KIBWE NA SAFARI YA AJABU (8)
Zephiline F Ezekiel
---
Jina: KIBWE NA SAFARI YA AJABU
Mtunzi: Sango Kipozi
SEHEMU YA NANE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Yule bibi aliondoka akiwa amechukia mno. Alikuwa akijifutafuta mafuta usoni kwake na mwilini, wakati Hanga akiwa ameduwaa na kumwangalia kwa tafakuri ya hali ya juu.
“Huyu ni nani? na anafahamu vipi mambo yote yale aliyoyasema?” Alijiuliza na kutafakari kuhusu huyo Mwana Mteule aliyetajwa, na hatari iliyokuwa ikiikabili sayari yao.
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
ENDELEA...
Wakati huohuo, alijutia sana utovu wake wa nidhamu alioudhihirisha kwa bibi kizee ambaye hakumkosea chochote. Haraka sana akapata wazo la kumfuata, kwanza akiazimia kumuomba radhi kwa kosa lake alilolifanya, na pili akitaka kupata majibu ya majanga yanayoikabili sayari yake. Akashuka ngazi za kasri la baba yake mbilimbili kwa wakati mmoja, ili aweze kumuwahi yule kizee kabla hajatoweka. Alipomkaribia alikuwa akipumua kwa kasi mno kwa jinsi alivyopiga mbio kutoka gorofani hadi chini!
“Bibi…bibi…! Tafadhali nisamehe bibi yangu! Nimekosea sana kufanya vile nilivyofanya bibi…naahidi sintarudia kukufanyia vile nilivyokufanyia, na wala sintamfanyia mtu mwingine yeyote matendo ya utovu wa heshima ya namna yoyote!” Hanga alimuomba radhi yule bibi huku machozi yakimtiririka.
Yule bibi alipomwangalia kijana yule, alihisi kuwa ni kweli alijutia kosa lake. Lakini pamoja na kumsamehe alimwambia kuwa mara nyingi ni bora kuzingatia mafundisho ya wazazi, badala ya kusubiri mafundisho ya ulimwengu, kwani ulimwengu ni mwalimu mkali mno kuliko waalimu wote.
“Lazima kwanza uumie kabla mafunzo ya ulimwengu hayajazama akilini mwako. Zingatia hivyo mjukuu wangu!”
Hanga akapiga magoti na kujibu, “Sawa bibi, siku zote nitakumbuka usia wako huu na kuuzingatia”
Lakini kwa kuwa Hanga alipenda sana kufahamu kazi anayoifanya ‘Mwana Mteule’ huko Kaskazini Mashariki, na akatamani sana naye apate fursa ya kumsaidia mwenzake huyo katika kazi yake ngumu, alimuuliza bibi Ajuza jinsi ya kufika kule ‘Paa la Dunia’ Kaskazini Mashariki ya Sayari yao.
Ingawa yule bibi alifahamu kuwa kijana yule hakuwa na vipaji wala uwezo kama alionao 'Mwana Mteule’, lakini alihisi kuwa alikuwa na hamu na nia ya kusaidia katika jukumu lile la aina yake.
“Ingawa haitakuwa rahisi kufika sehemu ile nyeti, lakini utakapowasili Kaskazini Mashariki katika eneo la Paa la Dunia, utakuta limezingirwa na majabali marefu sana yenye rangi nyeusi”. Alimwambia kuwa vilevile eneo lile hujulikana kwa jina la ‘Bam i Dunya’.
“Utafuata njia nyembamba iliyozungukwa na msitu mnene kwa pande zote, na msitu huo ni maarufu kwa jina la ‘Msitu wa Kindumbwe’ au kwa maana nyingine ‘msitu wa hatari’ Tahadhari sana kwani msitu huo unakaliwa na viumbe wengi hatari pamoja na mashetani na vibwengo.” Yule Ajuza alimweleza Hanga, na maelezo yake yale yalijaza hofu kubwa moyoni mwa yule kijana.
“Sasa bibi, ni nini hasa ninachotakiwa kukitafuta huko?” Alidodosa Hanga.
“Utakapofika mwisho wa njia nyembamba kama uchochoro wenye giza nene, utatokea katika mlango wa kuingilia kwenye pango lenye sanamu kubwa la shaba la kichwa cha simba, chenye mkufu mnene wa fedha shingoni na wenye vidani vitatu vya sanamu za fedha za kucha za simba. Kimoja kati ya vidani hivyo chenye kito cha rangi ya samawati ndani yake, ndicho chenye ujumbe ulioandikwa kwenye upande uliopinda wa sanamu ya ukucha huo”
Hanga alimsikiliza kwa makini sana, na alipouliza ataelewa vipi ni kidani kipi chenye kito kinachohusika, alipewa maelekezo ya kutosha kabisa.
“Usihofu lolote katika safari hii. Wewe nenda tu na maelekezo zaidi utayapata kadiri utakavyokuwa safarini, kwani huko kuna msaada hata usioutarajiwa!”
Hanga alipowafahamisha wazazi wake kuwa alitaka kufanya safari kwenda Kaskazini Mashariki ya dunia kufuatilia jambo muhimu sana kuhusu usalama wa sayari yao na jamii katika sayari, Malkia, mama yake alipinga sana jambo hilo. “Hapana mwanangu, usithubutu hata kidogo kuchukua hatua hiyo ya hatari.’” alionya. huku akilia machozi. “Unafahamu fika kuwa wewe ni mwana pekee tuliyejaaliwa na Rahmani baada ya miaka mingi ya kusubiri. Sasa unataka kuondoka utokomee sijui wapi huko mwanangu? Ukipatwa na madhara huko ughaibuni tutakusaidia vipi sisi?” Lakini pamoja na mama yake kumsihi sana, Hanga alishikilia uamuzi wake, akisema; “Kama mimi ni mwana pekee kwenu ninyi wazazi wangu, hamuoni fahari kama nikichukua hatua ya kipekee kutekeleza jukumu kubwa la kuinusuru sayari yetu? Mbona nasikia kuwa tayari yuko mwenzangu mwenye umri kama mimi anayeshughulikia jambo hilo na ambaye naye ni mwana pekee wa wazazi wake? Tafadhali mama niruhusu nami nikasaidie jukumu hili muhimu!”
Baada ya kuwasihi wazazi wake wawili kwa muda mrefu hasa mama yake, hatimae baba yake Hanga Sultani Hazari, akamuomba sana mkewe amridhie kijana wao aweze kulifuatilia jukumu lile zito lenye umuhimu mkubwa na manufaa kwa wengi. “Atakapojitosa katika jambo hilo na kuchangia jitihada za kuinusuru sayari yetu, bila shaka yeye pamoja na sisi wazazi wake tutapata sifa lukuki kwa jamii ya mataifa mbalimbali!” Sultani yule alimsisitizia Malkia wake, basi,Malkia aliridhia uamuzi wa mwanae. Kwa muafaka ule, mama yake Hanga aliandaa chakula rasmi kwa ajili ya safari ya mwanawe, ambacho ni mikate saba ya unga wa mchele aliyomfungashia pamoja na guduria la maji ya kunywa njiani. Sultani naye akaandaa farasi mkubwa madhubuti ambaye angeweza kuhimili mwendo mrefu wa safari aliyoiazimia mwanawe!
“Mungu awe nawe katika safari yako na akufanyie wepesi kwenye shughuli yako nzito mwanangu!” Mke wa Sultani Hazari alimwombea dua njema Hanga wakati akiagana naye, akimkumbatia huku machozi yakimtoka bila kizuizi. “Punguza wahaka katika nafsi yako na kila mara kumbuka kujiamini. Usikate tamaa kwa jambo lolote litakalotokea.” Sultani Hazari naye alimwambia mwanawe, akamshika mkono wake madhubuti wakati ule wa kuagana!
HANGA KATIKA PAA LA DUNIA.
Kwa muda wa siku saba Hanga alisafiri usiku na mchana, akavuka misitu, nyika na majangwa makubwa kupita kiasi. Alipita milimani na mabondeni hadi baada ya miezi kadhaa ya tabu na mnashaka, njiani akila matunda waliyokula ndege, alipofikamahali penye majabali manne meusi marefu sana, yaliyozingira uwanda wa milima yenye urefu wa zaidi ya mita elfu moja! Bondeni alikosimama chini ya yale majabali, Hanga alistaajabu sana kuona jinsi vilele vya yale majabali vilivyoonekana kama kwamba viligusa mbingu! Alistaajabu pia kuona jinsi msitu ulivyofunga katika lile eneo alilokuwepo, hali iliyomsababishia hofu kubwa kwake kutokana na giza nene lililosababishwa na miti mirefu kupita kiasi! Miti ile ilitoa majani kama mizizi katika matawi yake na mizizi kwenye mashina yake. Alishangaa kuona baadhi ya majani yaliyokuwa na upana wa ajabu mithili ya masikio ya tembo!
“Sijapata kuona majani ya namna hii tangu nizaliwe! Yamefunika kama miavuli!” Aliwaza.
Kwa kuwa alikua na njaa sana, aliketi chini ya kivuli cha majani yale mapana akawa anakula mkate wake wa unga wa mchele alioubakiza, na kunywa maji aliyofungashiwa na mama yake. Baada ya kupumzika kwa muda wa kutosha, Hanga akamwacha farasi wake mahali alipomfunga, na yeye akaanza kutafiti lile eneo ajuwe ni upande gani aelekee katika safari yake.
Alipoangalia kwenye jabali katika upeo wa macho yake, yule kijana akaona maporomoko ya maji yaliyokua yakitokea mwambani na kuanguka chini kwa kishindo kikubwa, yakishindana na michuruziko ya maji yaliyokuwa yakitiririka chini kutoka kulekule mwambani. Alitulia kidogo akizidi kustaajabu aina ya msitu ule wa kipekee, na vyote vilivyohusika ndani yake!.Ghafla wakati akitafakari kuhusu yote aliyoyaona na jinsi atakavyoendelea na safari yake, akasikia mwaliko wa mawe yakigongana gongana, yaliyotoa mlio kama mtambo wa aina fulani na sekunde chache baadae, akasikia vishindo vya milipuko kama mabomu, na alipoinua kichwa chake kuangalia angani kuona kilichokua kikitokea, akaona moshi mnene na mweusi sana umezagaa! Muda si mrefu kijana yule akiwa na hofu kubwa, aliona cheche za moto zilizofuatiwa na mwanga mkali wa moto juu kabisa ya anga!
Haraka sana Hanga aliruka na kukimbilia sehemu alikohisi kuwa kuna usalama, mbali na eneo lile hatari, kwenye jabali moja lililonekana katika upeo wa macho yake! Alijaribu kukimbilia nyuma ya mmoja kati ya milima iliyo uzingira uwanda mrefu, akivuka vijito, mawe na visiki vya miti pamoja na miti mirefu mno iliyoufanya ule msitu uwe gizani. Miti katika ule msitu ilijipanga katika safu mbili, katikati ikiacha njia nyembamba ambayo juu yake ilikutana na kuonekana kama paa la nyumba. Pembezoni mwa ile miti kwa kiasi cha kama kilometa mia mbili, ndiko yalikokuwepo yale majabali marefu mno, yaliyouzingira ule uwanda wa ‘Paa la Dunia’ alioutaja kibibi Ajuza “Huu ndio ‘Msitu wa Kindumbwe’ au ‘Msitu wa Hatari’ nilioambiwa na Ajuza!” aliwaza Hanga, akishindwa kuzuia kitetemeshi kwenye miguu yake iliyokuwa inapoteza nguvu kwa woga na wasiwasi aliokuwa nao!
Alipokuwa akikimbia kwa hofu na wahaka, mguu wake mmoja ulikamatwa na mizizi ya miti, kwa hiyo akarushwa mbele zaidi, na huko akajikwaa vibaya sana katika kisiki. Puuuuuuh! Alipiga mweleka wa nguvu na kufikia kwenye mawe makali kama wembe yaliyomchubua chubua na kumpa machungu makali mno! Kabla hajatulia kujisikilizia machungu aliyoyapata, jambo jingine la kushitusha na kumtia hofu likatokea! Mahali alipoangukia Hanga akasikia sauti ya mtu! Mwili mzima ukazizima kwa woga! “Hivi ni mwana wa nani wewe unaenikwaa mimi kizee cha Mungu? Nimekufanya nini masikini?” Kwa mastaajabu na hofu ya kusikia sauti ya mwanadamu asiyeonekana, Hanga alijizowazowa na kuruka hatua moja ya kama mita mbili nzima, akisahau kabisa kuyasikilizia machungu aliyoyapata muda mfupi uliopita, akiangukia mwenye dimbwi la maji lililokuwa mbele yake! Alipogeuka kila upande kuangalia ni mtu gani aliyemsemesha maneno yale bila mafanikio, hofu yake alizidi, akabaki akitetemeka na miguu yake ikizidi kunyong’onyea! Wakati ule akakumbuka jinsi alivyomuudhi ‘Ajuza’ nyumbani kwao Hazina, hivyo akaamua kumuomba radhi mtu mwenye sauti ile iliyosikika kama ya mzee wa kike. “Nisamehe sana bibi yangu kwa kukukosea. Kwa bahati mbaya sikufahamu kama nilipojikwaa nilikukwaa na wewe! Nisamehe sana bibi!”
Baada ya kumtaka radhi yule bibi ambaey wakati ule hakujua ni wapi alikokuwa, alinyamaza kimya kusikiliza kama bibi yule angejibu kitu. Pale alipokuwa, Hanga alizidi kupata wahaka kwa ukimya uliotawala msitu ule, baada ya ile milipuko ya awali iliyotokea kwenye majabali saa moja hivi iliyopita. Ni milio ya sauti za ndege tu iliyosikika! Wengine walilia “whu-whu-whuuuu! Whu-whu- whuuuu!” na wengine walilia “Tuu-tuuu tutututuuu! tuu-tuuu-tutututuuuu!”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni