KITABU CHA SHETANI (8)

Zephiline F Ezekiel
Mtunzi: Aziz Hashim

SEHEMU YA NANE
TULIPOISHIA...
“Nimeshawaua wanaume wengi sana Edmund, hata wewe ilikuwa ufe kwa njia hizohizo, nimekuokoa kwa sababu kwa mara ya kwanza maishani mwangu nimetokea kukupenda Edmund,

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

TUENDELEE...
nimechoka kuwa muuaji! Nimechoka naomba unisaidie kuondokana na hali hii,” alisema Samantha huku akianza upya kuangua kilio kwa uchungu.

Maelezo hayo yalimshtua mno Edmund, bado akawa anajihisi yupo ndotoni kwani ilikuwa vigumu sana kuamini kwamba Samantha alikuwa akiongea ukweli.

“Kwa hiyo... kwa hiy..o nini huwa kina...to..kea,” Edmund alimuuliza kwa sauti ya kukatakata huku akitetemeka mno kutokana na hofu kubwa iliyokuwa imemuingia, hasa baada ya kuambiwa kwamba hata yeye alitakiwa kufa ila akaponea kwenye tundu la sindano.

Samantha akamwambia kwamba anapotongozwa na wanaume, wakishakubaliana kwenda kukutana kimwili, kuna dawa huwa anaitafuna muda mfupi kabla ya tendo na kusababisha mwili wake wote uwe na sumu kali.

“Mwanaume akijaribu kuingia na mimi chumbani tu, hatafanikiwa kufanya mapenzi na mimi na huo ndiyo utakuwa mwisho wake kwani lazima nitamng’ata au kumchubua sehemu, kinachotakiwa ni damu yake kutoka hata kidogo tu!

“Ikitokea hivyo sumu yangu humuingia na kusababisha apoteze maisha ndani ya muda mfupi sana na baada ya hapo kazi yote hubakia kwa baba,” alisema Samantha huku akijifuta machozi na kamasi vilivyokuwa vinamtoka mfululizo.

“Kwa hiyo na mimi hicho ndicho kilichonitokea?”

“Ndiyo Edmund, naomba unisamehe mpenzi wangu, halikuwa kusudio langu ndiyo maana nimeamua kukusaidia, nimekuwahi mpenzi wangu,” alisema Samantha kwa hisia za hali ya juu, Edmund akashusha pumzi ndefu na kukosa cha kusema, ukimya ukatawala kati yao.

Ghafla, walishtushwa na kelele za mlango uliobamizwa kwa nguvu, mganga Shiwinga akaingia mbiombio na kumueleza Samantha kuwa ameliona gari linalofanana na la baba yake likija eneo hilo kutokea mbali.

“Mungu wangu, babu naomba nisaidie kutoroka na Edmund wangu,” alisema Samantha huku akianza kuhangaika, Mzee Shiwinga akamtuliza na kumwambia kuwa isingekuwa rahisi kumtoroka baba yake katika mazingira hayo kwani hakukuwa na njia nyingine ambayo angeweza kupita zaidi ya ile ambayo baba yake alikuwa akija nayo.

“Labda ninachoweza kukusaidia ni kwenda kumficha Edmund porini lakini jua kwamba ni hatari sana endapo akishtukia mchezo, bila shaka baba yako unamjua vizuri,” alisema mganga Shiwinga huku akimuinua Edmund pale alipokuwa amelala, harakaharaka akatoka naye na kuzunguka nyuma ya kibanda chake, vishindo vikasikika wakati akikimbia naye kutokomea porini.

Huku nyuma, Samantha alifuta ushahidi wote wa uwepo wa Edmund eneo hilo, akawa anapanga uongo wa kumwambia baba yake. Dakika chache baadaye, muungurumo wa gari lililoonesha lipo kwenye kasi kubwa ulisikika nje ya kibanda cha mganga Shiwinga kisha sekunde chache baadaye mlango ukawa unagongwa kwa nguvu.

Huku akitetemeka kuliko kawaida, Samantha aliinuka na kufungua mlango, akakutana uso kwa uso na baba yake aliyekuwa amefura kwa hasira kama nyoka cobra!

“Ulijua sitakupata si ndiyo?”

“Hapana baba, nimekuja kwa babu Shiwinga kuja kutibiwa, naona mambo yangu hayaendi sawa na mimi sipendi kukuudhi,” alisema Samantha huku akitetemeka kuliko kawaida.

Haikuwa rahisi kwa baba yake kuuamini uongo wa kitoto alioutoa kwani kwa macho yake alimshuhudia kuanzia anatoka hospitalini na jinsi alivyomkimbia alipojaribu kumfuatilia.

“Unanifanya na mimi ni mtoto mwenzako si ndiyo?”

“Kweli baba, kama huamini kamuulize hata babu Shiwinga.”

“Yuko wapi?”

“Ameenda kunitafutia dawa,” alisema Samantha lakini baba yake hakutaka kuamini, akamwambia dereva wake aliyekuja naye kusimama mlangoni na kuhakikisha hakuna mtu anayetoka ndani ya nyumba hiyo ya mganga. Akazunguka nyuma ya nyumba ya mganga na kuanza kuangaza huku na kule kama atamuona mganga huyo.

Muda mfupi baadaye, aliona vichaka vikitingishika mita kadhaa kutoka pale alipokuwa amesimama, akajua lazima kuna mtu. Alipoendelea kutulia huku macho yake akiwa ameyakaza, alimuona mganga Shiwinga kichakani

Mganga Shiwinga akiwa na rundo la majani ya porini na mizizi kadhaa, alitokeza kichakani huku akipiga ‘mbinja’ kwa nguvu, akajifanya hajamuona baba yake Samantha wala hana taarifa zozote za uwepo wake. Ni mpaka alipomkaribia ndiyo akajifanya kushtuka kumuona!

“Ni wewe baba?”

“Ni mimi mzee, shikamoo.”

“Marahabaa! Naona umeamua kuja mwenyewe, umefanya jambo zuri sana, nipo na Samantha,” alisema mzee huyo huku akimpita baba yake Samantha na kumpa ishara kwamba amfuate. Kwa jinsi alivyokuwa anamheshimu na kumuogopa mganga Shiwinga, zile hasira zote alizokuwa nazo baba yake Samantha ziliyeyuka kama siagi kikaangoni.

“Samahani kabla hatujaingia ndani, naomba nikuulize jambo.”

“Uliza tu baba.”

“Mwanangu Samantha amekuja na nani huku kwako?”

“Amekuja mwenyewe kama anavyofanya siku zote akiwa na tatizo lolote. Ameniambia kwamba anahisi nguvu zake zimepungua kwa sababu hawezi tena kufanya ile kazi tuliyompa kama ilivyokuwa zamani!

“Hivi hizi dawa unazoziona ni kwa ajili yake, nataka kumuongeza nguvu,” alidanganya mganga Shiwinga, baba yake Samatha akashusha pumzi ndefu kwani uongo alioambiwa na binti yake ulikuwa ukifanana na uongo wa mganga huyo.

Kwa kuwa hakuwahi kumdanganya hata siku moja, baba yake Samantha aliamini kwamba alichoambiwa na mganga ni ukweli mtupu, akashusha tena pumzi ndefu kisha wakaendelea kutembea kuelekea ndani ya kibanda chake.

“Naomba uzungumze na mjukuu wako, ukiachilia mbali kupungua kwa nguvu zake, siku hizi amekuwa mzembe sana. Hafanyi kazi na badala yake anaendekeza ujingaujinga tu. Hata ujio wangu hapa haukuwa wa heri kwa sababu kuna jambo amelifanya na yeye mwenyewe analijua.

“Ni kwa sababu ya heshima yako mzee ndiyo maana nimeamua kumsamehe, ila akirudia tena tusilaumiane,” alisema baba yake Samantha akiwa amekaa kwenye kiti cha miguu mitatu ndani ya kibanda hicho cha mganga, akiwa amefura kwa hasira.

“Samantha, kwani umemfanya nini baba yako?” alihoji mganga huku akijifanya hajui chochote kilichotokea, Samantha ambaye muda wote alikuwa amekaa kimya, hofu kubwa ikiwa imeutawala moyo wake, alishusha pumzi ndefu na badala ya kueleza alichoulizwa, alianza kulia na kumuomba baba yake amsamehe.

“Mueleze babu yako ulichokifanya, kulia hakukusaidii chochote,” alisisitiza baba yake Samantha lakini binti yake hakuwa tayari kueleza chochote, ikabidi yeye ndiyo aanze kumueleza mganga kilichotokea.

Kwa kuwa tayari walishakula njama, mzee Shiwinga naye alijifanya kushtuka kusikia kwamba Samantha alikuwa amemtorosha mtu aliyekuwa ameandaliwa kwa kafara.

“Ni makosa makubwa uliyoyafanya, baba yako ana kila sababu ya kukasirika, umekosea sana,” alisema mganga Shiwinga, akaacha hata kuchambua dawa na kuendelea kumsema Samantha. Kwa jinsi walivyokuwa wamepangilia vyema njama zao, haikuwa rahisi kwa mzee huyo kushtukia chochote.

Samantha akawa amejiinamia muda wote huku akiyalazimisha machozi ya uongo. Ilibidi baba yake asubiri mpaka binti yake huyo amalize kushughulikiwa na mganga Shiwinga. Alipomaliza tu, alimtaka waongozane naye kurudi jijini Dar es Salaam, nyumbani kwao.

Kwa jinsi alivyokuwa amembana, Samantha alishindwa jinsi ya kumtoroka, akaondoka kwa shingo upande huku akijiapiza kuwa ni lazima atarudi kuja kumfuata Edmund hata iweje.

Hatimaye msafara wa magari mawili uliianza safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam, Samantha akiwa amepanda kwenye gari alilokuwa anaendesha baba yake na dereva wao akiwa anaendesha gari la Samantha.

Mganga Shiwinga aliwasindikiza kwa macho mpaka walipopotea kabisa kwenye upeo wa macho yake, harakaharaka akaacha kila alichokuwa anakifanya na kukimbilia nyuma ya nyumba yake, akapotelea vichakani.

Edmund aliendelea kukaa kwenye pango alimofichwa na mganga Shiwinga, hofu kubwa ikiwa imetanda ndani ya moyo wake. Maelezo aliyopewa na Samantha kuhusu kilichomtokea usiku uliopita, yalimfanya ajihisi maisha yake yapo kwenye hatari kubwa mno.

Akiwa bado amezama kwenye dimbwi la mawazo ndani ya pango hilo lililokuwa na giza totoro, alisikia vishindo vya mtu akija mbiombio, hofu ikazidi kumuongezeka akihisi huenda baba yake Samantha ameshtukia mchezo na sasa alikuwa anataka kuja kummalizia mwenyewe.

Japokuwa alikuwa ameacha kwenda kanisani kwa kipindi kirefu, alijikuta akihitaji ulinzi wa Mungu wake kuliko kitu kingine chochote, mapigo ya moyo yakawa yanazidi kumuenda mbio huku akisubiri muujiza utokee.

Mara aliona jiwe kubwa lililokuwa kwenye sehemu ya kuingilia ndani ya pango hilo likisogezwa pembeni, akakazia macho sehemu hiyo akitaka kujua ni nani aliyekuwa anafungua. Alipogundua kwamba ni mganga Shiwinga, alishusha pumzi ndefu na kuinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake.

“Una bahati sana, yule bwana amekasirika mno, yaani kama angekukuta pale kwangu angekutafuna mzimamzima,” alisema mganga huyo huku akimsaidia Edmund kuinuka pale alipokuwa amekaa, akaupitisha mkono wake mmoja nyuma ya mabega ya Edmund na kuanza kumsaidia kutembea kwani bado mwili wake haukuwa na nguvu za kutosha.

Akamtoa nje ya pango hilo na kufunga sehemu ya kuingilia kwa jiwe kubwa, wakawa wanarudi nyumbani kwake huku bado Edmund akiwa haamini kama amesalimika.

“Nakushukuru sana babu.”

“Usinishukuru mimi, mshukuru Samantha, sijui umempa nini kwani kwa jinsi alivyo katili sijui kwa nini ameamua kukuokoa wewe,” alisema mganga huku akiendelea kumuandalia Edmund dawa nyingine kwa ajili ya kuitoa kabisa sumu iliyokuwa imeingia mwilini mwake.

Bado Edmund alibaki na maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu Samantha, akawa anajaribu kumdodosa mganga Shiwinga kama alikuwa anamjua vizuri msichana huyo.

“Namjua tangu akiwa kachanga, mimi ndiye niliyeshirikiana na wazazi wake kumfanya awe kama unavyomuona leo.”

“Mbona amesema kwamba kila mwanaume anayejaribu kufanya naye mapenzi ni lazima afe. Ni kweli?”

“Ni kweli, pale alipo hamjui kabisa mwanaume, yeye alizaliwa kwa sababu ya kazi moja tu, kumletea baba yake utajiri.”

“Sasa mbona ananiambia ananipenda ndiyo maana ameniokoa?”

“Hajawahi kupenda hata siku moja ndiyo maana nakuuliza kwamba sijui umempa nini.”

“Sasa itakuwaje na umeshasema kila mwanaume anayejaribu kufanya naye mapenzi ni lazima afe?” Edmund aliuliza huku akionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka majibu. Licha ya yote yaliyotokea, alishindwa kuuficha ukweli uliokuwa ndani ya moyo wake kwamba anampenda sana msichana huyo.

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)

Chapisha Maoni