Notification
Tidak ada notifikasi baru.

SHEREHE KUZIMU (29)

Mtunzi: Frank Silaa

SEHEMU YA ISHIRINI NA TISA
ILIPOISHIA...
Nuru inayopenyeza katika dirishani la chumba alicholazwa, inaonekana kukera macho yake na kusababisha ageuzie shingo yake ukutani.

Macho yake yanaonekana kuwa malegevu na yasiyokuwa na nguvu kabisa. Pamoja na hayo yote anaonekana kukunja ndita kutokana na maumivu anayohisi kwa mbali katika kichwa chake.

KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA NAYO...
Masikio yake yanafanikiwa kunasa sauti ya mitambo ya oygen inayonguruma kwa mbali sana wodini mule. Baada ya kuushughulisha ubongo wake kwa muda wa kama dakika tano, aligundua kuwa yupo wodini amelala huku dripu ikiingiza dawa katika mwili wake dhoofu.

“Sasa nimefikaje hospitalini?” alizidi kujiuliza maswali mwenyewe, kipindi ambacho fahamu zilikuwa zinazidi kumrejea. Swali hili ndilo lililompa tabu sana kuweza kupata jibu lake, kwavile alitafakari kwa muda mrefu hadi akapitiwa na usingizi. Lisaa limoja na robo baadae alizinduka usingizini. Katika kutafakari kwa mara nyingine, sababu iliyopelekea yeye kufika hospitalini pale, alikumbuka kipindi ambacho alikuwa akilia kwa uchungu akiomba msaada wa kumuokoa Benedict ambaye alikuwa amefukiwa na kifusi. Hisia kali za uchungu zinasababisha adondoshe chozi, baada ya kumkumbuka mpenzi wake Benedict.

“Sasa Benedict alipona au alikufa?” Adela alizidi kuwaza wakati moyo ulipokuwa ukimuuma pindi alipokuwa akikumbuka tukio lile la kutisha katika maisha yake. Alizidi kuwaza huku akibubujikwa na machozi. Ukimya uliokuwa wodini ulisababisha adumbukie moja kwa moja katika bahari ya mawazo dhidi ya mwanaume ampendae, Benedict. Baada ya muda kidogo daktari alifika mule wodini na kumkuta amezinduka, machozi yakimtiririka katika mashavu yake. Daktari alifurahi sana kuona mgonjwa aliyekuwa katika hali mbaya, sasa fahamu zimemrejea.

“Doctor what happed to Benedict?” (Dokta nini kilimpata Benedict?) Adela alizungumza kwa sauti ya unyonge huku machozi yake yakizidi kulowanisha mashuka ya kitanda alicholalia. Swali aliloulizwa daktari linaonekana kuwa gumu sana kwake, kwavile hakuwa akimfahamu mtu aliyekuwa akiuliziwa na mgonjwa ni nani.

Moja kwa moja daktari anaamua kuzungumza na Adela kwa kutumia maneno ya kumtia moyo kwa vile alijua saikolojia yake itakuwa imevurugika kutokana na ajali mbaya aliyokuwa ameipata. Adela anafarijika kwa maneno ya daktrai na hatimaye anapiga moyo konde.

Adela alizidi kupata nafuu kila jua lilipochomoza. Mwili wake ulizidi kupata nguvu na maumivu yalikuwa yanapotea kabisa mwilini mwake. Siku ya nne wakati adela akiwa bado wodini, alipata wazo la kuwatafuta wazazi wake ili aweze kuwaeleza mkasa mzito aliokuwa ameupata wakati alipokuwa safarini kuelekea shuleni.

Aliona msaada pekee kwa wakati ule upo kwa wazazi wake. Hivyo basi aliazima simu ya daktari kisha akaingiza numerali za rununu (namba za simu) za mama yake ambazo alikuwa amezikariri kisha akabofya kitufe cha ‘OK’ katika simu ile. Kwa bahati mbaya muda ule simu ya mama yake haikuwa hewani. Kwahiyo daktari alimuahidi kumuazima kwa wakati mwingine ili ajaribu tena.

Wakati wa jioni daktari alikuwa akipita katika wodi za wagonjwa kuangalia afya zao zinaendeleaje. Alipofika katika wodi ya Adela, Adela alitumia nafasi hiyo kumuomba simu kwa mara nyingine ili aweze kuwasiliana na mama yake. Daktari hakuwa na shaka, alimuazima Adela simu. Kwa bahati nzuri simu iliita upande wa pili.

“Tririi! tririii!” baada ya sekunde kadhaa simu ilipokelewa, lakini cha kushangaza ni kwamba, simu ya mama yake ilipokelewa na mtu mwingine ambaye hakuweza kumfahamu kwa haraka. Ghafla Adela alikata simu ile haraka, ili aweze kuzichunguza vema zile numerali za rununu, kwani alihisi amekosea. Baada ya kuchunguza numerali zile mara mbili mbili aligundua kuwa hajakosea chochote.

“Sasa mbona simu ya mama inapokelewa na mtu mwingine?” Adela aliwaza huku akijaribu kuitafuta namba ile kwa mara nyingine tena ili aweze kufahamu kulikoni.

“Haroo.” Sauti nzito ya lafudhi ya kikurya, ilisikika upande wa pili.

“Heloo, habarii.” Adela alisalimia huku akiitegea sikio vema sauti ile ili aweze kuitambua.

“Nzuri, mambo vipi.”

“Safi, samahani namwomba mwenye simu.” Adela alisikika.

“Ndio mimi ninayeongea. Unasemaje?”

Adela alishikwa na bumbuwazi kwavile sauti aliyokuwa anaisikia alishindwa kuitambua kwa kuihusianisha na mazingira ya pale nyumbani kwao. Haikuwa sauti ya kaka yake ambaye pengine ndiyo angeweza kupokea simu ya mama yake ingawa uwezekano bado ni mdogo sana.

“Lakini mbona hizi namba za simu ni za mama yangu?” Adela alihoji.

“Embu jaribu kuhakiki namba zako vizuri, utakuwa ume wrong number.”

“Poa poa.” Adela aliitikia kwa shingo upande, huku kidole gumba kikiwa tayari kwenye kitufe cha kukata simu. Ubongo wa Adela ulikuwa ukifanya kazi kama kompyuta ili aweze kubaini sauti ile kwenye simu ya mama yake ni ya nani. Ilibidi aushughulishe ubongo wake vilivyo kwa kuwa, alikuwa na uwakika hajakosea namba. Ndani ya sekunde kadhaa kabla Adela hajakata simu aliweza kuifananisha sauti ile na ya mwanaume alionyesha hisia za kumuhitaji kimapenzi kwa muda mrefu, Marwa.

“Lakini samahani kaka, kwani unaitwa nani na upo wapi?” Adela aliuliza kwa lengo la kuthibitisha hisia zake.

“Jina rangu ni Marwa nipo shinyanga vijijini.” Adela alihisi ulimi umekuwa umzito ghafla baada ya kulisikia jina hilo. Ukimya ulitawala kwa muda wa sekunde kadhaa wakati Adela alipokuwa ameshindwa kuongea tena kwa kuhisi mate yamemjaa kinywani.

“Unamaanisha Marwa kaka yake Maige?” Adela alihoji zaidi.

“Ndio mimi, halafu kweli wewe sio Adela unacheza na akili yangu?” Marwa naye alifanikiwa kuigundua sauti ya Adela kwenye simu.

“Ndiyo mimi.”

“Sasa mbona unanichanganya wakati unafahamu fika hizi ni namba zangu za simu. Au ndiyo unanitega mrembo?”

Ilibidi Adela atoe simu sikioni ili aweze kuitazama kwa mara nyingine namba zile za simu, kwavile bado alikuwa haamini amini. Katika hali ya kushangaza Adela aligundua kuwa namba zilizokuwa zinaonekana katika kioo cha simu, hazikuwa namba za simu za mzazi wake badala yake ni namba zingine ambazo wala hazifahamu. Kilichomshangaza zaidi ni kwamba hakuwahi kukariri namba za simu za Marwa. Tukio lile lilimshangaza mno, kiasi kwamba ikapelekea kujifinya finya ili aweze kuzinduka usingizini kwasababu alihisi kama vile yupo ndotoni kumbe sio kweli.

“Lakini nimezihakiki namba hizi mara nyingi nyingi, inakuwaje sasa naziona tofauti na ilivyokuwa awali?” Adela aliwaza huku akitoa macho kama vile mtu aliyezinduka katika usingizi wa pono. Hata hivyo anajikuta akipata shauku ya kutaka kuendelea kuzungumza na Marwa jambo ambalo halikuwa la kawaida.

“Sawa bwana, kumbe kweli nimekosea namba. Naomba radhi kwa usumbufu.”

“Usiwe na shaka Adela.”

“Nimekumiss sana Marwa nahitaji kukuona.”

“Kwani wewe upo wapi?” Marwa alizungumza huku akitabasamu baada ya kusikia Adela anahitaji kuonana na yeye. Alipata furaha ya ghafla kwavile hakuamini kama dawa ya mganga itafua dafu kwa mwanamke mrembo kama yule.

“Hapa nilipo, nipo hospitali nimelazwa baada ya kunusurika kufa katika ajali ya tetemeko la ardhi mjini Moshi. Kwahiyo nilikuwa namtafuta mama ili niweze kumtaarifu kuwa nimelazwa KCMC.”

“Masikini, pole sana. Vipi unaendeleaje kwa sasa?” Marwa aliongea kwa masikitiko makubwa baada ya kusikia kuwa Adela alipatwa na matatizo. Lile tabasamu bomba lililokuwa limechanua katika uso wake lilitoweka ghafla.

“Naendelea vizuri kwa kweli. Basi naomba uwajulishe nyumbani kwetu, uwape namba hizi za daktari ili iwe rahisi kunipata.”

“Usijali, nitakwenda sasahivi kuwapa taharifa zako.”

Baada ya mazungumzo hayo, Adela alimkabidhi daktari simu yake. Daktari aliendelea na utaratibu wake wa kupita chumba hadi chumba kuangalia hali za wagonjwa. Adela alibaki peke yake wodini akisubiri nesi aweze kwenda kumchoma sindano majira ya saa moja na nusu. Kwanzia muda huo alipomaliza kuzungumza na Marwa, basi moyo wake unajikuta ukimpenda mwanaume huyo kupita kawaida.

Banedict alifutika ghafla katika mawazo yake. Akili yake pamoja na fikra zake zinaonekana kuwa mateka kwa Marwa. Kuisikia sauti ya kijana huyo kwenye simu imekuwa kama sumu kwake, kwavile haishi kumuwaza kila sekunde, kila dakika na kila saa.

Siku iliyofuata mama yake Adela alimpigia simu yule daktari na kuzungumza naye kwa kirefu sana, kuhusiana na hali ya Adela. Pesa za malipo ya matibabu alitumiwa daktari ikiwa ni pamoja na pesa za matumizi ya Adela kwa muda wa wiki mbili, ambazo bado alitakiwa kuwepo hospitali pale, akiendelea kutumia dawa pamoja na sindano. Mara baada ya mama yake kutuma pesa hizo, mapema siku hiyo Adela alimuagiza daktari akamnunulie gauni jipya, viatu pamoja na simu. Usiku wa siku hiyo hiyo Adela anaamua kutoroka hospitalini. Saa kumi na moja kasoro siku inayofuata anaanza safari yake ya kuelekea Shinyanga kwenda kuonana na mpenzi wake Marwa.

MUHIMBILI.

Madaktari kadhaa wanaingia katika chumba cha upasuaji ili waweze kuokoa maisha ya mgonjwa. Kisu kilichokuwa kimenasa tumboni, ndicho kilichokuwa kinakwenda kutolewa katika upasuaji huo. Matabibu hao wanaonekana kuchangamka sana katika kila walichokuwa wanakifanya. Haraka haraka hizo ni katika kuhakikisha kwamba mgonjwa hapotezi maisha japokuwa hali yake ni tete sana kwavile ametokwa na damu nyingi. Upasuaji ulifanyika kwa muda mfupi na ulifanikiwa kwa asilimia mia moja. Kisu kilitolewa ingawa kwa kiasi kikubwa kiliharibu utumbo wa mgonjwa. Kilichofanyika ni kwamba matabibu hao walitumia ujuzi wao wote ili kuweza kuhakikisha kwamba mgonjwa anapona. Uangalizi wa kiafya uliongezeka zaidi kwa Benedict kwasababu hali yake haikuwa ya kuridhisha kabisa. Kufikia muda ule hakuna mtu aliyeweza kufika hospitalini pale na kudai kuwa yule mgonjwa ni wake. Kwahiyo madaktari walijawa na huruma sana na pia walipata moyo wa kumuudumia ukizingatia kwamba alipata matatizo juu ya matatizo.

Wiki moja baadae, waandishi wa habari waliweza kufika hospitalini, ili kuweza kufahamu hali ya yule mgonjwa aliyechomwa kisu. Katika mahojiano yaliyofanyika katika ofisi ya mganga mkuu kwa takribani saa moja, mganga huyo alithibitisha hali ya mgonjwa inaendelea vizuri baada ya upasuaji mdogo. Siku ya pili yake magazeti mbalimbali nchini yalipambwa na habari za Benedict kama ifuatavyo.

“AHUENI KWA MGONJWA ALIYECHOMWA KISU WODINI.” Gazeti la Mwananchi

“HALI YA MGONJWA ALIYENUSURIKA KIFO WODINI, YAZIDI KUHIMARIKA.” Gazeti la Mtanzania.

“MGONJWA ALIYECHOMWA KISU AENDELEA KUDUNDA.” Gazeti la Kiu.

Licha ya magazeti mbalimbali kupambwa na habari hiyo lakini pia redio, televisheni, na mitandao ya kijamii iliripoti maendeleo ya Benedict hospitali.

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi
Sherehe Kuzimu
Jiunge kwenye mazungumzo
Chapisha Maoni