
Mtunzi: Richard Mwambe
SEHEMU YA KUMI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
zaidi ya hilo alibofya kitufe cha kuruhusu sauti isikike kwa nguvu ‘loud speaker’ kisha akajituliza kitini. Akishika hiki na kile juu ya meza yake mara mlango uligongwa na kufunguliwa na mgongaji aliyejitoma ndani bila kukaribishwa, hakuwa mwingine ni yule boss wake bwana Shikuku aliyeingia akiwa amefura kwa hasira ambayo ilimtisha hata Melchior,
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
akajitupa kwenye kiti cha upande wa pili na kushusha pumzi ndefu,
“Mr Ndege, FBI wapo hapa” alimwambia Melchior ambaye alionekana kushtushwa kidogo kwa taarifa hiyo
“Oh shit, wataharibu mipango yetu” Ndege alimjibu huku akiiweka kalamu yake mezani na mkono kuuelekeza shavuni.
“Sio wataharibu, wameshaharibu,” bwana Shikuku alitamka hayo huku akitikisa kichwa, kisha akamuangalia melchior na kumwambia, “Wameshatuomba tujitoe kwenye huu mkakati ili wao wafanye kazi ya kumnasa bwana Bill, wameniuzi”
“What?!” bwana Ndege aliuliza kwa mshangao mkuu.
“Ndiyo hivyo,” Shikuku akajibu kwa mkato huku akiangalia pembeni.
“Bill hawezi kuondoka mikononi mwetu kijingajinga wakati tunajua wazi jinsi alivyoendesha mambo ya kijasusi katika Afrika Mashariki, na sasa yupo kwetu tena, kule Tanzania alitoroka hatukuweza kumtia mkononi kwa sababu hizi hizi, sasa na leo tena haiwezekani,” Melchior aliongea kwa uchungu, kisha akatulia na baadaye kumtazama boss wake, “Bill nitamtia mkononi kabla ya wao kufanikisha hilo” alimwambia boss wake huku akifungafunga vitabu vyake, akasita kidogo na kusema, “Lazima tujue nyuma ya mauaji ya kasisi kuna nini, mpaka Bill ahusike, tusipompata Bill hatutaweza kutatua juu ya kifo hiki cha utata, mimi nina mwanzo wa mkasa na Bill ana hatima ya mkasa, lazima nimpate mimi na siyo FBI”
˜˜˜
5
Dar es salaam – Tanzania
MVUA kubwa iliendelea kunyesha katikati ya jiji la Dar es salaam, maji yalizijaza barabar zote na kufanya ugumu wa watembea kwa miguu kuonekana dhahiri, akina mama viatu mkono wakizikunja nguo zao kwa juu huku mifuko ya plastiki ikiwa imefunika vichwa vyao ili kuokoa nywele za gharama zisiharibike, magari nayo yalipita shida kwa namna moja au nyingine, yakitumbukia kwenye mashimo ya liyojitengeneza kutokana na mvua hiyo, basi jiji lote lilikuwa vururuvururu. Kila mtu alionekana kuchukia hali ile ambayo serikali inaifumbia macho mara zote, shida kubwa ikawa kwa wale waishio mabondeni waliokuwa wakifukuzwa kila siku tangu enzi za mheshimiwa Makamba lakini waling’ang’ana utafikiri walizaliwa hapo, huyu akisonya, yule akimkashifu kiongozi Fulani wa chama na serikali.
“Bora tuwachague wapinzani mwaka ujao” mwingine alisikika akisema hayo huku akiwa juu ya moarobaini uliokuwa ndani ya maji nusu nzima. Ilhali anasahau kuwa mvua hizo ni mabadiliko ya tabia nchi ambayo mimi na wewe ndio visababishi.
“Ila mi Mabwepande ndio siendi” alijibiwa na yule aliyekuwa juu ya paa lanyumba iliyochoka ambayo kwayo uhai wake ulifika tamati, alisahau kabisa kuwa haikomoi serikali bali anawaumiza watoto wake ambao hakuhusika katika kuchagua eneo la kuishi.
Wakati upande mwingine watu wakiwa wamejazana katika daraja kubwa la Tabata Matumbi wakivumilia harufu kali ambayo ilisemekana ni ya mwili wa binadamu uliokwama katika maji yam to Msimbazi huku jeshi la polisi likisaidi kazi hiyo, wengine walikuwa wakichanganya vichwa, akili na mawazo yao vikiwa tofauti na matakwa ya mioyo yao.
Ndani ya jengo la JM MALL, ghorofa ya saba mlango namba 705 ni watu wawili tu mwanamke na mwanaume walikuwa wameketi wakitazamana mmoja akishindwa kuamua na mwingine akishindwa kushauri nini cha kuamua. Wakiwa bado katika kushangaana wawili hawa mara mlango ulifunguliwa na bibi mmoja wa makamo ambaye nywele zake zilishahitilafiana na weusi wake wa asili na kuubeba weupe ambao wengi hupenda kuuita mvi, aliingia moja kwa moja na kuketi kwenye kiti kikubwa ambacho kilikuwa pembeni kidogo ya meza ile safi iliyozungukwa na mapambo murua ambayo ukiketi basi yatakupa burudani ya macho na kuondosha ile ambayo muandishi wa kitabu cha SHIDA, Ndyanao Balisidya aliita ‘kiwi cha macho’.
“Karibu Madam S” Kamanda Amata alisimama na kupeana mkono na mwanamama huyu aliyebobea kwenye kazi za kikachero tangu usichana wake.
“Nimekaribia Kamanda” akajibu huku akijiweka vizuri pale kochini ambapo aliweza kuonana na mrembo aliyemkuta ofisini humo. Mara baada ya kujiweka sawa alimtzama Amata na kumpa bahasha moja ya khaki ambayo juu yake imeandikwa maandishi yanayoitambulisha kuwa ni mali ya serikali, akaitupia mezani na Kamanda Amata akaichukua na kuifungua, baada ya kuisoma akaitupia mezani,
“Nairobi tena! Kuna nini madam?” Kamanda Amata aliuliza
“Mauaji ya Kasisi, jasusi Bill Van Getgand yuko Nairobi, FBI na taasisi nyingine za kikachero zimetuma watu wao kumnasa, lakini sifikiri kama ni vyema wakamchukua ndani ya ardhi yetu wenyewe, huyu ameshatekeleza mambo Fulani ya kijasusi katika nchi yetu na zingine za Afrika Mashariki” madam S alikuwa akiongea bila mapumziko akionekana wazi amehamanika kwa hilo.
“Madam, mi niko safarini,” kamanda Amata alitoka katika meza yake na kuchukua vifaa vyake vichache vya kiofisi, akamwita Gina na kumpa maagizo Fulani Fulani ya kiofisi kisha akatoka na madam S, boss wake wa miaka mingi na kuondoka zake.
˜˜˜
BOEING 737 ilishuka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta. Ilikuwa alasiri tulivu uwanjani hapo palipoonekana kuwa na ulinzi mkali wa polisi na ule wa vyombo binafsi vya ulinzi.
Baada ya itifaki zote kukamilika, kamanda Amata alitoka nje na kukamata tax moja kabla ya kuamua wapi anataka kwenda mchana huo. Alijiweka katika saiti ya nyuma na kumwambia dereva ampeleke katika hoteli kubwa ya nyota tano katikati ya jiji hilo la Nairobi.
Kamanda Amata alifika katika Hotel Intercontinental, katika mtaa wa Posta na kuweka kambi yake hapo akiwa naa kazi moja tu aliyotumwa na serikali yake ama kumkamata Bill ili ajibu kwa yale aliyoyafanya siku za nyuma au uhai wake ubaki Afrika Mashariki na mwili wake urudi kwao, ilikuwa ni moja kati ya hayo lililotakiwa kutekelezwa. Amata alitupia begi lake kitandani na kuchukua kifaa chake maalum kilichoweza kung’amua kama humo ndani kuna aina yoyote ya mlipuko au chombo chochote kitakachoweza kuhatarisha maisha yake, aliporidhika na usalama wake, akalisogelea dirisha kubwa na kuvuta kidogo pazia lake na kutupa macho yake nje upande wa chini ambako pilikapilika za wakazi wa Nairobi waliokuwa wakirudi majumbani kutokea makazini zilikuwa kubwa, kana kwamba hakuridhika na kile alichokua akikitazama alivuta kibegi chake na kutoa kiona mbali na kukisogeza karibu na macho yake, naam kile alichokiangali kilikuwa kikionekana kwa uzuri wa hali ya juu, vijana waliokuwa wakijidunga madawa ya kulevya katika moja ya mitaa hiyo ulioonekana wazi kuwa haukuwa ukitumika na wapita njia, alitazama kwa makini vijana wale walivyojidunga mpaka kuanza kusinzia pale chini, Amata alitikisa kichwa kwa masikitiko, ‘Nguvu kazi ya taifa inatoweka’. Akiwa katika kutafakari hayo mara alisikia ving’ora vya polisi na kufuatiwa na gari mbili zilizopita kwa kasi kuelekea upande wa pili wa eneo hilo, ‘Shughuli za kiusalama hizo’, alijiwazia kwa mara nyingine na kutoka pale dirishani kisha kuketi katika kochi moja lililopo pale chumbani. ‘Bill Van Getgand, umekuja tena, sasa hakika hutoponyoka kwenye mikono hii,’ akaivuta laptop yake na kuanza kuperuzi habari mbalimbali za jasusi huyo, akirejea hasa yale matukio yaliyofanywa na mtu huyu pale Dar es salaam …
Miaka mitano iliyopita
Kamanda Amata aliuangalia mwili usiokuwa na uhai uliokuwa ukielea katika bwawa la kuogelea la hoteli hiyo kubwa ya kimataifa iliyopo pembezozi mwa bahari ya Hindi. Watu kadhaa walizunguka eneo hilo wote wakiwa wametokwa na hamu ya kujiburudisha kwa maji hayo ambayo sasa yalikuwa mekundu kwa damu ya mtu huyo aliyeonekana kuwa na asili ya America. Akiwa amepiga goti moja pale katika ukingo wa bwawa hilo, kamanda Amata aliinua kichwa chake na kutazama uelekeo ambao labda muuaji alikuwapo, kwa maana mtu huyo aliuawa kwa risasi iliyotoka katika bunduki aina ya Sniper Rifle ya Kimarekani, naam macho yake yalitua mahali sawia, dirisha moja lililokuwa katikati kama ghorofa ya nane hivi katika jingo lililokuwa na benki ya Meridian Biao enzi hizo. Alipotuiliza macho yake alishuhudia pazia la dirisha hilo likifungwa ghafla kana kwamba aliyekuwa hapo dirishani alikuwa akimtazama Amata pia. Ili asimpoteze maboya mtu huyo Kamanda Amata kwa kutumia simu yake maalum iliyounganishwa na saa ya mkononi alipeleka ujumbe wa sauti kwa Madam S aliyekuwa upande wa pili wa jingo hilo, nae bila kusita alituma kikosi cha watu wanne kwenda kufanya uchunguzi katika ghorofa hiyo.
Hisia za Amata hazikuwa bure, jasusi Bill Van Getgand lilikamilisha kazi yake kupitia ofisi ya mtu Fulani ndani ya jingo hilo kwa kutumia bunduki ya Sniper Rifle, wakati vijana wale wakigawana majukumu mmoja apande kwa lift, mwingine kwa ngazi ya kawaida na wengine wabaki nje kutazama kinachoendelea, ndipo yule aliyepanda kwa ngazi alipopishana na Bill aliyekuwa akishuka huku akitanguliwa na mwanadada mmoja mwenye umbo dogo aliyekuwa amebeba koba kubwa la kuhifadhia guitar lakini akiwa kwenye hali ya kutojiamini, yule afisa usalama alitulia kidogo na kuwaangali huku akipishana nao na mara hiyo akatoa taarifa kwa walio nje kumwafuatilia watu hao bila kuwapoteza.
Kwa uchunguzi wa muda mfupi uliofanyika katika chumba kilekile ambacho Amata alikihisi tangu mwanzo liliokotwa ganda moja la risasi ambayo ni ile iliyotumika kumuua bwana yule.
Kamnda Amata alilitazama ganda lile na kutikisa kichwa kukubali hisia zake.
“Mnasema mmeweka watu wawafuatilie hao mnaowahisi?” aliwauliza wale vijana chipukizi katika kazi hiyo.
“Ndiyo na tunatumaini bado wanawafuatilia” alijibu mmoja wao. Kamanda Amata akainua simu yake ya upepo na kuwauliza vijana wale waliopewa kazi,
“Ndiyo, tupo hapa Red Carpet Upanga, wameingia ndani na bado hawajatoka, gari yao ipo hapa nje inawasubiri,” jibu lilimridhisha Amata, aliingia garini na mara moja kuelekea Upanga, akawakuta vijana wake wakiwa wametega pa si kuwaona watu hao, masaa mawili yalikuwa yamepita, Amata aliteremka na kuzunguka lile jingo la ghorofa mbili na alipofika nyuma yake alitikisa kichwa kwa kuugundua upumbavu wa vijana hao waliobaki ndani ya gari wakati nyuma ya jingo kuna ngazi zinazoweza kumtoa mtu yoyote aliye ndani ya jingo hilo, akarudi mpaka mbele na kuwapa taarifa hiyo ambayo iliwafanya wafadahaike sana kwa ujinga walioufanya.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi