
Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA ISHIRINI NA TATU
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Benedict aliendelea kufanya mambo mengi mazuri kwaajili ya msichana ambae alitokea kumpenda kwa moyo wake wote. Kwa kadiri siku zilivyozidi kwenda ndivyo ambavyo moyo wa Adela ulivyozidi kulainika.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Adela ni msichana mrembo, tena bado bikira. Hata yeye mwenyewe anafahamu kwamba amejaliwa ulimbwendwe haswa. Achilia mbali uzuri aliojaliwa lakini pia amejaliwa utashi wa hali ya juu. Jamii nzima iliyokuwa inamzunguka ilikuwa inamuheshimu kwasababu yeye pia alikuwa anajiheshimu. Nguo zake zilikuwa ni za heshima, na pia marafiki zake walikuwa ni wa heshima pia. Alikuwa na malengo marefu ya kufika mbali kielimu. Hakuwa msichana wa kupayuka payuka kama walivyo mabinti wengi wa siku hizi. Lakini pia hakuwa mtu wa kupenda njia fupi ya mafanikio kama ambavyo wasichana wengi wa karne hii ya 21 wanavyopenda. Hivyo basi ndio maana pia imekuwa vigumu kwa wanaume wengi kuweza kufanikiwa kumshawishi kimapenzi kwasababu alikuwa anashughulisha ubongo wake ipasavyo kutafakari maneno ya wanaume waliojitokeza kumtongoza. Mwonekano wake wa mvuto uliwavutia watu wenye fedha na hata mafukara. Waliojiweza kifedha walijaribu kumuhonga vitu mbalimbali lakini alikumbuka maneno ya mwalimu wake wa somo la uraia (civics) siku moja alipokuwa darasani.
“Development is the gradual process. Means it is taking place in stages over an extended period of time. Frankly speaking development is not steep or abrupt.” (Maendeleo ni mchakato wa taratibu. Inamaana kwamba suala la maendeleo huenda ngazi kwa ngazi ndani ya kipindi fulani. Kwa ufupi maendeleo sio mteremko au jambo la ghafla.)
Maneno hayo yalikuwa ni kikwazo kikubwa ambacho kiliwazuia watu wenye jeuri ya pesa kumpata. Yote hayo ni kwakuwa hakupenda njia rahisi ya mafanikio na pia kwasababu alifahamu kwamba muda wa kuvipata hivyo vitu alivyokuwa anahongwa haujafika. Muda ukifika atavipata na hiyo ndiyo itakamilisha maana halisi ya neno maendeleo katika maisha yake. Kusema kweli Adela alikuwa ni msichana imara asiyekubali kuyumbishwa yumbishwa kama bendera. Suala la mahusiano ya kimapenzi aliliweka kando kabisa na maisha yake. Mshauri mkubwa katika maisha yake alikuwa ni mama yake mzazi, ambaye mara kwa mara amekuwa akimsisitiza kutojiingiza katika mahusiano ya kimapenzi wakati bado anaendelea na masomo.
Pamoja na hayo yote lakini jitahada za Benedict kumshawishi Adela ili wawe wapenzi zilimgusa kwa kiasi kikubwa. Alianza kuhisi anampenda kijana huyo ambae amesoma nae tangu kidato cha tatu. Wakati mwingine alikuwa anajitahidi kujizuia kuingia katika mawazo dhidi ya Benedict lakini alikuwa anashindwa. Hakuwahi kuwaza hata siku moja kwamba ipo siku ataweza kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na rafiki yake huyo. Kilichommaliza zaidi nguvu ni kwamba kwa kipindi chote ambacho ameishi na Benedict hakuwahi kukwazika hata siku moja. Alivutiwa sana na tabia ya upole aliyokuwa nayo kijana ambaye alionyesha dhamira ya dhati ya kutaka kuwa naye.
“Ooh my Gosh! I cant believe I have fall in love with Benedict.” (Ooh Mungu wangu! Siamini hisia zangu zimeangukia kwa Benedict.) Adela alijikuta akizungumza peke yake katika hali ya mawazo.
Ukoo aliokuwa anatokea Adela ni ukoo ambao unateswa sana na mizimu. Mwanaume yeyote ambae atakuwa wa kwanza kulala na msichana wa ukoo huo na hatimae kuuondoa usichana wake, basi ni lazima mwanaume huyo afe siku inayofuata. Hivyo ndivyo ilivyo kutokana na mizimu ya ukoo huo. Adela hakujua kwamba kuna mizimu ya aina ile katika ukoo wao, ingawa alishasikia fununu lakini hakuzitilia maanani kwasababu aliona ni mambo yasiyokuwa ya msingi katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia.
Wanawake wa ukoo huo walishahisi kwamba kuna nguvu fulani mbaya inawaandama. Kwasababu haiwezekani wanawake wote katika ukoo, wakapatwa na mkasa unaofanana. Matambiko mbalimbali yalifanyika kwaajili ya kuzuia mizimu hiyo iliyokuwa inawafuatilia wanawake wa ukoo huo lakini bado iliendelea. Ilifanyika kila namna ya kimila ili kuweza kumaliza tatizo hilo lakini ilishindikana, hatimae wazee wa ukoo walikata tamaa ya kuendelea kufanya matambiko kwasababu hawakuona mabadiliko yeyote, kwani bado mabinti waliendelea kulalama juu ya tatizo hilo miaka na miaka.
Kikao kilichokuwa kinaendelea katika hoteli ya Lake zone, jijini mwanza kilimalizika usiku mnene. Maazimio yaliyoafikiwa katika kikao hicho kilichohusisha wafanyabiashara wakubwa wa nguo jijini humo, ni kwamba, Nelson pamoja na mkewe wanatakiwa kutekwa na kisha kuuwawa ndani ya masaa 24 yajayo. Bashingwa ambae ndie aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho, alikabidhiwa jumla ya fedha zote zilizochangwa kwaajili ya kutafuta vijana wahuni watakaoweza kufanya kazi hiyo ya mauwaji haraka iwezekanavyo. Waliondoka hotelini pale na kila mmoja alipanda kwenye gari lake na kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwake. Usiku wa siku hiyo haukuwa mwema kabisa kwao, kwani kila mmoja aliandamwa na ndoto za umauti.
Bashingwa aliota amekufa yupo ndani ya jeneza anaagwa na ndugu jamaa na marafiki. Ulimi wake ulikuwa mzito sana kuzungumza maneno ya kujitetea ili asizikwe. Kope za macho yake zilikuwa hazipepesi ingawa alikuwa anaona kila kilichokuwa kikifanyika. Mwili wake ulikuwa kama vile umepigwa gazi ya kiwango cha juu sana, kwasababu alijitahidi kufurukuta lakini ilishindikana. Vilio vilitawala sana ingawa alikuwa anaona kabisa kilichokuwa kikiendelea ila alishindwa kuzungumza kuwanyamazisha watu waliokuwa wanamlilia. Alitamani kunyanyuka ndani ya jeneza ili aweze kuwatuliza ndugu zake lakini hakufanikiwa.
Baada ya mwili wake kuagwa alishangaa jeneza ambalo alikuwa ndani yake likinyanyuliwa na kisha kupelekwa katika kaburi lililokuwa limechimbwa pale nyumbani kwake. Jeneza hilo lilidumbukizwa ndani ya shimo na kisha watu wakaanza kurudisha udongo kwa kasi shimoni. Udongo wote ulirudishwa kwenye shimo huku akitamani kuzungumza kujitetea asizikwe kwasababu hakuwa maiti lakini mdomo wake ulishindwa kutii amri ya ubongo. Moyo ulimuuma sana kwasababu alishuhudia akizikwa ili hali hakuwa mfu. Kwa kadiri udongo ulivyokuwa unazidi kufunika jeneza ndani ya shimo ndivyo ambavyo giza nene lilizidi kuchukua hatamu kufunika nuru hafifu iliyokuwa kwenye mboni ya macho yake. Kabla giza halijamaliza kufunika nuru katika mboni zake alishtuka katika usingizi mzito aliokuwa amelala kisha akaketi kitandani.
Alitazama upande wa pili alipokuwa amelala mke wake lakini hakumwona. Moyo ulikuwa unamwenda mbio sana, kwasababu ndoto aliyokuwa ameiota ndio ndoto ambayo ilikuwa mbaya kuliko ndoto zote ambazo aliwahi kuota tangu alipotoka tumboni mwa mama yake. Jasho jingi lililokuwa likitiririka katika mwili wake lililowanisha mashuka yote kitandani. Mawazo yake yalimtuma kwamba huwenda mke wake alikuwa chooni. Kwahiyo hakuwa na mashaka, aliendelea kumsubiri mke wake ili aweze kumsimulia ndoto mbaya aliyokuwa ameiota. Baada ya dakika kumi mke wake bado hakuwa amerejea kitandani. Hofu ilizidi kutambaa ndani ya moyo wake. Aliteremka kitandani kisha akatembea taratibu hadi katika mlango wa choo ambacho kilikuwa ndani ya chumba chao. Taratibu alifungua mlango wa chooni kisha akachungulia ndani lakini hakumwona mke wake. Akili yake ilimtuma achungulie na bafuni pia lakini napo hakumwona.
“Aagh! atakuwa amekwenda wapi usiku huu.” Bashingwa alizungumza, kwa hasira peke yake huku akibamiza mlango wa bafuni baada ya kumkosa mke wake.
Kitendo cha Bashingwa kumkosa mke wake chooni na bafuni pia, kilimuweka katika wakati mgumu sana. Alijaribu kufikiri mara kumi kumi ni wapi ambapo mke wake alikuwepo kwa wakati ule ili hali bado ulikuwa ni usiku mnene. Baada ya kumkosa mke wake chumbani, alipata wazo la kwenda kumtafuta sebuleni na katika vyumba vingine. Bashingwa alipofika katika mlango wa chumbani ili aweze kufungua atoke, alipatwa na mshtuko mkubwa nusura adondoke chini. Mlango wa chumba chake ulikuwa bado umefungwa. Ufunguo wa kitasa ulikuwa unaning’inia kwa ndani na pia makomeo makubwa yaliyokuwa kwa ndani ya chumba bado yalikuwa yamefungwa barabara.
“Sasa hata kama ametoka amepitia wapi?” Bashingwa aliwaza huku akihema kwa pupa.
Moyo uliongeza kasi ya mapigo mara dufu. Punde alihisi haja ndogo na kubwa zote kwa pamoja. Alitoka mbio na kuingia katika choo cha chumbani kwake ili aweze kumaliza haja zake zilizomjia ghafla. Mwili wake ulikuwa unatetemeka kutokana na hofu kubwa iliyokuwa ndani ya moyo wake. Alipomaliza kujisaidia alijikaza kiume na kuelekea katika mlango wa chumbani kisha akafungua na kutoka. Alifanya ukaguzi wake sebuleni pamoja na kwenye vyumba vingine bila mafanikio. Alizidi kutekwa na wimbi la mawazo kutokana na mauzauza yaliyokuwa yanaendelea ndani ya nyumba yake kwa wakati ule.
Alikosa kabisa jibu pindi alipojitahidi kutafakari kwa kina kuhusu mazingira ya mke wake kutoweka. Baada ya kuridhika na ukaguzi wa nguvu alioufanya katika kona zote za nyumba yake, aliamua kurudi chumbani kwake. Katika hali isiyokuwa ya kawaida Bashingwa alipofungua mlango wake wa chumbani ili aweze kuingia, alishangaa kumwona mke wake akiwa amelala fofofo kitandani. Bashingwa alipatwa na mshtuko ambao alishindwa kuuhimili hatimae alikosa nguvu na kisha kudondoka sakafuni na kupoteza fahamu.
“Puuuuh.” Ni kishindo kilichomzindua Bi Diana usingizini baada ya mume wake kudondoka chini kwa kishindo cha ajabu. Harakaharaka alishuka kitandani na kwenda kumsaidia mume wake ambae alionekana kupatwa na matatizo. Kwa bahati nzuri mzee Bashingwa alizinduka baada ya kupepewa kwa muda wa kama dakika kumi.
Mara baada ya fahamu kumrejea barabara na kumwona mke wake mbele ya macho yake alizirai kwa mara nyingine tena. Alishindwa kuelewa mke wake amefika vipi pale kitandani wakati alimtafuta katika kila kona ya nyumba bila mafanikio. Bi Diana hakujua chochote kilichokuwa kinaendelea kwasababu alikuwa amelala. Kwahiyo alizidi kumpepea mume wake ili aweze kuzinduka halafu amuulize kulikoni yupo katika hali ile wakati hakusikia akilalama kwamba anahisi maumivu ya sehemu yeyote ya mwili wake. Baada ya dakika kadhaa Bashingwa alirejewa na fahamu zake. Hofu iliyokuwa inatambaa kifuani mwake ilisababisha mapigo yake ya moyo yaende kwa kasi isiyomithilika. Mwili wake uliishiwa kabisa nguvu na pia tumbo lilikuwa linanguruma kutokana na wasiwasi mwingi uliokuwa ndani ya mtima wake.
“Unaumwa?” Bi Diana alimuuliza mume wake ambae bado alikuwa anashangaashangaa kama vile abiria aliyeachwa na gari, stendi.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi