KITABU CHA SHETANI (6)

Zephiline F Ezekiel
Mtunzi: Aziz Hashim

SEHEMU YA SITA
TULIPOISHIA...
Tayari yule daktari aliyempiga kikumbo alishamsogelea na kutaka kumtoa kwa nguvu lakini alipoendelea kusisitiza kwamba alikuwa na dawa ya kumsaidia mgonjwa huyo aliyekuwa kwenye hatua za mwisho za uhai wake,

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

TUENDELEE...
madaktari walitazamana kwa sekunde chache kisha wakapeana ishara ya kumruhusu awasaidie kwani nao walishaonesha kushindwa.

Aliporuhusiwa tu, harakaharaka alisogea mpaka kwenye kitanda alichokuwa amelazwa Edmund ambaye bado alikuwa akiendelea kutapatapa, akamchomoa mpira wa kumsaidia kupumua aliokuwa amevalishwa puani na mdomoni kisha kwa kasi ya ajabu akaanza kumpuliza mdomoni.

Aliendelea kumpuliza kwa nguvu, baada ya takribani sekunde thelathini za kufanya hivyo, Edmund aliacha kutapatapa, akaendelea kumpuliza na katika hali ambayo hakuna aliyeitegemea, mapigo ya moyo wake yalianza kupanda.

Yalipofika katika kiwango ambacho Samantha aliona kinafaa, aliacha kumpuliza na kumvalisha tena ile mashine ya kupumulia, akamgeuza kidogo ili apate nafasi ya kuiona vyema shingo yake.

Muda mfupi baadaye, aliliona jeraha alilomsababishia kijana huyo shingoni muda aliojifanya anamtoa ‘love bite’. Harakahaharaka akapeleka mdomo wake eneo hilo na kuanza kulinyonya jeraha la Edmund kwa nguvu, madaktari wakawa wanashangaa wakiwa hawaamini walichokuwa wanakiona. Urembo wa Samantha na alichokuwa anakifanya, vilikuwa vitu viwili tofauti.

Mara Samantha akasimama huku mdomo wake ukionesha kujaa, akachukua kikarai kidogo kilichokuwa pembeni na kutema kile kilichokuwa mdomoni mwake, madaktari wakashtuka mno. Ilikuwa ni damu ambayo ilibadilika rangi na kuwa nyeusi kutokana na sumu iliyokuwa imeingia ndani ya mwili wa Edmund.

Akarudi tena kwenye shingo ya Edmund na kuendelea kumnyonya kisha akaenda tena kutema kwenye kile kikarai, aliendelea kufanya hivyo mfululizo, nguo alizokuwa amevaa zikachafuka vibaya kwa damu lakini mwenyewe hakujali.

Kadiri alivyokuwa anaivuta sumu hiyo kwa mdomo, ndivyo Edmund alivyokuwa anazidi kubadilika, ile mishipa ambayo ilikuwa imevimba kama inataka kupasuka, ikaanza kurudi kwenye hali yake ya kawaida, ngozi yake ambayo ilikuwa nyeusi kama mkaa, nayo ilianza kubadilika rangi na kurudi kwenye hali yake ya kawaida, madaktari wakawa bado wanashangaa, kila mmoja akijihisi yupo kwenye ndoto.

Samantha aliendelea kufanya hivyo mpaka kile kikarai kikakaribia kujaa, tayari nje kulishaanza kupambazuka, lile giza la alfajiri likawa linafifia taratibu na kumezwa na mwanga wa jua lililoanza kuchomoza kwa mbali.

“Endeleeni na kazi yenu lakini msimwambie yeyote juu ya hiki nilichokifanya, nitakuja baadaye kumuona,” alisema Samantha huku akiwaelekeza madaktari hao kukisafisha vizuri kidonda kilichokuwa kwenye shingo ya Edmund.

Samantha aliendelea kufanya hivyo mpaka kile kikarai kikakaribia kujaa, tayari nje kulishaanza kupambazuka, lile giza la alfajiri likawa linafifia taratibu na kumezwa na mwanga wa jua lililoanza kuchomoza kwa mbali.

SASA ENDELEA...

“Endeleeni na kazi yenu lakini msimwambie yeyote juu ya hiki nilichokifanya, nitakuja baadaye kumuona,” alisema Samantha huku akiwaelekeza madaktari hao kukisafisha vizuri kidonda kilichokuwa kwenye shingo ya Edmund.

Akachukua kile kikarai kilichokuwa na damu iliyochanganyikana na sumu mpaka nje, akainamisha uso wake ili mtu yeyote asimuone sura yake na kuondoka harakaharaka eneo hilo mpaka kwenye gari lake ambapo alichukua chupa iliyokuwa na maji, akayamwaga na kumimina ile damu yote.

Kama alivyoingia hospitalini hapo, alitoka kwa kasi kubwa akiwa ndani ya gari lake la kifahari, dakika chache baadaye, tayari alishatoka nje ya uzio wa hospitali hiyo, akawa anakanyaga mafuta kwa nguvu huku akishusha pumzi ndefundefu.

“Ni lazima nikulinde Edmund, sijali kitakachonipata kutoka kwa baba yangu, nahisi kukupenda sana kutoka ndani ya moyo wangu,” aliwaza Samantha huku akiendelea kukanyaga mafuta.

Muda mfupi baadaye, tayari alikuwa amewasili kwenye jumba lao la kifahari, hakutaka kupiga honi ili mlinzi afungue geti kama kawaida yake kwani alihisi baba yake atasikia, akapaki gari pembeni ya geti na kushuka, akabonyeza kengele ya mlango mdogo wa geti. Sekunde chache baadaye, tayari mlinzi alishafungua mlango.

“Mungu wangu! Umefanya nini mbona umelowa damu kiasi hicho?” mlinzi alihoji huku akionesha kupatwa na mshtuko mkubwa mno. Hakujua atamjibu nini bosi wake kwa kumruhusu Samantha atoke halafu arejee akiwa kwenye hali kama hiyo.

“Sijaumia popote wala usiwe na wasiwasi, baba aliniulizia?”

“Kweli hujaumia? Na hizo damu zimetoka wapi?” mlinzi alisema huku akimgeuza Samantha kwa hofu.

“Niamini mimi, hapa nikienda kubadilisha nguo hakuna atakayejua chochote. Nakuuliza baba hajaniulizia?”

“Ulipotoka alisikia muungurumo wa gari, akaamka na kuja kuniuliza kwa nini nimekufungulia geti wakati bado hakujapambazuka, nikamwambia umepatwa na dharura. Amekasirika sana, bado kidogo aninase vibao,” alisema mlinzi huyo, kauli iliyomfanya Samantha aanze kutetemeka.

Alikuwa akimfahamu vyema baba yake alivyo mkali, akajua lazima moto utawaka. Hata hivyo, kwa sababu alishajiapiza kumlinda Edmund, alipiga moyo konde na kuingia ndani, akatembea harakaharaka mpaka kwenye mlango wa kuingilia ndani, akaingiza namba maalum kisha mlango huo ukafunguka.

Akavua viatu vyake na kuvishika, akawa ananyata kuelekea chumbani kwake huku hofu ikiwa imeutawala moyo wake.

“Umetoka wapi?” sauti kali ya baba yake ilimshtua mno Samantha, akajikuta viatu vikimponyoka mikononi na kuanguka chini. Hakutegemea kama baba yake anaweza kuwa sebuleni muda kama huo, akabaki anatetemeka.

“Nazungumza na wewe, umetoka wapi? Halafu mbona uko hivyo?”

“Ni..me..toka ku..fanya ka..zi uliyonituma,” alisema Samantha huku akitetemeka, tayari baba yake alishamsogelea, akawa anamtazama machoni kwa umakini.

“Kazi gani muda huu.”

“Ya kafara ya da...mu ba..ba,” Samantha alisema uongo ambao baba yake aliushtukia mapema.

“Tangu lini kafara ikafanyika alfajiri? Halafu mbona unaonesha kuwa na wasiwasi kiasi hicho? Unanidanganya si ndiyo?”

“Hapana baba, ni kweli,” alisema Samantha, mzee huyo akaendelea kumbana na kumwambia asijaribu kumdanganya kwa sababu anaujua ukweli wa kila kitu alichokifanya, kauli iliyomshtua sana Samantha.

“Jana kuna kijana tulikuandalia mazingira ya kukutana naye, kila kitu kikaenda vizuri mpaka usiku ulipotimiza kazi yako lakini ghafla ukabadilisha mawazo kwa sababu ya mapenzi. Umenisikitisha sana mwanangu! Unafikiri sijui kwamba umetoka Hospitali ya Mwananyamala kumsaidia huyo kenge mwenzio?

“Ni mwezi wa pili sasa unaisha hujafanya kazi hata mara moja. Jana tumetumia nguvu kubwa kukutengenezea mazingira lakini matokeo yake umetanguliza udhaifu mbele. Hujui kwamba mapenzi ni udhaifu? Unataka huu utajiri wetu uishe? Kwa nini unavunja masharti? Unaijua hatari ambayo iko mbele yetu kwa ujinga unaoufanya?”

“Lakini baba...”

“Lakini nini? Sasa kwa taarifa yako, mimi siwezi kukubali ujinga unaoufanya unigharimu, kama umeshindwa kufanya kazi itabidi wewe ndiyo utolewe kafara, hujui ni kwa namna gani nimekupigania mpaka hapo ulipofika? Nitakuua.

“Nakupa saa 24 ya kwenda kumuua huyo mshenzi anayekufanya uvunje masharti vinginevyo damu yako ni halali yangu,” alisema mzee huyo kwa ukali kisha akageuka na kutembea kwa kasi kuelekea chumbani kwake, akamuacha Samantha amepigwa na butwaa akiwa ni kama haamini alichokisikia kutoka kwa baba yake.

Kwa jinsi alivyokuwa anamfahamu, alijua endapo hatafanya jambo haraka, anaweza kwenda kummalizia Edmund mwenyewe kule hospitalini kwani nguvu za giza alizokuwa nazo zilikuwa zinaweza kumfanya akajua kila kitu kinachoendelea na kuamua nini cha kufanya.

“Na akigundua kwamba nimeshamtoa sumu mwilini, anaweza kweli kuniua na mimi kama alivyofanya kwa kaka Samuel,” aliwaza Samantha akiwa bado amesimama palepale koridoni, kijasho chembamba kikimtoka.

Japokuwa alikuwa anapenda maisha ya kifahari waliyokuwa wanaishi kama wapo peponi, Samantha alikuwa hakubaliani kabisa na mchezo wa baba yake wa kuwatoa kafara watu wasio na hatia, wakati mwingine hata ndugu zake wa damu wakiwemo watoto wake wa kuwazaa ili kulinda utajiri wake mkubwa.

Mara kwa mara alijaribu kujitoa kwenye mtego huo lakini alikuwa akishindwa kwani baba yake alikuwa akijua kila kitu anachokifanya au anachokaribia kukifanya na kumkwamisha.

“Lazima nikuokoe Edmund, hata kama itanigharimu maisha yangu, nimechoshwa na maisha haya,” alijisemea Samantha na kutembea harakaharaka kuelekea chumbani kwake. Hakutaka kupoteza muda, harakaharaka alivua zile nguo na kukimbilia bafuni, akaoga kisha akarudi na kuvaa baibui na nikabu iliyouficha kabisa uso wake na kuyaachia macho tu.

Akatoka na zile nguo zilizokuwa zimelowa damu na kwenda kuzitupa kwenye pipa la takataka nje. Harakaharaka akatoka mpaka nje na kumuacha mlinzi akitingisha kichwa chake kwa masikitiko. Sekunde chache baadaye, muungurumo wa gari ulisikika nje ya geti na Samantha akaondoka kwa kasi akiwa ndani ya gari lake.

Tayari kulishapambazuka, barabarani kukawa na watu na magari mengi, hali iliyomzuia Samantha kuendesha kwa kasi kama ilivyokuwa awali.

Baada ya kuhangaika sana, alifika Hospitali ya Mwananyamala akiwa amevaa vilevile, akapita mpaka mapokezi ambapo ilibidi avue nikabu, yule nesi aliyemkuta akamkumbuka kwani muda mfupi uliopita walikuwa pamoja.

“Nina shida nyingine dadaangu, nataka mgonjwa wangu ahamishwe hospitali, kwa jinsi hali yake ilivyo anahitaji huduma bora zaidi kwa hiyo nataka kumpeleka hospitali ya kulipia,” Samantha alidanganya.

“Inabidi ukazungumze na madaktari wanaomtibu,” alisema yule nesi na kumsaidia kupita hadi wodini ambako aliwakuta madaktari wakiwa wameshamsafisha Edmund kidonda na kumfunga vizuri.

Akazungumza nao kuhusu mpango wake ambapo walimkubalia, akaandikiwa barua ya rufaa na kusaidiwa kumtoa mgonjwa wodini, akiwa bado hajitambui. Samantha alikuwa akishinikiza kila kitu kifanyike harakaharaka kwani alijua muda wowote baba yake anaweza kufika hospitalini hapo na kuvuruga kila kitu.

“Ambulance imepeleka wagonjwa wengine Muhimbili, inabidi usubiri.”

“Hapana, sihitaji ambulance, nimekuja na gari langu,” alisema Samantha huku akivaa tena ile nikabu yake na kuuficha uso wake, manesi na madaktari wakasaidiana kumpakiza mgonjwa kwenye gari kisha baada ya hapo daktari mkuu akataka manesi wawili waongozane naye lakini Samantha alikataa,

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)

Chapisha Maoni