
Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Miongoni mwa wagonjwa wanaoonekana kuwa na hali mbaya zaidi ni pamoja na Benedict. Hivyo basi hali yake mbaya inapelekea jopo la madaktari kukusanyika kwa pamoja ili waweze kuokoa maisha yake.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Mapigo yake ya moyo yanadunda kwa mbali sana. Hivyo matumaini yanazidi kuwapotea madaktari wanaomuudumia kwa nguvu zao zote. Kiukweli hali ya kijana huyu ni mbaya sana kwasababu madaktari wanajaribu kubusti mapigo yake ya moyo bila mafanikio.
Hali ya Adela nae bado ni mbaya sana kwasababu, fahamu bado hazijamrejea. Kwa mujibu wa madaktari, wamebaini kuwa binti huyu ameumia zaidi kichwani. Kwahiyo wanaendelea na jitihada za kuokoa maisha yake. Hali tete aliyonayo, imepelekea sura yake ya mvuto kuonekana kama vile ya kikongwe. Ule uzuri wake ambao ulikuwa ukimchanganya Benedict hauonekani tena. Ngozi yake yake ya mwili, iliyokuwa nyororo mithili ya mtoto aliyezaliwa jana, inaonekana kubadilika na kuwa nyeusi tii. Adela amelazwa kitandani amefunikwa kwa shuka jeupe, anapumua kwa msaada wa mashine. Mkononi ana dripu inayoingiza dawa kwa kasi katika mishipa yake.
Inavyoonekana hali ya Adela inakwenda sambamba na hali ya Benedict, kwani wote wanaonekana kuwa katika njia moja ya umauti. Hadi kunapambazuka, idadi ya watu waliokusanyika katika hospitali ya KCMC kutafuta ndugu zao inazidi kuongeza. Waume kwa wake, wazee kwa vijana wanaonekana katika majonzi mazito ya kupotelewa na ndugu zao. Majonzi mazito yanapelekea baadhi ya watu kudondoka na kupoteza fahamu kutokana na hisia za machungu mioyoni mwao. Jeshi la polisi wakishirikiana na uongozi wa hosipitali ya KCMC wanasimamia vema zoezi la watu kwenda kutambua miili ya ndugu zao waliopoteza maisha katika ajali ya tetemeko la ardhi.
*********
Sauti ya Adela akipiga kelele kuomba msaada ilisikika katika masikio ya kijana mmoja, ambaye alihisi huruma moyoni mwake na kuamua kuuvaa ujasiri kuokoa maisha ya binti aliyekuwa akimsikia kwa muda mrefu akilia kwa huruma, kuomba msaada. Kijana huyu ambae alikuwa umbali wa kama mita mia mbili na ushee, aliamua kuhatarisha maisha yake kwa kujitolea kwenda kuokoa maisha ya mtu ambaye alikuwa hamfahamu. Moyo wa huruma unasababisha anachukua maamuzi ya fastafasta kwenda kunusuru maisha ya mtu, aliyekuwa anaomba msaada kwa kilio cha uchungu.
Anakimbia huku akisikiliza sauti ile ilipokuwa ikitokea ili aweze kufika kwa wakati na kutoa msaada. Hata hivyo kwa bahati mbaya wakati anakaribia kufika katika eneo la tukio, sauti ya binti aliyekuwa anaomba msaada inazimika ghafla. Hofu kubwa inamjaa kijana huyu, ambaye amejitolea kufanya kazi ya uokoaji katika mazingira hatari. Anaongeza mwendo ili aweze kusogea mbele zaidi kwavile alihisi pengine mtu aliyekuwa anaomba msaada amekumbwa na matatizo makubwa zaidi.
“Kimemsibu nini, mbona ametulia kimya?” kijana alijiuliza swali mwenyewe, huku akizidi kusonga mbele katika giza totoro.
Baada ya kama dakika mbili na sekunde kadhaa, wakati alipokuwa akizidi kusonga mbele asipopajua, moyo wa kijana huyu ulilia paa! kwa mshtuko, baada ya kuhisi amekanyaga mwili wa mtu. Kijana huyu anatazama chini kwa umakini huku akitetemeka kwa woga na kugundua kuwa ameukanyaga mkono wa mtu ambae anaonekana kufukiwa eneo kubwa la mwili wake.
“Jesus Christ.” Kijana msamaria mwema, anaonekana kushtuka zaidi baada ya kuuona mwili wa mwanamke mtupu pembeni yake, huku fahamu zimempotea.
“Inawezekana huyu ndiye aliyekuwa akiomba msaada, lakini sasa mbona yupo uchi?” Kijana alijikuta akizungumza peke yake wakati alipokuwa akijaribu kuchunguza kama bado wote wapo hai ama la!.
Katika uchunguzi wa harakaharaka anaoufanya, anagundua kuwa wote bado ni wazima ingawa hali zao ni mbaya. Kwahiyo anaamua kuchukua jukumu la kuwasaidia kuwatoa katika eneo la hatari. Kwa kadiri ya nguvu zake zote kijana huyu anajitoa kuufukua mwili wa Benedict ulionasa katika kifusi na kisha anawabeba na kuwasogeza katika eneo lenye usalama. Jeshi la wananchi wa Tanzania tayari walikuwa katika eneo la tukio wakiendelea na shughuli ya uokoaji. Hivyo basi ambulensi ya jeshi inawachukua na kuwakimbiza katika hospitali ya KCMC kupatiwa matibabu. Kwahiyo huo ndio ukawa mwanzo wa Benedict na Adela kulazwa katika wodi za wagonjwa mahututi hospitalini hapo.
*********
Mawazo yanazidi kuandama kichwa cha Marwa baada ya mganga kushindwa kumsaidia. Anachukua uamuzi wa kwenda kwa mganga mwingine ambaye nae sifa zake zinavuma. Lakini kama wasemavyo waswahili ‘siku ya kufa nyani, miti yote huteleza’ ndicho kilichokuwa kinamtokea kijana Marwa, kwani kwa mara nyingine mganga mwingine anashindwa kumsaidia kutimiza hitaji lake la kutaka kumuuwa Benedict ili aweze kumpata Adela. Moyo wake unazidi kufuka hasira dhidi ya kijana Benedict. Akili yake inaenda mbali zaidi na kumtuma adhani kwamba huwenda Adela anampenda Benedict kwasababu ya nguvu za kichawi.
“Haiwezekani Adela asinielewe kwa nyimbo zote nilizomwimbisha, lazima kuna kitu huyu fala kafanya.” Marwa aliwaza kwa hasira huku machozi na makamasi yakimdondoka kwa pamoja.
“Siwezi kukubali kushindwa kibwege, nilazima nipambane mtoto wa kiume mpaka kieleweke.” Mawazo yalizidi kutikisa kwa fujo kichwa cha Marwa.
Hata hivyo kushindwa kwake kwa mara ya pili katika safari yake ya kwa mganga, hakumkatishi tamaa. Anaamua kurudi kwa mganga Ahmedi, kwa mara nyingine akiwa amebadili mbinu ya kumpata Adela. Mbinu mpya aliyoiwaza kijana huyu ni kwamba, mganga afanye awezalo ili Adela aweze kumpenda kupita maelezo. Popote pale alipo fikra zake na moyo wake umuwaze yeye tu na wala sio mwingine. Wazo hili linaonekana kufanikiwa kwa asilimia zote, baada ya mganga kuwaunganisha Adela na Marwa kwa njia ya kichawi. Zoezi la Adela na Marwa kuunganishwa kichawi lilifanyika usiku wa saa sita na nusu nyumbani kwa mganga, siku ya alhamisi kuamkia ijumaa.
Mganga alitandika shuka jeupe juu ya mkeka kisha akachukua mshumaa mnene ulioandikwa kwa pini maneno haya mara tatu ‘MAPENZI YAKO YOTE YAJE KWANGU’. Wakati mshumaa ulipokuwa ukiwaka, Marwa alikuwa akinena kwa sauti ndogo maneno ambayo aliagizwa na mganga. Baada ya mshumaa kumalizika kuwaka mabaki ya mshumaa yalifungwa katika kitambaa cheupe alichokuwa amekikalia kijana Marwa wakati alipokuwa kwa mganga. Kisha mganga alimuamuru atoke nje, aelekee kaskazini huku akiita jina la ADELA kwa mara saba halafu baada ya hapo arudi ndani bila kuangalia nyuma. Alipomaliza kufanya zoezi hilo, mganga alimkabidhi mabaki ya mshumaa iliyokuwa imefungwa kwenye kitambaa cheupe na kumuamuru kwenda kukificha katika sehemu ambayo haita onwa na mtu yeyote.
“Na endapo sintahitaji kuwa mapenzini tena na mwanamke huyu nifanyaje?” Marwa alitaka kujua.
“Ni rahisi, ni rahisi, ni rahisi sana, ahahaha ahahaha!” mganga alizungumza kwa sauti ya juu huku akijichezesha chezesha wakati akiwa ameupinda mgongo wake.
“Tawire mganga.”
“Utachukua haya mabaki ya mshumaa halafu utayachoma moto au uyazike katika njia panda, au uyatupe katika mfereji wa maji yanayokwenda au utupe katika shimo la choo amaa jalala. Kwa kuchagua njia moja wapo itapelekea mapenzi yenu kuyeyuka kama maji yaliyomwagwa juu ya ardhi ya mchanga mchanga.”
“Tawire mganga.”
“Nimemaliza, nimemaliza, unaweza kuondoka.” Sauti ya mganga Ahmedi ilisikika wakati alipokuwa akizungumza mithili ya mtu aliyepandwa na majini.
“Tawire mganga.”
“Usigeuke nyuma hadi utakapofika nyumbani kwako.” Mganga alizidi kumpa masharti Marwa.
Usiku wa saa tisa kasoro, Marwa aliondoka nyumbani kwa mganga na kuelekea nyumbani. Moyo wake ulikuwa na amani kwa kiasi fulani kwasababu mganga alimuhakikishia kwamba, asiendelee kuangaika kumtafuta Adela kwasababu Andela ndiye atakayemtafuta yeye kwa udi na uvumba popote pale atakapokuwa.
Naam! Nelson anajikuta katika lindi kubwa la mawazo, baada ya kusikia vifo vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi mkoani Kilimanjaro. Anahisi kuchanganyikiwa kwasababu alikuwa anafahamu fika, kwamba ni lazima mwanae alale gesti mjini moshi ili siku inayofuata ndiyo aweze kwenda shuleni. Hiyo yote ni kwasababu alijua kwamba, Benedict atafika moshi usiku sana, kiasi kwamba hataweza kupata usafiri wa kumfikisha katika shule aliyopangiwa kwenda kuanza kidato cha tano. Kwahiyo habari ya vifo vilivyotokea inaonekana kumchanganya kabisa akili yake. Anakosa raha, moyo wake unajawa na masononeko makubwa, kwa kuhisi huwenda kijana wake nae ameweza kukumbwa na janga hilo.
Anachukua uwamuzi wa kuutafuta uongozi wa shule ya Lyamungo sekondari ili aweze kufahamu kama mwanae alifika salama shuleni hapo ama la! Hata hivyo anazidi kujikuta akiangukia katika wakati mgumu zaidi baada ya kuelezwa na uongozi wa shule hiyo kwamba, Benedict hajafika shuleni hapo na pia muda wa kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano haujafika. Kiukweli Nelson anazidi kuwa katika wakati mgumu, anapojaribu kufikiri mwanae kipenzi atakuwa katika hali gani. Anajikuta katika mawazo mazito ambayo yanapelekea ajione kama vile ametoswa baharini ili hali hafahamu kupiga mbizi.
********
Baada ya Vivian kuonekana kufanya vizuri katika kutekeleza majukumu ya kuzimu, malikia mkuu wa kuzimu, anaonekana kufurahishwa sana na mwenendo wa binti huyu. Kwahiyo analazimika kumuandaa ili aweze kumuachia kiti chake cha umalikia, baada ya kumuoana anafaa kukalia kiti hicho chenye hadhi ya kipekee. Kitu cha kwanza cha msingi kinachohitajika ili Vivian aweze kukalia kiti cha umalikia, ni lazima afunge ndoa nyingine kule kuzimu.
Kwahiyo malikia anamshauri Vivian ili aweze kufunga ndoa kule kuzimu, kusudi aweze kuwa malikia mkuu. Jambo hili linaonekana kukubaliwa na Vivian bila shaka yeyote. Vivian anaonekana kutokuwa na chaguo jingine tofauti na Nelson, kwahiyo anaamua kumweleza malikia kwamba yupo tayari kufunga ndoa na Nelson ambaye ni mume wake wa duniani. Malikia anaridhia chaguo lake bila kuonyesha chembechembe zozote za pingamizi, kitu ambacho kinaamsha hisia za furaha ndani ya mtima wa Vivian.
Pamoja na hayo yote lakini pia ili ndoa hiyo iweze kufungwa, Vivian alipaswa kumtoa mwanae Benedict kama kafara ya kufanikisha ndoa hiyo. Sambamba na hilo, Vivian alipaswa kutoa kafara ya watu wasiopungua 300 kama kuonyesha heshima kwa malikia ambaye amekubali kumuachia kiti kwa hiyari. Bila wasiwasi wala kusita, Vivian anakubaliana na vigezo vyote alivyoelezwa na malikia ili ndoa yake iweze kufungwa na hatimaye akabidhiwe cheo.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi