
Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA PILI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Ndugu jamaa na marafiki walipoteza maisha baada ya kuuwawa na mama huyu ambae sura yake na matendo yake ilikuwa ni vitu viwili tofauti. Alikuwa mwanakamati mkuu wa sherehe kuzimu kwahiyo kila mara alikuwa akishiriki katika mauwaji mbalimbali halafu damu na nyama za marehemu zinasherehekewa kuzimu.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Kwa hakika mama huyu alikuwa ni hatari sana. Jamii nzima iliwatenga, kwasababu walikua wanafahamu fika mama yule sio mtu wa kawaida. Wakati mwingine watu walihisi kuwa alikuwa ameshamuingiza binti yake katika masuala ya kichawi ndio maana hata wanaume wengi walikuwa wanamkwepa Vivian.
Mtazamo huo ulijengeka katika akili za watu wengi kutokana na hofu waliyokuwa nayo dhidi ya mama yule lakini haikuwa kweli kwamba Vivian pia alikuwa mchawi. Vivian alikuwa anasikia lawama kwa majirani na kwa bahadhi ya ndugu kuwa mama yake ni mchawi lakini hakuwahi kumwona akifanya jambo lolote ambalo lilimthibitishia kweli mama yake ni mchawi. Hakufahamu pia kuwa mama yake ndie aliekuwa sababu ya vifo vya ndugu zake pamoja na baba yake. Shutuma za kwamba mama yake alikuwa ni mchawi zilikuwa zikimuumiza sana lakini hakuwa na la kufanya.
Mtaani hakuwa na rafiki hata mmoja. Marafiki zake wengi walikuwa shuleni kwasababu walikuwa hawafahamu kuwa anatokea katika mazingira gani. Kitendo cha kuwa na marafiki wengi shuleni kilisababisha apende sana shule. Alikuwa na mahudhurio mazuri sana shule kwasababu alipenda jinsi alivyokuwa anabadilishana mawazo na marafiki zake. Muda mwingine alijilazimisha kwenda shule hata pale alipokuwa mgonjwa sana, jambo ambalo lilikuwa likiwashangaza marafiki zake kwanini huwa hapendi kupumzika nyumbani wakati anapokuwa mgonjwa. Hayo yote yalisababishwa na upweke ambao alikuwa anaukwepa pindi anapokuwa nyumbani kwao.
Kama ilivyokuwa kwa wasichana wengine kumpenda sana Nelson ndivyo ilivyomtekea pia Vivian. Kiukweli hisia zake zilitekwa haswa na mwonekano wa Nelson. Alisubiri kwa hamu Nelson amtamkie kuwa anampenda ili na yeye aweze kuzionyesha hisia zake kwake lakini hilo lilishindwa kufanyika kwa muda muwafaka. Wakati mwingine alitamani laiti angekuwa mwanaume angeshamtamkia Nelson kuwa anampenda. Ingawa baadhi ya walimu pamoja na wanafunzi wenzake walimtongoza lakini hakushawishika kabisa kwasababu hisia zake zilikuwa kwa mtu mwingine.
Muda mwingi aliupoteza akimuwaza Nelson. Alimwomba Mungu siku moja aweze kumkutanisha kwa mara nyingine na mwanaume yule ambae alihisi kuwa hawezi kuishi bila yeye. Alifanikiwa kumaliza kidato cha nne salama lakini kwa bahati mbaya hakubahatika kuendelea na kidato cha tano jambo ambalo lilizidi kumkatisha tamaa ya kuonana na Nelson. Aliumia sana, kibaya zaidi ni kwamba Nelson hakubahatika kufahamu nyumbani kwao. Japokuwa kunakipindi alimsindikiza karibia na nyumbani kwao lakini alimzuia kufika moja kwa moja mtaani kwao akihofia asisikie maneno ya vitisho kutoka kwa watu waliokuwa wanamfahamu. Maisha ya Vivian yalijawa na upweke wa hali ya juu.
Hakuwa na rafiki hata mmoja wa kuweza kubadilishana nae mawazo pale mtaani kwao. Hakuna hata mwanaume mmoja aliejitokeza na kumtamkia neno ‘nakupenda’ pamoja na uzuri wote aliokuwa amejaliwa na Mwenyezi Mungu. Ulikuwa ni wakati mgumu sana kwake kwasababu alichoshwa na maisha ya kunyanyapaliwa. Marafiki aliohitimu nao kidato cha nne walipotezana kabisa kwasababu hawakuwa na mawasiliano ya aina yeyote. Nyumba yao ilikuwa ni kama kisiwa kilichozungukwa na maji kwasababu tangu Vivian alipokuwa mdogo hakuna hata siku mmoja alisikia mtu akibisha hodi nyumbani kwao isipokuwa ilitokea kwa mara chache sana kwa baadhi ya watu waliokuwa wakipotea njia. Alijitahidi kumsahau Nelson lakini alishindwa kabisa. Taharifa za ufaulu wa Nelson alizipata kwa kupitia vyombo vya habari. Alifurahi sana ingawa alisikitika baada ya kusikia kuwa amepata ufadhili wa kwenda kusoma Marekani. Alizidi kumuwaza na kumkumbuka kila mara japokuwa alihisi kukutana naye kwa mara nyingine ni kama ndoto.
************
Nelson baada ya kufika marekani alianza masomo yake ambayo yalikuwa yanahusiana na uhandisi wa majengo. Licha ya kwamba alikuwa mbali na mazingira ya nyumbani lakini hakuona tofauti yeyote kwasababu alibahatika kupata marafiki kadha wa kadha ambao walimfanya ajihisi kama vile yupo Tanzania. Uwezo wake darasani uliendelea kuwa gumzo hata alipokuwa chuo kikuu. Wahadhiri mbalimbali chuoni walimpenda kutokana na juhudi zake katika masomo. Alitokea kuupenda mchezo wa kikapu, ambapo alijifunza na hatimae alifanikiwa kuwa mchezaji mzuri jambo ambalo lilifanya jina lake lizidi kukuwa zaidi na zaidi katika chuo alichokuwa anasoma.
Kwajinsi alivyokuwa anafahamu jinsi ya kuchangamana na watu wengine ilisababisha watu wamuone kama mmarekani mweusi lakini kumbe sivyo. Alipomaliza mwaka wa kwanza wa masomo, mawazo juu ya Vivian yalipungua kidogo. Ingawa bado alizidi kumuomba Mungu aweze kumkutanisha na mwanamke yule kwa mara nyingine tena wakati atakaporudi Tanzania. Mjomba wake alizidi kumtia moyo katika masomo yake pindi walipokuwa wakiwasiliana. Kitendo hicho kilimfanya apate moyo wa kuongeza mapambano ya kusoma kwa bidii ili aweze kumridhisha mjomba wake, pamoja na mama yake kipenzi.
Mwaka wa nne ambao ndio ulikuwa mwaka wa mwisho wa masomo yake ulitimia, ambapo alifanya mitihani yake salama na matokeo yalipotoka alifanikiwa kupata ufaulu wa juu kabisa, yaani daraja la kwanza (GPA of 4.9) Ufaulu huo wa kishindo aliupata yeye na mwanafunzi mwenzie wa nchini India. Taharifa za ufaulu wa Nelson unafika kwa balozi wa Tanzania nchini humu bwana Johnson Rogart Marwa na kuamua kumfanyia tafrija fupi nchini humo kwaajili ya kumpongeza kwasababu aliweza kuvunja rekodi ambayo haikuwai kuvunjwa na mwanafunzi yeyote kutoka Tanzania katika kipindi cha uongozi wake. Taifa la Marekani linamshawishi Nelson abaki marekani ili waweze kufanya nae kazi lakini anakataa.
Baada ya hapo Nelson anarejea nyumbani akiwa na furaha sana. Aliona kukubali kufanya kazi nje ya nchi ndio sababu ya yeye kupotezana moja kwa moja na Vivian. Nelsona hakutaka kuamini kuwa hatamuona tena mwanamke ambae alihisi kuwa ndiye mwanamke wa ndoto zake. Anaweka nadhiri ya kuhakikisha anamsaka kila kona hadi ampate. Saa 2. 45 usiku Nelson alitua katika uwanja wa ndege wa mwalimu Julius nyerere kwa ndege aina ya Boeing 767-300ER-Condor. Kwasababu alikuwa na shauku ya kutaka kukutana na mama yake alichukua tax ambayo ilimpeleka moja kwa moja hadi keko machungwa alipokuwa anaishi mama yake.
“Ngo! Ngo! Ngo!” saa 3.17 usiku mlango wa mama Nelson ulisikika ukigongwa. Mara baada ya kugonga kwa mara kadhaa sauti ya mama yake ilisikika ndani.
“Nani?” mama aliuliza aliekuwa akigonga ni nani kwasababu hakuwa na taharifa za ujio wa mwanae.
“Mwanao, Nelson.” Nelson alijibu.
Baada ya mama kufungua mlango sura yake ilikutana ana kwa ana na mwanae jambo ambalo lilisababisha hisia za furaha kumpanda kwa kasi hadi machozi yakawa yanamdondoka mfululizo.
“Kwashaa’mbe!” (Pole kwa safari mwanangu.) mama alizungumza kilugha huku akiwa amemkumbatia mwanae kwa furaha kubwa sana.
“Ekaa’ma.” (Asante mama.) Nelson nae alimjibu mama yake kwa kilugha huku akidondokwa na machozi kwa furaha kwasababu ilikuwa imepita kitambo kirefu bila hawajaonana.
Mama alisaidiana na mwanae kuingiza mabegi ndani. Nelson alimpigia simu mjomba wake na kumweleza kwamba tayari amefika salama Tanzania kwahiyo siku inayofuata ndio atakwenda Arusha. Nelson alisikitika sana kuona mama yake bado anaishi maisha ya shida. Chumba alichokuwa anaishi kilikuwa hakina umeme wala feni. Chemba za choo zilikuwa zinatoa harufu kali sana ambayo ilikuwa ni kero hadi ndani ya nyumba. Jirani na nyumbani kulikuwa na baa iliyokuwa ikipiga mziki kwa sauti ya juu sana kiasi kwamba ilibidi awe anazungumza na sauti kubwa ili aweze kuelewana na mama yake.
Wingi wa vitu vilivyokuwa vimejazana ndani ya chumba kimoja alichokuwa anaishi mama yake ilisababisha msongamano mkubwa ambavyo ulidhihirisha kwamba suala la usafi lilikuwa ni sifuri. Chumba kilikuwa kimegawanywa kwa pazia. Maisha aliyokuwa anaishi mama yake hayakuwa na tofauti yeyote na maisha ya miaka kumi iliyopita wakati walipokuwa wakiishi pamoja. Nelson aliwaza kwamba suala la kwanza endapo atapata pesa ni kuhakikisha kwamba mama yake anapata mahali pazuri pa kuishi. Pamoja na hayo yote alifurahi sana kumuona mama yake akiwa ni mzima wa afya tele. Walipiga stori nyingi sana na mama yake. Alijisikia faraja sana kuzungumza na mama yake ambae alikuwa anampenda kuliko kitu chochote hapa duniani. Alijaribu kumuuliza mama yake habari za baba yake lakini alijuta kuuliza kwasababu aliyoelezwa yalimchoma mtima wake.
“Nilipata habari kwamba, kwa sasa anaishi Tabata kimanga, ameoa mwanamke mmoja wa kindengereko pia wana watoto watatu na maisha yao yanakwenda vizuri bila shida.” Mama alizungumza kwa masikitiko makubwa sana, nusura machozi yanidondoke.
“Hivi mama kwanini baba alitutelekeza?” Nelson alijikuta anamuuliza mama yake swali hilo ambalo lilikuwa limemkereketa kwa muda mrefu sana.
“Kiukweli hata mimi mwenyewe sielewi. Kwasababu aliniacha katika mazingira magumu mno kwani ndiyo nikiwa mzazi kwako. Kuondoka kwake kulikuwa kama utani utani tu kwasababu alikuwa ni mlevi kupindukia. Wakati mwingine alikuwa haonekani nyumbani kwa wiki nzima, kwahiyo hata alipoondoka nilijua yupo kwa wanawake zake lakini kwa kadiri siku zilivyozidi kwenda ndipo niligundua kuwa nilikuwa nimetekezwa.” Mama alizungumza hadi akaanza kulia kwa uchungu sana. Nelson alimbembeleza mama yake kwa muda kidogo na hatimae hasira ya mama ilishuka. Saa ya mkononi ilionyesha ni saa 6.39 usiku. Mama alikwenda kulala katika kitanda chake. Nelson alijiegesha katika kochi lililokuwepo mle ndani hadi palipokucha asubuhi ambapo alimuaga mama yake na kuondoka kuelekea Arusha kwa mjomba wake kumsalimia ikiwa ni pamoja na kumsaka Vivian.
Saa 12.06 asubuhi, Nelson alifika ofisi ya ‘Kilimanjaro express’ iliyopo shekilango jijini Dar es salaam. Alikata tiketi na kuondoka na basi la saa 12.30 kuelekea mkoa wa Arusha. Alipendelea kusafiri kwa basi kwasababu alikuwa amemisi mazingira ya Tanzania kwa muda mrefu. Kichwa kilimuuma kwasababu aliwaza kwa muda mrefu namna ya kwenda kuanza msako wa kumtafuta Vivian. Akili mwake alitambua kuwa itakuwa ni zoezi gumu lakini, alijidhatiti kuhakikisha kwamba anafanikiwa. Jioni ya saa 11.55 aliteremka kwenye basi katika kituo cha Mianzini ambapo alimkuta mjomba wake anamsubiri kumlaki.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi