
Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Sifa njema waliyoijenga ya kuzungumza na watu vizuri ndiyo iliyopelekea duka la nguo la Vivian alilolifungua katikati ya jiji hilo kupata mafuriko ya wateja. Kama ilivyokuwa jijini arusha duka la Vivian bado liliendelea kuendeshwa katika namna ya kuwaunganisha watu na kuzimu pasipo wao kufahamu kilichokuwa kikiendelea.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Bidhaa zenye mvuto wa hali ya juu zilizokuwa dukani kwa Vivian zilikuwa zinatokea kuzimu. Majini yaliendela kufanya kazi ya kuwavuta wateja ili waweze kwenda kwa wingi katika duka hilo. Ndani ya kipindi kifupi Vivian alifanikiwa kuwateka wateja wa wafanya biashara wenzake. Nelson alifurahi sana alipokuwa anaona duka la nguo alilokuwa amemfungulia mke wake linafanya vizuri katika mauzo.
Hakujua kwamba kuna namna ambayo ilikuwa inatumika kuwavuta wateja katika duka lake. Badala yake alidhani kwamba kauli nzuri waliyokuwa wanazungumza na wateja ndiyo iliyokuwa inawapa mafanikio makubwa kiasi kile katika kazi zao. Kutokana na faida kubwa waliyokuwa wanaipata katika biashara ya nguo, walifungua maduka mengine kadhaa, kwajili ya kuuza nguo pembezoni mwa jiji la mwanza. Maisha yalizidi kuwa safi kwasababu pesa ziliwanyookea sana. Nelson alisimamisha biashara zake zingine na kuamua kuwekeza nguvu kubwa katika biashara ya kuuza nguo baada ya kuona kwamba inamlipa kuliko biashara zingine. Kampuni pia ilimpandishia mshahara kutokana na bidii kubwa aliyoionyesha kazini. Morali ya kujituma katika kazi, iliongezeka baada ya kuona kwamba uongozi wa kampuni unamjali kwa kiasi kikubwa.
Mafanikio waliyozidi kuyavuna katika biashara aliyokuwa anaiendesha Vivian waliwekeza katika ununuzi wa nyumba na viwanja. Ambavyo pia Vivian aliviunganisha na ulimwengu wa kuzimu kwa maana kwamba kwa yeyote ambae atafanikiwa kununua nyumba yake au hata kupanga kwa muda basi atakuwa ameingia katika maagano na kuzimu. Hayo yote Vivian aliyafanya wakati mume wake hafahamu chochote kilichokuwa kinaendela. Japokuwa mafanikio waliyokuwa wanayapata yalikuwa na kasi isiyokuwa ya kawaida, lakini Nelson pamoja na usomi wake hakufanikiwa kugundua chochote. Aliona kila kitu ni sawa, ingawa baadhi ya marafiki zake walishangazwa na mafanikio makubwa aliyoyapata, ndani ya kipindi kifupi.
Suala la Vivian kuwapiga bao wafanyabiashara wenzake halikuwa jema kabisa, kwani ilisababisha kuendelea kujengeka kwa chuki na uhasama wa chini kwa chini. Walishindwa kuelewa Vivian alikuwa anatumia uchawi wa nchi gani kwasababu vimbola vyao vya biashara vilishindwa kufanya kazi kama ilivyokuwa mwanzo. Hata mzee Bashingwa ambae nae alikuwa mfanyabiashara mashuhuri kwa uuzaji wa nguo mjini mwanza aliathiriwa na ujio wa Vivian. Licha ya kwamba mzee huyo anafahamika na wafanyabiashara wenzake kwamba ni mshirikina mkubwa katika mambo ya biashara lakini haikusaidia. Siku hadi siku biashara yake ilizidi kufifia. Chuki isiyomithilika iliyokuwa imejengeka moyoni mwake, alishindwa kuidhibiti na kupelekea kuionyesha kwa kukunja sura pindi macho yake yalipokutana na Nelson ama mke wake.
Nelson alijiuliza sababu ya mzee yule kumchukia ni kitu gani wakati mwanzoni alikuwa ni rafiki mwema kwake. Kwa akili ya harakaharaka Nelson alihisi kwamba mzee yule alijenga chuki kwasababu ya wivu wa kibiashara. Kwahiyo hilo halikumpa changamoto kubwa kwasabababu alifahamu ni mambo ya kawaida kwa wafanya biashara kuoneana wivu katika kazi. Akili ya Bashingwa ilikuwa ikifanya kazi kama umeme ili aweze kupata njia ya kuokoa biashara yake ambayo ilikuwa inaelekea kupotea moja kwa moja. Alipata wazo la kuhitisha kikao cha siri kwa wafanyabiashara wote wakubwa wa nguo jijini mwanza bila Vivian na mume wake kufahamu kilichokuwa kikiendelea. Madhumuni makubwa ya kikao hicho ilikuwa ni kutafuta mbinu ya kumpoteza kabisa Vivian katika ramani ya biashara jijini humo. Bashingwa alifanikiwa kuwakutanisha wafanyabiashara wote wakubwa wa nguo na kikao kilifanyika usiku katika hoteli ya Lake zone, iliyopo mjini humo.
Kwasababu wote walikuwa wameathirika kiuchumi walihitaji ndani ya siku hiyohiyo wapate hitimisho ambalo litawawezesha kutatua changamoto iliyokuwa mbele yao. Mapendekezo kadhaa yalipendekezwa ili kumaliza kabisa tatizo lile. Lakini katika mapendekezo yote yaliyopendekezwa, mapendekezo mawili yalionekana kupewa kipaumbele. Kwamba, maduka yote ya nguo yaliyokuwa yanamilikiwa na Vivian ndani ya jiji na pembezoni mwa jiji yateketezwe kwa moto. Na pia pendekezo la pili ni kwamba Vivian na mume wake watekwe wauwawe.
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Bashingwa alitamani pendekezo la pili lipitishwe kwasababu aliona ndiyo kiboko ya yote. Mvutano wa mawazo uliendelea katika kufanya maamuzi ya mapendekezo mawili yaliyokuwa mezani dhidi ya wafanyabiashara Vivian na Nelson. Baada ya majadiliano ya muda mrefu walikubaliana kwamba Nelson na mke wake wanatakiwa kutekwa na kuuwawa kimya kimya. Wafanyabiashara 12 waliokutana katika kikao hicho usiku huo, kila mmoja alichanga fedha taslimu milioni moja kwaajili ya kuwezesha zoezi la kutekwa na kuuwawa kwa wapinzani wao wa kibiashara. Baada ya mchango, mzee Bashingwa alikabidhiwa kitita cha fedha ili aweze kutafuta watu wa kufanya kazi hiyo haraka iwezekanavyo. Mwisho wa yote walikula kiapo cha kutokutoa siri hiyo nzito ya mipango ya mauwaji ya Nelson na mkewe.
***********
Benedict alihitimu elimu ya kidato cha nne kwahiyo alikuwa nyumbani akisubiri matokeo ya kuendelea na kidato cha tano. Katika shule ya sekondari Green Views aliyokuwa anasoma Benedict, alifanikiwa kuingia katika urafiki na binti mmoja ambae alikuwa ni mzaliwa wa Shinyanga katika wilaya ya Ibinzamata. Binti huyo alifahamika shuleni kwa jina la Adela, ingawa kijijini kwao alikuwa anafahamika kwa jina la Nyamoza, jina ambalo ni la marehemu bibi yake. Adela alikuwa ni binti mwenye uwezo mkubwa sana katika somo la hisabati. Aliogopeka na wanafunzi wote shuleni hapo na nje ya shule kutokana na utata wake katika somo hilo. Alikuwa na uwezo wa kipekee katika ukokotozi wa mahesababu magumu.
Sifa hiyo ndiyo iliyojenga urafiki kati yake na Benedict kwasababu Benedict vilevile alikuwa na uwezo mkubwa katika somo hilo. Tangu kidato cha kwanza Adela ndiye mwanafunzi ambae alikuwa ananyakua vikombe vya mashindano katika somo la hisabati ndani ya wilaya ya Ilemela. Lakini Benedict alipohamia shuleni hapo kidato cha tatu alishiriki kwenye mashindano hayo ambapo bila kutegemewa na mtu yeyote matokeo yalibadili historia iliyokuwa imewekwa na Adela. Benedict aliibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho cha kumsaka mkali wa somo hilo ndani ya wilaya hiyo. Ushindi huo ndio uliosababisha Benedict na Adela kuwa marafiki waliotokea kupendana sana.
Muda mwingi walionekana kuwa pamoja jambo ambalo lilipelekea wanafunzi wenzao kuwapa jina la utani ambalo ni ‘kumbikumbi.’ Ukaribu mkubwa uliokuwa kati yao ulitiliwa mashaka na wanafunzi wenzao kwamba huwenda ni wapenzi wa kisirisiri lakini haikuwa kweli. Japokuwa Benedict alionekana kummezea mate Adela kutokana na umbo lake kuwa zuri kuliko wanafunzi wote shuleni hapo. Fauku na hilo lakini pia sura yake ilikuwa ni nzuri na yenye mvuto wa hali ya juu. Kila muda Benedict alipokuwa akimwona Adela akitembea, mapigo ya moyo wake yalikwenda sambamba na mitetemo ya maungo ya binti huyo mrembo. Benedict alihisi kumpenda Adela lakini alishindwa kumweleza kwasababu Adela alionekana kuwa makini sana na shule. Kwahiyo alihofia kujitosa kumweleza kuhusu hisia zake kwani aliona kuna kila dalili ya ombi lake kupuuzwa. Mtazamo huo ulijengeka kichwani mwake tangu alipohamia shuleni hapo hadi alipohitimu kidato cha nne. Kwa kipindi chote walichokuwa shuleni walipendana na kuheshimiana kama kaka na dada.
Benedict aliendelea kuwasiliana na Adela ambae alirudi nyumbani kwao kijijini baada ya kumaliza kidato cha nne. Hisia za Benedict zilimtesa kwasababu hakuzoea kukaa mbali na Adela. Alishindwa kuendelea kukumbatia hisia zake, kwahiyo siku moja usiku alipokuwa kitandani kwake alipata mgogoro mkubwa kati ya nafsi na moyo. Alihisi kuna nguvu ilikuwa inamsukuma ampigie Adela simu amueleze ukweli kwamba anampenda, kwa wakati huohuo alihisi kunanguvu nyingine inamkataza kufanya hivyo. Mwisho wa yote nguvu iliyokuwa inamsukuma kumpigia Adela simu ilishinda kwahiyo Benedict alichukua uwamuzi wa kumpigia simu Adela na kumweleza jinsi moyo wake unavyopata taabu juu yake.
“Sawa Benedict nimekuelewa, ila ninasikitika sana kwasababu ninafikiri jibu langu halitakufurahisha, ila naomba ujitahidi kunielewa. Ukweli ni kwamba kwa sasa sipo tayari kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na mwanaume yeyote kwasababu bado ninasafari ndefu sana ya kimasomo.” Adela alizungumza maneno ambayo alisababisha moyo wa Benedict ulie “Paaaah” kwasababu ya mshituko mkubwa alioupata.
“Please Adela let me be yours, I wont break your heart ever.” (Tafadhali Adela naomba unifanye niwe wako, katu sinta uumiza moyo wako.)
“No thank you, Benedict.”
“But I love you!” (Lakini nakupenda!) Benedict alizungumza kwa sauti ya upole.
“I love you too, but let us continue to live as brother and sister.” (Nakupenda pia, lakini naomba tuendelee kuishi kama kaka na dada.)
Moyo wa Benedict uliuma sana baada ya kusikia msimamo wa Adela. Alijuta kutii ile nguvu iliyokuwa inamsukuma kumtamkia Adela kwamba anampenda.
“Don’t give up.” (usikate tamaa.) “women are weak.” (wanawake ni wadhaifu.) ile nguvu iliyokuwa inamsukuma mwanzo ili aweze kumtamkia Adela kwamba anampenda, alihisi imemletea mitazamo miwili ambayo itamuwezesha kumnasa mwanamke aliyempenda kwa dhati.
Benedict alitabasamu, baada ya kukumbuka kwamba aliwahi kusoma katika shajara (diary) ya Adela, kwamba anapenda sana kusoma vitabu vya hadithi vilivyoandikwa kwa lugha ya kiingereza. Moja kwa moja aliona hiyo inaweza ikawa njia ya kuendelea kuziteka hisia za Adela. Kwahiyo siku iliyofuata asubuhi na mapema alikwenda katika duka la vitabu akanunua kitabu kimoja cha hadithi ambacho kimetokea kupendwa na wapenzi wengi wa riwaya duniani.
Kitabu hicho kinafahamika kwa jina la ‘Harry potter and the sorcerer’s stone’ kilichoandikwa na ‘Rowling J.K’ baada ya hapo alikwenda katika kituo cha mabasi yaendayo mkoa wa shinyanga, akalipia bei ya kutuma kisha kikasafirishwa ambapo jioni ya siku hiyohiyo zawadi ilimfikia Adela. Benedict aliendelea kufanya mambo mengi mazuri kwaajili ya msichana ambae alitokea kumpenda kwa moyo wake wote. Kwa kadiri siku zilivyozidi kwenda ndivyo ambavyo moyo wa Adela ulivyozidi kulainika.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi