MAUAJI YA KASISI (9)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA TISA
ILIPOISHIA...
mara alivuta kabrasha hili mara lile lakini hakujua anachotaka kufanya kwa muda huo, akiwa katika hali hiyo aligutushwa na hodi iliyogongwa mlangoni mwake kisha mwanamama mmoja aliyevalia kiraia aliingia kwa ukakamavu na kubana miguu yote miwili kuonesha nidhamu ya kijeshi.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
“Jambo afande?” Inspekta asitoti alisabahi

“Jambo!” alijibu yule mwanamke au kana anavyojullkana Sargeant Maria, “Afande natoa taarifa ya kuumia afande Otho’ katika mapano na moja kati ya majambazi tunayoyatafuta”

“Oh! Pole sana afande, nieleze kwa kina,” Inspekta Saitoti aliomba aelezwe huku akimpa ishara ya kuketi kitini sergeant Maria.

Alipokwishakueleza kinagaubaga kila kilichojiri, alitulia kitini kimya akisubiri amri ya boss wake itasema nini, mara Inspekta Saitoti alikohoa kuashiria kuuvunja ukimya ule.

“Ok! Sasa kutokana na hilo, naomba afande Otho nimuondoe kwenye operesheni hii na nikupe kijana mwingine machachri wa kukusaidia, koplo Kariithi, au we unasemaje?” alimuuliza huku akimkazia macho,

“Sina neno afande, kijana yupo kamili na anaweza kazi,” Maria alijibu kwa sauti ya ukakamavu hasa.

“Ok basi nitampa taarifa na mara moja ataungana na wewe katika hili, hakikisheni tunawatia mbaroni wauaji ili sheria ichukue mkondo wake,” sergeant Maria alisimama na kubana miguu yake sawia, “Sawa afande!” alijibu, akageuka na kutoka nje.

Inspekta Saitoti alibaki tena peke yake mle ofisini, sasa hakuwa anagongagonga ile peni tena pale mezani bali alikuwa akibofya namba za simu yake ya mezani na kuweka kile kisikilizio sikioni mwake kusubiri sauti ya upande wa pili iongee lolote.

Alipokwisha kuongea na mtu wa upande wa pili alitulia tena kitini na kufungua runinga yake ndogo iliyowekwa ofisini humo na kufuatilia habari za kimataifa. Mara mlango uligongwa na alipomkaribisha mgongaji, aliingia kijana wa makamo, mwenye kadiri ya miaka kama ishirini na minane hivi, mwenye siha nzuri ya kuvutia, aliyejengeka kimazoezi, alisimama mbele ya Inspekta kikakamavu, Inspekta Saitoti alimtazama kijana huyu, kisha akavuta motto wa meza na kutoa bahasha ya khaki akamkabidhi, na maneno machache yakafuatia ya kumpa majukumu ya afande Otho ambaye kwa kipindi hicho alikuwa hospitalini akiuguza jeraha lake. Kariithi alirudi nyuma hatua mbili na kupiga mguu chini kisha akageuka kikakamavu na kutoka nje ya ofisi ile.

˜˜˜

Sergeant Maria alikuwa akimuelekeza mambo Fulani Fulani koplo Kariithi juu ya wapi wameishia na nini cha kufanya juu ya sakata hilo la mauaji ya Kasisi.

“Ok, mi nafikiri sasa cha kufanya ni kufuatilia nyendo za hawa jamaa ili tuweze kuwatia mkononi” Kariithi alitoa ushauri.

“Ni sawa, lakini bado hatujajua adui yetu anapenda kuonekana wapi,” Maria alieleza dukuduku lake katika hilo.

“Nimekuelewa afande, hapa kuna sehemu kubwa nne za kufanya doria, Dagoreti Corner, Kawangware, Korogocho na Uthiru Kenoo, nafikiri tukifanya doria kali pande hizo tunaweza kama si kuwatia mkononi basi kupata japo harufu yao” koplo Kariithi alieleza kwa kujiamini na mkakati ukapangwa wa kufanya doria ya kimyakimya maeneo hayo yote.

Ulikuwa ni usiku wa balaa katika mitaa hiyo, hakuna aliyekamatwa kwa maana polisi hao waliwajua wanaowatafuta, hawakufanya kamatakamata kama za huku kwetu Bongo.

Uthiru Kenoo…

“Leo hii lazima tumalize kazi!” Cheetah aliwaambia wenzake huku aking’ata pande kubwa la mutura na kulishushia na tusker, akabeua na kuwatazama wenzake kwa zamu, “Maisha hayana guarantee, hasa haya yetu, Bill atatulipa pesa nyingi sana ukizingatia pesa tu aliyomlipa yule kahaba Rose ni ndefu itakuwaje kwetu sisi?”

Mellina alionekana kuwa mbali kabisa kimawazo, walipomgutusha wenzake alionekana kama mtu aliyetoka katika usingizi,

“We vipi? Mbona hauko nasi kabisa?” Wambugu alimuuliza

“Ah! Nafsi yangu inanisuta sana, hivi kwa nini tunafanya unyama huu kwa sababu ya pesa? Tumemuua kasisi wa watu bila kosa,” Mellina alionekana kusikitika sana.

“Aaa ha ha ha ha Mellina, wewe ni jambazi wa kike, muuaji ambaye hata Mungu hana muda wa kukusamehe, leo hii ujutie kifo cha mtu mmoja, mtu asiye na faida, hana watu wanaomtegemea wala nini, pesa pesa Mellina, hata Yuda Iskariote alimtoa Yesu auawe kwa vipande thelathini vya fedha, nini wewe!!!” Cheetah aliongea huku akiwa amesimama akigonga meza yake kwa ngumi, tayari pombe ilikuwa imekwishafanya kazi yake kichwani, alihema kwa nguvu na kuwatazama tena kwa zamu, “Ninawaamini sana vijana wangu, kwa kuwa Mellina ameonesha mashaka sasa nabadili program, leo hii tunaenda kuibeba hiyo Mostrance, lazima ipatikane, kwa udi na uvumba, kama jina la riwaya ya Innocent Ndayanse, leo hii ili kesho Bill atupe dolari zetu na kila mtu atawanyike kivyake, kama kukamatwa na akamatwe kivyake,” amakweli pombe mwana haramu, Cheetah alitoa bastola yake na kuifutafuta vumbi hakujali kama watu walikuwa wakimwangalia, Wambugu akainuka na kumnyang’anya ile bastola kisha kumvutia nje na kumuingiza kwenye gari, alishaona kuwa sasa Cheetah hakuwa yeye.

Mellina alikaa nyuma ya usukani na kutaka kuiondoa gari ile lakini alikuta mbele yake kuna watu wawili wamesimama wakimtazama, ‘Polisi’ alijiwazia huku akikanyaga clutch na kutumbukiza gia ya kwanza, alipoanza kukanyaga accelerator wale polisi wakatoa bastola zao tayri kwa mashambulizi,

“Shiiittt!” Mellina alikanyaga mafuta kwa nguvu na huku bado mguu haujatoka sawasawa katika clutch na kuuzungusha usukani, norinda iliyotokea hapo haikuwa ya kawaida, vumbi lilitimka usiku huo na watu walio jirani walisikika wakipiga mayoe ya woga, Cheetah na Wambugu tayri bastola mikononi wakishambulia upande ule walipo wale askari, lakini umahiri wa Mellina katika usukani uliwafanya wakose shabaha, ile Subaru iliizunguka na kuingia barabarni kisha Mellina akatumbukiza gia ya pili mara ya tatu na kuwaacha watu midomo wazi. Mwendo haukuwa wa kawaida kuelekea mjini huku baadhi ya gari ya polisi zikifuata nyuma kwa kupiga ving’ora ili kupisha njia kumbe kwa jinsi hiyo walimpa mwanya Mellina kuchanja mbuga, dakika kama tano kulikuwa na pengo kubwa kati ya polisi na Mellina.

“Weka gari pembeni,” aliamuru Cheetah kisha akafungua mlango na kuwaamuru wenzake kumfuata, wote walitoka na moja kwa moja wakaenda katika maegesho ya NAKUMATT supermarket maeneo ya Westland na kuingi kwenye Toyota Prado, kwa kutumia funguo za bandia waliiwasha ile prado na kuitoa pale maegeshoni na kuileta barabara kubwa, waliyaacha mafgari ya polisi yapite kisha wao wakaingia nyuma yao na kufuata taratibu.

“Sasa tunakwenda moja kwa moja kuchukua ile Mostrance sasa” Cheetah aliamuru na kila mmoja akajiweka sawa kwa hilo, bastola zilizoshindiliwa risasi za kutosha zilikuwa tayari mikononi na viunoni mwao.

˜˜˜

“Ah!” koplo Kariithi alitikisa kichwa kwa kuchelewa kufika eneo la tukio,

“Vipi koplo?” sergeant Maria alimuuliza huku akiweka vizuri jacket lake.

“Yaani ningewapata hawa leo, nakuhakikishia afande ungeijua shabaha yangu leo” Kariithi alimueleza huku akivuta hatua fupifupi kuwaelekea wale polisi wawili waliokuwa pale kwa doria ambao ndiyo waliwapigi redio ili wafike hapo.

“Siku yao ipo! Usiku huu halali mtu mpaka tuwatie mkononi kwa gharama yoyote ile” sergeant Maria alimueleza koplo Kariithi. Kishapo wote wakaingia garini na akabla hawajatoka eneo lile walipata taarifa kuwa gari aina ya Subaru forester iliyotumiwa na majambazi hao imeonekana maeneo ya Westaland imetelekezwa, nao wote wakaenda hapo kuiona, kama walivyoambiwa waliikuta pale imetulia.

“Koplo, tunapambana na watu makini, tujiweke vyema” Maria alimtahadaharisha Kariithi.

Wakiwa wanajiandaa kuondoka wakati huohuo polisi wakifanya mchakato wa kuiwekea mtego ile gari labda watarudi kuichukua, mara walikatishwa na kelele kutoka katika maegesho ya supermarket hiyo.

“Oooh my car my car” (Oooh gari yangu, gari yangu), Sergeant Maria alitega sikio na kushuka katika gari yao kisha akaelekea kule kwenye ile kelele, mama mmoja wa kizungu alikuwa akilia kwa uchungu kuwa gari yake imeibwa, sergeant Maria alimtuliza na kumuuliza maswali machache kisha akamchukua na kwenda nae kituo cha karibu kwa ajili ya kuanza uchunguzi, alipokwishamkabidhi kwa wahusika, akarudi garini na kumkuta Kariithi akiwa bize kusikiliza muziki uliokuwa ukipigwa ndani ya gari hiyo, aliingia na kujifungia mlango.

“Koplo, kwa vyovyote Cheetah na wenzake wameiba ile gari,”

“Nilikuwa nafikiri hivyo pia, afande huu lazima uwe usiku wa kazi” Kariithi alisisitiza.

“Endesha gari!” Maria aliagiza

“Twende wapi afande?”

“Twende tukabane karibu na kanisa kuu kwa muda kidogo tukisubiri taarifa nyingine, labda tutaokota kitu huko.” Kariithi akaitoa ile gari kujiunga na magari mengine kuelekea katikati ya mji. Ilikuwa imetimu saa nne usiku, bado foleni ilikuwa kubwa ya magari katika jiji la Nairobi.

˜˜˜

Ngumi ya hasira ilitua juu ya meza ya chuma katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya Nairobi, huku akiuma meno aliuangalia mwili wa Fr Gichuru uliolala kwenye kitanda hicho ukiwa ndani ya mfuko maalum wa plastiki.

“Bill, Bill, Billllllllll !!!!! lazima ulipe kifo hiki kwa gharama yoyote,” Melchior Ndege alijikuta akiongea peke yake mle ndani ya chumba kile kidogo cha kuhifadhia maiti.

Hali ya utulivu ilitawala nje ya eneo la jingo hilo kubwa, watu waliokaa kwa utulivu kwenye vibenchi vidogo vilivyowekwa maalumu kwa kazi hiyo. Melchior Ndege alitoka akiwa kama mtu asiyejielewa na moja kwa moja aliingia kwenye gari yake na kuliacha eneo hilo kurudi ofisini.

Aliketi na kutulia akiwa na mawazo mengi sana juu ya hili sakata, sasa aliona kuwa kazi inaanza rasmi, kumsaka Bill na genge lake, kujua ni nani yuko nyuma ya Bill katika hili.

Mlio wa simu ulimshtua Melchior mawazoni, akaitazama simu ile iliyokuwa ikipiga kelele bila kunyamaza, akainyanyua na kuiweka sikioni, hakuongea kitu bali alijaribu kusikiliza sauti ya upande wa pili, nako kulikuwa kimya, walitegeana…

....zaidi ya kusikia pumzi inayopanda na kushuka kutoka upande wa pili, melchior hakuna alichosikia kutoka kwa mpiga simu, akaitua taratibu na kuiweka mezani bila kuirudisha kwenye kitako chake na kuifanya iendelee kuwa hewani, zaidi ya hilo alibofya kitufe cha kuruhusu sauti isikike kwa nguvu ‘loud speaker’ kisha akajituliza kitini. Akishika hiki na kile juu ya meza yake mara mlango uligongwa na kufunguliwa na mgongaji aliyejitoma ndani bila kukaribishwa, hakuwa mwingine ni yule boss wake bwana Shikuku aliyeingia akiwa amefura kwa hasira ambayo ilimtisha hata Melchior,

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni