Notification
Tidak ada notifikasi baru.

SHEREHE KUZIMU (35)

Mtunzi: Frank Silaa

SEHEMU YA THELATHINI NA TANO
ILIPOISHIA...
Mume wake na mwanae walikuwa tayari wameshatangulia mkutanoni. Baada ya kupingana kwa muda mrefu na nguvu ile iliyokuwa inamsukuma hatimaye alijikuta njiani, akitembea kwa mwendo mkali kuelekea kule kwenye mkutano.

KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA NAYO...
Kwa vile hapakuwa mbali sana muda mfupi baadae alifika eneo la tukio. Ghafla mapepo yaliyokuwa ndani yake yalianza kufurukuta kwa vile lile eneo halikuwa la kawaida. Wahudumu walijaribu kumshika lakini hakushikika kwa vile alikuwa na nguvu zisizo za kawaida. Alianza kukimbia kuelekea madhabauni ambapo kulikuwa na watumishi mbalimbali wa Mungu.

Watu wote waliacha kusikiliza mahubiri na kumtazama Vivian ambaye alionekana kuwa na mapepo hatari. Alikuwa akilia kama paka, wakati mwingine alijongea mithili ya nyoka mwenye sumu kali. Watumishi wa Mungu, walianza kufanya maombezi ya kukemea mapepo yaliyokuwa ndani yake. Yalifanyika maombi mazito ya kuvunja maagano ya Viviana na kuzimu. Ilikuwa ni shughuli kwelikweli kwavile alikuwa na maagano mengi katika ulimwengu wa giza. Wachungaji waliomba maombi ya kuvunja maagano yale. Watu wote waliokuwa uwanjani pale walishiriki katika mapigano makali ya kiroho, kumpigania Vivian ambaye alikuwa mateka wa siku nyingi katika ulimwengu wa kuzimu.

Kwa kuwa hakuna nguvu inayoweza kusimama juu ya nguvu ya Mungu, maagano yote ya kuzimu yalivunjwa na hatimaye VIVIAN akawa huru.

Alipewa nafasi ya kutoa ushuhuda pamoja na kumshukuru Mungu. Alipokea kipaza sauti na kuanza kuzungumza huku akilia. Kwa masikitiko makubwa alisimulia kila kitu ambacho aliwahi kukifanya yeye na mama yake wakishirikiana na ulimwengu wa kuzimu. Ilikuwa ni hadithi iliyokuwa inaonekana kama vile ya kusadikika lakini ilikuwa na ukweli wa asilimia mia moja.

Alipomaliza kutoa ushuhuda wake alishangaa kumuona mume wake pamoja na mwanae wakimfuata pale madhabauni na kumkumbatia huku wakilia sana. Waumini walishangilia kwa vigelegele baada ya kuona tukio lile. Isaka alishangaa sana kumuona rafiki yake pale mbele akikumbatiana na mwanamke yule. Alimpa kipaza sauti na yeye aweze kuzungumza na ndipo alingundua kuwa yule ni mke wake.

Nelson na mwanae walilia sana baada ya kugundua kuwa vifo pamoja na matatizo yote waliyokuwa wakipitia katika familia yao, yalisababishwa na Vivian ambaye, hawakuwai kumdhania hata siku moja kwamba anaweza kufanya mambo makubwa namna ile. Pamoja na hayo lakini waliishia kumshukuru Mungu kwa kumkombo katika mapito ya kuzimu.

Mtumishi wa Mungu alimuongoza Vivian katika sala ya toba na hatimae akampokea Yesu kuwa bwana na mokozi wa maisha yake. Baada ya hapo aliagiza kile kibuyu cha kichawi kikaletwe ili kije kuchomwa. Vivian alikwenda hadi hotelini na kukichukua na kisha kukifikisha kwa mchungaji. Kilipokelewa na mchungaji kisha kikachomwa palepale uwanjani huku watu wakishangilia kwa ishara ya ushindi. Baada ya maombezi Nelson na familia yake walirudi katika hoteli waliyokuwa wanaishi kwa muda.

********

Ndani ya wiki hiyo hiyo kulifanyika mkutano mwingine wa injili kijijini kwa kina Adela. Mtumishi wa Mungu, Abeli kutoka nchini Kenya aliongoza huduma ya maombezi na uponyaji. Adela na ndugu zake walihudhuria mkutano huo ambao ulifanyika jirani kabisa na nyumbani kwao. Roho mtakatifu alimuonyesha mtumishi wake kwamba, ukoo wa akina Adela ulikuwa katika mateso makubwa ya mizimu. Yalifanyika maombi ya kuvunja na kuharibu kabisa nguvu ya mizimu hiyo, iliyokuwa inawafuatilia miaka na miaka, hatimae wakawa huru.

********

Siku chache baadae Nelson na familia yake waliwasili London International airport kwa ndege aina ya Boeing 222-400ER-Condor. Walipokelewa na Mr Lee na kisha wakafikishwa katika nyumba iliyokuwa imeandaliwa kwaajili yao. Siku iliyofuata Nelson alisaini mkataba wa kufanya kazi na taasisi ile kwa muda wa miaka 10 kama mhandisi mkuu. Walianza maisha mapya huko nje ya nchi huku wakiendelea kumtumikia Mungu kwa furaha.

Miaka kumi baadae Nelson na mke wake walikuwa na mafanikio makubwa ya kimwili na kiroho.

**********

Ulipoanza mwaka mpya wa masomo, Benedict alianza kusomeshwa bure kama ambavyo baba yake aliahidiwa mwanzoni. Elimu yake ya kidato cha tano na sita, alisoma katika shule iitwayo Heven star high school iliyopo jijini London. Shule hiyo ilikuwa chini ya taasisi ‘spiritual health.’ Baada ya miaka miwili, alipata ufaulu wa juu sana na kufanikiwa kujiunga na chuo kikuu cha Harvard kilichopo nchini marekani, kusomea Bachelor of science in mathematics (yaani shahada ya sayansi katika hisabati). Alifurahi sana kuwa mmoja wa wanafunzi wa chuo kile kwasababu, ilikuwa ni ndoto yake tangu alipokuwa sekondari. Marafiki zake wote ambao aliwahi kusoma nao, walikuwa wanafahamu jinsi ambavyo alikuwa anakipenda chuo hicho.

Aliendelea kupenda somo la hesabu, kwasababu ilikuwa ikimkumbusha kipindi cha nyuma, alipokuwa na mpenzi wake. Aliapa kulipenda somo hilo hadi mwisho wa maisha yake kama ishara ya kumuenzi Adela. Hakuwa na matumaini ya kuonana nae tena kwasababu hakujua kuwa ni mzima ama ni mfu. Walipotezana katika kipindi kigumu mno. Umbali wa kijeografia ndiyo uliopoteza kabisa ndoto zake za kuonana na binti huyo kama endapo angekuwa ni mzima. Hakuwa na matumaini ya kurejea Tanzania ili hali wazazi wake hawana mpango huo.

*******

Adela alipohitimu kidato cha sita alifanikiwa kuongoza kitaifa katika mitihani ya taifa. Jina lake lilitikisa kwenye vyombo vya habari vya hapa nchini, kwa vile alifanya vizuri sana, katika masomo yake yote. Kwa bahati nzuri alipata ufadhili wa kwenda kusoma katika chuo kikuu cha Harvard cha nchini Marekani. Alifurahi na kufarijika sana kwasababu katika kumbukumbu zake anakumbuka kwamba kipindi alipokuwa sekondari alikuwa akimsikia Benedict akisema kuwa, anatamani siku moja kusoma katika chuo hicho maarufu duniani.

Siku moja Adela alikwenda kufanya manunuzi ya vyakula katika supermarket iitwayo Morton Williams iliyopo jirani kabisa na chuoni. Baada ya manunuzi hayo wakati anatoka nje, ghafla mlangoni alikutana na Benedict anaingia ndani. Wote kwa pamoja walishikwa na bumbuwazi kwavile hakuna aliyekuwa akiamini kwamba amemwona mpenzi wake. Adela alidondosha mifuko iliyokuwa mikononi mwake na kisha akakumbatiana na Benedict huku wote wakilia kwa furaha.

“Are you the one?” (Hivi ni wewe jamani?) Adela alizungumza huku uso wake akiwa ameuangalizia mgongoni mwa mpenzi wake wakati alipokuwa amemkumbatia kwa nguvu zote.

“Naam!, ndiyo mimi Benedict wala hujakosea mpenzi.” Kijana alizungumza kwa furaha huku mikono yake ikifanya kazi ya kufuta machozi yaliyokuwa yanaendelea kumdondoka mwenzie.

“Nilijua ulifia katika ajali ya moto iliyoteketeza nyumba yenu.”

“Hapana, familia yetu iliondoka katika nyumba ile baada ya kufukuzwa na uongozi wa kampuni ambayo baba alikuwa akifanya kazi. Kwahiyo waliopoteza maisha katika ajali ile ya moto walikuwa ni watu wengine ambao walihamia pale.” Benedict alisikika.

Siku ile ilikuwa ni ya furaha, kuliko siku zote ambazo waliwahi kufurahi maishani mwao. Walianza kusimuliana yaliyojiri tangu ile siku waliyopotezana, hadi sababu zilizopelekea kufika chuoni pale. Walipohitimu chuo kikuu, Benedit alimpeleka Adela nyumbani kwao Uingereza kwenda kumtambulisha kwa wazazi wake. Walipokelewa vizuri sana na kutakiwa kila heri katika maandalizi ya harusi, ambayo walipanga kufanyia jijini London.

Wote walikuwa na bahati sana kwakuwa walipata kazi yenye kipato kizuri, siku chache baada ya kuhitimu elimu yao. Mwaka mmoja baadae walioana kwa harusi kubwa ambayo ilihudhuriwa na ndugu na marafiki wa pande zote mbili. Adela hakupenda kuwa mbali na mama yake kwahiyo, alifanya mpango mama yake na kaka yake wakaamia nchini humo miezi michache baadae.

Funzo:
Usichoke kumtumainia MUNGU katika maisha yako kwavile huijui kesho yako.

AHSANTE SANA.

MWISHO

Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi
Sherehe Kuzimu
Jiunge kwenye mazungumzo
Chapisha Maoni