SHEREHE KUZIMU (1)

Zephiline F Ezekiel
0
Mtunzi: Frank Silaa

SEHEMU YA KWANZA
Shule ya sekondari ya wavulana Ilboru inapatikana jijini Arusha. Shule hii ina historia ya kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani mbalimbali ya kitaifa kwa miaka mingi. Historia hiyo imejengeka kutokana na kwamba, wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na shule hii ni wale wanaoaminika kuwa na vipaji maalumu. Kwa maana hiyo ili uweze kujiunga na shule hii ni lazima uwe na ufaulu mzuri sana. Kwa hakika shule hii inamchango mkubwa kitaifa, kwani imefanikiwa kuzalisha wataalamu wa mambo mbalimbali na pia wanasiasa mashuhuri. Nelson alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo mwenye heshima kubwa kutokana na uwezo wake darasani. Nelson ameishi katika maisha ya shida sana. baba yake alimtelekeza mama yake tangu alipokuwa na miezi mitatu.

Mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi katika shule ya Mgulani iliyopo Keko jiji Dar es salaam, alipata ufaulu wa juu sana wa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Azania. Ugumu wa maisha unasababisha mama yake ashindwe kumwendeleza kimasomo. Na ndipo mjomba yake anayehishi Mianzini jiji Arusha analazimika kumchukua na kumuhamishia katika shule ya sekondari Ilboru. Uwezo mzuri darasani unasababisha kijana huyu anapewa jina la utani na wanafunzi wenzake kwa kumuita ‘profesa’. Ufaulu mzuri wa mitihani ya ndani na nje ya shule inasababisha kijana huyu kupata marafiki wengi. Ingawa wanafunzi wengi wa kike wa shule za jirani wanajipendekeza kwake ili waweze kumnasa lakini jitihada zao zinagonga mwamba. Nelson alisoma kwa bidii sana ili siku moja aweze kurudisha furaha ya mama yake iliyokuwa imepotea kwa kitambo kirefu. Alimpenda sana mama yake kwasababu alimlea katika mazingira magumu mno.

Mapenzi ya dhati yaliyokuwa yamejengeka moyoni mwake dhidi ya mama yake ndio yaliyokuwa yakimsukuma kusoma kwa bidii. Nelson alifanikiwa kufika kidato cha nne akiwa bado hajawai kujiingiza katika mahusiano yeyote ya kimapenzi, ingawa mabinti wengi walionekana kuvutiwa sana na yeye. Ilikuwa ni jioni ya saa 11.11 siku moja Nelson akiwa ametokea mitaa ya Kaloleni kufanya majadiliano ya kimasomo na wanafunzi wa shule mbalimbali, alikutana na binti mmoja ambae alikuwa amevaa sare za shule. Binti huyo alikuwa anakuja katika uelekeo ambao Nelson alikuwepo. Nelson alishangaa baada ya kuhisi mapigo yake ya moyo yanaongezeka kwa kadiri alivyokuwa anazidi kumtizama binti yule ambae alikuwa amevaa sare ya wanafunzi wa shule ya Ekenywa iliyopo jirani na shule aliyokuwa anasoma.

Uzuri aliojaliwa mwanamke aliyekuwa anamuona akija mbele yake hakuwai kuuona kwa mwanamke wa aina yeyote tangu kuzaliwa kwake. Rangi ya ngozi yake ilikuwa mithili ya chokoleti, hakuwa mnene wala mwembamba halikadhalika hakuwa mrefu wala mfupi. Ingawa alikuwa ndani ya sare za shule lakini uzuri wake bado ulidhihirika. Hakika alikuwa ni mzuri kama malaika. Kwa jinsi hatua zake zilivyokuwa zinazidi kumkaribia Nelson ndivyo ambavyo uzuri wake ulizidi kuteka hisia na kijana. Macho ya binti yalikuwa ni meupe ya kuvutia ingawa yalijawa na soni sana. Mwendo wake ulikuwa ni wa madoido mithili ya twiga. Nelson aliona liwalo na liwe lakini sio kuacha kuzungumza na msicha yule ambae alikuwa na uzuri ambao ulimfanya ahisi kuchanganyikiwa.

KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA NAYO...
“Mambo vipi.” Nelson alijitosa kumsalimia binti yule ingawa hakutegemea kuitikiwa salamu yake na msichana yule ambae kwa hakika alikuwa na sifa za malaika.

“Poa! Mambo.” Huku wakipishana, binti aliitikia salamu bila maringo, jambo ambalo lilimuongezea Nelson kujiamini zaidi.

“Safi tu, samahani.” Nelson alizungumza huku mapigo yake ya moyo yakizidi kumwenda mbio sana kwasababu hakuamini kwamba ni yeye ndie aliekuwa akizungumza na yule msichana.

“Bila samahani.” Sauti nyororo na yakuvutia ilitoka kinywani mwa binti na kuzidi kumpagawisha Nelson.

“Naitwa Nelson. Sijui wewe mwenzangu unaitwa nani.”

“Nafurahi kukufahamu Nelson. Mimi naitwa Vivian.”

“Unasoma kidato cha ngapi?” Nelson aliuliza.

“Ooh! Nasoma kidato cha pili.

“Hongera sana. Ingawa nimekutangulia madarasa mawili mbele.”

Nelson alizidi kutengeneza mazingira ya urafiki kwa Vivian kwasababu alitokea kuvutiwa sana na mwonekano wake. Muda ulikuwa umesonga sana kwahiyo walizungumza kwa muda mfupi, kwasababu binti alikuwa anaishi mbali. Akili ya Nelson haikuwa ya darasani pekee kwani akili hiyohiyo ndio iliyomwezesha kufanikiwa kuingia katika urafiki na binti mrembo Vivian. Wote hawakuwa na simu za mkononi kwasababu walikuwa ni wanafunzi kwahiyo iliwawia vigumu kuwasiliana mara kwa mara. Kutokana na changamoto ya mawasiliano wakati mwingine Nelson alidiriki kumsubiri njiani ili aweze kumuona. Kiukweli hisia za Nelson zilikuwa ni mateka kwa Vivia.

Nelson aliteseka sana kwasababu hakuwahi kupenda kabla kwahiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza. Alitamani muda wote Vivian awepo mbele ya macho yake lakini haikuwezekana. Muda wa kufanya mitihani ya kidato cha nne ulifika. Nelson alifanya mitihani yake salama na kuendelea kuishi kwa mjomba wake ambae alikuwa akimpenda sana. Alifunga safari ya siku chache ya kwenda Dar es salaam kumsalimia mama yake na hatimae alirudi jijini arusha kuendelea kusubiri matokeo. Uwepo wake kwa mjomba wake ulimfanya apate urahisi wa kuendelea kukutana na Vivian mara kwa mara. Matokeo ya kujiunga na kidato cha tano yalitoka. Nelson alifanikiwa kupata ufaulu wa daraja la kwanza (division one) ambapo alipangiwa katika shule ya ‘Tabora boys.’

Hakufurahi kabisa kupangiwa shule hiyo kwasababu ilimfanya awe mbali na mwanamke aliekuwa anampenda. Pamoja na kwamba moyo wake ulitokea kumuhusudu sana binti yule lakini bado hakuwa amemweleza juu ya hisia zake kwasababu aliona muda muwafaka bado haukuwa umefika. Wakati mwingine alijilaumu ni kwanini hakumweleza mapema ili akae akijua lakini aliishia kujifariji kwa msemo usemao ‘kama ipo ipo tu’ akimaanisha kwamba kama Mungu amepanga siku moja Vivian awe mke wake basi atakuwa tu kwa namna yeyote. Nelson alipofika Tabora waliendelea kuwasiliana kwa njia ya barua walizokuwa wakitumiana kwa njia ya posta lakini kwa kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga ndivyo ambavyo mawasiliano yalianza kupungua na mwishowe yalikwisha kabisa.

Ubize wa mambo ya shule ndio uliopelekea mawasiliano yao yakatoweka. Nelson aliendea na shule ingawa mawazo juu mwanamke alieziteka hisia zake vilivyo, zilikataa kabisa kufutika katika kichwa chache. Hakuwa na namna isipokuwa kusoma kwa bidii sana ili kuweza kutimiza malengo aliyokuwa amejiwekea. Uwezo wake darasani ulizidi kutukuka hata alipokuwa Tabora. Wanafunzi wenzake walimpenda sana kwasababu licha ya kufanya vema darasani lakini alikuwa na vituko vya kuchekesha sana. Kama ambavyo alipewa jina la utani alipokuwa Ilboru ndivyo ambavyo pia alipewa jina jingine la utani alipofika Tabora ambalo ni ‘Socret’ jina ambalo ni la mwanafalsafa maharufu sana duniani. Miaka miwili ya kidato cha tano na sita ilikwisha. Nelson na wanafunzi wote wa kidato cha sita nchi nzima walianza mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari.

Baada ya kumaliza kidato cha sita alirudi jijini Arusha kwa mjomba wake lakini hakufanikiwa kukutana tena na Vivian. Hisia kali juu ya msichana yule zilimsababishia mateso makubwa ya nafsi, kwasababu kila sekunde, kila dakika alikuwa akimuwaza na hata wakati mwingine alikuwa akimuota ndotoni. Matokeo ya kidato cha sita yalipotoka jina la Nelson lilitikisa magazeti mbalimbali nchini. Alipata ufaulu wa juu sana kwani alifanikiwa kuwa mwanafunzi wa kwanza kitaifa. Kwa watu waliokuwa wanamfahamu wala hawakushangaa kwasababu walikuwa wanafahamu uwezo wake ulikuwa ni wa juu sana.

Alizua gumzo nchi nzima kwasababu imezoeleka kuwa wanafunzi wanaoshika nafasi za juu kitaifa ni wale wanaosoma katika shule za watu binafsi kutokana na ufundishaji wao kuzidi shule za serikali. Vyombo mbalimbali vya habari vilimuhoji ili kuweza kufahamu sababu iliyomfanya kuibuka kidedea katika mitihani yake. Hakuna cha ziada alichokizungumza isipokuwa alisema kuwa ufaulu wake ulisababishwa na juhudi kubwa katika masomo yake pamoja na kumtanguliza Mungu kwa kila kitu alichokuwa akikifanya. Furaha aliyoipata mama yake baada ya kusikia kuwa mwanae kawa wa kwanza kitaifa ilikuwa ni sawa kabisa na furaha aliyoipata mjomba yake ambae ndie aliekuwa akimsomesha.

Nelson alipata ufadhili wa kwenda kusoma nje ya nchi katika chuo kikuu kinachojulikana kwa jina la ‘University of Central Florida’ kilichopo nchini Marekani. Alifurahi sana kupata nafasi ile kwasababu hakuwahi kuwaza kama ipo siku atasoma nje ya nchi tena katika chuo kikuu maarufu sana duniani. Matumaini ya kumpata Vivian yalipotea kabisa akilini mwake. Alijua sio rahisi mwanamke yule alieumbika kama malaika aweze kuishi peke yake bila kuingia katika mahusiano ya kimapenzi. Ingawa roho ilimuuma sana lakini hakuwa na la kufanya kwasababu elimu nayo ilikuwa ni ya muhimu sana, kwahiyo hakuwa na sababu ya kutengua maamuzi yake ya kusoma nje ya nchi. Aliamini hakuna mwanamke mwingine mzuri huku duniani kama alivyokuwa Vivian. Alitamani awe na kipaji cha kuimba ili aweze kumtungia wimbo kwa imani ipo siku utamfikia lakini ilishindikana.

****************

Vivian ni kitinda mimba katika familia ya watoto 11. Kwa bahati mbaya wenzake wote walishafariki dunia nyakati tofauti tofauti katika mazingira ya kutatanisha. Katika familia yao alibaki yeye na mama yake kwani baba yake pia alisha fariki. Mama yake alikuwa anampenda sana binti yake. Alikuwa ni kama mboni ya jicho kwake. Kama simba alivyo mkali kwa kitu chochote kinachocheza na mwanae ndivyo na mama Vivian alivyokuwa mkali kumlinda bintie. Mama huyu ni mchawi mkubwa. Anaogopwa na kila mtu katika mtaa anaoishi. Pamoja na kwamba ana binti mzuri sana lakini hakuna hata kijana mmoja mtaani aliejitosa kumtaka kimapenzi Vivian. Kwani kufanya hivyo ni sawa na kujichimbia kaburi lako mwenyewe. Mama huyu ndie alieua watoto wake kumi pamoja na mume wake. Ndugu jamaa na marafiki walipoteza maisha baada ya kuuwawa na mama huyu ambae sura yake na matendo yake ilikuwa ni vitu viwili tofauti. Alikuwa mwanakamati mkuu wa sherehe kuzimu kwahiyo kila mara alikuwa akishiriki katika mauwaji mbalimbali halafu damu na nyama za marehemu zinasherehekewa kuzimu.

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)