SHEREHE KUZIMU (21)
Zephiline F Ezekiel
---

Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Japokuwa pamoja na misukosuko mikubwa iliyokuwa inaikumba kuzimu, lakini bado waliendelea na vikao vyao kwa shida ili waweze kumuangusha mchungaji na kanisa lake. Maisha ya Nelson yaliendelea kama kawaida ingawa yalitawaliwa na upweke sana.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Alizoea kupokea ushauri kutoka kwa mama yake. Wakati mwingine alipokuwa akikata tamaa kutokana na changamoto za dunia hii, mama yake alimtia moyo. Hata wakati alipokuwa akifiwa na watoto wake bado alihisi faraja ndani ya moyo wake kutokana na uwepo wa mama yake. Sambamba na hayo yote lakini pia alideka pindi alipokuwa anaiona sura ya mama yake ikitabasamu mbele ya macho yake. Kifo cha ghafla cha mama yake kilipelekea Nelson ahisi kama vile ametelekezwa peke yake jangwani. Muda mwingi alikuwa ni mtu wa kulia pindi anapokuwa anawaza mapenzi ya mama yake.
Hakuona pakuipatia faraja kama ambayo alikuwa anaipata kutoka kwa mamae, hakuona wa kumdekea kama mamae, hauona wa kumuonyesha mapenzi kama aliyokuwa anayapata kutoka kwa mama yake. Ama kweli Nelson alikuwa katika wakati mgumu sana ambao hausimuliki. Mawazo yalimnyonya na kumfanya aonekane kama vile mgonjwa. Chakula kilishindwa kupenyeza katika koromeo lake, muda mwingi alikuwa anajiona ameshiba wakati haikuwa kweli. Hakuwa na hamu ya chakula wala maji. Machungu ya vifo vya watoto alijumlisha na machungu ya kifo cha mama yake na kuonekana kama vile chizi. Aliona kama vile dunia imemuonea, kwasababu alikuwa ni mtu wa misiba kila iitwapo leo. Kilichomuumiza zaidi ni kwamba vifo vya watu wake walikuwa wanakufa katika mazingira yakutatanisha sana.
Mjomba alijitahidi sana kumfariji Nelson ili aweze kukabiliana na hali, kwani alibaini kuwa Nelson anateseka katika msongo mkubwa wa mawazo. Mara kwa mara alizungumza nae kwa namna ya kumpa ushauri kwasababu Nelson alionekana kuathirika kisaikolojia. Kwa kiasi fulani mjomba alifanikiwa kumuweka Nelson sawa, japokuwa haikufikia katika kiwango cha kawaida.
***********
Baba yake Nelson ambae alikuwa ameoa mke mwingine dare s salaam alipata taharifa ya kifo cha mke wake wa kwanza lakini hakuhudhuria mazishi. Aliendelea kujivinjari na mke mdogo pamoja na familia yake. Kitendo kile kiliendelea kumuumiza Nelson, kwa kujiuliza ni kipi hasa ambacho mama yake alimkosea baba yake hadi adiriki kususia mazishi yake. Nelson alimuona baba yake kama vile muuwaji, mnyama asie na hata chembe ya utu ndani yake. Alikumbuka pia vifo vya watoto wake hakuwahi kumwona baba yake wala kupata salamu za pole kutoka kwake. Ingawa Nelson alijitahidi kutafuta ukaribu na baba yake katika nyakati tofauti tofauti lakini baba yake alionekana kutokuwa na habari nae. Kadi ya harusi yake aliipeleka kwa mikono yake hadi alipokuwa akiishi baba yake na kumkabidhi lakini cha kusikitisha ni kwamba baba huyo hakufika harusini.
Nelson baada ya kuliona hilo hakushtuka sana aliwaza pengine labda baba yake kwa siku hiyo alikuwa ametingwa katika shughuli zake za utafutaji wa riziki. Matukio ya vifo ndiyo yaliyomdhihirishia Nelson kwamba baba yake hayupo katika upande wake. Muda mwigi Nelson huwaza na kuishia kudondokwa na machozi kwasababu alimisi sana upendo wa baba yake, ila hakuwa na namna isipokuwa kumuachia Mungu. Alisoma kwa bidii sana ili siku moja aweze kuja kuwa mfano mzuri wa baba bora kwa wanae lakini ndio hao walikuwa wanapuputika kwa vifo vya ajabu. Moyo ulimuuma zaidi alipokumbuka wakati mwingine alikuwa akikesha usiku kucha akisoma kwa bidii ili siku moja aweze kuirudisha furaha ya mama yake iliyokuwa imepotea kwa miaka mingi, lakini pia mama hakuwepo tena.
Maisha ya Nelson yalizidi kutawaliwa na misukosuko mingi. Mwaka mmoja baada ya kifo cha mama yake, mjomba yake alipata ajali mbaya ya gari wakati alipokuwa na mke wake na wote walipoteza maisha. Moyo wa Nelson ulizidi kutawaliwa na simanzi isiyokuwa na mfano. Furaha ilitoweka kabisa katika mtima wake, kutokana na magumu mengi aliyokuwa anapitia maishani mwake. Msongo wa mawazo ulisababisha azidi kupoteza ufanisi kazini halikadhalika katika biashara zake siku hadi siku. Muda mwingi alikuwa ni mtu wa kuwaza. Hakujua hatima ya maisha yake itakuwaje wakati watu wake wa karibu ndio walikuwa wanapoteza maisha kila mara. Mwili wake ulidhoofu sana na kupelekea kuonekana kama vile muathirika wa virusi vya ukimwi. Mawazo yalimfanya ashindwe kula chakula na kupelekea kupata ugonjwa wa vidonda vya tumbo. Hakuwa na mtu wa kumfariji akafarijika katika matatizo aliyokuwa anakumbana nayo katika maisha yake. Marafiki walijitahidi sana kumfariji lakini haikuwezekana.
Kifo cha mjomba pamoja na mke wake kilisababisha Frank na Christopha wabaki yatima. Hawakuwa na mtu wa kuweza kuwasaidia ili waweze kutimiza ndoto zao. Hivyo basi Nelson alilazimika kwenda kuwachukua na kuwaamishia nyumbani kwake kusudi aweze kuwalea mpaka watakapoweza kujitegemea kwasababu bado walikuwa ni watoto wadogo. Kiukweli Nelson alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kuwapa malezi bora watoto wa mjomba wake. Aliona ndio muda muwafaka wa kulipa fadhila kwa mjomba wake kwasababu mafanikio makubwa ya kielimu aliyokuwa nayo yalisababishwa na marehemu mjomba wake. Kichwani mwake aliweka malengo ya kuhakikisha kwamba watoto hao wanafanikiwa kufika elimu ya juu bila kukumbana na changamoto yeyote ambayo itaweza kuwakwamisha kufikia malengo hayo.
Ajali iliyosababisha kifo cha mjomba pamoja na mke wake, ilisababishwa na Vivian baada ya kibuyu cha kichawi alichokuwa amekabidhiwa na mama yake, kuhitaji damu. Vivian alizidi kuwa hatari sana katika majukumu yake kuzimu. Vifo mbalimbali ndani ya ukoo na nje ya ukoo vilizidi kupamba moto. Kila siku ilikuwa ni ya mazishi, watoto kwa vijana walipoteza maisha. Alisababisha ajali nyingi ambazo ziligharimu maisha ya watu wengi sana. Watu walishindwa kuelewa ni kwanini vifo vilikuwa vinafululiza kila siku. Ila kwasababu akili za watu wengi zilikuwa zimefungwa walishindwa kuelewa kwamba chanzo alikuwa ni Vivian. Nelson na ujanja wake alishindwa kutambua kwamba ndani alikuwa anaishi na shetani mkubwa. Vivian ni mwanamke aliyejaliwa sura nzuri sambamba na umbo zuri la mwili wake. Sauti yake ilikuwa ni ya upole na pia uso wake ulikuwa ni wa tabasamu muda wote. Muonekano wake ni tofauti kabisa na matendo yake.
Biashara ya nguo aliyokuwa anaifanya Vivian aliiunganisha na kuzimu. Nguo zilizokuwa zinauzwa zilikuwa zinatoka moja kwa moja kuzimu. Kwa kupitia biashara yake ya nguo alifanikiwa kuwapeleka watu wengi sana kuzimu. Majini walikuwa na kazi ya kuwavuta watu waweze kwenda kwa wingi katika duka lake na hilo lilifanikiwa kwa asilimia kubwa. Hakuna duka lililokuwa linauza kama duka lake mjini arusha. Kwa makadirio ya haraka haraka kwa siku moja aliweza kupokea wateja hadi 300. Wafanya biashara wenzake waliokuwa jirani naye, hawakumpenda kwasababu walikosa wateja kabisa. Wateja wengi walionekana kupenda sana nguo zilizokuwa zinapatikana katika duka la Vivian, bila kufahamu kwamba duka lile lilikuwa linauza ngozi za binadamu ambazo zinachunwa kuzimu na kuletwa duniani. Ufahamu wao ulikuwa umefungwa ndio maana walishindwa kufahamu kilichokuwa kikiendelea katika duka lile. Laiti kama wangeweza kuona kilichokuwa dukani kwa Vivian wangeweza kuzirai kwasababu vilikuwa ni vitu vya kutisha japokuwa watu waliona kama vile ni nguo nzuri za kuvutia. Sherehe za kuzimu zilizidi kufana kwasababu upatikanaji wa damu na nyama ulikuwa ni wa uwakika. Duniani vilio viliongezeka kutokana na vifo kuchachamaa. Kila siku watu walichinjwa na kuliwa nyama kuzimu.
Ndugu wa Nelson walifariki kwa wingi ndani ya muda mfupi. Nyumba nyingi zilifungwa kwasababu hapakuwa na watu wa kuishi katika nyumba hizo. Kibaya zaidi vifo vilikuwa vinazidi kutokea kila siku iyendayo kwa Mungu. Pamoja na jitihada za wazee kufanya matambiko mbalimbali za kimila wakiamini kwamba labda watakuwa wamekosea mizimu ya mababu lakini ilishindikana. Waganga wengi waliojitokeza kutafuta ufumbuzi, walipoteza maisha katika mazingira ya kutataisha. Matukio hayo ya kusikitisha yalisababisha watu washindwe kuelewa kilichokuwa kikiendelea. Nelson alizidi kubaki njia panda roho ikiwa juujuu.
Akilini mwake alijua ipo siku na yeye atapoteza maisha katika mazingira yaleyale ya kutatanisha. Japokuwa alikuwa anapitia katika wakati mgumu sana lakini hakumkumbuka Mungu kwasababu ufahamu wake ulikuwa umefungwa. Kwahiyo hakuwa na muda wa kwenda kanisani wala kusoma biblia. Wakati mwingine alikuwa anafanya maandalizi makubwa siku za jumamosi ili siku inayofuata aweze kwenda kanisani lakini cha kushangaza mara nyingi siku za jumapili huamka huku akijihisi mgonjwa. Alishindwa kuelea hali ile ilikuwa inasababishwa na nini. Maisha yalizidi kusonga huku akizidi kuwa mbali na uso wa Mungu. Moyo ulimuuma lakini hakuwa na namna ya kuweza kujinasua katika mtego uliokuwa umemnasa.
MWANZA.
Kampuni binafsi iliyojulikana kwa jina la ‘Build Africa’ iliamishia makao makuu katika wilaya ya Ilemela jijini mwanza. Nelson akiwa mmoja kati ya wafanyakazi wakubwa wa kampuni hiyo alilazimika kuondoka na familia yake jijini Arusha na kuhamia mkoa wa mwanza kikazi. Nelson alifurahi sana kufungua ukurasa mpya wa maisha mkoani mwanza. Alihisi pengine labda kukaa mbali na mkoa wa arusha kungemfanya kusahau mapito aliyoyapitia ndani ya kipindi kifupi kilichopita. Kwahiyo Nelson aliuza nyumba na kuhamia moja kwa moja mkoani mwanza. Arusha hakuacha chochote kwani hata biashara zake zote alizihamisha, hakutamani tena kumbukumbu za jiji hilo ziweze kumrudia akilini mwake.
Frank na Christopha pamoja na Benedict walihamishiwa katika shule zingine mkoani humo. Nelson alifikia katika nyumba ya kisasa ambayo iliandaliwa na kampuni kwaajili yake. Marafiki wapya pamoja na majirani wapya angalau walisaidia kupunguza mawazo lukuki yaliyokuwa kichwani mwa Nelson. Watu walimpenda sana kwasababu alionekana kuwa mgeni mwema asiyekuwa na makuu japokuwa alikuwa anajiweza kifedha kwa kiasi fulani. Tabasamu usoni mwa Vivian mbele ya majirani ilisababisha wamzoee mapema bila kujua tabasamu lile lilikuwa ni la kuwapoteza maboya. Ndani ya muda mfupi walifahamika na majirani wote katika mtaa waliokuwa wanaishi. Sifa njema waliyoijenga ya kuzungumza na watu vizuri ndiyo iliyopelekea duka la nguo la Vivian alilolifungua katikati ya jiji hilo kupata mafuriko ya wateja. Kama ilivyokuwa jijini arusha duka la Vivian bado liliendelea kuendeshwa katika namna ya kuwaunganisha watu na kuzimu pasipo wao kufahamu kilichokuwa kikiendelea.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni