SHEREHE KUZIMU (28)
Zephiline F Ezekiel
---

Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA ISHIRINI NA NANE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Baada ya kufika ghorofa ya tatu, Nelson alikuwa akihema kwa kasi sana kwasababu ngazi zilikuwa zimemchosha halafu maumivu bado yalikuwa yanamuandama.
Kwa jinsi alivyokuwa anajihisi vibaya, aliinama akiwa ameshika magoti kwa uchovu huku akisikilizia jinsi moyo ulivyokuwa ukimwenda mbio.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Mwili wake ulikuwa unavuja jasho jingi ambalo lilipelekea shati lake kulowa jasho mithili ya mtu aliyenyeshewa na mvua kubwa. Hata hivyo kwasababu alikuwa na siku ya pili mwili wake haujagusa maji, makwapa yake yalikuwa yanatoa harufu kali.
Baada ya dakika tano akiwa ameinama anahema juu juu, alinyanyua kichwa chake na kisha macho yake yakakutana na kibao kidogo kilichobandikwa kwenye mlango uliokuwa mbele yake. Ukiwa umeandikwa namba 7 kwa rangi nyeupe. Moja kwa moja akaanza kutembea kufuata korido ili aweze kufika katika wodi namba 17 ambayo ndiyo Benedict kalazwa.
Palikuwa ni karibu mno, lakini kwa mwendo wa Nelson wa kujikongoja ilimgharimu kama dakika kadhaa kuufikia mlango huo. Nelson aliufikia mlango wa wodi lakini alisita kuufungua, kwasababu kulikuwa na tangazo linalosomeka “USIINGIE BILA RUHUSA”
Alizidi kutafakari cha kufanya kwa muda kidogo lakini kutokana na shauku ya kutaka kumuona mwanae, dhamira yake ilimsukuma kuufungua mlango ili aweze kuingia ndani. Huku mkono wake ukiwa katika kitasa tayari kufungua mlango alishangaa kuona mlango umefunguliwa ghafla kabla yake. Kisha akakumbana na kikumbo kikali kutoka kwa watu wawili waliovalia mavazi mithili ya madaktari.
“Au tummalize na huyu?” Nelson alisikia sentensi hiyo kutoka kwa mmoja wa watu wale wakati akiwa ameanguka chini baada ya kupokea kikumbo kikali kutoka kwa watu hao ambao hakujua ni wakina nani na dhamira yao ni nini hasa.
“Achana nae, tuondoke haraka.” Mmoja wa watu wale alijibu huku akionekana kumvuta mwenzie ili waweze kutokomea kusiko julikana. Nelson anawakodolea macho watu wale na kugundua kuwa huwenda sio watu wema kwasababu walikuwa wametapakaa damu katika mikono yao.
Mapigo ya moyo wa Nelson, yanaongeza kasi mara dufu kutokana na woga alioupata baada ya kukumbana na watu wale. “Lakini mbona wamevalia mavazi yaa kidaktari sasa kwanini wa behave like this?” Nelson aliwaza huku akijishika na ukuta ili aweze kusimama aweze kuingia ndani ya wodi kuangalia kilichokuwa kikiendelea.
“Aagh” Nelson anaonekana kukasirika baada ya kuona shati lake linadoa ya damu.
“Inamana kwa kikumbo kile ndiyo tayari nimeshaumia?” Nelson alijiuliza wakati alipokuwa akijipapasa sehemu mbalimbali za mwili wake, ili aweze kujua jeraha lililosababisha damu kwenye shati lake lipo wapi katika mwili wake. Katika kujipapasa huko kwa takribani dakika nzima, anafahamu kuwa, hana jeraha lolote mwilini mwake. Kwahiyo anagundua kuwa huenda ni watu wale ndio walimpaka damu wakati walipompa kikumbo cha nguvu pale mlangoni.
Nelson aliona ni bora aingie wodini kumjulia hali mwanae kwavile mashaka yalizidi kumtawala baada ya kuhisi, watu aliotokea wodini hapo muda mfupi uliopita sio watu wazuri. Kwa haraka anafungua mlango wa wodi na kisha anaingia ndani taratibu. Ukimya wa kutisha umetawala wodini. Taa zinawaka huku mitambo ya oxygen ikisikika kunguruma kwa mbali.
Nelson anazidi kupiga hatua taratibu na kwa uwoga, kuusogelea mwili wa mtu uliolazwa kitandani hapo, huku ukiwa umefunikwa kwa shuka jeupe hadi kifuani. Macho ya Nelson yanaonekana kutizama zaidi uso wa mgonjwa ili aweze kujua kama ni mwanae au sio.
Lakini majibu ya ubongo wa Nelson baada ya kumtazama vizuri mgonjwa aliyelala kitandani, wakati alipokuwa anazidi kumsogelea, aligundua kuwa ni mwanae ingawa sura yake ilikuwa imebadilika kwani ilionekana kujaa. Nelson alianza kudondosha machozi huku makwapa yakionekana kuvuja jasho kwa kasi, kutokana na hali ya mwanae ilivyokuwa inaonekana kuwa mbaya.
Yote tisa, kumi ni kwamba baada ya Nelson kufikia vizuri kitanda cha mwanae aligundua kuwa kunadoa kubwa la damu ubavuni mwa Benedict. Kwa mshtuko wa hali ya juu ilibidi afunue lile shuka jeupe ili aweze kujua damu ile ilikuwa inatoka wapi.
“OOH MY GOD!” (Mungu wangu!) Nelson alizungumza kwa sauti kubwa wakati alipokuwa wodini peke yake. Ni baada ya kuona kisu kimezama ndani ya tumbo la mwanae. Kitendo kile kilimpa maumivu yasiyokuwa na mfano ndani ya moyo wake.
Alipata uchungu na gadhabu kali ambayo ilipelekea anyanyuke mithili ya ndege ya kivita ili ajaribu kuwafuatilia watu wale, ambao sura zao bado zilikuwa zipo ndani ya mboni ya macho yake. Mwili wake ulipata nguvu ghafla kutokana na kitendo cha kinyama alichokuwa ametendewa mwanae. Mara baada ya kufungua mlango kwa kasi ya ajabu alikumbana na nesi aliyekuwa anaingia wodini humo akiwa na trei la vifaa vya kitabibu.
Kutokana na kikumbo anachopigwa na Nelson nesi huyo anadondosha trei lake la vifaa na kisha yeye anadondoka kando na kwabahati mbaya anatenguka mkono wake wa kushoto. Pamoja na hayo yote lakini Nelson haonekani kujali kwani anaendelea kukimbia kuelekea ghorofa ya chini kuwatafuta waalifu wake.
Kilichotokea sio jambo la kawaida kabisa, kwahiyo nesi yule anajitahidi kusimama ingawa anahisi maumivu makali katika mkono wake. Chapchap anazama ndani ya wodi kuangalia usalama wa mgonjwa kwavile alipata mashaka kutokana na kilichotokea muda mfupi.
Wasiwasi wake dhidi ya usalama wa mgonjwa ulikuwa ni sahihi kabisa kwavile, alipofika ndani ya wodi alikuta mgonjwa amechomwa kisu na hali yake ni mbaya sana kwasababu tayari alikuwa anakoroma. Kwahiyo aliamua kutoka mbio kwenda kutoa taarifa kwa mkubwa wake wa kazi. Mwendo wake mkali unaishia katika ofisi ya mganga wa zamu. Huku akihema kama vile mwizi aliyetoka kufukuzwa, alianza kujieleza kwa daktari yule.
“Daktari ku..na mgonjwa kacho..mwa kisu tumboni hali yake ni mbaya sana?” nesi alizungumza huku akikatisha katisha maneno yake kwasababu moyo ulikuwa unamwenda mbio sana kwasababu ya kukimbia.
“What? Where?” (nini? Wapi?) Kwa mshangao daktari alitaka kuelezwa vizuri juu ya tukio lenyewe.
“ICU wodi namba 17, kwa yule mgonjwa aliyeletwa jana kutokea KCMC.” Nesi alizungumza harakaharaka huku wakiongozana kwa mwendo wa haraka kuelekea kwenye wodi yenyewe. Hadi wanafika katika wodi aliyokuwa amelazwa Benedict nesi alikuwa tayari ameshamweleza daktari kila kitu alichokuwa amekishuhudia, ikiwamo kikumbo alichopigwa na Nelson pale mlangoni. Walipofika wodini walikuta Benedict anarusha rusha miguu kwa ishara ya kukata roho. Kwa hali aliyokuwa nayo Benedict inapelekea daktari kutingisha kichwa kwa ishara ya kukata tamaa.
“Ukimwona huyo mwalifu utaweza kumtambua?” Daktari alimuuliza nesi swali, wakati alipokuwa akipiga simu kituo cha polisi.
“Bila shaka dokta, nitaweza kumfahamu.” Nesi alijibu swali huku mkono wake wa kuume ukiwa chini ya kiwiko cha mkono wa kushoto kutokana na maumivu makali aliyokuwa nayo.
“Oky fine.” (sawa)
Baada ya dakika kumi polisi walifika pale wodini wakiwa wameongozana na waandishi wa habari. Nelson anapigwa picha mbalimbali na waandishi hao ili waweze kuripoti tukio hilo. Nesi yule alichukuliwa na polisi kwenda kutoa maelezo yatakayowawezesha kukamilisha upelelezi wao juu ya tukio hilo la kusikitisha.
Hata hivyo wakati polisi walipokuwa wakiongozana na nesi yule, kutokea ghorofa ya tatu kushuka chini lilipokuwa gari ya polisi. Macho ya nesi yule yalifanikiwa kumuona Nelson umbali wa kama mita sabini, akiwa ameweka mikono kichwani anazungukazunguka mithili ya mtu aliyechanganyikiwa.
“Jamani mualifu mwenyewe si mwingine bali ni yule pale aliyeweka mikono mfukoni anazunguka zunguka.” Nesi yule alizungumza na maaskari aliokuwa nao wakati akimnyooshea kidole Nelson ambaye tayari alikuwa ameshatoa mikono kichwani na kudumbukiza ndani ya mifuko ya suruali yake.
“Unauwakika?” askari aliuliza.
“Ndiyo ninauwakika asilimia mia moja, amevaa shati jeupe na suruali nyeusi nyuma ya shati lake karibu na ubavuni kuna doa la damu.” nesi yule alizidi kuzungumza kwa msisitizo kuonyesha kwamba habahatishi. Askari wawili waliokuwa wameshika mitutu yao barabara, walianza kumfuatilia mtu ambae alikuwa anadhaniwa kuwa ndiye muuwaji.
Nelson alibaki ameduwaa baada ya kuwaona watu wale wakipanda katika pikipiki na kisha kutokomea kusipojulikana. Pamoja na kutoka kote nduki kuwafukuzia lakini hakufanikiwa kumtia mkononi hata mmoja. Alitamani angekuwa na usafiri wake aweze kuwafukuzia watu wale ambao walikuwa zaidi ya wanaharamu kwake. Alibaki na majeraha ya maumivu ya moyo yasiyokuwa na tiba ya haraka.
Alijua kwa namna moja ama nyingine ni lazima mwanae atakuwa amepoteza maisha kwavile kisu kile kilikuwa kimezama chote ndani ya tumbo lake. Mawazo katika kichwa chake kuhusu hali ya mtoto wake ndiyo iliyopelekea aonekane kama vile amerukwa na akili. Ubongo wake ulikuwa mzito kutoa maamuzi ya haraka yatakayomwezesha kufumbua fumbo gumu lililokuwa mbele yake kwa wakati ule. Alibaki akikodolea macho pikipiki iliyoondolewa mbele ya macho yake kwa mwendo mkali ambao hakuwahi kuuona popote. Alishindwa kabisa kuzuia hisia kali za maumivu zilizokuwa zikitembea katika mishipa yake ya fahamu, kwahiyo machozi yalikuwa yakimbubujika mfululizo.
Hata hivyo baada ya kuona kwamba hakuna namna ya kuweza kuwapata watu wale, aliamua kuchukua uwamuzi wa kuweza kurudi wodini kwenda kucheki mustakabali wa maisha ya mwanae. Kwahiyo wakati alipokuwa anageuka ili aweze kushika njia ya kuelekea wodini, alishangaa macho yake kukutana uso kwa uso na maaskari wa jeshi la polisi waliokuwa wameshika mitutu ya bunduki.
“Upo chini ya ulinzi. Unatuhumiwa kushiriki katika shambulio la mauwaji katika wodi namba 17.” Askari mmoja alizungumza huku wakimtazama kwa makini mtuhumiwa.
“Jamani mimi sio muuwaji.” Nelson alizungumza kwa uchungu huku akilia kama mtoto mdogo mbele ya maaskari wale lakini haikuwa sababu ya yeye kuweza kueleweka kwa haraka. Nelson alipigwa pingu na kisha kufikishwa katika kituo cha polisi cha Muhimbili.
Hapa ni wapi?” ni swali analozinduka nalo Adela baada ya kupoteza fahamu kwa muda wa siku kadhaa, tangu alipoangukiwa na kitu kizito kichwani katika ajali ya tetemeko la ardhi mkoani Kilimanjaro. Kivivu anazungusha macho yake huku na kule pale wodini alipolazwa kusudi aweze kutambua alipo. Nuru inayopenyeza katika dirishani la chumba alicholazwa, inaonekana kukera macho yake na kusababisha ageuzie shingo yake ukutani.
Macho yake yanaonekana kuwa malegevu na yasiyokuwa na nguvu kabisa. Pamoja na hayo yote anaonekana kukunja ndita kutokana na maumivu anayohisi kwa mbali katika kichwa chake.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni