MAUAJI YA KASISI (24)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE
ILIPOISHIA...
akasoma maelezo ya Wambugu na kuitazama picha yake, akaangalia na maelekezo mengine mengi, akaichukua namba ya simu iliyojitokeza hapo ambayo Amata aliitumia kuchukua maelezo hayo, akatabasamu na kumsifu Amata kimoyomoyo kwa jinsi alivyokuwa mtundu wa kufikiri pindi anapohitaji maelezo Fulani.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Alikumbuka jinsi anavyoweza kuiga sauti na saini za watu pindi anapohitaji kufanya hivyo, hakushangaa kusikia kuwa ameweza kupenya mtandaoni kwa kutumia password yake.

Alijiuliza mwenyewe, nani anaweza kukaa katika cheo cha Kamanda Amata na akatosha katika kila idara, mapambano ya mikono, utumiaji wa silaha za aina na aina, lugha za kutumia, utundu wa kuendesha vyombo vya ardhini, majini na angani, utundu wa kuiga sauti za watu, saini za watu, vyote hivi nani angeweza, kama isingehitajika watu wawili au zidi kufanya kazi ya mtu mmoja. Jambo moja tu lililomuuzi ni wanawake, Kamanda Amata alikuwa mdhaifu sana mbele ya mwanamke, na adui zake wengi walimuweza kwa hilo tu, walimkamata kwa hilo tu. Lakini bado walipokuja kuona jinsi na njia aliyotumia kutoroka walibaki hoi. ‘Kamanda atabaki kuwa Kamanda tu,’ Madam S alijisemea huku akiifunga laptop ile ndogo na kuirudisha mahala pake.

EMBU – KENYA

EMBU, mji uliopo kilomita takribani 120 kutoka Nairobi, upande wa Kaskazini mashariki kuelekea mlima Kenya. Ukifika miezi ya kumi na kumi na moja utafurahi kuona barabara na viunga vyake vilivyopambwa kwa maua ya rangi ya zambarau kutoka katika miti ya Jacaranda.

SAA 4:15 USIKU


KWA KUTUMIA mwendo wa miguu, Wambugu alivuta hatu kuelekea katika hoteli hiyo iliyopo katikati ya mji katika mtaa ya Haille Selasie, moyoni mwake alikuwa na amani sana kuwa sasa kafanikiwa kulitoka jiji la Nairobi. Akitegemea kukutana na mtu wake, Bill siku inayofuata huko Iryamurai, kabla hajaifikia kaunta ya hotel hiyo simu yake ikatikisika mfukoni mwake, akaitoa na kuitazama, private call, ilijiandika, hakuipokea akaenda kaunta na kuchukua chumba.

Akiwa ndani ya chumba chake Wambugu aliiona tena simu yake ikiita, akainyakua na kupoke,

“Wambugu, nikipiga simu upokee mara moja, unafuatwa, hapo mahali si salama, ondoka mara moja, nenda utafute sehemu salama,”

Ile simu ikakatika, Wambugu akabaki ameduwaa, hajui la kuamua, ‘Nani ananifuata?’ alijiuliza, ‘Bill amejuaje?’, ulikuwa ni wakati mgumu sana kwa Wambugu kufanya uamuzi, kwa kuwa alikuwa akijiandaa kuoga, ilibidi aahirishe zoezi hilo na kujipanga kutoka katika hoteli hiyo, alirudi kaunta akiwa kaweka mkono wake mfukoni, kashikilia bastola tayari kwa lolote ambalo litatokea. Alikabidha funguo na kuaga kuwa atarudi muda si mrefu. Alitoka na kuzishuka ngazi kadhaa za mlango huo na kupotelea kwenye kichochoro Fulani ambacho kilimleta katika maduka na mchanganyiko wa watu, ‘niende wapi?’ akajiuliza, hakupata jibu, usiku ulizidi kuwa mnene, kichwa kikimuuma, mawazo yake yakivurugika, mipango ikigoma kupangika, ulikuwa wakati mgumu.

Wambugu alivuta hatua ndogo ndogo kuelekea kituo cha tax, pale alizikuta tax chache zinazongoja abiria wa usiku, akiwa kutahamaki hivyo mara gari moja aina ya Jeep Cherokee ilisimama ghafla miguuni mwake, mlango ukafunguliwa kwa haraka na Kamanda Amata akatoka bastola mkononi, Wambugu akajua hapo kazi nzito, alipiga risasi moja kwenye kioo cha dereva, wakati Kamanda Amata anazunguka gari kiufundi ili kumfiikia Wambugu, kumbe mwenzake alishaliona hilo, akalala chini na kupita uvungu wa gari akatokea upande wa pili kisha risasi mbili zilifumua matairi nay a tatu ikalenga tank la mafuta. Kamanda Amata alipogeuka nyuma alishuhudia ile gari ikipaishwa juu kwa mlipuko huo, akajishika kichwa kwa sekunde kadhaa kisha akaikimbilia ile gari na bila kujali, alifungua kwa taabu mlango wa dereva, na kumtoa Ndege ambaye alipigwa risasi begani na Wambugu, akamvuta na kumtoa nje, hali ya Ndege haikuwa nzuri kwani jeraha la risasi na ule moto almanusura vimmalize. Haikuwa na aja ya kumtafuta Wambugu aliomba msaada wa wananchi na kumkimbiza hospitali ya Agha Khan.

Wambugu baada ya kuona kafanikisha hilo, alikimbilia kwenye viunga vya mji na kutokomea mbali kidogo na mji. Alitembea polepole na kutafuta mahali pa kujihifadhi usiku huo maana aliona sasa hakuna sehemu yanye usalama kwake.

Polisi wa Embu, walifika katika hospitali hiyo na kukutana na Kamanda Amata aliyekuwa pembeni mwa kitanda cha Ndege wakati mwenyewe akiwa katika chumba cha upasuaji.

“Tunataka tujue ni nani jambazi na nina mwanausalama?” askari mmoja alieonekana kuwa ndio mwenye sauti aliuliza. Kamanda Amata alimtazama kwa tuo askari huyu aliyeonekana anajua sana kuongea. Akamuonesha kitambulisho chake, lo, Yule askari alilowa ghafla na kutoa salamu ya kiaskari kwa ukakamavu wa hali ya juu.

“Sasa sikia, kuna jambazi hili hapa,” akachukua simu ya Ndege na kumuonesha ile picha, Yule polisi akashtuka kidogo na kushangaa akiwa kakunja ndita si kitoto, “Huyu, kafika hapa, ni mtu hatari sana tunamtafuta nchi nzima mpaka nje ya mipaka, ok sasa kama unaruhusu nianze doria usiku huu,” Yule polisi alimueleza Kamanda Amata, baada ya kufikiri kidogo, akaona hiyo ni njia nzuri ya kujua ni wapi huyo mtu anaweza kuwapo. “Ok, hakikisheni mnampata akiwa hai maana kuna maelezo nayataka kutoka kwake,” Yule askari alipopokea hiyo amri, akapiga saluti na kuondoka.

Usiku huo mchakamchaka ulianza, kila kona kila mtaa ni gari za polisi kumsaka Wambugu. Kila nyumba ya wageni ilipekuliwa usiku huo na akila aliyefanana alibebwa na kupekwa kituoni.

Melchior Ndege alirudishwa wodini baada ya lisaa limoja kwa oparesheni iliyofanikiwa sana ya kuitoa risasi iliyokwama katika mifupa ya bega lake la kulia, majeraha ya moto hayakuwa mabaya sana, aliweza kuongea kama kawaida japo chupa ya damu ilikuwa ikiendelea kuingia mwilini mwake.

“Kamanda! Siwezi tena,” alimwambia kamanda Amata kwa sauti ya chini kidogo, wakati huo Kamanda Amata alikuwa ameketi kwenye kiti jirani kabisa ya kitanda kile,

“Kwa nini kaka? Tupo pamoja usijali,” Amata alijibu.

“Sikia, nina hasira sana na Wambugu kama wewe ulivyo na hasira na Bill, nenda kamsake popote alipo, nitapona tu nikisikia kuwa umempata na umemtoa roho, nenda Kamanda kamalize kazi kabla hawajajua kuwa tuko pamoja,” Ndege alimueleza maneno hayo Amata. Wakapeana mikono, Kamanda Amata akatoka pale hospitali na mlangoni wakakutana na Yule polisi, “Vipi?” alimuuliza, lakini Yule polisi hakujibu kitu, nyuma yake kulikuwa na polisi wengine watatu, “Kamanda Amata, upo chini ya ulinzi kwa kuwa unaifanya kazi hii kinyume cha sheria,” Yule polisi mkubwa akasema hayo, “Nani aliyekwambia?” Kamanda Amata akauliza, “Tumepata taarifa kutoka makao makuu ya polisi Nairobi kwa uthibitisho kutoka katika ofisi yako huko Tanzania, twende kituoni,” Yule askari alimuamuru Kamanda. Kamanda Amata hakuwa na ubishi, alitii sheria bila shuruti, akapakiwa katika gari na kuondolea hospitalini hapo.

Wambugu alipoona hali si nzuri, polisi kila upande alijua kuwa sasa mambo yameharibika, alichomoka kutoka maficho yake na kutega barabara kuu kuona kama kuna gari litakalotokea. Mara akaona pikipiki ikija upande wa kulia kwake akaokota jiwe na kumpiga nalo Yule mwendesha pikipiki, kisha akajitokeza barabarani na kuokota ile pikipiki, akakaa juu yake na kuitia moto, akaondoka kwa kasi kubwa.

Gari iliyokuwa imemchukua Kamanda Amata ilikuwa ikipita barabara hiyo na mara wakaiona ile pikipiki ikija kwa kasi sana, dereva akapunguza mwendo kuona ni nani huyo, “Msimamishe tafadhali,” Yule mkuu akamwambia polisi mwingine, ambaye kwa haraka aliruka chini na kutua barabarni kisha akasimama katikati ya barabar kumsimamisha jamaa huyo, lakini akiwa katika hali hiyo, mlio wa risasi ukasikika na mara Yule polisi akawa chali barabarani, Kamanda Amata akatzama huku na huku akishuhudia Yule dereva akishuka kumsaidia mwenzake, akaruka upande wa mbele kwa dereva na kuigeuza gari kwa fujo kuifuata ile pikipiki, mwendo uliokuwa ikiendeshwa hiyo land cruiser haikuwa ya kitoto, Kamanda Amata alikanyaga mafuta kwa ustadi wa hali ya juu, akaiona ile pikipiki ikikata kushoto na kuingia barabara nyingine nae alipofika pale vivyo hivyo akakunja kuelekea kushoto akiendelea kuifuata ile pikipiki.

§§§§§

Usiku wa manane, Madam S alipata taarifa ya kukamatwa kwa Kamanda Amata, taarifa zilitoka katika ofisi za ubalozi usiku huo, likaandaliwa gari kwa ajili ya kwenda Embu kutoka ubalozini kwa minajiri ya kumchukua Kamanda na kumrudisha Tanzania. Aliamka kwa kusuasua, na kujiandaa, alipokuwa tayari aliteremka kwa lifti mpaka chini ambako aliikuta gari hiyo ikimsubiri, akaketi kiti cha mbele na kuanza safari na watu wengine wawiliyaani dereva na Mashaka, Yule kijana waliekutana pale uwanja wa ndege.

Upande mwingine bwana Shikuku alishtushwa na taarifa za kijana wake Ndege kupigwa risasi na Wambugu pia kupata ajali ya moto uliosababishwa na mtu huyo huyo, moyo ulimchafuka na usiku huo akapanga safari yake ya kwenda Embu kujua nini kinaendelea. Akiwa njiani alikuwa akijaribu kuwasiliana na watu wa usalama upande huo kujua hali kwa ujumla ikoje, na kama ni chuki basi hakuna mtu aliyemchukia wakati huo kama Wambugu, aliapa moyoni lazima amtie nguvuni na atumikie kifungo chake kwa mateso makali.

Kwa ujumla usiku huo kila mtu alikuwa akiwaza yake juu ya Wambugu. Madam S alikuwa ametulia kitini haongei chochote, aliwaacha dereva na Mashaka waongee.

Haikuwachukua muda mrefu usiku huo, masaa mawili na nusu tu tayari walikuwa Embu na moja kwa moja walienda katika kituo kikuu cha polisi na kukutana na mkuu wa polisi wa kituo hicho. Madam S alijitambulisha kwao na kuonesha kitambulisho chake.

“Tunasikitika kuwa kijana wako ametoroka,” ilikuwa kauli ya mkuu Yule. Mashaka akamtazama Madam S ambaye alikuwa ameketi bila kuongea neno lolote, “Na isitoshe ametoroka na gari ya polisi,” akaongeza tena Yule mkuu wa polisi. Madam S alikuwa akitikisa kichwa tu kuashiria kuwa ameelewa anachoambiwa.

“Atarudi tu, msiwe na shaka,” madam S akajibu kwa kifupi, kisha akanyanyuka na kumuamuru dereva waelekee hospitali ya Agha Khan ili akamuone bwana Ndege aliyejeruhiwa katika sakata hilo. Alipofika tu pale hospitali alikutana na Bwana Shikuku, kila mmoja alimkumbuka mwenzie, waksalimiana kwa bashasha kwa kuwa ni miaka mingi hawajaonana. Baada ya hapo wote wawili wakaelekea ndani ya hospitali hiyo kumuona Ndege aliyekuwa amelala usingizi.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni