
Mtunzi: Juma Hiza
SEHEMU YA TATU
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Kimuonekano alikuwa ni kijana mtanashati, kiukweli nilitokea kumpenda kwa moyo wangu wote. Kipindi nipo katika mahusiano naye nilisahau shida na matatizo yote niliyokutana nayo katika maisha yangu,
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
sikutaka kukumbuka kitu chochote kilichotokea nyuma.
Oscar alinipenda sana, ahadi zake za kunioa ndizo zilizonifanya nikazidi kumuamini mara dufu, bila kujali nikamkabidhi mwili wangu ambao aliutumia autakavyo.
Maisha yalibadilika kwa kiasi fulani, nilikuwa nikiishi maisha yenye furaha, Oscar aliendelea kunijali, alinipa matunzo pamoja na mapenzi moto moto.
Kiukweli wazo la kurudi nyumbani kichwani mwangu halikuwepo kabisa kwa wakati huo, niliona ni jambo gumu mno kurudi katika maisha ya kimasikini niliyozaliwa katika familia yetu.
Nilikuwa nikiishi maisha ya furaha yaliyogubikwa na amani tele, sasa kwanini nikumbuke maisha ya kimasikini ya nyumbani kwetu?
Hilo lilikuwa ni jambo gumu mno kutokea.
Siku ziliendelea kukatika huku penzi likizidi kupamba moto, Oscar aliendelea na kazi yake ya upiga picha, muda mwingi aliutumia katika kazi yake hiyo, mwanzoni sikuwa na wasiwasi wowote, niliamini katika mapenzi ya dhati pamoja kazi yake, sikutaka kumuwazia vibaya.
Baada ya kupitia mwezi mmoja nilianza kusikia maneno ya chinichini kutoka kwa majirani ambao tayari nilianza kuwazoea. Waliniambia kuwa Oscar alikuwa ni mume wa mtu na kipindi hicho mke wake alikuwa amesafiri.
Nilipoyasikia maneno hayo sikutaka kuamini hata kidogo, nilihisi walipanga kutugombanisha hivyo sikutaka kuyapa uzito maneno yao.
Maisha yaliendelea huku kila siku maneno yakiwa ni yaleyale. Mwanzoni nilionekana kuyapuuzia lakini nilipoona yamezidi ilibidi nimuulize Oscar.
"Nani kakuambia maneno hayo?" aliniuliza huku akionekana kukubwa na mshangao.
"Kuna watu wameniambia," nilimjibu.
"Nilikwambia usipende kuamini kila unachoambiwa," aliniambia.
Kiukweli ilikuwa ni vigumu kuamini kama Oscar alikuwa akinidanganya, alionekana kumaanisha kila kitu alichokuwa akikizungumza, hakutaka kuona nikiendelea kuyasikiliza maneno ya watu ambayo yangeweza kuvuruga amani ya mapenzi yetu.
Hilo lilizidi kunifanya nimuamini sana Oscar kupita maelezo hata pale nilipokuwa nikitahadharishwa na watu sikutaka kuwasikiliza, niliwaona ni binadamu wenye nia mbaya kwangu, hawakupenda mafanikio yangu.
"Binti utajiingiza katika matatizo huyo unayeishi naye ni mume wa mtu," aliniambia Mama mmoja niliyemfahamu kwa jina la Mama Musa.
"Si kweli," nilimwambia huku nikiamini hakukuwa na ukweli wowote.
"Shauri yako binti unachokitafuta utakipata tu," aliniambia huku akionekana kunihurumia.
Bado sikutaka kuyaamini maneno yao, niliendelea kuwa katika mahusiano na Oscar. Miezi iliendelea kukatika hatimaye mwaka huo ukapita, ulipoingia mwaka 2011 mwezi wa kwanza ndipo nilipofanikiwa kubeba ujauzito wa Oscar.
Nilifurahi sana baada ya kuubeba ujauzito huo, niliamini huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuyaanza maisha mapya ya familia lakini ilikuwa ni tofauti kabisa na mawazo yangu.
Oscar alibadilika ghafla! baada ya kumpa taarifa hizo za ujazito, hakuwa Oscar yule niliyekuwa nikimfahamu, hakutaka kuamini kama nilikuwa nimebeba ujauzito wake, hilo lilizidi kumchanganya sana.
Nilishindwa kuelewa ni nini kilichokuwa kikiendelea, nilishangazwa na mabadiliko yake na hata nilipomuuliza nilishangaa akinigombeza na kunitolea maneno makali.
Nilihisi kuchanganyikiwa, sikutaka kuamini kama Oscar aliukataa ujauzito wake, hilo lilizidi kuniumiza sana, nilishindwa kuvumilia machozi yakaanza kunidondoka mfululizo.
Wakati nilipokuwa katika maumivu ya kukataliwa ujauzito ndipo hapohapo ambapo nilipokea maumivu mengine nisiyoyatarajia katika moyo wangu, Oscar aliamua kunieleza ukweli wa maisha yake.
Aliniambia alikuwa ni mume wa mtu na kipindi hicho mke wake ndiyo alikuwa akikaribia kurudi kutoka safarini.
Nilihisi kuchanganyikiwa baada ya kusikia maneno hayo, niliyakumbuka yale maneno niliyowahi kuambiwa na baadhi ya majirani lakini kutokana na kiburi changu sikutaka kuwasikiliza.
Mapenzi hatimaye yakaniingiza katika dunia ya maumivu na machozi, sikujua nilitakiwa kulia na nani kwani kama kuonywa nilionywa sana lakini sikutaka kusikia la mwadhini wala la mnadi swala.
“Kwahiyo unaamuaje?” nilimuuliza.
“Kuhusu nini?” aliniuliza.
“Huu ujauzito wako?”
“Mwajuma wewe ni chizi, mpumbavu, mshenzi, fala, hujielewi kabisa hivi unahisi ninaweza kuwa baba wa huo ujauzito wako? nenda katafute Baba halali lakini siyo mimi,” aliniambia Oscar maneno yaliyonifanya nitokwe na machozi. Nilishindwa kuzungumza, niliendelea kulia.
Kama ni makosa tayari nilikuwa nimeshayafanya. Kitendo cha kuishi na mwanaume bila ndoa, nikamuamini pasipokutegemea kama mwisho wa siku ningeweza kuvuna maumivu, hakika lilikuwa ni kosa kubwa mno nililolifanya.
Hatimaye Oscar aliweza kunifukuza, nikaanza kuishi maisha ya kutangatanga mitaani. Sikuwa na ndugu wala rafiki kusema labda ningeenda kumuomba hifadhi kwa muda, nilikuwa ni mimi na ujauzito wangu pekee.
Maisha yangu yalikuwa ni ya kutangatanga mitaani huku nikiomba msaada wa pesa na wakati mwingine nilikuwa nikienda kwa Mama Ntilie kuomba chakula, usiku ulipoingia nilikuwa nikilala nje, kiufupi hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu tangu nilipoweza kufukuzwa na Oscar.
Mwanzoni niliona ugumu kuishi maisha hayo lakini kadri siku zilivyokuwa zikizidi kusonga mbele, nilijikuta nikizoea na kuona ni maisha ambayo ni ya kawaida kuishi.
Siku moja nilikutana na msichana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Savela, aliponiona alihitaji kunisaidia. Nilipojitambulisha Savela alianza kunisifia, nikashangazwa na sifa zake yaani iliwezekana vipi msichana mwenzangu kama yeye akaanza kunisifia kama mwanaume?
Hilo lilinifanya nianze kuogopa, nilihisi Savela hakuwa mtu mwema kwangu, nilipokuwa nikimuangalia nikatamani anipe pesa kisha niondoke zangu.
Baada ya Savela kunihoji na kugundua mengi yaliyokuwa yamenitokea, alihitaji kunisaidia.
Nilisita kuchukua maamuzi ya haraka lakini baada ya kujifikiria maisha ambayo tayari nilikuwa nikiishi nilijikuta nikikubali tena bila kipingamizi chochote.
Alinichukua na kunipeleka mpaka nyumbani kwake alipokuwa akiishi maeneo ya Tegeta. Kwa muonekano wa nyumba yake jinsi ilivyokuwa ikionekana ilikuwa ni vigumu kuamini kwamba Savela ndiye ambaye alikuwa mmiliki wa nyumba hiyo, hakufanania kabisa.
"Hapa ni kwako?" nilijikuta nikiropoka na kumuuliza.
"Ndiyo hii ni nyumba yangu," alinijibu huku akionekana kuwa kawaida, hakujali lolote.
"Hongera ni nyumba nzuri sana," nilimwambia huku macho yangu yakiendelea kutazama sehemu za nyumba hiyo.
"Unaishi na nani?" nilimuuliza.
"Peke yangu," alinijibu.
Ilionekana kuwa ni nyumba kubwa iliyokuwa na vyumba vingi sana, kitendo cha Savela kuniambia kuwa aliishi peke yake kilinishangaza sana, sikutaka kuamini lakini huo ndiyo iliyokuwa ukweli.
Siku hiyo ikapita huku nikiwa nimeshapata bahati ya kufadhiliwa na Savela ambaye alionekana kuwa na moyo wa kipekee sana.
Hapa ngoja nikwambie kitu, nilikuwa mchafu sana, sikuwa na nguo zaidi ya niliyokuwa nimeivaa. Siku iliyofuata Savela aliamua kunipeleka kwenye duka la nguo maeneo ya Kinondoni, tulipofika huko alininunilia nguo, alinipeleka saluni ambapo huko nikazidi kupendezeshwa, ndani ya masaa kadhaa nilikuwa nimebadilika, sikuwa Mwajuma yule mchafu ambaye nilishindia nguo moja.
"Kwanini unayafanya yote haya?" nilimuuliza.
"Usijali Mwajuma nafanya haya kama masaada wangu kwako, najua umepitia magumu mangapi, sitaki kuona ukirudi kule wakati wewe bado ni msichana mrembo, unavutia, wasichana wenzako kama wewe mjini hawafi njaa, wanafanikiwa kiulaini," aliniambia maneno ambayo aliniacha nayo njia panda.
"Unamaanisha nini?"
"Usijali muda ukifika utajua namaanisha nini au wewe hupendi kuona ukiwa na maisha mazuri, ukamiliki nyumba ya kifahari, ukamiliki gari la gharama, ukawa mfanyabiashara mkubwa sana hapa mjini yaani kila mtu akawa anakuzungumzia wewe tu?"
"Napenda ila..."
"Basi kila kitu kinawezekana, mimi binafsi nimewahi kuishi kama yako, niliteseka mno, hakukuwa na mtu wa kunisaidia yaani kama sio mimi mwenyewe kujitambua sijui leo hii ningekuwa wapi?" alisema Savela kisha akaendelea kuzunguza.
"Umeiona ile nyumba yangu ya Tegeta nimeinunua juzi tu, nafanya biashara inayoniingizia pesa nyingi mno, sijasoma lakini nimeweza kufanya vitu vikubwa ambavyo wasomi wameshindwa kuvifanya," aliniambia Savela.
Kwa muda ambao Savela aliutumia kuzungumza na mimi tayari alikuwa ameipandikiza mbegu ya tamaa ya mafanikio ndani yangu, alijua kunishawishi, alijua kuzungumza yaani maneno yake yalitosha kunifanya nitamani kujua ni biashara gani hiyo ambayo alikuwa akiifanya.
Siku ziliendelea kukatika huku ujauzito nao ukiendelea kukua, mwanzoni nilimficha Savela hali niliyokuwa nayo lakini kama unavyojua mimba haiwezi kufichika mwisho wa siku alifahamu kila kitu.
Hakuonekana kuchukia baada ya kufahamu ukweli ambao nilimficha hapo awali, alinikumbusha kuhusu msaada ambao aliamua kunipa ulikuwa ni wa lengo la kufanya biashara. Ilibidi nimuulize ni biashara gani hiyo ambayo kila siku alikuwa akinidokeza na ndipo hapo ambapo aliniambia ukweli, aliniambia biashara hiyo ilikuwa ni ya uchangudoa yaani ilitakiwa nijiuze ili niweze kupata pesa, alienda mbali zaidi na kuniambia kuwa mafanikio yake yote yalisababishwa na biashara hiyo uchangudoa.
Nilihisi mwili wote ukipigwa na ganzi baada ya kuyasikia hayo, sikutaka kuamini hata kidogo, kuna muda nilidhani labda alinitania lakini hakukuwa na utani kati yangu na yake.
“Baba wa huo ujauzito ni nani?”
“Ni Oscar.”
“Anajua?”
“Ndiyo ila anifukuza, aliukataa.”
“Sawa, sasa kwenye kazi hii ya uchangudoa ujauzito hautakiwi, utakupotezea wateja," aliniambia Savela.
Licha ya kuwa nilitokea katika maisha ya kimasikini pamoja na kukutana na changamoto zote mpaka kufikia hatua ya kukutana na Savela bado nilikuwa mwenye tamaa.
Tamaa ya utajiri ilishakwishaniingia, kila nilipokuwa nikimuangalia Savela pamoja na mafanikio aliyokuwa nao katika maisha yake sikutaka kuamini kama biashara hiyo ya uchangudoa ndiyo iliyomletea mafanikio yote hayo, kuna muda nilikataa lakini mwisho wa siku nilijikuta nikiamini.
Kwa kuwa nilikuwa tayari kufanya lolote Savela alinishauri niende hospitali nikautoe ujauzito niliyokuwa nao kwa madai kuwa ingeniharibia soko la biashara yangu ya uchangudoa.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi