MAUAJI YA KASISI (32)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA THELATHINI NA MBILI
ILIPOISHIA...
Hellen alimtazama Kamanda Amata hakummaliza, akaingia za mkono wake mkobani na kutoa kitu kama kikebe cha wino wa mhuri, akakifungua, ndani yake mlikuwamo na sigara tano na kiberiti cha gesi, vyote viliweza kutosha ndani ya kikebe kile. Akachomoa sigara moja na kuiweka mdomoni, akamtazama Kamanda Amata, kabla hajafanya lolote Kamanda Amata aliitambua ile sigara,

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
haikuwa sigara bali ni mfano wa sigara ambayo ukiiweka mdomoni na kusukuma pumzi kwa nje, sio kwa ndani kama kawaida ya kuvuta sigara, hutoa vumbi jepesi sana ambalo litakupa usingizi ndani ya sekunde kumi tu.

Kamanda Amata alimnyang’anya ile sigara na kuitupa pembeni, Hellen alipiga kelele, na kitendo hicho kilimfanya Kamanda Amata kukanyaga breki za ghafla akiwa katika mwendo mkali. Hellen alikuwa hajafunga mkanda hivyo alichomoka kwenye kioo cha mbele na kutoka mpaka nje akadondokea barabarani. “Bull shit!” aling’aka Amata, akakanyaga klachi ya gari hiyo na kuweka gia ya kurudi nyuma na gari ile ikatii amei pale alipoachia klachi na kutimba pedeli ya kusukuma mafuta, kona moja kali ikamgeuza kutazama alipotoka na kutupia namba moja, kisha mbili, mara tatu, akawa amemuacha Hellen pale barabarani akiwa hoi na yeye kurudi kwa kasi alikotoka. ‘Mwanamke mpumbavu sana huyu,’ alijisemea moyoni huku akiongeza kasi ya gari lile ambalo injini yake bado ilikuwa ikidai gia ya sita wakati tayari zilikuwa zimekwisha zile zilizopo. Akiwa katikati ya mawazo yale na kumsonya Yule mwanamke huku akimtukana kimoyomoyo, aliona taa kali zikimmulika usoni akashindwa kupambanua njia halisi iko wapi na hicho pele ni kitu gani.

Puuuuuuuu!!!!! Kishindo kikubwa kikasikika, gari aliyokuwa akiendesha Kamanda Amata ilikutana uso kwa uso na katapila la kutengeneza barabara, ilijipiga kwenye jembe la chuma cha pua, ikapinda boneti yote kuelekea kwenye kioo cha mbele, kisha lile katapila likainamisha jembe lake na kuiangusha ile gari na kuibonda vibaya, ikaibeba tena na kukokota mpaka kwenye jalala la kutupa magari mabovu. Yule operetta wa lile katapila aina CAT aliinua simu yake ya upepo na kuongea na watu walio upande mwingine, “Kazi tayari boss (…) hawezi kutoka mpaka Yesu arudi amtoe kimiujiza,” kisha akakata ile simu na kuegesha katapila lake pembeni. Range Rover Vogue, lilifika katika jalala lile ambalo halikuwa mbali sana na pale ilipotokea ajali ile ya kutengenezwa, ikasimama na watu wanne wakashuka, Bill akiwa mmoja wao mkononi akiwa na ile fimbo yake ya kutembelea.

“Mali hiyo hapo boss,” Yule operetta akamwambia Bill huku akimuonesha kwa mkono ile Marcedes ilivyopondwa na kuwa chuma chakavu kwa ghafla namna hiyo.

“Vizuri sana, alikuwa ananiumiza kichwa sana huyu jamaa, akapumzike kwa amani, jivu kwa jivu. Vumbi kwa vumbi,” Bill alipomaliza kusema hayo, akampa Yule jamaa kitita cha noti kama shukrani kwa kazi hiyo ndogo aliyoifanya. Kisha wao wakarudi garini na kuondoka usiku ule, akaigeuza taratibu Yule drva na kuchukua uelekeo ule waliojia, Bill akainua fimbo yake na kuigemeza dirishani, ncha ya kutembelea ikwa imetazama kule aliko Yule operetta, akakifyatua kijichuma kidogo kilichoupande wa mshikio na kukivuta kwake, lo, Yule jamaa alikuwa akishangaa kuiangalia ile Vogue huku akiwa haamini kupata kile kitita cha noti, alijikuta akipenywa na kitu kama msumari kifuani mwake, mara akadondoka na kuanza kuona macho yake yanakuwa mazito kama yaliyojawa na ukungu, tayari kulikuwa ni giza muda huo lakini giza linguine zito lilimfunika, roho yake ikaacha mwili. Bill alikuwa amemuua operetta Yule kwa risasi kutoka katika hiyo anayoifanya ni fimbo ya kutembelea. Kijana mmoja kati ya wale waliokuwa garini pamoja na Bill akashuka na kwenda mpaka pale kwa Yule operetta marehemu, akachukua ile pesa na kurudi garini, akamkabidhi Bill. “Kazi ngumu lakini imekwisha bila jasho, alale pema peponi Kamanda,” Bill alizungumza na ile gari ikaondoka eneo lile.

§§§§§

DON ANDREAS hakuamini anachoambiwa na Bill kuwa Kamanda Amata hayupo duniani. Akiwa katika sebule yake kubwa pamoja na mgeni wake kutoka Vatican, Fr Gustav Maker wakijivinjari kwa vinywaji vikali, wote waliifurahia taarifa hiyo kutoka kwa Bill. Dakika chache baadae Bill aliungana nao hapo sebuleni na tafrija isiyo rasmi ikaendelea.

“Kazi haikuwa rahisi mjomba,” Andreas alikuwa akimsimulia Fr Gustav juu ya mkakati mzima mpaka kuipata ile Monstrance.

“Pole sana mjomba lakini maadam umeipata basi utajiri wako utakuwa wa milele,” Gustav alimwambia Andreas, akinua glass yake iliyojaa kinywaji na kujimiminia kinywani mwake, kisha akamwangalia Andreas na Bill, “Iko wapi hiyo Monstrance?” akauliza.

“Ipo katika chumba cha siri,” Andreas akajibu, “Unataka kuhakikisha kuwa ipo au la?” akamtupia na swali.

“Yeah, hilo ni la msingi, nipeleke nikaione,” akaomba. Andreas aliinuka pamoja na Bill kisha wakafuatwa na Fr Gustav. Wote watatu wakaingia chumba cha siri ambacho ni mtu mmoja tu mwenye dhamana ya kukifungua, Andreas mwenyewe kwa kuwa mlango wake unahitaji, namba maalumu ya kubonyeza, alama ya kidole gumba na alama za macho, vyote hivyo ni vya Andreas, walipofika pale alifanya hayo yote, kisha wqakafunga kwa ndani na kuingia huko ilikohifadhiwa hiyo monstrance.

Fr Gustav, akaitazama ile monstrance kwa makini sana ikiwa imelazwa juu ya kijisanduku kidogo ambamo ilitosha kabisa, akainyanyua na kuigeuzageuza, ilikuwa iking’aa sana kutokana na taa iliyokuwa ikiwaka ndani ya chumba kile, ilikuwa ni dhahabu safi ambayo haijachakachuliwa bado. “Niliambiwa kuwa monstrance hii ina siri kubwa sana ndani yake, lakini mpaka sasa sijaijua,” Andreas alimwambia Fr Gustav.

“Ni kweli, na nimekuja hapa kwa sababu hiyo tu, hii Monstrance lazima irudi Vatican,” Kwa kauli hiyo, Andreas na Bill walibaki wakitazamana kabla ya wote kumgeukia Fr Gustav. “We una kichaa ee!” Andreas alimwambia Gustav.

“Hata kama nina kichaa, lakini monstrance hii lazima irudi Vatican, siri iliyomo nitakwambia lakini hiki chombo lazima kirudi”

Gustav akaishika katikati ile monstrance mkono mmoja upande wa kitako na mkono mwingine upande wa juu akainyoga katikati kama anaivunja au anaifungua, ikafunguka, kisha akaweka kitako chini, akabaki na kipande cha juu. Don Andreas alikuwa bado akishangaa hakujua kuna nini kinafanyika. “Na hii ndiyo siri iliyomo katika chombo hiki,” Gustav akawaambia huku akiinamisha na kikaratasi kirefu kikatoka ndani ya kile kibomba kidogo ambacho hushika kitako na sehemu ya juu ya chombo kile.

Gustav akaiweka chini ile monstrance na kuchukua ile karatasi, akaifunjua kunjua kwa uangalifu, ilikuwa ni ramani kubwa sana inayoonesha njia za kupita mpaka kwenye hazina kubwa ya madini ya dhahabu iliyojificha huko kwenye milima ya Peramiho, kusini mwa Tanzania, mawe makubwa amabayo chini yake kulikuwa na kama mapango yenye madini ya thamani. Andreas ilikuwa nusu azimie kwa kkile anachokiona, alikuwa akisoma maandishi yale ya kijerumani huku akiwa na tabasamu pana kuliko sura yake. Alipomaliza kuitazama ile ramani na kuyasoma kwa ufasaha yale maandishi yaliyoandikwa karne kwa karne lakini hayakuwa yamefutika, bado yalionekana kwa upya wake. Andreas alitingisha kichwa chake kuashiria kweli amekubali maneno ya babu yake. “Gustav, tumekuwa matajiri wa maisha,” Andreas alimwambia Gustav. “Ni kweli, lakini unajua hazina hiyo hiko wapi?” akauliza.

“Tanganyika kwa maelezo haya, ambayo ni Tanzania ya sasa,” Andreas alijibu.

“Na utaendaje huko kufanya hiyo kazi?” lilikuwa swali la Gustav.

“Aaah Gustav, hiyo sio shida, ni kwenda pale na kununua eneo lote lile, pesa ninayo, watanikubalia tu wale masikini kisha tunachimba. Siri ni uwekezaji tu, tukishawapa kishika mkono basi viongozi wataachia njia,” Andreas alisema kwa kujiamini.

“Haya nakutakia kila la kheri, lakini mmefanya kosa kubwa moja ambalo mimi sikulifurahia,” Gustav akaikatisha furaha ya Andreas.

“Kosa gani?” akauliza.

“Kosa ni watu uliowatumia, kumuua Fr Gichuru ni kosa kubwa sana ambalo usipoangalia litakugharimu,” Gustav akamwambia Andreas.

“Kama amekufa amekufa tu,” Bill akashindilia msumari wa mwisho katika hilo. Andreas akaiweka ile ramani juu ya kijimeza kidogo kwa minajiri ya kuja kuisoma vyema baadae, kisha wote watatu wakatoka nje ya chumba hicho na kikafungwa tena kama klilivyokuwa mwanzoni.

§§§§§

10

KAMANDA AMATA alijikunguta vumbi, alijitazama hapa na pale alikuwa na michubuko michache lakini alisikia maumivu makali sana katika mkono wake wa kulia, akajaribu kuunyoosha na kuufanyisha mazoezi. Kidogo ukakaa sawa. Akajiangalia zile silaha zake nyeti ambazo huzificha ndani ya nguo zake, bastola yake ilikuwepo, camera na vitu vingine vyote vilikuwa vimetimia, kwa hatua za taratibu alijivuta kurudi barabarani.

Ulikuwa ni usilku mnene sana ambapo hakukuwa na magari mengi katika barabara hii ya kutokea nje ya mji wa Aachen, zaidi yalipita malori. Alitembea hatua za taratibu akipandisha kilima kidogo kilichokuwa hapo, alipofika juu, alikuta kuna Motel, taa zilikuwa bado zikiwaka na magari machache yalikuwa yamepaki nje yake. Akaiendea motel hiyo na kuingia ndani, kulikuwa na watu wachache ambao walionekana washari washari hivi, wakiwa wamevaa kiuni, wengine wakilewa [pombe na wengine wakiwa wanacheza kamali.

“Nahitaji msaada,” alimwambia Yule mwanadada wa kaunta.

“Tukusaidie nini?” Yule dada alijibu kwa Kijerumani safi. “Mna box la huduma ya kwanza?” akauliza Amata. “Ndiyo; bila shaka,” Yule mhudumu wa kaunta akajibu na kuingia nyuma ya kaunta akatoka na kikasha chenye alama ya msalaba mwekundu akampatia, Kamanda Amata akafungua ndani yake, akatazama akakuta kuna dawa aina ya Iodine akaichuku, bomba moja la sindano na kijichupa kidogo cha dawa aina ya Diclofenac, akavua shati, akaliweka pembeni, katika mkono wake palikuwa na jeraha kubwa kiasi kutokana na mburuzo alioupata alipokuwa akiruka kutoka ndani ya ile gari kabla haijagongana na katapila, akajipaka ile iodine huku akikunja sura kutokana na maumivu ya dawa hiyo, akaijiwekea na pamba kisha akamuomba Yule mhudumu wa kaunta amfunge bandeji naye akatekeleza hilo. Kamanda Amata alipoona kuwa hapo amekamilisha akajidunga sindano ya Diclofenac kutuliza maumivu.

Akaismama na kutoa shukrani kwa Yule dada, akavaa shati lake jeupe ambalo sasa lilikuwa halitamaniki kwa vumbi. Alipokuwa akitoka, mlangoni alikuta kuna majaketi yametundikwa, akajichagulia moja la rangi nyeusi akajitupia juu yake na kutoka nje, hakuwa na usafiri. Akatazama magari yaliyoegeshwa hapo, akaona moja inayomfaa.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni