MAUAJI YA KASISI (7)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA SABA
ILIPOISHIA...
“Salama tu Fr, leo tumeonana tena, sina mazungumzo mengi na wewe leo ila ninachohitaji ni ile Monstrance, tuambie ilipo tukaichukue usiku huu kisha tutakuachia huru, mimi sipendi kumwaga damu isiyo na hatia kama yako Reverent Father Frederick Gichuru

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Bill aliongea kwa pozi huku akiruhusu pumzi zake kumtoka kwa shida. Fr Gichuru alimtazama mtu huyu mnene na kisha kuwatazama wale wengine watano, mara moja akamtambua Gichui, yule jambazi waliyekutana naye kanisani akipekuwa makabati.

“Muulizeni huyu kama ameiona” alimueleza Bill huku akimtazama Gichui, “Ile ni mali ya kanisa ninyi mnaitakia nini?” akawauliza. Wote wakatazamana.

“Gichuru, kama hutaki kutueleza utataulazimisha kufanya kitu tusichokitaka, haya mi natoka nawaacha vijana wangu utawaelekeza” Bill mtu mnene alizungumza na kutoka katika kile chumba akifuatiwa na wengine wawili, pale ndani wakabaki watatu. Cheetah na wenzake walimuadhibu vikali Fr Gichuru kwa mapigo makali sana kumlazimisha aseme, lakini Fr Gichuru hakufungua mdomo wake badala yake alikuwa akisali kwa kilatini ambacho wale jamaa hawakuelewa kitu. Mateke ya tumboni, mbavuni, mikanda ya kijeshi vyote vilikuwa ni masluub kwa Fr Gichuru.

Lakini baada ya kumtesa kwa zaidi ya lisaa limoja Fr Gichuru alipoteza fahamu kabisa na kulala kama mfu.

“Amekufa?” Mellina aliuliza

“Hajafa huyu kazirai tu, lete maji baridi” Wambugu alimueleza Mellina, ndoo ya maji ikafika na kummwagia mwilini Fr Gichuru, akashtuka na kuhema kwa nguvu, akawatazama wale watesi wake mmoja baada ya mwingine.

“Baba uwasamehe maana hawajui watendalo” baada ya kusema maneno hayo alianguka na kupoteza fahamu kwa mara nyingine…

Kwa mbali alisikia mlango ukifunguliwa, ilikuwa ni ndoto tamu iliyomfariji moyo, alimuona Malaika akija pale alipolala na kumfungua zile kamba. Haikuwa ndoto kiuhalisia, mlinzi wa godown lile aliingia kwa kunyata ndani ya kile chumba kidogo alimfungua kamba na kumbeba mabegani mwake Fr Gichuru aliyekuwa hana fahamu na kujaribu kutoroka nae, alipita kandokando ya magari mabovu ili walinzi wenzake wasimuone kasha kwa kutumia kijimlango kidogo cha nyuma alitoka nje huku akiwa kambeba fr Gichuru kwa mtindo ule ule, baada ya mwendo mfupi alimuhifadhi katika nyumba ndogo jirani tu na eneo hilo, kasha yeye akaenda zake tena lindoni kwake, hakuna mtu aliyemgundu kwa hicho alichokifanya aliingia tena kimyakimya na kuendelea na majukumu yake kama kawaida.

Baada ya masaa machache Fr Gichuru alirudiwa na fahamu zake na kujikuta mahali tofauti na mwanzo, alijitazama na kujikuta hana zile kamba mikononi, yuko huru isipokuwa maumivu makali katika maeneo ya tumbo na mbavu yalikuwa yakimsumbua, hakujua ni jinsi gani amefika eneo lile, alijaribu kuinuka kutoka pale alipokuwa amelala, akaketi na kuegemea kabati kuukuu lililokuwa ndani ya kijichumba hicho na kushusha pumzi ndefu alipogundua kuwa hapo kwa vyovyote ni mahali salama. Akiwa katika tafakari hiyo alisikia nyayo za mtu zilizokuwa zikipitapita huku na huko upande wa nje, akajituliza kimya na kubaki kusubiri kuona ni nani huyo; mara kelele za mlango ambao bawaba zake zimekosa mafuta zilisikika na mlango ule uliacha kijinafasi cha kupenya mtu mwembamba, na punde tu mtu mmoja alijipenyeza na kuurudishia huo mlango nyuma yake.

Kutoka ndani ya koti lake alitoa mfuko wa plastiki uliondikwa UCHUMI na kuuvirigua kisha akatoa kachombo ka plastiki na kufungua mfuniko wake.

“Father, kula chakula, najua una njaa sana” yule mtu alimwambia Fr Gichuru. Ndani ya kichombo kile kulikuwa na chakula aina ya mokimo (mchanganyiko wa maharage, mahindi na viazi kisha husongwa kama ugali), Fr Gichuru alikula na kunywa maji yaliyokuwa jirani hapo bila kuangalia yana hali gani.

Baada ya kumaliza kile chakula, akajiweka vizuri na kumtazama yule mtu, sasa akagundua kuwa alikuwa ni mzee sana lakini bado likuwa na nguvu zake.

“Wewe ni nani?” Fr Gichuru alimuuliza

“Mimi ni bwana Melchior Ndege, mtu wa huko Iriyamurahi

“Hapa nimefikaje na ni wapi?”

“Tangu unafikishwa pale godown mimi nilikuona na sura yako si ngeni kwangu, nakufahamu sana, wewe ni Fr Gichuru wa kanisa kuu siyo?”

“Sawa kabisa! Zaidi ya hapo wewe ni Malaika kwangu, hakika Mungu amekutuma”

“Napenda tuzungumze kidogo” yule mzee alimwambia Fr Gichuru. Fr Gichuru alimwangalia kwa makini yule mzee aliyekaa mbele yake juu ya kiti kidogo cha miguu mitatu.

“Father, kwa nini hawa jamaa wamekuteka wewe? Maana kama hela huna!”

“Bwana Ndege, hii ni hadithi ndefu sana” Fr Gichuru akatulia kidogo kisha akaanza kumueleza kila kitu mzee yule, hakumficha hata jambo moja, kuanzia safari yake ya Roma mpaka aliporudi, mpaka alivyotekwa na jinsi ilivyokuwa. Mzee Melchior Ndege alitulia tuli kama maji ya mtungini, alimwangalia yule kasisi asiye na kosa kisha akakohoa kidogo.

“Father, mimi ndiyo niliyekuleta humu ndani, ndiye niliyekutoa kule, wala si mbali ni mtaa wa tatu tu hapo, nimekufuatilia kwa muda mrefu sana na hata mpango wa wewe kutekwa mi niliujua mapema.” Maelezo yale yalimshtua sana Fr Gichuru, alishindwa kuelewa inakuwaje mzee huyo kumfuatilia na kujua hata kutekwa kwake.

“Sijakuelewa bado bwana Melchior!” Fr Gichuru aliuliza kwa mshangao

“Na hiyo nayo ni hadithi ndefu father Gichuru, nitakwambia jiweke tayari” akachukua chupa yake ya maji na kupiga mafunda kadhaa kisha akaiweka chini na kuendelea, “Bill, ni mtu anayetafutwa sana kila kona ya dunia hii, ni jasusi la kutisha la kimataifa linalotumiwa na makundi mengi kuekeleza mauaji au wizi wa kimataifa, hapa ninavyokwambia tayari FBI wameshafika Kenya kwa ajili ya kumnasa mtu huyu, Bill hawezi kuja hapa kwa kuitaka hiyo monstrance tu kama alivyosema, ama kuna kitu kingine nyuma yake au hiyo monstrance ina jambo lingine ambalo ninyi hamlijui, mimi hapa usinione mzee, mi siyo mzee” yule mzee aliposema hayo aliingiza mkono wake ndani ya kofia aliyojifunika ambayo ilikuwa imeunganishwa na jacket lake na kwa kutumia nguvu alivua kitu kama gozi nene usoni mwake na kulitupa chini kisha akajifuta vizuri na kumtazama Fr Gichuru ambaye alikuwa amepigwa na butwaa akmtazama kijana huyo mtanashati kwa sura, kumbe alivaa sura bandia.

Siku chache zilizopita

Simu ya mezani kwa Melchior Ndege iliita, mara moja aliacha kazi aliyokuwa akiifanya na kuitazama simu hiyo alisita kidogo kuipokea, lakini kelele za simu ile zilimfanya aipokee

“Hello!” aliita

“…aa! Ok, sawa (…) sasa hivi nashughulikia”

Melchior aliinuka kwenye kiti chake na kuingia kwenye lift iliyompeleka juu kama ghorofa tano hivi katika jengo la KICC, aliuendea mlango Fulani na kuufungua kisha kuingia ndani

“Karibu sana Ndege, keti, maana kwa jinsi unavyohema itakuwa unahabari nzito” Gallus Shikuku alimkaribisha Ndege ofisini kwake.

“Nimepata simu kutoka ofisi ndogo ya uwanja wa ndege” Melchior alianza kuzungumza

“Mh niambie kijana!” alijiweka vizuri kitini na kuiegemea meza yake kubwa akimtazama Melchior Ndege.

“Mtu tunayentafuta kwa udi na uvumba ameingia nchini, Bill”

Gallus Shikuku hakuamini anachokisikia kwa kijana huyo alimkazia macho na kumuuliza tena swali lilelile, naye akapata jibu lilelile.

“Bill…” Gallus Shikuku alilirudia jina hilo, “Kaja kufanya nini tena? Kajileta mwenyewe” aliongea peke yake.

“Ok! Ndege nimeisikia hiyo habari, sasa vijana kazini, naomba umchunguze Bill anavyoketi na anvyosimama na wakati huo mimi nawasiliana na vyombo vyote vinavyomsaka ili tupate usaidizi maana huyu mtu ni wa hatari sana na tukienda vibaya anatumaliza.”

Melchior alitoka ofisini kwa boss wake bwana Gallus Shikuku na kurudi ofisini kwake kujipanga kwa kazi aliyopewa. Bwana Gallus Shikuku alijishika kichwa na kuzunguka kutoka huku na huku, aliiona sasa bahati imekuja kwao ya kumtia mkononi mkorofi huyu, Bill, aliyeshindikana, FBI wanamtafuta, Interpool wanamsaka kila kona ya dunia, lakini jinsi anavyowatoroka ni utata mtupu, wengine wakadiriki kusema ni mchawi lakini haikuwa hivyo.

Gallus Shikuku aliketi kitini na kuvuta laptop yake na kufungua sehemu ya kuandika ujumbe, baada ya kuhakikishiwa kuwa aliyeonekana ni Bill na watu wake walio uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta kumtumia picha za haraka na yeye kuzifikisha katika kitengo maalumu cha utambuzi, picha hizo zilitoa jibu lilelile, Bill Van Getgand. Shikuku alitoa taarifa kwa vyombo husika vya usalama ambavyo tayari vilisambaza habari na picha ya jasusi huyo popote duniani atakapoonekana basi mara moja wataarifiwe ili atiwe nguvuni.

Melchior Ndege aliondoka na kuliacha jengo la KICC na kujichanganya mjini kadiri ya maelekezo aliyopewa na watu wanaomfuatilia Bill, ili kujua ni wapi amefikia. Haikuwa kazi kwani alimuaona mtu huyu mnene akiwa na ile fimbo yake ya kutembelea, mara hii Ndege alishtuka kidogo, hakuambiwa kuwa huyu jamaa anatembea kwa msaada wa fimbo, alichukua kamera yake kubwa aina ya Cannon Cibershot na kumpiga picha kadhaa akiwa pale nje ya Plazza Hotel akilipana na muendesha tax, mara moja zile picha aliziingiza katika computer yake ndogo na kuzituma kwa bosi wake na maelezo machache.

Bill Van Getgand alipanga chumba namba 207 katika hotel hiyo, akiwa kaja Nairobi kwa kazi moja tu ndogo ya kuhakikisha anaipata monstrance aliyotumwa na tajiri wake kutoka Ujerumani, Don Andreas, kwa pesa nyingi sana.

Melchior Ndege, aliweka vijana eneo lile kuhakikisha wanapata nyendo zote za Bill mchana huo ili wajue jinsi ya kumtega.

* * *

Melchior Ndege aliendelea kubaki pale nje ya hotel hiyo akifuatilia kujua ni wakati gani bwana Bill atatoka ili na yeye afanye kazi yake, alilolisubiri likatimia, muda kama wa saa nne usiku hivi Bill alitoka na kwenda kusikojulikana, alipopotelea na gari hilo alilolikodi, Melchior alitoka katika gari yake na kuchukua vifaa vyake vichache na kuelekea katika hoteli ile, moja kwa moja hakupitia katika ofisi ya mapokezi, aliingia katika lifti na kupanda mpaka ghorofa ya pili, alikitafuta chumba namba 7, haikuchukua muda alikipata, kwa kutumia funguo zake maalum alicheza na kitasa kile na mlango ule ukafunguka, akaingia na kuurudisha nyuma yake. Akatazama kile chumba kwa macho ya kiintelijensia kisha akakiendea kile kitanda kikubwa na kuivuta droo ya kitanda hicho kisha kwa upande wa chini akabandika kidubwasha maalum kisha akafanya hima kutoka katika chumba hicho. Alipofika chini, pale alipoegesha gari lake aliingia na kuketi ndani,

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni