KITABU CHA SHETANI (5)

0
Mtunzi: Aziz Hashim

SEHEMU YA TANO
TULIPOISHIA...
Kwa bahati nzuri, alfajiri hiyo hakukuwa na foleni, dakika kadhaa baadaye wakawa tayari wameshawasili kwenye Hospitali ya Mwananyamala, akapokelewa na wahudumu waliokuwa zamu na kumlaza juu ya kitanda chenye magurudumu,

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

TUENDELEE...
harakaharaka akakimbizwa wodini.

“Amepatwa na nini?” aliuliza daktari kwa mshangao baada ya kuona hali isiyokuwa ya kawaida kwenye mwili wa Edmund.

“Hata hatuelewi, tumeshtukia akianguka na kupoteza fahamu.”

“Mungu wangu! Hebu nipisheni kwanza, tokeni nje,” alisema daktari huku akiinua simu ya mezani iliyokuwa ndani ya wodi hiyo na kupiga namba fulani, wale wapangaji wenzake Edmund na baba mwenye nyumba wakatoka huku nao wakiendelea kuulizana maswali yaliyokosa majibu. Mshtuko aliouonesha daktari ulizidi kuwachanganya, wakawa wanasubiri miujiza tu kwani kwa hali aliyokuwa nayo Edmund, chochote kingeweza kutokea.

Muda mfupi baadaye, madaktari wengine wawili waliingia harakaharaka kwenye wodi aliyokuwa ameingizwa Edmund, wakasogea na kukizunguka kitanda alichokuwa amelazwa huku wakimtazama daktari mwenzao aliyewaita.

“Kuna huyu mgonjwa ameletwa lakini hali yake inashangaza sana, inaonesha kama ameng’atwa na nyoka au mdudu mwenye sumu kali lakini ukiangalia jeraha jinsi lilivyo, halifanani na jeraha la kung’atwa na nyoka.”

“Mh! Mbona anabadilika rangi na kuwa mweusi kama mkaa?”

“Halafu mbona mishipa yake ya damu mwili mzima imevimba kiasi hiki?”

“Tangu nianze kazi sijawahi kukutana na hali kama hii, mpaka naogopa,” alisema daktari yule, kila mmoja akawa amepigwa na butwaa, hakuna aliyekuwa anajua waanzie wapi kumtibu.

“Mapigo yake ya moyo yapo chini sana na kadiri muda unavyozidi kwenda mbele ndivyo yanavyozidi kushuka,” alisema daktari aliyekuwa anampima Edmund kifuani kwa kutumia kifaa maalum cha kupimia mapigo ya moyo kiitwacho Stethoscope.

“Atundikiwe dripu za maji kwanza wakati tukiendelea kuchunguza ni sumu ya aina gani iliyopo kwenye damu yake,” alisema mwingine, wazo lililoungwa mkono na wenzake.

Edmund ambaye bado hakuwa na fahamu akatundikiwa dripu lakini kilichozidi kuwashangaza madaktari hao, dripu ilikuwa ikitiririka kwa kasi kubwa kuingia kwenye mishipa yake, hali iliyoashiria alikuwa na upungufu mkubwa mno wa maji.

Dakika chache tu baadaye, tayari dripu ya kwanza ilikuwa imeisha, ikabidi atundikiwe nyingine ambayo nayo licha ya madaktari hao kujaribu kuiseti kitaalamu, iliendelea kutiririka kwa kasi kubwa mno, kila mmoja akazidi kupigwa na butwaa huku hofu ikianza kuingia ndani ya moyo wa kila mmoja kwani kulikuwa na dalili zote kwamba ugonjwa aliokuwa nao Edmund, haukuwa wa kawaida.

***

Samantha aliendelea kulia kwa kwikwi chumbani kwake, akiwa amejifungia mlango kwa ndani huku akijilaumu sana kwa kitendo alichomfanyia Edmund. Alikuwa anajua fika nini kitakachomtokea baada ya saa chache kupita, hata hivyo hakuwa na cha kufanya. Alitamani muda urudi nyuma ili arekebishe makosa aliyoyafanya lakini hilo halikuwezekana.

“Hustahili Edmund, wewe ni mwanaume wa kipekee, hustahili kabisa mateso ya kiasi hicho,” alisema msichana huyo huku akiendelea kulia. Alipotazama saa ya ukutani, tayari ilikuwa imefika saa kumi za usiku lakini hakuwa amepata hata lepe la usingizi, macho yake yakiwa yamevimba na kuwa mekundu sana kutokana na kulia kwa muda mrefu.

Ghafla, akiwani kama aliyekumbuka kitu muhimu, Samantha alikurupuka pale kitandani kwake. Kwa kuwa hakuwa amebadilisha nguo alizokuwa amevaa siku iliyopita, alichukua viatu vyake na kuvishika mkononi kwani hakutaka mtu yeyote amsikie.

Akafungua mlango na kunyata kwenye korido ndefu mpaka sebuleni, akafungua kwenye droo zilipokuwa zinawekwa funguo za magari, akachukua funguo ya gari analopenda kutembelea, Jeep Grand Cherokee (New Model) na kunyata kuelekea kwenye mlango wa kutokea.

Alipofika mlangoni, aliingiza namba maalum za kufungulia mlango kisha akafungua na funguo, akatoka nje na kuangaza huku na kule.

“Vipi dada mbona mapema namna hii?” mlinzi aliyekuwa na bunduki, akiwa amevalia sare maalum, alimuuliza kwa mshangao kwani haikuwa kawaida ya Samantha kutoka nyumbani muda huo.

“Shhh! Njoo nikwambie,” alisema Samantha na kumvutia mlinzi huyo karibu yake, akamdanganya kwamba amepatwa na dharura na ni lazima aondoke alfajiri hiyo lakini hataki baba yake au mama yake ajue chochote.

Mlinzi akawa anatingisha kichwa kuashiria kumuelewa, akaingiza mkono kwenye pochi yake na kumtolea noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi, harakaharaka mlinzi akaenda kufungua geti, Samantha akaingia ndani ya gari lake na kuliwasha kisha akatoka kwa kasi kubwa, akaingia barabarani na kutokomea gizani, akamuacha mlinzi akihangaika kufunga geti.

“Sijui kama nitamuwahi kabla hali haijawa mbaya,” alisema Samantha huku akitazama saa yake ya mkononi, gari likikimbia kwa kasi kubwa ajabu. Bahati nzuri asubuhi hiyo hakukuwa na magari mengi barabarani kwani kwa mwendo aliokuwa akiendesha, ingekuwa rahisi mno kusababisha ajali.

Hakuwa akijali chochote barabarani, hata sehemu zenye matuta au kona kali alikuwa akipita bila kupunguza mwendo, dakika chache baadaye, tayari aliwasili nyumbani kwa Edmund. Akapaki gari palepale alipopaki usiku uliopita na kutembea harakaharaka kuelekea kwenye chumba cha Edmund.

Mazingira aliyoyakuta yalizidi kumchanganya kwani alikuta mlango ukiwa wazi huku matapishi ya damu yakiwa yametapakaa kila sehemu. Kwa bahati nzuri, alimkuta mama mwenye nyumba akiwa nje, akiwaandaa wanaye kwa ajili ya kwenda shule. Alipomuuliza, mwanamke huyo alimueleza kwamba Edmund amekimbizwa Mwananyamala baada ya kuzidiwa ghafla.

Bila hata kuaga, alikimbilia kwenye gari lake na kuondoka kwa kasi kubwa mithili ya madereva wa mbio za magari. Dakika kumi baadaye, tayari alikuwa amewasili Hospitali ya Mwananyamala, akateremka kwenye gari na kuanza kutembea harakaharaka kama aliyechanganyikiwa mpaka mapokezi.

“Samahani nesi naomba kuuliza,” alisema Samantha huku akihema mithili ya mwanariadha aliyetoka kukimbia mbio za mita mia moja. Japokuwa ilikuwa ni alfajiri na kulikuwa na kiubaridi cha asubuhi, Samantha alikuwa akitokwa jasho, jambo lililomshangaza yule nesi aliyekuwa pale mapokezi.

“Kuna mgonjwa anaitwa Edmund, eti ameletwa hapa alfajiri hii?”

“Mh! Kuna mgonjwa mmoja tu aliyeletwa alfajiri hii, ngoja niangalie jina lake,” alisema nesi huyo huku akipekua kwenye daftari kubwa la usajili wa wagonjwa wanaoingia hospitalini hapo.

“Ndiyo! Amepelekwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi, hali yake ni mbaya sana na madaktari wote wameelekea huko kumsaidia,” alisema nesi huyo, majibu yaliyozidi kumpandisha Samantha presha.

“Samahani sana nesi, niko chini ya miguu yako, naomba uniruhusu nikamuone.”

“Dada! Mgonjwa ndiyo kwanza ameletwa na amepelekwa wodi ya wagonjwa mahututi, unataka ukamuone ili iweje? Hakuna anayeweza kukuruhusu, waache madaktari wafanye kazi yao,” alisema nesi huyo huku akifunika daftari hilo na kuendelea na shughuli nyingine.

Samantha akaona asipotumia nguvu za ziada, kweli Edmund anaweza kupoteza maisha muda wowote kwani mapambazuko yalikuwa yamekaribia sana na endapo asingefanya jambo mpaka jua litakapochomoza, tafsiri yake ni kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa Edmund, jambo ambalo hakutaka kuona likitokea.

Harakaharaka akaingiza mkono kwenye sidiria yake na kutoa noti tatu za shilingi elfu kumikumi, akampa yule nesi na kumtaka amuoneshe wodi ya wagonjwa mahututi ilipo.

“Lakini madaktari hawatakuruhusu.”

“We nioneshe nikifika nitajua mwenyewe,” alisema Samantha huku akiendelea kuhema kwa nguvu. Nesi akazisunda zile fedha kwenye mfuko wa gauni lake jeupe na kuinuka, akamuelekeza Samantha sehemu ilipo wodi hiyo.

Harakaharaka akawa anatembea kuelekea wodini, hakuwajali watu kadhaa aliowapita kwenye korido ya kuelekea kwenye wodi hiyo, akapita kwa kasi na kuelekea mpaka kwenye mlango, akaanza kugonga kwa nguvu.

***

Dakika chache baadaye, dripu ya pili aliyokuwa ametundikiwa Edmund pale kitandani nayo iliisha, ikabidi atundikiwe dripu ya tatu huku hali yake ikazidi kuwa tete. Bado madaktari hao hawakuwa wanajua wafanye nini.

Wakati dripu ikiendelea kutiririka kwa kasi kuingia kwenye mishipa yake, majibu ya damu tayari yalishatoka, madaktari wote wakawa wanayajadili kwani licha ya kuonesha kwamba damu ya Edmund ilikuwa na sumu kali, vipimo vilishindwa kuonesha ni sumu ya aina gani, jambo lililosababisha wasijue dawa sahihi ya kuitumia.

“Why can’t we use trial and error method?” (Kwa nini tusitumie njia ya kujaribu na kujifunza kupitia makosa?) alisema daktari mmoja, wazo lililokubaliwa na wenzake wote.

Harakaharaka daktari aliyekuwa anahusika na kitengo hicho akatoa orodha ya dawa zinazotumika kutibu watu walioumwa na nyoka na kwa pamoja wakakubaliana kuanza kutumia dawa ya Polyvalent Anti–Snake Venom Serum ambayo ilikuwa na uwezo wa kupambana na sumu kali zaidi.

Hata hivyo, wakati dawa hiyo ikiendelea kuandaliwa, Edmund alianza kuonesha dalili zilizozidi kuwachanganya madaktari wote mle wodini.

Alianza kutapatapa, akirusha mikono na miguu kama anayekaribia kukata roho huku akitokwa na povu lililochanganyikana na damu puani na mdomoni, jambo lililoashiria kwamba tayari sumu iliyokuwa ndani ya mwili wake ilishafika kwenye moyo.

Kifaa maalum cha kumsaidia kupumua alichokuwa amevalishwa puani na kuunganishwa na kompyuta, kilianza kupiga kelele kwa nguvu kuashiria kwamba mapigo ya moyo ya Edmund yalikuwa yakishuka kwa kasi na hakuwa tena na uwezo wa kupumua.

Wakati madaktari wakiwa wanahangaika kumsaidia, walishtuka baada ya kusikia mlango wa wodi ya wagonjwa mahututi waliyokuwa ndani yake, ukigongwa kwa nguvu, jambo ambalo halikuwa la kawaida. Walimpuuza aliyekuwa anagonga, wakaendelea na kazi ya kumhangaikia Edmund ambaye dalili zote zilionesha kwamba yupo kwenye hatua za mwisho kabisa za uhai wake.

Walipoona mtu huyo anazidi kugonga, ilibidi mmoja wao aache kazi na kwenda kufungua.

“Unasemaje binti?” aliuliza daktari aliyefungua mlango lakini cha ajabu, Samantha alimpiga kikumbo na kusababisha mlango wote ufunguke, kufumba na kufumbua tayari Samantha alikuwa ndani ya wodi hiyo.

“Ninayo dawa ya kumsaidia kupona! Naomba mniamini! Ninayo dawa,” alisema Samantha huku akihema kwa nguvu, mikono yake akiwa ameiinua juu kama ishara ya kuonesha kwamba hakuwa na lengo baya.

Tayari yule daktari aliyempiga kikumbo alishamsogelea na kutaka kumtoa kwa nguvu lakini alipoendelea kusisitiza kwamba alikuwa na dawa ya kumsaidia mgonjwa huyo aliyekuwa kwenye hatua za mwisho za uhai wake,

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)