nilifikiria ni jinsi gani ambavyo ningeweza kulala humo lakini hilo halikuwa tatizo. Yule mwanaume aliniambia kuwa nilitakiwa kulala kitandani na yeye angelala chini na maisha yangeendelea hivyo.
Ngoja nikuambie kitu msichana mwenzangu, kijana mwenzangu unayeisoma simulizi hii. Unajua kwenye haya maisha unaweza ukakutana na vikwazo vingi lakini baadhi ya watu wanaokutazama wakakuchukulia kuwa hayo yote unayopitia ni haki yako, wengine wanaweza kwenda mbali zaidi na kukutukana na kukulaumu kwa ujinga uliyoufanya.
Yote haya yanaweza yakatokea katika maisha na kitu unachotakiwa kukifanya ni kujua ni jinsi gani ambavyo unatakiwa kupambana nayo na si muda wa kujilaumu na kuona kama wewe ni mkosani mbele za Mungu na hutakiwi kusamehewa.
Kwanini nakwambia haya ni kwasababu ya makosa niliyoyafanya katika maisha yangu, ujinga niliyoufanya, sitaki urudie makosa yangu sitaki urudie kufanya ujinga wangu, nataka ujifunze kitu kupitia simulizi hii ya maisha yangu.
Angalia kwa muda ambao niliweza kukutana na mwanaume ambaye hata sikuwa nikilifahamu jina lake tayari nilimuamini, niliukubali msaada aliyohitaji kunipa, bila kufuata taratibu zozote nikajikuta nikiingia ndani kwake na maisha yakaanzia hapo.
Mwanzoni alionyesha moyo wa kunisaidia kweli, aliguswa na simulizi yangu ya kufukuzwa, hakujua nini kilisababiaha ila moja kwa moja aliamini nilionewa hivyo alihitaji kunisaidia.
Maisha yalianzia hapo huku kila siku mwanaume huyo akiniaga kwenda kwenye mihangaiko yake. Aligeuka kuwa msaada mkubwa sana kwangu, alinihudumia kwa kila kitu nilichokuwa nikikihitaji, maisha yalikuwa rahisi kwangu.
Ama kwa hakika penzi ni kikohozi kama wasemavyo wahenga, baada ya kupita siku kadhaa nikajikuta nikiwa katika mahusiano na mwanaume huyo ambaye nilifanikiwa kulifahamu jina lake tayari. Nakumbuka alijitambusha kwa jina la Oscar, ni katika penzi hili ambalo lilienda kunipa funzo lingine jipya la maisha yangu.
Nilijikuta nikizama kwenye dimbwi la kimapenzi na Oscar, huyu alikuwa ni mpiga picha, alikuwa akimiliki studio yake ya picha iliyokuwepo Sinza Palestina.
Kimuonekano alikuwa ni kijana mtanashati, kiukweli nilitokea kumpenda kwa moyo wangu wote. Kipindi nipo katika mahusiano naye nilisahau shida na matatizo yote niliyokutana nayo katika maisha yangu,
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi