
Mtunzi: Nyemo Chilongani
SEHEMU YA PILI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
“Utanilisha nini?” aliniuliza swali dogo sana ambalo lilikuwa na maana kubwa.
Nilibaki kimya nikimwangalia, sikutarajia kupata swali kama hilo kutoka kwake. Ni kweli alikuwa na uhuru wa kuuliza kuhusu majukumu yangu kama mwanaume kwake.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
ENDELEA...
Alikuwa akipendeza sana, hii ilimaanisha kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakifanya kazi hiyo, yaani kulikuwa na mwanaume aliyekuwa akishughulika na mavazi tu, mwingine nauli za usafiri mwingine viatu na mwingine make up, sasa mimi ningeshughulika na nini? Hata kama angeniambia nishughulike na vocha tu nisingeweza kutokana na kiasi cha pesa kilichokuwa kikihitajika.
“Kwani wewe unataka nini?” nilimuuliza ili nijue.
“Matunzo! Mtoto mzuri kama mimi nitunzwe, nitolewe out, niletewe baga, pizza, ice cream, uninunulie pafyumu, ninukie, au hutai demu wako ninukie vizuri?” aliniuliza.
“Nataka! Tena napenda sana.”
“Sasa je! Utaweza kunitunza?” aliniuliza.
Mtu mzima sikujua nimjibu nini, hilo swali lilikuwa kubwa kuliko uwezo wangu. Nilimwangalia tu, kwa kawaida hata kama huwezi, kwa mwanaume ni MARUFUKU kusema neno siwezi, ni lazima useme unaweza halafu umkimbie.
“Kwa nini nisiweze? Tena umenikumbusha, nataka siku nikuchukue tukale pizza,” nilimwambia.
“Waooo! Lini bebi?”
“Tufanye Ijumaa!” nilimwambia, siku hiyo ilikuwa Jumatatu.
Sikia! Mimi nilikuwa nasikia sana kuhusu pizza ila kiukweli sikuwahi kula hata siku moja. Nilitamani vyakula vinono lakini sikuwa na pesa. Hebu fikiria, kwa siku napokea elfu tano, halafu hapo pizza inauzwa elfu kumi na mbili mpaka nyingine elfu hamsini, hivi ningeweza kumgharamia yote hiyo? Kwangu ilikuwa vigumu, ila nilimwambia kwamba ningemtoa out kwa sababu tu nilitaka kujitia ubabe mfukoni.
“Basi naisubiri hiyo siku! Zimebaki siku nne, nitakutafuta bebi nikale pizza,” aliniambia kwa tabasamu na kisha kuagana huku moyo wangu ukijisikia burudani sana kwa kuamini kwamba nimeshinda vita kumbe ndiyo kwanza nilikuwa nikiingia kwenye vita na watu waliokuwa na nguvu kuliko mimi.
Nilichanganyikiwa, sikujua ni kitu gani nilitakiwa kufanya ili niingize pesa kabla ya siku husika kufika. Niliumiza kichwa changu kwani kiasi cha shilingi elfu tano kwa siku kilikuwa kidogo sana kiasi kwamba kisingeweza kunisaidia kwa lolote lile.
Wakati nikifikiria sana ndipo nikakumbuka kwamba hapo katika Mtaa wa Kongo kulikuwa na uhaba wa walinzi wa kulinda eneo hilo, wale wachache waliokuwa wakilinda walilipwa kiasi cha shilingi elfu kumi kila siku asubuhi.
Nakumbuka niliwahi kuulizwa kama niliitaka kazi hiyo kipindi cha nyuma, niliikataa kwa kuwa niliamini ningekuwa nachoka sana, ila kwa sababu huyo Aisha nilimwambia Ijumaa ilikuwa ni siku ya kuonana na kwenda kula pizza, basi niliona hiyo kazi ilinifaa sana.
Nikaelekea katika ofisi moja iliyokuwa hapohapo ambayo ilikuwa chini ya mzee Juma, nilizungumza naye na kumwambia kwamba niliitaka kazi hiyo. Kuipata haikuwa kazi kwani alinifahamu, nilikuwa mtu wa hapohapo hivyo akanipa nafasi hiyo na kuniambia nianze siku hiyo.
Moyo wangu ukafarijika, na mpango wa kwanza kabisa kabla ya kupanga maisha ilikuwa ni kwenda mtoko huo na Aisha, ilikuwa ni lazima nimuonyeshe kwamba nilikuwa na uwezo mkubwa wa kumchukua msichana na kwenda naye sehemu.
Siku zilikwenda taratibu sana, kwa kuanzia Jumatatu mpaka Alhamisi ilimaanisha kwamba ningepata kama shilingi elfu arobaini kupitia kazi ya ulinzi lakini pia ningepata shilingi elfu ishirini kwa kazi ya usafi, kwa maana hiyo mpaka Ijumaa nilitegemea kuwa na shilingi elfu sitini mfukoni.
Kwa mwaka huo wa 2016 zilikuwa pesa nyingi kutokana na hali ya uchumi, maisha kubana hivyo niliamini kwamba siku hiyo ningefaidi sana na Aisha na kubwa zaidi ni kwamba ningeonekana kwamba nilikuwa na pesa na hakukuwa na chochote cha kunibabaisha.
Wakati nikifikiria kuhusu Aisha, kichwa changu kilikuwa kinaniuma mno kila nilipofikiria kuhusu Issa, niliamini kwamba alinizunguka na kutembea na msichana huyo kwani lisingekuwa jambo jepesi kumuona akichangamkiana naye na wakati niliamini hawakuwa wameonana kabla.
Hilo sikutakiwa kuhofu sana kwa kuwa niliamini kabisa kwamba mara baada ya kuwa naye faragha basi huyo Issa asingemfikiria kabisa kwa sababu nilijiamini kupita kawaida.
“Ila subiri! Cha msingi ni kumuonyeshea mapenzi makubwa,” nilijisemea.
Wakati hayo yote yakiendelea bado sikuacha shobo zangu kwa wanawake wengine waliokuwa wakija hapo Kariakoo kufanya manunuzi yao mbalimbali, nadhani nilikuwa mtu niliyeongoza kusalimia kuliko watu wengine Tanzania. Macho yangu yalikuwa magumu kuvumilia kila nilipokuwa nikiwaona wanawake wazuri ilikuwa ni lazima niwafuate na kuanza kuongea nao kidogo.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu kabla ya kufanikiwa. Mpaka leo ninapokaa na kukumbuka miaka miwili nyuma, maisha yalivyobadilika na kuwa hivi yalivyo, huwa ninaamini kabisa Watanzania tunabaki masikini kwa sababu tu hatuna mitaji, hatuna pesa za kuanzia biashara na ndiyo maana tupo hivi.
Sikuacha kumfuata Issa na kumuomba simu yake kuzungumza na Aisha, alinipa na kuongea naye sana na hata siku ya Ijumaa ilipofika, akaja palepale alipokuwa akinikuta, nilimchukua na kuondoka naye.
Njiani nilikuwa nikiongea naye, mfukoni nilikuwa na shilingi elfu arobaini kwani nyingine nilitumia kwenye matumizi yangu mengine.
Hatukuchukua muda mrefu tukafika sehemu ya kununulia pizza na kununua kisha kuondoka, tulikula huku tukitembea, siku hiyo nilijiamini kuliko siku nyingine na nilichokihitaji kilikuwa kulala na Aisha tu.
Kwa Kariakoo nisingeweza kupata chumba kwa kuwa ilikuwa ni gharama sana hivyo kama kweli nilihitaji kufanya naye basi haikuwa na jinsi kuondoka kuelekea Magomeni au Manzese.
Sikutaka kujificha, mwili wangu ulikuwa ni kama umewaka na hakukuwa na kitu cha kunizuia kufanya mambo yangu, nilimwambia ukweli kwamba network ilikuwa ikisoma na nilichohitaji ni kulala naye.
Aisha alinizoea sana, akaniambia kwamba hakuna tatizo, kama nilikuwa na hela ya kumtoa basi hakukuwa na shida. Hapo nilipata swali moja, huyu Aisha alikuwa akijiuza ama kwa sababu kwa msichana wa kawaida angeniacha mimi nifanye naye halafu mambo ya kupeana pesa yangekuja baadaye.
“Kiasi gani unataka?” nilimuuliza huku nikimwangalia usoni.
“Yoyote ile, isiwe elfu kumi, isiwe chini ya elfu kumi,” aliniambia huku akitoa tabasamu lililonimaliza kabisa.
Mfukoni nilikuwa na shilingi elfu ishirini na tano hivyo hakukuwa na tatizo, nikamchukua na kwenda Mburahati ambapo kulikuwa na nyumba ya wageni ya bei rahisi na kumalizia mambo yetu humo.
Wanawake wa mjini wanapenda pesa, kama hauna pesa, huwezi kumpata msichana yeyote yule. Hebu fikiria, mwanamke kama Aisha nilitumia kiasi cha pesa ambacho kwangu kilikuwa kikubwa mno, hii inamaana kwamba unapokuwa na pesa basi una uwezo wa kufanya mapenzi na msichana yeyote uliyekuwa ukimtaka.
Hilo likanifanya kuendelea kuuchukia umasikini, sikuamini kwenye kufanya kazi kwa bidii ndipo ufanikiwe, siku zote niliamini kwamba utajiri ni bahati tu, mtu anaweza leo akawa masikini na kesho akaamka na kuwa tajiri mkubwa.
Niliamini kwamba kuna siku ningetajirika sikujua ni siku gani lakini niliamini kwamba kuna siku tu ingetokea ningefanikiwa na kuwa tajiri mkubwa.
Niliporudi Kariakoo nikaanza kumwambia Issa kwamba nilifanikiwa kumalizana na Aisha, kwa jinsi alivyoonekana tu niliamini kwamba hakuwa mtu mzuri, hakuitikia kwa furaha, alionekana kama kuchomwa na kitu chenye ncha kali moyoni mwake.
Hilo likanipa uhakika kwamba Issa alitembea na Aisha, nilikasirika sana, kwa jinsi tulivyokuwa marafiki sikuamini kama angeweza kufanya kitu kama hicho.
Aliniumiza, wakati yeye akicheka, moyoni mwangu kulikuwa na majonzi makubwa, sikutaka kukubali, kama yeye alitembea na msichana ambaye alijua kwamba alikuwa wangu, akaniumiza basi na mimi ilikuwa ni lazima nimuumize.
“Nitamuumiza, kuna siku nitatembea na dada zake wawili, halafu nitatembea na demu wake,” nilijisemea.
Urafiki wetu ukaendelea lakini haukuwa kama kipindi cha nyuma, yaani siku ambayo nilikwenda kulala na Aisha ndiyo ilikuwa siku iliyobadilisha kila kitu.
Niliendelea kufanya kazi, sikuwasiliana tena na Aisha kwa sababu hata simu Issa hakutaka kunipa kwa kuniambia kwamba alikuwa bize nayo. Kwani simu shilingi ngapi bhana? Nilijidunduliza na kununua yangu, tena ilikuwa ile ya kupangusa.
Huko, nikafanikiwa kuwasiliana na Aisha kwa WhatsApp, tulikuwa tunaongea mengi, aliniambia kuhusu Issa kwamba alikuwa akimfuatilia sana kiasi kwamba mpaka ikawa kero.
“Ikawaje?” nilimuuliza.
“Ikawa hivyohivyo...yaani alikuwa kero,” aliniambia.
“Ikawaje? Yaani namaanisha baada ya kero zake, nini kilifuata?” nilimuuliza.
“Nilifanya naye mapenzi, alinishawishi sana, aliniambia kwamba wewe ni masikini, huna pa kulala, unalala kwenye maduka, unapenda kujipendekeza kwa kila mtu ili upate pesa,” aliniambia.
“Yaani Issa alikwambia yote hayo?”
“Ndiyo! Nadhani hiyo ilikuwa sababu ya kulala naye. Naomba unisamehe,” aliniambia, nilishikwa na hasira mno lakini sikuwa na la kufanya.
Sikumlaumu Aisha, alikuwa msichana aliyekuwa akitafuta mwanaume mwenye pesa, mimi sikuwa nazo, nilikuwa masikini hivyo kama kulikuwa na mwanaume alimfuata kwa kisingizio cha pesa niliamini mwanamke yeyote yule angeweza kudanganyika.
“Ila huyu Issa, ni lazima nitadili naye,” nilijisemea huku nikionekana kuwa na hasira.
Niliona kama nachelewa kupata mafanikio, mtu wa kwanza ambaye nilitakiwa kufanya mikakati ya kuwa naye alikuwa Shamila. Huyu ndiye yule mdogo wake na Issa ambaye nilimtamani sana kwa kuwa niliamini baada ya Issa kugundua kwamba nimelala naye basi angenichukia maisha yake yote. Hiyo ndiyo ilikuwa maana ya kisasi.
Nikaanza kupiga ndogondogo, nikaanza kuzungumza naye kila siku kwa furaha, nilichangamka kiasi kwamba mpaka yeye mwenyewe alinishangaa.
“Mkeka wako umetiki nini?” aliniuliza huku akiniangalia.
“Kwa nini?”
“Unaonekana una furaha sana!”
“We’ acha tu. Ila Shamila wewe mzuri sana,” nilimwambia huku nikimwangalia.
Alichukia, hiyo ndiyo ilikuwa kawaida yake. Shamila alijua kabisa kwamba nilimpenda tangu zamani ila hakutaka kunikubalia kwa sababu tu alijua sikuwa na pesa, sikuwa na makali yoyote yale ya kumfanya mtoto wa kike anikubali.
Bila kunificha akaniambia kwamba hanipendi, tena nisifikirie kuwa naye hata kidogo. Unadhani niliumia, walaaa! Shamila alikuwa msichana mrembo, kusema kwamba sikustahili hata kutembea naye kwangu mimi ilimaanisha kuwa nitafute pesa, nikipata nimtafute.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi