
Mtunzi: Nyemo Chilongani
SEHEMU YA NNE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Alininunulia kitanda cha chuma, chumba kikapigwa rangi na kunipa kiasi cha shilingi milioni moja kwa ajili ya matumizi yangu mengine.
Kumbuka mpaka kipindi hicho sikuwa nimeiuza ile almasi kwa sababu sikujua soko lipo wapi na sikuwa na mtu wa kumwamini hata kidogo.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
Wakati hayo yakiendelea, upande wa pili niliendelea kutafuta soko taratibu. Siku ziliendelea kukatika na baada ya siku mbili nikapata taarifa kwamba rafiki yetu, Mrisho aliuawa na mwili wake kutupwa baharini.
Nilishtuka sana, huyu Mrisho alikuwa mlinzi mwenzangu pale Kariakoo na alikuwa miongoni mwa watu ambao tulimsaidia yule mzee kumpeleka hospitalini.
Msiba wake uliwagusa watu wengi, alikuwa kijana mpole, sasa ilikuwaje awe na maadui na wakati kila wakati alikuwa mcheshi na hakubagua ni nani wa kuongea naye?
Tulihuzunika sana hivyo tulichokifanya ni kwenda kwenye mazishi na baada ya kumzika tukaendelea kufanya mambo mengine kama kawaida.
Katika hayo yote, sikuacha kuwasiliana na msichana Aisha. Nilimkumbuka na wakati mwingine alikuwa akija na kwenda naye chumbani. Aisha alikuwa malaya tu lakini kitu cha ajabu kabisa alionekana kunikubali kupita kawaida.
Nilikuwa masikini, aliujua ukweli lakini wala hakujali kiasi kwamba nikawa nashangaa kwamba ilikuwaje anikubali kiasi kile?
“Hivi unanipenda kweli ama?” nilimuuliza.
“Nakupenda sana Edward! Huamini?”
“Naamini ila si unajua tena jinsi nilivyo! Mtoto mzuri kama wewe kuwa na mimi, huwa naona kama naota,” nilimwambia huku nikitoa tabasamu pana.
Maisha yaliendelea, sikumwambia mtu kuhusu ile almasi, niliificha chumbani sehemu salama kabisa. Siku zikakatika, baada ya wiki mbili tukapata msiba mwingine wa jamaa yetu wa karibu (Selemani) ambaye alikuwa mlinzi kama mimi.
Taarifa za awali zilisema kwamba jamaa alichomwa kisu na mtu asiyejulikana usiku wa manane nyumbani kwake kwa sababu siku hiyo hakuja kazini.
Kama ulivyotuuma msiba wa kwanza, hata huo ulituuma sana kwa kuwa alikuwa Selemani alikuwa kama Mrisho, kijana mchangamfu ambaye alizungumza na kila mtu. Ilituuma sana lakini hatukuwa na jinsi, Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihidiwe.
Siku hiyo usiku wa saa tisa nilipokuwa nimekaa sehemu nikiyafikiria maisha yangu huku nikiendelea kufanya kazi ya ulinzi hapo sokoni nikaanza kujiuliza swali moja muhimu sana.
Lilikuja tu kichwani, nadhani kama Mungu alihitaji kunifumbua kitu fulani. Nikaanza kujiuliza kuhusu vifo vya watu waliokuwa wameuawa. Nilichanganyikiwa kidogo kwa sababu niligundua kwamba walikuwa walinzi, kwa nini wauawe ndani ya siku chache?
Wakati nikiendelea kujiuliza hilo, moyo wangu ulikuwa na shaka mno, nilihisi kabisa kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea. Sikutaka kubaki kimya, nikawaita wenzangu na kuwaambia kuhusu maswali niliyokuwa nikijiuliza, kwamba kwa nini waliokuwa wakiuawa walikuwa walinzi?
“Unaogopa sana! Acha kuogopa mtoto wa mama,” alisema Fred huku akiniangalia, sura yake ilikuwa na tabasamu pana.
“Fred! Unajua siriazi wazee inabidi tujiulize kuhusu haya mauaji!” niliwaambia.
“Kwa hiyo unahisi watu wanaanza kutuua sisi walinzi? Kama wanatuua, kwa nini hawaibi?” aliuliza mwingine, huyu aliitwa Msekwa.
Kiukweli hili lilinichanganya kichwa sana lakini wenzangu hawakuwa na hofu hata kidogo. Nilichanganyikiwa mno ila kwa kuwa wenzangu hawakuonekana kuwa na hofu, basi na mimi nikajifariji kwamba hakukuwa na tatizo hivyo sikutakiwa kuhofia hata kidogo.
Japokuwa nilikubaliana nao lakini sikutaka kupotezea kabisa, kichwa changu kiliniambia kwamba kulikuwa na jambo lililokuwa likiendelea nyuma ya pazia.
Asubuhi ilipofika, huku nikiwa katika chumba changu, Nurat akapiga simu kwamba alikuwa akija kuniona kwa kuwa hakwenda chuo siku hiyo.
Nikamkaribisha! Ndani ya dakika chache, akafika, akatulia na kumwambia niende kumnunulia kinywaji dukani. Alikataa lakini si unajua lazima mwanaume uonyeshe umwamba, nikaenda hivyohivyo huku yeye akinisubiri ndani.
Duka halikuwa mbali sana na mahali hapo, kulikuwa na vichochoro vichache kabla ya kuingia kwenye barabara kubwa iliyokuwa na maduka mengi.
Nilipofika kwenye barabara hiyo, macho yangu yakatua kwenye gari moja lililosimama pembeni, ilikuwa Noah Nyeusi. Sikulitilia maanani, nilielekea dukani, nikanunua soda na kuanza kurudi.
Ghafla mlango wa gari lile ukafunguliwa na mwanaume mmoja kuteremka huku akiwa na sigara mkononi. Akaniita kwa kuniomba sana, nikamsogea.
“Samahani ndugu yangu, wewe ni mwenyeji maeneo haya?” aliniuliza huku akiniangalia.
“Ndiyo! Kuna nini bosi?”
“Unamfahamu huyu?” aliniuliza huku akinionyeshea picha ya mwanamke mmoja.
Niliiangalia kwa makini, sikuwa nikimfahamu na sikuwahi kumuona hata siku moja. Nilimrudishia na kumwambia kwamba sikuwa nikimfahamu.
“Haina shida! Unaweza kuingia ndani ya gari twende tukazungumze?” aliniuliza huku akiwa na tabasamu pana.
“Ndani ya gari? Hapana! Nina haraka,” nilimwambia.
“Kweli?” aliniuliza huku akinionyeshea bastola yake iliyokuwa kiunoni.
Nilishtuka mno, nilitamani kukimbia lakini nilipokumbuka kwamba bastola ilikuwa na uwezo wa kukuua hata ukiwa mbali, niliogopa kupita kiasi.
Sikumjua mtu huyo alikuwa nani, alihitaji nini ila alichotaka ni mimi kutii kile alichokuwa akiniamba. Sikubisha, mlango ukafunguliwa, ndani ya gari hilo kulikuwa na watu wengine kama watatu hivi, wote kwa kuwaangalia tu sura zao zilikuwa ngumu, yaani zilionyesha kuwa ni watu wasiokuwa na masihara hata kidogo.
“Ingia fasta dogo tusije kukumwaga utumbo,” alisema mwanaume mmoja aliyekuwa ndani ya gari, kusikia hivyo, haraka sana nikaingia ndani. Gari likawashwa na kuondoka mahali hapo.
Nilikuwa na hofu, nilijua kabisa kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wangu. Niliogopa na kutetemeka mno, nilitekwa na majamaa hao waliokuwa kwenye Noah Nyeusi, nililia lakini sikutakiwa kuongea kitu chochote kile kwani vinginevyo wangeweza kuniua.
“Tukifika tutakuuliza swali moja tu kuhusu almasi, na ukijifanya kuwa mjanja kama wale walinzi wenzako, tutakuua kama tulivyowaua,” alisema mwanaume mmoja huku akinipigapiga kibao shavuni.
Moyo wangu ukapiga paaa! Kumbe hawa ndiyo majamaa wale waliowamaliza marafiki zangu, sasa zamu yangu ilifuata.
Ndani ya gari nilikuwa nikitetemeka, niliona kabisa kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wangu, sikuwafahamu watu wale, kwa jinsi nilivyokuwa nikiwaangalia tu walionyesha kwamba ni watu wenye roho mbaya kuliko wote katika dunia hii.
Waliniambia kuhusu almasi, hicho ndicho kitu nilichokuwa nikikitegemea kuniondoa kutoka katika maisha niliyokuwanayo. Umasikini wangu ule ungeondolewa na almasi hiyo ambayo niliichukua na kuificha chumbani.
Leo, waliniteka na kuniambia kuhusu almasi, hii inamaana kwamba kama ningewaambia mahali ilipo au hata kuwapa basi ningekuwa masikini kama nilivyokuwa milele yote.
Sikutaka kuona hilo likitokea, kwenye ishu ya almasi, nilikuwa radhi kupigwa, kuteshwa, kulawitiwa lakini si kuikabidhi ile almasi mikononi mwao, yaani nilijitolea kufanywa kila kitu lakini si kuwapa kwa mkono wangu.
Gari liliondoka hapo Kariakoo na kuchukua njia ya kwenda Jangwani, niliambiwa nitulie, nilifanya hivyo huku moyoni nikianza kusali sala yangu ya mwisho.
Kumbuka kwamba kule nyumbani nilimuacha Nurat, alikuwa akinisubiri, nilitekwa na nilikuwa na uhakika hakujua mahali nilipokuwa muda huo.
Gari liliendeshwa mpaka lilipofika Kinondoni, nikachukuliwa na kuingizwa kwenye jumba moja kubwa, kwa ndani lilikuwa zuri lakini nilipopelekwa katika chumba nilichotakiwa kuhifadhiwa, nilishangaa kuona chumba hicho kuwa cha kutisha sana.
Ni kama mule ndani walikuwa wakifanya upasuaji wa watu, pembeni kulikuwa na mguu wa mtu, haukuwa na vidole, kulikuwa na minyororo imefungwa ukutani, yaani mtu unasimamishwa, unafungwa minyororo na kupewa mateso mahali.
Ukiachana na hivyo, kulikuwa na pasi ya umeme, nilijua kazi yake, pia kulikuwa na michirizi ya damu, kila nilipokuwa nikiangalia hali ya chumba kile, nilijua tu kwamba watu hao walikuwa siriazi kutaka almasi yao.
“Bora waniue lakini si kusema mahali almasi ilipo,” nilijisemea huku nikiwekwa kwenye kiti kimoja.
Muda wote huo mpaka naingizwa ndani sikuwa nimeongea kitu chochote kile, nilionyesha ujasiri fulani mkubwa kwani wanaume hao hawakuwahi kuona mtu aliyekuwa mbishi kama mimi.
Mmoja aliniambia kwamba inawezekana mimi niliwahi kufa, nilifufuka na hivyo kutakiwa kufa tena na ndiyo maana sikuonekana kuogopa kwa sababu wenzangu waliokuwa wamechukuliwa hapo kabla, walikuwa wakilialia mpaka kujikojolea.
“Wewe mwamba sana. Unajiamini mno, wenzako walikuwa wanajikojolea, wewe upo hivyohivyo. Ila bro! Humu ndani ukitoka salama, shukuru Mungu. Unauona huo mguu, ni wa mshikaji wako, macho yake yapo humo kwenye ndoo,” aliniambia, nilijua tu kwamba yote hiyo ilikuwa ni kunitisha ili niwaambie mahali almasi ilipokuwa.
Nilibaki ndani ya chumba hicho, nilijifikiria ni kwa namna gani ningeweza kutoroka. Niliogopa, kama nisingefanya harakati za kutoroka inamaanisha kwamba ningeteswa na hata kuuawa kwa kuwa mimi mwenye nilikuwa mbishi.
Baada ya nusu saa, kijana mmoja akaingia, japokuwa ilikuwa ni asubuhi lakini humo kulikuwa na giza zito na ni taa tu ndiyo iliyokuwa imewashwa. Kwanza taa ikazimwa, wakati nikijiuliza nini kilitakiwa kuendelea pale kwenye kiti nilichokuwa, nikashtukia nikipigwa ngumi nzito iliyonifanya nianguke chini.
“Tunaanza. Hii muvi ina season tano, hii ndiyo episode ya kwanza, Na kila season ina episode arobaini. Ukimaliza season zote tano, wewe mwamba,” aliniambia huku akiiwasha taa, akachukua mjeredi, akanifunga ile minyororo huku nikiwa kifua wazi, mgongo ukageukia kwake na kuanza kunichapa.
Nilisikia maumivu makali mno, mwanaume yule alinichapa mjeredi ule kwa nguvu kubwa pasipo kuanza kuniuliza swali lolote lile kuhusu ile almasi.
Nilisikia maumivu makali kupita kawaida. Alinichapa kwa dakika tano nzima, mgongo mzima ulijaa damu, nilikuwa nikilia kama mtoto mdogo huku nikimuomba aniachie kwani sikuwa nikijua kitu chochote kile.
Baada ya kumaliza, akanifungua na kuniweka kwenye kiti, mgongo wote ni kama ulikuwa na ganzi na kwa jinsi damu zilivyokuwa zikichirizika ni kama mtu alichukua ndoo ya maji na kunimwagia mgongoni.
Kwenye kiti kile wakaniweka na kuanza kuniuliza maswali kuhusu yule mzee niliyekuwa nimemuokoa na almasi. Nilichokigundua ni kwamba hawakujua ni mlinzi gani aliyekuwa amemuokoa yule mzee na mbaya zaidi hawakujua ni nani alikuwa na almasi waliyokuwa wakiitaka.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi