Vita vya Mapenzi (18)

0

SEHEMU YA KUMI NA NANE
TULIPOISHIA...
Hali ya raha na amani vikaanza kua ni msamiati wa kichina kwa Suhail, Shubiri ikatumbukia katika bwawa la raha alilokua amebweteka akiogelea, Suhail na Sharifa wakawa mithili ya Chui nap aka kwa jinsi walivyoanza kuishi kwa uadui huku kila mmoja wao akimuona mwenzie kua ndie tatizo. 

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
Nyumba ikawa haikaliki, chakula hakiliki, hakuna jambo wala Cheko. Hii yote ni baada ya Sharifa kutambulisha msimamo wake mpya kwa Suhail kua anaitaka haki yake ya Ndoa japo aliamini kua mumewe ni ‘Mbovu’, alichotaka yeye ni kuanza kutembea kwa wataalamu kutafuta tiba ya tatizo hilo la mumewe kitu ambacho Suhail alikipinga na kukikwepa sana kwani aliamini kua kwa kufanya hivyo ni kujihatarishia maisha yake kwani endapo wataanza kutembea kwa matabibu mwishowe mkewe huyo ataangukia mpaka kwa waganga wa kienyeji ambao kama atapatikana mjuzi kama Mzee Atrash basi mambo yote yatawekwa hadharani na itakua balaa.

“..Nakwambia hivi Suhail mimi ni mwanamke makini ninaejitambua, nimeshakugundua kua wewe una hila unaiendeleza kisirisiri nd’o maana unakwepa hatua za kujitibu, sasa kwa taarifa yako nimeshakuchoka mwanaume wewe na nimedhamiria kabisa kutafura njia mbadala ikiwemo kuwaeleza wazazi juu ya tatizo hili,” Sharifa alikua akiongea kwa ghadhabu huku akimuangalia Suhail aliekua amevaa fulana nyeupe huku akiwa amejilaza kitandani baada ya kutoka kuoga, Suhail aliogopa sana kusikia mkwara ule mzito kutoka kwa mkewe, ulikua ni mkwara uliomuingia sana na hakutaka jambo lile lifikie huko hivyo sasa ikampata kazi ya ziada ya kumbembeleza a kumsihi mkewe asithubutu kufanya hivyo

“Mke wangu leo umefikia hatua hii ya kutaka kunidhalilisha na kunifedhehesha kwa wazazi kwa kutoa siri zetu za ndani?! Hebu jitafakari upya we ni mke bora kweli..” Kabla Suhail hajaendelea kuitafuta huruma ya Sharifa akakatishwa tena na mkewe huyo aliekua amefura kwa hasira

“NO Suhail, hii sio siri tena, hili ni tatizo, tea kubwa hasa ambalo kama mimi na wewe tumeshindwa kuelewana kulitatua ni lazima sasa wazazi wasimame katika nafasi yao’

“Aliesema mimi na wewe tumeshindwana ni nani? Tatizo we unadhani mimi nimebweteka tu, Hapana nimeshahangaika vya kutosha mpaka nikachoka.. Na hapa ninajiandaa wiki ijayo niende Nigeria nimeambiwa kuna mtaalamu mwingine wa Tiba hizi”

“We usiichezee mimi hauendi popote nimeshakutilia shaka, utatumia dawa za hapahapa Tanzania mpaka tukihakikisha umenyoosha mikono ndipo tutafungua miguu kwenda mbele zaidi, na kila Tabibu tutakaempata ni lazima na mimi niende pamoja nawe kujihakikishia.. Na tunaanza sasa” Mbinu ya Suhail ya kutaka kusingizia kua ataenda kutibiwa Nje ili aonekana anafanya jitahada saa ikagonga ukuta kwa kukutana na masharti imara kutoka kwa mwanamke mwenye msimamo, Masharti hayo yakamshinda Suhail kuyatekeleza hivyo kuzidisha minyukano baina yao.

Maisha ya hofu, huzuni na mashaka yaliendelea kumtesa Suhail akawa kama mwehu sasa maana ilifikia hatua akawa anaongea peke yake barabarani, hata kazini kwake huko Wafanyakazi wake waliomzoea kupita kiasi waligundua kua hali ya Boss wao haikua sawa wakati mwingine alizidiwa na mawazo mpaka hufikia kutiririsha machozi kama aliefiwa. Nyumba haikaliki tena, zaidi ya Salamu hakuna kingine isipokua ni malumbano kila kukicha, Hali hiyo ilimnyima Suhail amani kabisa japo ilimuonngezea umakini mkubwa hasa awapo na mkewe kitandani maana wakati mwingine alijikuta akitaka kuzidiwa kwa vitimbi na mitego ya mwanamke Yule mzuri wa Sura na Umbo, alihofia kuuingia mtego ambao ungeyagharimu maisha yake

Mara kadhaa ambazo Suhail alikwenda kulala kwa Shekhia ndipo walau alipata utulivu wa nafsi japo napo alizidi kupewa Msisitizo wa tahadhari endapo atadiriki kuvunja makubaliano kwa kukutana kimwili na Sharifa mkewe halali, Vioja!

Ikawa sasa kila anapokimbilia kuna vitisho na vimbwanga vyake. Kadri siku zilivyozidi kuyoyoma ndivyo ghadhabu za Sharifa zilivyozidi kuchagiza maamuzi magumu ndani ya kichwa chake, akaamua sasa kuanza kupitapita kwa Wataalamu kutafuta dawa, kila dawa alizopatiwa alimuwekea Suhail katika chakula kisirisiri na alijiapiza kupambana mpaka pumzi yake ya mwisho na kwamba endapo atashindwa basi lazima awashirikishe wazazi wao wote wa pande mbili.

***Vita ni Vita...!

Nyumba ikazidi kua chungu, mke amepamba moto, ndani hakuna kusikilizana, mizozo na mitafaruku kila kukicha. Hata raha ya maisha haionekani tena, Ladha ya chakula kwa Suhail ikawa ni msamiati wa kichina. Kila siku alikua akitafuta namna ya kupambana na tatizo lililo mbele yake, wakati mwingine alifikia hatua ya kutaka hata kuua au kujiua mwenyewe ili mradi tu aondokane na tatizo hilo, siku moja likamjia wazo kichwani mwake na baada ya kulichekecha akalipitisha na kulipa nguvu ya kisheria ndani ya halmashauri ya kichwa chake.

Wazo lake hilo lilionekana kua ndio suluhu ya tatizo lake lakini ili alitimilize alilihitaji mtu mwingine tofauti na yeye alitekeleza kwa umakini na usiri mkubwa ikiwezekana hata kwa kumlipa pesa, aliamini kua sasa atapunguza kama si kumaliza kabisa tatizo lake endapo atalifanikisha zoezi lile kwa kadri ya kichwa chake kilivyopitisha azimio hilo, lakini sasa huyo mtu makini kumpata ikawa ni shida, alijaribu kuwafikiria watu kadhaa lakini hakuna alieonekana kukidhi vigezo vyake, alihangaika kwa siku kadhaa bila kupata mtu mwenye sifa alizozihitaji.

Ndipo siku moja akiwa analifikiria jambo hilohilo kengere ya ukumbusho ikagonga kichwani mwake, akamkumbuka rafiki yake wa karibu aitwae Msigwa. Hakika Msigwa alikidhi vigezo vyote kwa fikra zake yeye Aliamini kua atakua ndio funguo ya tatizo lake kama ataelewa somo na kukubali kumsaidia.

Suhail na Msigwa ni marafiki wa siku nyingi walioshibana haswa, walikutana kwa mara ya kwanza walipokua wakijiunga kidato cha kwanza katika shule ya ‘MILAMBO HIGH SCHOOL’ iliyopo mkoani Tabora ambapo Msigwa alikua akitokea mkoani Iringa na Suhail akiwa ni kijana wa mkoa huohuo wa Tabora aliebahatika kuchaguliwa kujiunga na shule hiyo akitokea shule ya Sekondari Isevya ya hapohapo mkoani Tabora, Kwa kiasi kikubwa urafiki wao ulitokana na kupangiwa bweni moja lililokua likiitwa ‘RUGAMBWA’ na pia wakawa katika chumba kimoja kilichopo juu ghorofani.

Kwa Msigwa ilikua ni bahati zaidi kumpata rafiki ambae ni mwenyeji wa mkoa huo wa Tabora ambao kwake yeye ulikua ni mkoa mgeni sana ikiwa ndo mara yake ya kwanza kufika hivyo alikua na uhakika wa kupata huduma za muhimu na msaada wowote endapo utahitajika kufanywa na watu wa nyumbani kwao. Na kweli Suhail akaenda kumtambulisha nyumbani kwao kwa Mzee Kusekwa pamoja na mkewe waishio mtaa wa Rufita ikiwa ni hapohapo katika manispaa ya Tabora

Hakika nao walimpokea kijana yule kwa mahaba kama mtoto wao wa kumzaa hivyo mara kadhaa hasa katika siku za mwisho wa wiki viajana hawa marafiki wakawa wanakwenda nyumbani kwao kutembea na kubadili ladha ya ugali maharage wanaoufakamia huko shuleni kila siku japo hata hali ya uchumi ya Baba yake Suhail haikua nzuri lakini walau Mchicha na kisamvu kiliwaliza sana vijana hawa, wakati mwingine hata Suhail asipoenda nyumbani kwao lakini Msigwa aliweza kwenda peke yake na kushinda huko kama kijana wa pale tu.

Hata siku moja ulipotokea Mgomo mkubwa sana shuleni hapo kutokana na wanafunzi kupinga huduma mbovu za chakula na ufundishaji wanazopewa, wakasusia kulala mabwenini na kutokula chakula cha shule hapo kwa takribani siku tatu mfululizo na walipoona hakuna hatua za makusudi za kuwasikiliza wakafanya ghasia kubwa sambamba na uharibifi wa mali za shulehali iliyopelekea mkuu wa Shule hiyo kutangaza kuifunga shule hiyo mpaka watakapotangaziwa vinginevyo hivyo wanafunzi wakatakiwa kuondoka shuleni hapo ndani ya masaa arobaini na nane kitu ambacho kilikua kigumu ukizingatia wengi wa wanafunzi wanatokea mikoa ya mbali na hawana pesa za haraka haraka lakini kwakua tayari hali ilikua ni ya hatari hivyo serikali ikasaidia kupeleka askari wa kutosha kuwadhibiti watakaokaidi agizo hilo la shule, ilikua hali mbaya sana kwani baadhi ya vijana waliuza vitu vyao vya thamani huku wengine wakikimbilia kuomba msaada katika nyumba za ibada ili wapate ahueni ya maisha na nanuli za kuwapeleka makwao.

Lakini kwa Msigwa licha ya kua anatokea mbali sana lakini hakupata tabu yeye na Suhail walikimbilia nyumbani kwao mtaa wa Rufita ambapo waliishi vizuri tu wakisubiria tangazo la kufunguliwa kwa Shule, familia ya akina Msigwa huko Iringa ilipopata habari ile walitaka kuchanganyikiwa lakini baadae Mzee Kusekwa akawasiliana nao na kuwatuliza kua kijana wao yupo salama na anapata huduma zote nyumbani hapo.

Hiyo ikawa ni hatua nyingine ya muhimu kati ya familia mbili za vijana wale, Wazazi wakawa marafiki kama walivyo watoto wao. Na hata Shule ilipofunguliwa vijana wakaendelea na masomo, na wakati wa Likizo ukifika Mzee kusekwa akawa anafungasha zawadi kadhaa anampa Msigwa apeleke huko Iringa kwa Wazazi wake ambao nao walimfungashia mara tu aliporejea masomoni Tabora, Ikawa ni kama udugu sasa

*****

Kupitia historia hiyo fupi Suhail na Msigwa walikua wameshibana sana kama ndugu wa damu, lakini baada ya kumaliza masomo yao ikawabidi kusambaana kila mmoja akiendelea na hatu nyingine mbele ambapo Suhail alijiunga na Chuo kikuu cha Dar es salaam wakati msigwa alipata chuo huko jijini Mwanza ambapo alikua akisomea uandishi wa habari.

Baada ya miaka takribani minne ndipo tena Suhail na Msigwa wakakutana Jijini Dar es Salaam ambapo Suhail alikua akifanya biashara zake na Msigwa akiwa ameajiriwa na Kampuni moja kubwa ipatikanayo Ilala, jijini Dar es Salaam iitwayo TuwaKadabra Production, ni kampuni mashuhuri inayozalisha magazeti kadhaa ya kila wiki, inajishughulisha na uchapaji na usambazaji wa vitabu, pia inamiliki kipindi maarufu cha luninga katika vituo kadhaa vya luninga nchini.

Kwa muda mfupi ambao Msigwa amekua akiandika habari katika magazeti ya ‘Mdadisi’ na ‘Haki’ yote yakiwa chini ya kampuni hiyo ya TuwaKadabra Production amejizolea umaarufu mkubwa sana kutokana na habari anazoziandika katika magazeti hayo, ni habari za kipelelezi na kichokonozi kuhusiana na watu mashuhuri nchini katika Nyanja za Siasa, michezo, na muziki.

Mbali ya umaarufu huo aliojizolea lakini pia Msigwa alikumbana na matatizo kadhaa ikiwemo kutishiwa na mara kadhaa kukoswakoswa kuuwawa na baadhi ya vigogo wa serikalini kwa tuhuma kadhaa alizowaandika, na wengine walidiriki kumfikisha mahakamani wakidai anawachafua lakini huko kwenye mikono ya Sheria aliwabwaga vibaya kutokana na ushahidi wa matukio ayaandikayo

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)